USISAHAU CHANGAMOTO @UjanaMajiYamoto

Na.
 Omar Zongo

Ishi nami kwa furaha ila tambua siku moja kuna karaha hivyo usisahau kujiandaa!
Usisahau changamoto ambazo kwa jicho langu naziona zimejaa pomoni!
kupendana angali vijana ni suala lamaana lina taadhima na kubwa heshima!
lakini usisahau kuwa ujana ni laana, jumba la usahaulifu na upotofu na kwa taarifa yako wengi waliouvamia sasa hivi ni wafu!
walio hai wanasubiri andiko litimie!, afya zao dhalili, wakenda kama walevi, wamedhoofu mwili, nguvu zao kumbukizi, kwao naona dalili ya kupoteza nguvu kazi, ni baya suala hii UJANA kweli maradhi.
Usisahau changamoto ya kwanza kwetu Ni Ujana!
tena hii ni ya Moto yapasa kuomba sana.
tuvuke mito, vijito tukeshe kuombeana!
kwenye baridi na joto tubaki tumeshikana.
Tena tuache utoto laa sivyo tutaachana.
Ujana ni changamoto naomba kumbuka sana!
wengi eti tulizo wanasema lipo kwa wazee! eti "vijana mzozo bora tuwapotezee" mapenzi sio mchezo yanaumiza
aisee!
singeni khabari hizo mchumba uzirejee, sikio lako chotezo changamoto zipokee
tena silete mchezo amani nisogezee!
ujana una kiburi dhahiri chaonekana! tena dakika sifuri tayari tumegombana ninani wakusubiri ujana subira hauna.
kijana bado nalipa nguvu tele maungoni.
ukizingua nasepa wasemavyo wa mjini.
anitakae nampa damu changa mauongoni, ujana unayo pupa
tulia na wako ndani.
mwisho wa ujana aibu kwa wale waso busara!
tulia wangu muhibu tuichore wote dira!
kesho tukiwa mababu simulizi yetu bora.
ujana wangu nalewa jaribu kunielewa pambana na hali yako katika kunikomboa
tumia utashi wako nipate kujielewa nimimi ndio mwenzako sahihi wa rika lako watoto nitakugea iweje uende zako sihadaike na wakubwa, wazee watakufia.
navaa nguo dhalili maungo yangu yawazi
na hizi ndizo dalili za ujana ipo wazi endelea kuhubiri nibadilishe mavazi usiseme wasubiri kitafakari kizazi.
watoto wetu wawili wataurithi ushenzi.
watu wazima muhimu wanajua kukutunza.
mie kijana nidhamu yangu yakuokoteza. haya yote nafahamu ila changamoto tunza.
hata wao walikuwa enzi zao kama mimi chamsingi vumilia tupendane kama nini.
wazee watakufia usalie kilioni ipite miaka mia ujutie mauongoni maradhi kashakugea na watoto yatimani.
chamsingi vumilia mimi na wewe pamoja
makosa kujirudia ujanani si kioja heshima kuzingatia ndio jambo nalingoja,
endapo kinipatia watatuzika pamoja,
kupendana ujanani ni suala lapendezea kutulia mahabani ni jambo adimikia alaaniwe shetani balaa katuletea wazee wakazi gani acha kuwasujudia.
ujana wao wanani mpaka uzee wa kwako epuka uhayawani tulia nami mwenzako.
enzi zao ni zamani walikuwa rika lako,
ujana wako ni shani
tumia na rika lako.
wao watu adhimu, adimu na wa muhimu kupata kwao wosia ni jambo la tabasamu,
na sio kukuchumbia kwangu ni jambo dhalimu.
ndio nina changamoto rika langu potofu sijauacha utoto mambo yangu pungufu,
kichwani nina ndoto ya kuwa maarufu
na kumiliki watoto warembo walinganifu.
haya yote yataisha ukiwa mkamilifu,
usiache kunikumbusha usichoke uvumilivu.
Usiufate mkumbo tengeneza nyumba yako!
watakupiga kumbo wakung'ong'e wenzako!
hili sio fumbo nasema na nafsi yako!
sasa kamata nyundo uponde ujana wako.
nami napanda upendo uote pembeni yako.
Usisahau Hii Changamoto nikubwa isiyo mithilika tena sio ya kitoto imesheheni vibweka!
moshi kugeuka moto ni jambo latambulika
tone kijito na mto hatua zahesabika,
haiwi bahari kuu bila ziwa kuvukika.
Andiko hili ni lako wahuba nikupendae wala sio la mwenzako ni wewe nikutakae samehe makosa yangu ujana wangu uelewe nataka nibaki kwako wivu wako uondoe.
najitambua mwenzako ujana kuudhibiti ingawa wanizidia una nyingi tashtiti Mungu kumrudia ni mbinu tuidhatiti
Muhimu kudhamiria tufike wote Tamati.

