THAMANI YA WAZAZI

Naitwa Omar Bin Zongo, wakati mwengine hua napenda kujiita Bin Zongo sababu yakufananisha thamani ya kilichopo ndani yangu na mimi maana mara zote umbile langu halifanani na busara zangu labda pengine nikimtanguliza baba yangu mbele watu watasema amerithi kwa huyo Zongo.

najivunia zaidi na napenda ukiniita Bin Zongo...

leo nina ujumbe maridhawa nataka kukugea.

Baba yangu alifariki dunia mwaka 1995 mimi nikiwa mdogo sana siijui hata sauti ya mzazi wangu huyo wakiume.

mama yangu amefariki mwaka 2014 nikiwa na ufahamu wangu hakika maumivu ya kifo chake bado yangali moyoni mwangu.

kuanzia mwaka huo wa 2014 niliishi bila ile nguvu ya faraja itokanayo na kujua kuwa mama au baba yupo nyuma ya hatua zako.

hakuna faraja inayofariji kwa kiwango kikubwa sana duniani kama faraja ile yakukutana na magumu ukahisi mama au baba yako atasimama kwako kwa ushauri na hata muongozo mwengine wowote utakaokuwa unauhitaji kutoka kwao.

hiyo ndio nguvu itokanayo na tumaini la kujua kuwa wazazi wako wapo duniani.

leo ujumbe wangu unazungumzia thamani na umuhimu wa wazazi hapa duniani.
hakika nakuambia hakuna wivu uumizao kama wivu wakumuona rafiki au jirani yako anakumbatiwa nakufurahi na wazazi wake ilihali wewe wakwako walishapotea katika uso wa dunia hii na hakuna hata bahati mbaya ya wewe kuonana nao tena.
hakuna wivu unaojeruhi ngome ya furaha kama unaposikia mtu amefanyiwa kitu flan na baba au mama yake, au kwenye hafla wewe umeenda mwenyewe lakini wenzako woote waliohuduria kila mmoja ameenda na wazazi wake, wanacheka nakufurahi huku kila mmoja akionekana amepambwa na tumaini la kuwa na wazazi wake maishani.

naamini Mara zote Rabbuka hamtupi mkono mtu mpweke duniani humfariji kwa siri nakumfanya atangamane na wengine bila kuonesha dalili yoyote yakuwakumbuka wazazi wake lkn ni ukweli iliofichika kuwa kumbukumbu za wapendwa wazazi wake lazima zinajirudia nakumtonesha kidonda kisichopona chakuondokewa na watu hao muhimu zaidi duniani.

kuna dawa gani yenye uwezo wakufuta kovu la kuondokewa na wazazi hapa duniani?

jibu ni hakuna na kama ipo basi ni usingizi ambao hukujia kwa muda fulani tu na ukishtuka kovu hilo lingali bado nawe.

nakumbuka nilimwambia rafiki yangu mmoja aitwae Kaijage dakika chache tu baada yakutoka ofisini kwa baba yake Mzee Kabanza.

nilimwambia kwa mtindo wa ujana zaidi utani ukiwa mwingi lakini nilihitaji sana anielewe na azingatie ninachomwambia.

nilimwambia mimi sio mtu wakawaida kaijage nadhani hilo unalijua sasa naomba uzingatie ninachokwambia.

mwenzako mimi sina baba wala pia sina mama, najua madhila ya upweke yatokanayo na kuwakosa watu hawa.
nilimwambia kuwa mimi niko tofauti nayeye sababu mimi nimekosa wazazi yeye anao tena shukrani kwa mola alijaaliwa kuwa nao wote wazazi wenye furaha ambao nilijifaghiri sana kufahamiana nao na nakumbuka niliwaambia nawapenda muda mchache tu nilipoonana nao.

nakumbuka nilimwambia Kaijage asifanye hata kosa la bahati mbaya kuwaudhi wazazi wake.nilimsisitiza kuwapenda sana nakujitoa maisha yake yote kuwatazama wazazi wake kwa jicho lakuwatengenezea furaha na wajivunie kuwa wazazi.

nakumbuka nilimwambia kaijage, ni kijana mwenzangu ambaye tulizoeana sana na urafiki wetu uligeuka kuwa udugu.

na nakumbuka vema kipindi namueleza hayo nilivunja ratiba zangu zote Dar ili kwenda Tanga nyumbani kwao kulikuwa na shughuli ya komunio kwa mdogo wake aitwae Jenifer.

