ZILIKUWA ni shamrashamra za kuiaga karne ya 20.
Huu ulikuwa ni usiku wa kuikaribisha karne ya 21.
Huu ulikuwa ni usiku wa kuikaribisha karne ya 21.
Usiku ambao walinzi wa dunia hii
walijisahau na kunywa mvinyo kupitiliza hadi kusababisha walewe mno
Walisahau kabisa kazi yao ya ulinzi na kufanya Jitu Adui kuingia duniani
kirahisi mno.
Jitu Adui ndilo
lilikuwa jina lake alilopewa na wazazi wake huko atokako lakini kutokana
na utukutu wake na kutokuwa mtiifu alijipa jina la utani ambalo
lilijulikana zaidi ADUI WA MAADILI.
Huku
walinzi wakiwa na silaha zao wakikoroma na kumwaga ute Jitu Adui
aliingia kwa tahadhari huku akiukokota mzigo wake uliojaa Rushwa, Utovu
wa nidhamu, Uasherati, Uzinzi na Udanganyifu wa hali ya juu.
Jitu
Adui alikuwa makini mno wakati anawapita walinzi wale hakutaka hata
kuruhusu unyayo wake utengeneze sauti ndogo ambayo aliamini ingewafanya
walinzi wale washtuke na hiyo ingekuwa hasara kubwa sana kwake.
Jitu Adui alitetemeka mno alipokuwa akiona walinzi wale wakijigeuza, walinzi maarufu duniani ambao walipewa jina la Wahenga!
Kutokana
na umakini wake Jitu Adui akafanikiwa kuingia ndani ya dunia hii na
wakati amefanikiwa kuwapita walinzi wale moyo wake ulilipuka furaha sasa
akiamini kuwa azma yake ya kuipotosha jamii itafanikiwa.
"Mimi ndio Jitu Adui a.k.a Adui wa Maadili, nitahakikisha dunia hii inapotoka kimaadili.
Nimenyanyasika
sana katika karne zote zilizopita watu walijifanya wapo makini
kusimamia utu wao lakini sasa wameniruhusu kuingia kwenye himaya yao,
waache tu washerehekee kuipokea karne ya 21 mimi acha kwanza niingie
klabu nikawachore kuona udhaifu wao. Mimi ndio Jitu Adui nitahakikisha
nawapa majanga hawa watu....shenzi"
Alijiwazia
Jitu Adui huku mzigo wake ukionekana kumuelemea, alikuwa na furaha
isiyo kifani aliona namna ambavyo ataitumbukiza dunia katika jehanamu la
laana na vituko visivyoisha.
Hatua zake za uchovu zilizodhihirisha kuwa atokako ni mbali ziliishia katika ukumbi mmoja wa starehe duniani.
Hakuwa
na pesa hata sumni ya kuingilia mule ukumbini lakini kutokana na
shamrashamra na furaha za kuikaribisha karne ya 21 binadamu walijisahau
na ndipo Jitu Adui akapenya ukumbini mule na kwenda kukaa nyuma kabisa
ya spika zilizokuwa zikisikiliza muziki.
"Wapo
wachache sana humu! Halafu mavazi yao bado yana heshima fulani hivi!
Nitahakikisha wanajaa klabuni wengi na mavazi yao yanabadilika,
nitapigania nguo za nusu uchi..." Alijisemea Jitu Adui, huku akitoa
waraka wake aliokuwa ameuhifadhi katika koti lake kubwa alilokuwa
amevaa.
Aliufunua waraka huo kisha
akaanza kuusoma, Yalikuwa maneno mengi na kila neno liliwekwa kwa
namba, neno la kwanza kabisa liliandikwa AKILI ZAO, Jitu Adui alisoma
neno hili tu kisha akatabasamu na kuufunga waraka wake na kuurudisha
kwenye koti lake.
Alitaka aanze kucheza na akili za binadamu, Hii ndio mbinu yake ya kwanza kabisa aliyoipa kipaumbele.
"Akili
zao zinaimarishwa sana na vitabu, wakisoma hupata uelewa na kujikuta
wana ufahamu mkubwa, Nitahakikisha napoteza kabisa mvuto wa vitabu vya
nidhamu na maadili, na nina uhakika nitafanikiwa na hili nikicheza na
akili za waandishi"
Aliyawaza haya Jitu Kuu ambaye kwa kweli alidhamiria kufanya mapinduzi makubwa ya kimaadili duniani.
* * *
Mishale
ya alfajiri ndio walinzi wanashtuka kutoka katika lope la usingizi. Ni
mmoja kati yao ndiye aliyeweza kuona nyayo za mtu.
Alishtuka
sana na kuwashtua wenzake, nao walishtuka na wasijue ni nyayo za nani.
Hivyo wakaamua kumuita mtaalamu wa kutambua nyayo naye alipozitazama kwa
makini akajikuta akisema kwa nguvu "Tumekwisha".
iNAENDELEA......