USINIACHE MUNGU WANGU!

Naandika kwa mtindo wa kuomba, maombi ambayo yametawaliwa na unyenyekevu na sura yangu ina dalili zote za kuonesha kuwa nina uhitaji wa ninachikiomba! tena sio uhitaji mdogo nina uhitaji mkubwa wa nikiombacho leo.

Yupo mpumbavu mmoja, ambaye daima sura lake analikunja kwa jazba kila anaposikia nataja jina lako kwa unyenyekevu nakumuita yeye kwa kiburi tena nikimtukana kumuita Mwanakharamu.
ni yeye ndiye ambaye ananitamani kuninyakua nakuniadhibu vikali, anatamani niwe mtumwa wake, ananiwinda kwa juhudi zake zote na hata siku moja hajachoka kunifatilia.

ni huyu maaluni ndio leo amenifanya ninyooshe mikono yangu kwako nikiomba kwa unyenyekevu nikikusihi kamwe usiniache maana dude hili linanitamani leo kesho niwe rafiki ake.
lengo lake nikuasi Mungu wangu na nifanye yale uloyakataza

hakika nakuambia sijawahi kumpenda kiumbe huyu tangu nilipoijua dhamira yake kwangu.
leo nina machache nataka kukwambia MUNGU wangu na nakuomba sana unipe msaada wako kwa kuniitikia Amina.

kwanza naomba ujue kuwa nina uhasama mkubwa na huyu Mpumbavu mwenye majina mengi yalaana.

niyeye ndio anaitwa Shetani, ibilisi na pia ndio huyu kiongozi wa waovu ambaye daima anapenda kunishawishi nitende uovu.

Ponya yangu ni jina lako MUNGU wangu na kinga yangu ni Imani ya dhati kwako Mungu wangu.
kwa sababu yako nimetangaza vita na mjinga huyu na simuogopi kamwe lakini chamsingi tambua MUNGU wangu bila wewe siziwezi hila zake.

usiniache Mungu wangu hata kwa sekunde moja maana nina hofu anaweza kuitumia sekunde hiyo kuniangamiza daima.

mimi nina kiburi kwake napingana na matakwa yake na niyeye pekee ndiye ambaye naweza kutangaza mbele za watu kuwa simpendi! namchukia mfanowe hakuna.

ninapowaza safari hii bila wewe kiukweli hofu yangu dhidi yake yanizidi mauongoni lakini ujasiri hunizidi kila ninapokumbuka uwepo wako kwangu.

usiniache mungu wangu hakika nina hofu na shari za kiumbe huyu bila wewe siwezi kumudu kupingana nae maana nia yake ovu nikunigombanisha nawewe.

Mungu wangu usiniache ili niendelee kumtukana nakumlaani mpumbavu huyu mwenye nia yakunipeleka jahanamuni.

natunishiana nae misuli kwasasa nikitegemea wewe upo, namtemea mate usoni kwa dharau na kumkejeli kwa maneno ya shombo yeye hanifanyi kitu sababu anajua upo na wewe ndio mtetezi wangu

sura lake baya lenye jazba dhidi yangu naliona na nina uhakika akipata hata kajiupenyo kadogo tu kakunizuru basi atafanya hima ili niangamie.

mwanzoni alinirimbikizia mikosi, nikakosa hata vinavyonistahili.

akanidhulumu haki zangu nikaishi kwenye udhalili na pia haitoshi akanifanya muovu mwenzake.
ni uwezo wako Mungu wangu na huruma zako ulizo nazo ghafla anashagaa yale yote aliyonilimbikizia yamegeuka neema zinazonifanya nikusujudie nakukutukuza wewe MUNGU wangu.