nakumbuka nilipita ardhi ya muheza kama sipajui, ardhi ambayo ulihifadhiwa mwili wa Mama yangu! nakumbuka wakati napita muheza niliumiza sana niliporejea nyuma kimawazo nakukumbuka malezi aliyonipa mama yangu juu ya ardhi nyekundu ya wilaya ile.

nakumbuka vema nilimwambia kaijage na kumkazia sauti hasa pale alipoleta utani wakati me nazungumza kumueleza umuhimu wakuwajali wazazi wake.

nilimsisitiza sana asiuchezee ule muda ambao yeye na wazazi wake wote wana pumzi. nilimwambia achunge ulimi wake anapozungumza nao, matendo yake anapokuwa mbele yao na mara zote apige goti kuwaombea afya n uzima wazazi wake wale.
kaijage nilimwambia haya muda mchache tu kabla yakupanda gari lakurudi dar huku yeye akiahidi kuendelea kuwa tanga kwa siku mbili zaidi.

nilipanda gari nikafunga mkanda nakuanza kuombea safari kabla haijaanza kisha nikaanza kurejea ukarimu ucheshi na upendo wa wazazi wake Kaijage.

hakika nilibaini kuwa wale ni mfano wazazi wote duniani! ni hapa ndipo pia nilipomkumbuka marehemu Mzee Zongo na Mama yangu, ni hapa ndipo kwa mara nyengine nikaumia tena sababu yakubaini mimi sina wazazi.
ona thamani ya wazazi wako rafiki yangu, wapende kwa maisha yako yote, waheshimu kwa akili yako yote na ujitoe kwao kusimamia furaha na amani ya nafsi zao.

ile nukta unayobaini yupo baba na mama yako basi itumie kuwajulia hali hata kama upo mbali nao,

kutwa nzima jiwekee ratiba yakufurahia nao wafanye wahisi upo karibu nao kwa kujadiliana nayo masuala mbalimbali yanayojiri kitaifa na kimataifa.

watanie, waombe ushauri wafanye waione thamani yao, kamwe usifanye kosa hata kwa bahati mbaya kuwaudhi maana nafsi yako itakuja jutia siku moja.

mimi tangu nikose mama duniani, ninapokutana na mama wa mwenzangu namuita mama kwa kumaanisha ili walau niikate kiu yangu yakuita jina hilo.
 hakuna maumivu yanayoumiza kama unapoona mtu anamkaripia mzazi wake, anamdharau nakumpuuza,

unaumia sababu ni wewe pekee ndio unajua kuwa yule hajui atendalo, anachezea muda ambao yatima wanautamani wautumie vizuri kuonesha taadhima yao mbele ya wazazi wao.

tumia vema muda ule ambao unabaini kulia kwako yupo mama na kushoto kwako yupo baba,

pia shukuru Mungu hata kwa kukupa mzazi mmoja wapo kati ya hao muombee mmoja aliyetangulia apumzike kwa amani na uliyebaki naye muoneshe thamani yake na aione furaha unayoitafuta kwa ajili yake.
kwa wewe ambaye una mgogoro wa nafsi kutokana na makosa aliyowahi kukukosea mzazi wako au anayokukosea sasa piga goti muombe MUNGU akupe ujasiri wakumsamehe mzazi wako na huyo huyo mungu muombe amnyooshe mzazi wako,

kwa wewe uliyewakosa wazazi wote piga goti pamoja nami muda huu kwa sauti ya upole na unyenyekevu tuzungumze maneno haya kwa MUNGU wetu
Asante mungu kwa kuwachukua wazazi wangu, nakushukuru sababu haukosei katika mipango yako wewe ni mkamilifu, nina ombi moja mola wangu ambalo hua nalirudia sana hasa ninapowakumbuka wao, ombi lakuwasamehe dhambi zao nakuwahurumia kwa kuwapunguzia adhabu zako, wahurumie sababu ni wao ndio walikuwa wakinihurumia enzi za utoto wangu,
ni wewe ndio mungu unaejua maumivu gani hua nayapata kila nikiwakumbuka wao nakuomba uzidi kunipa faraja niweze ishi bila kufarijiwa na upendo wao.

watunze vema wazazi wa rafiki zangu duniani kote maana kwa sasa ni wao ndio wazazi wangu ninaojivunia nao kwa kuwaita mama nakuwaomba ushauri inapobidi.

ahsante Mungu na nisamehe makosa yangu nami daima niwe mzazi mwema kwa watoto wangu na wa wenzangu! nifanye niwe mzazi ambaye watoto wangu hawatakuja kulilia jina langu kwa mateso ya mama yao.
na kukabidhi amani ya wazazi wote duniani na walinde wewe kwa malaika wakowatukufu amin...

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »