Naitafakari
siku, ilivyoishia vema
Tena Kwa
nyingi shauku, nilitamani kusema
Na hali
yangu kapuku, akili ikazizima
Asante kwa chozi lako, nimeijua thamani
Anililiaye nani, kwa uchungu wa mapendo
Nalijihisi katuni, tena nisiye vishindo
Nitesekae jangwani, nisipate maji fundo
Asante kwa chozi lako, nimeijua thamani
Kutangatanga msafiri, nisietua mizigo
Ninazipanga safari, zilizo nyingi mitego
Sasa natafakari, ingawa mekupa zogo
Asante kwa chozi
lako, nimeijua thamani
Neno gani nikwambie, huenda ukaelewa
Unisikilize mie, tayari nimechachawa
Ububu nijivikie, usije ona melewa
Asante kwa chozi
lako, nimeijua thamani
Nalikutoa machozi, na wala sikukufuta
Yalidondoka kwe ngozi, hukutaka kupukuta
Nilijifanya ajizi, nisiyejua chakufata
Asante kwa chozi
lako, nimeijua thamani
Asante kwa chozi lako, limeniweka furahani
Najua thamani yako, sitokutoa moyoni
Sikuliliwa mwenzako, wewe wa kwanza amini
Asante kwa chozi
lako, nimeijua thamani
Ujuaye hali yangu, na bado ukathamini
Nakuapia kwa Mungu, sitaitema amini
Sitayasikia majungu, wakitema midomoni
Asante kwa chozi
lako, nimeijua thamani
Sijui nawaza nini, kujibu yaso kichwani
Nashukuru ukibaini, niyasemayo betini
Ndiyo yaliyo moyoni, tena hayo ya sirini
Asante kwa chozi
lako, nimeijua thamani
Huruma
pendo la kweli, hujifichama moyoni
Huna jicho la tapeli, kujisafi tu usoni
Huzuni yako ya kweli, naitazama machoni
Asante kwa
chozi lako, nimeijua thamani
By
Fulgence Makayula