anashangaa ukarimu wako, umenipokea! ukanisamehe nakunijaza nguvu na kinga! anashangaa ule mzoga wake aliokuwa anautumikisha umekingwa na malaika wazuri kutoka kwako.
Usiniache MUNGU wangu maana mie sijui hata sura ya mpumbavu huyo lkn sifa zake zenye kutu nimezijua kupitia wewe.

usiniache MUNGU wangu nakuomba endelea kunikinga na huyu kiongozi wa wachawi wenye kuroga, mahasidi wenye kuhasidi, makafiri wenye kukufuru na waovu wenye kusujudia maovu.

Usiniache MUNGU wangu maana bila wewe naogopa kwakweli maana huyu MJINGA atanigeuza kiti chake kule Motoni na kunifanya tena MTAJI wake hapa duniani.

Ninajikinga kwako Nashetani Mungu wangu! usiniache kamwe.

@IshiKikamilifu
          2017

MASIKINI "MSAMAHA" @thamani yako haipo!!


uko wapi rafiki yangu msamaha, kusema kweli nimegundua leo kuwa haupo katika dunia hii maana mimi mwenyewe nimeshindwa kujisamehe mpaka muda huu kwa uzembe wakupoteza andiko langu la mwanzo.
Na
Omar Zongo
Andiko langu lakwanza kukuhusu lilikuwa zuri lapendeza nililipamba kwa vazi la mafumbo juu yake nikalivika joho zuri la tenzi kisha nikalipulizia marashi yenye misamiati ya lugha adhimu ya kiswahili!
ndio!!
andiko kukuhusu wewe MSAMAHA nililipamba likawa kamili kwa kusomwa lakini sijui ninini masikini ya MUNGU ghafla bin vuu tsunami la teknolojia ya simu inayohitaji chaji kuwa pomoni muda wote likanivaa simu ikazima kabla ya andiko langu kukuhifadhi ukahifadhika.
kwa namna ambavyo nilikupangilia ukapangika wallah naapa sikuwahi kupangilia vizuri andiko lolote kabla yako!
nafsi ikiwa imejawa lawama yakutokuwa makini na chaji yangu nikakumbuka kujiomba msamaha na nilipofanya hivyo angalau nafsi ikawa huru lakini nikaja gundua kisasi na simu yangu hakikuniisha moyoni nilitamani kuibamiza chini.
ufukara ndio ukanionya nakuniambia niibamize nione kama nitapata tena simu nyengine hivi karibuni.
tuachane na hayo leo nimedhamiria kuweka sononeko langu kwako wewe MSAMAHA!
Hivi ulizaliwa lini na kipindi gani uliishi duniani hapa na kifo chako kama kimetokea ilikuwaje na kama ulizikwa ulizikwa makaburi ya wapi???
nakuuliza hivi nikiwa na sababu lukuki maana kwasasa thamani yako siioni!
waja tumekuwa wagumu kusamehe! kwasasa ukikosea jiandae kulipiziwa na tena unafiki wenye sura ya msamaha umetawala hivyo kufanya mtu awe rahisi kusema amekusamehe ilhali roho yake ikiwa na dukuduku lisiloisha.
uko wapi rafiki yangu msamaha, kusema kweli nimegundua leo kuwa haupo katika dunia hii maana mimi mwenyewe nimeshindwa kujisamehe mpaka muda huu kwa uzembe wakupoteza andiko langu la mwanzo.
nijuavyo mimi MSAMAHA wewe nineno la thamani sana tena hautamkwi kiholela kwa mtu aso namaana.
mfano mie sidhani kama watu kumi wameshafika ambao nimewahi kuwatamkia neno hilo.
nikirudisha fikra nyuma nagundua niwachache mno ambao niliwakosea na kutokana na utu wao na thamani kubwa walio nayo nikawatamkia neno wewe MSAMAHA!
huwezi kuamini kuna wengine kama bado wapo hai kamwe hawawezi tena kupata neno hilo kutoka kwangu na hiyo yote nikwasababu enzi za thamani yao kwangu huenda imeshaisha.
huo ni mfano wakukujulisha kuwa wewe ni miongoni mwa mja uliye na thamani utokapo kinywani! na sio wote wanastahili kukupokea.
kama mtu huna mpango nae wala hauna umuhimu nae itawezekana vipi kumkosea nimegundua leo tena baada yakukutafakari sana nimeona kuwa tunawakosea tulio nao karibu kwasababu ndio watu wetu wamuhimu katika kukamilisha furaha yetu nandio maana umuhimu wa neno MSAMAHA huwahusu sana watu hawa.
lakini pia katika tafakuri yangu leo nimegundua kuwa ni watu hawa ambao nao hawaoni tena thamani ya neno wewe MSAMAHA.
wanakudharau vijana wa kileo wanasema UNACHUKULIWA POAH sana siku hizi.
enzi za wahenga msamaha ni tamko ambalo lilikuwa limebeba majabari mazito matatu Hekima, Busara na Uvumilivu.
majabari hayo yalikuwa ngao kwa anayeomba msamaha na anayepokea msamaha huo nakusamehe! tofauti na sasa.
enzi za dot.com msamaha ni neno ambalo analitoa mtu dhalili, mwenye uhitaji na fakiri mbele ya anayemuomba Msamaha.
nimetumia staha lakini kutokana na kuwa ashahkum si matusi basi acha nifunguke kuwa wakileo msamaha hutafsiri kuwa ni lofa, mzembe ambaye hawezi kujizuia kukosea.
thamani yako haipo Msamaha! watu waleo wamekosa uvumilivu kamwe hawataki kuvumilia makosa!
wapo wachache ambao mara moja watakusamehe lakini hawatasahau na ukiteleza mara ya pili hukumu kali ya machungu itakuhusu tena usije ukathubutu kuleta falsafa za Isaah Bin Maryam eti Samehe Saba mara sabini, watakutukana matusi yanguoni.
iko wapi thamani yako rafiki yangu msamaha mbona ninaowathamini hawashtuki tena hata nikikukimbilia wewe nakukutamka mbele yao.
mbona wananihukumu wakati wewe umeletwa ili kufidia mapungufu tuliyoumbwa nayo wanadamu.
kwani nani asojua kuwa nisisi waja ndio hujifunza kwa wingi kutokana na makosa na pia asiyetambua kuwa ni dunia hii ndio haina kiwango maalumu cha makosa yaani yapo tuu yameumbwa kwa mtindo tofauti tofauti na wakati mwengine unaloona wewe kosa mwenzako analiona ni sahihi kabisa.
Msamaha jitokeze basi kuokoa dunia hii ikibidi kukosoa pia zile sheria ambazo kiini chake ni UMOJA WA MATAIFA.
zikosoe na uziambie kuwa katika kanuni na taratibu za kumuadhibu mtu wangeweka pia sheria yakusamehe maana sio wote wakosefu kutoka ndani mioyo yao.
natamani ungejidhiri machoni mwangu MSAMAHA ningechukua hata harufu ya jasho lako nikaiweka chumbani kwa mwanamke wangu ili aione thamani ya kusamehe na anisamehe hata kwa makosa ya kesho na keshokutwa.
ningechana hata upande wa vazi lako nikawaonesha wote ninaohitaji msamaha wao wa makosa yote yaliyo na yanayokuja ili wanisamehe kwa dhati ya moyo wao.
KUMBUKA KUWA UMEUMBWA KWA MAKOSA NA UTAKOSEA, LEO KESHO NA HATA KESHOKUTWA KAMA UTAKUWEPO UTAKOSEA TU.
KAMWE HUWEZI KUYAEPUKA MAKOSA MPAKA UKAMILIFU WAKO UTAKAPODHIHIRIKA KATIAKA ILE SIKU YA MWISHO YA PUMZI YAKO!
USICHOKE KUSAMEHE SAMEHE KADIRI YA UWEZO WAKO!
NAWEWE UTASEMEHEWA SIKU MOJA!
tena utasemehewa siku ambayo una uhitaji kweli MSAMAHA!

KESHO HAIJULIKANI @Ishi Ki kamilifu

Na
Omar Zongo

Siku za mwisho kabla ya kifo chako nakiri niliona mabadiliko ya kitabia! ulipenda kukaa mwenyewe! upole ulikuvaa na hata chakula kilikuwa hakipandi jambo ambalo silakawaida kwako, kiukweli upweke niliuona kupitia macho yako na sijui kwanini nilikupuuza.

leo natamani kujua nini chanzo cha wewe kuwa hivyo lakini sina namna yakusikia sauti yako ikinieleza.

je ni hali ngumu ya maisha ulikosa dira na muongozo???

mimi sijui..

je ni mapenzi yalikuvuruga kiasi kwamba ukakosa ushauri wangu mimi kaka ako hivyo ukaamua kujimaliza???

hili pia mimi sijui

wakati mwengine nawaza labda kutokuwa karibu tena nawewe tukibadilishana mawazo, kucheka na kutaniana ndio chanzo maana ni ukweli kuwa ulinizoea sana na ni mimi pekee ndio nilikuwa kaka na rafiki yako pia.

bado hili nalo sina uhakika nalo pia.

kwa ufupi nateseka kwa kutaka kujua kilichokufanya ukakatisha pumzi yako.

sijui kwanini sikutilia maanani nilikupuuza uliponiomba kuzungumza nami hata sauti yako ikiniomba kuzungumza nami bado inajirudia masikioni mwangu "bro nina shida naomba tuongee kidogo" ulikuwa huchoki kuniomba kwa kusema aina hii ya maneno.

ukubwa kweli jalala sikujua najutia!

leo hii nagundua kuwa mimi ndiye sababu ya kifo chako ukweli nina hatia!

uliniganda kwakweli mpaka nikaona kero, ukaka nikasahau nikajawa na kiburi nikakukwepa waziwazi nikidai niko busy laiti kama ningejua ningekuacha tuwe wote,nikusikilize na nijue unakabiliwa na nini mdogo wangu.

nimimi na wewe tuu mama etu katuzaa mdogo angu kipenzi huzuni inanijaa laiti kama ningejua ningekuazima sikio.

sio kawaida yako kuja kwangu asubuhi, ulikuwa mpole sana furaha hukuwa nayo, utani na shem wako hata haukuwa nao na haikuwa tabia yako upole ulio nao sikuyajua mwenzako maisha ni mapitio nakumbuka sura yako mdogo wangu Kihiyo.

hukutaka chakula changu wala hata senti yangu, hukutaka kulala kwangu wala chochote chakwangu ulitaka faraja yangu sikujua mdogo wangu kwanini hukuniambia nikaacha ujinga wangu.

nahisi maisha yalikupiga mbele yako giza tupu dili zote hazitiki ukata ulikuzonga, kila unachotamani kukipata vigumu hakuna matumaini ninani wakumwambia!?

mitihani ya maisha msomi ila masikini, kazi zakubahatisha kesho yako haijulikani nimimi ndio kaka yako ulitaka nikupe moyo ndio mana ukaja kwangu nami nikawa mchoyo kukupa tu muda wangu nikaona ni gharama masikini mdogo wangu ulizidi kukosa dira.

sikupata muda asilani wakusema nawe japo kidogo usiku niliporudi nilijifungia chumbani kwangu tena ulinisikia nikicheka na mke wangu.

kudamka mapema ikawa tabia yangu mradi nisisikie una nini mdogo wangu nilipo nina kilio nasutwa na nafsi yangu!

nilisahau kabisa vifo vya wazazi wetu aliyeanza ni mama na baba akamalizia hivyo mimi kubaki nawe sikuweza kupinga.

mimi nikawa baba na mama kukufariji namlaani shetani kunisahaulisha wajibu.

ghafla nikapuuza kwamba mimi ndio mfariji wako mwanzo nilikuwa nakupa moyo usome kwabidii nakukusihi usikate tamaa utafanikiwa lakini mara nikasahau kabisa kuwa nimimi ndio nilikuwa nguvu yako pale unapokwama.

kiburi cha pesa kilinifanya nisahau kuwa wewe bado mdogo hujakomaaa na ungehitaji muongozo wangu hasa unapokosa muelekeo.

nilisahau kabisa kuwa maisha ni magumu mno na yana mitihani na yoyote anastahili kupewa moyo!
nilisahau kabisa kuwa neno langu la faraja ni tumaini kwako kuliko pesa na chakula.

leo hii sijui hata nini kilikusibu mpaka ukakosa raha na ukakata tamaa nakuamua kujiua!


muda wangu niliuona una thamani sana na hata ulipoomba kuzungumza nami nilisema "tutaongea baadae dogo" bila shaka ulishangazwa na tabia yangu hii maana siku zote za ukuaji wako nimimi ndiye nilikuwa wakwanza kukufuta machozi ukilia na ulipoanguka nimimi ndiye nilikuwa pale kukuokota.

maisha yamenibadili yamenifanya nijidanganye kuwa umekuwa na sipaswi kuwa karibu yako bila kujua kuwa mimi pekee duniani ndio ndugu yako.

nilizoea kugusa nywele zako kwa upendo nikikubembeleza ulale enzi za udogo wako siamini leo kama nagusa majani namchanga kwenye hili kaburi lako.

nisamehe mdogo wangu! nisamehe sana kwakutokupa nafasi yakusikiliza kile kinachokutatiza maishani!

siamini kama sipo nawe tena leo nimepata funzo!

NI VEMA KUMUAZIMA SIKIO KILA ANAYEKUOMBA KUONGEA NAWEWE PENGINE KATIKA MAONGEZI YENU NENO LAKO MOJA LIKAWA MSAADA MKUBWA KATIKA MAISHA YAKE NA LIKAMUONGEZEA SIKU ZA KUISHI AU LIKAMBADILISHIA MAISHA YAKE!

TUMAINI LA WANAOTUPENDA LIPO KWETU TUSILIZUIE KUWAFIKIA HASA WANAPOLIOMBA!

MAISHA NI MAFUPI MNO HAKUNA KINACHOUMIZA KAMA KUGUNDUA HAYUPO TENA DUNIANI ULIYEPESA KUMFANYA AWEPO NI DHAHIRI UTAKUWA MWENYE HATIA MAISHA YAKO YOTE UTAJIONA MUUAJI!.

tabasamu lako, ucheshi, upendo na maneno mazuri yatokayo kinywani kwako ni zaidi ya majumba, magari na vyote ujuavyo vina thamani, amini na uweke akilini kuwa sio muda wote watu wako wakaribu hasa walio chini yako wanataka pesa kumaliza matatizo yao, faraja nisuluhisho na muongozo wenye sababu nyingi za kumfanya mwanadamu asonge mbele bila woga wa magumu yaliyo mbele yake.

kamwe usipuuze kutoa tumaini kwa wanaokutamainia!

TWENDAPO WAZEE HAWATAKUWEPO!!!

"Huko twendako, siku baada ya hizi nina uhakika wazee watakuwa viumbe adimu kuonekana katika sura ya dunia hii! sababu ni nyingi lakini chache kati ya hizo ndizo nitakazoziwekea mkazo katika andiko langu la leo!"

Na
Omar Zongo

Baridi kali inayopuliza mwilini inasababisha mwili usisimke kwa woga vinyweleo visimame, hali hii ya hewa ni sababu tosha kwa wavivu kuvuta shuka hasa mishale hii ya asubuhi lakini kwangu ni tofauti, saa kumi kamili za alfajiri niko macho natafakari utashi wa MUNGU.

tafakuri yangu hiyo inaenda sambamba na vitendo vyangu takatifu vyakujiandaa kwenda masjid kumsujudia mwenye dunia hii, mwenzenu imani yangu ni muislamu lakini namshukuru MUNGU sijawahi kukashifu imani za wengine.

vitendo vyangu vya maandalizi yakujiweka safi kimwili na kiimani vinachukua kama dakika kumi na tano hivi, najipuliza marashi, navaa msuli wangu kwa kuukunja vema mkwiji, shati langu safi nililoliandaa kwa ajili ya swala ile kisha nalisindikizia na koti kubwa ili angalau kuzuia ubaridi usiendelee kunipa adhabu!

Sasa nimekalimika kwenda kumsujudia aliyeniumba mimi na kuumba kila unachokifahamu ulimwenguni hapa! msikiti uko mbali kidogo hivyo nina kama mwendo wa hatua elfu mbili mia tano ili kuufikia lakini nitafanyaje na wakati nina nia yakuswali na waumini wenzangu, Njiani nipitapo waja wachache mno.

ndio, lazima wawe wachache maana sio wote wenye ujasiri wakudamka mishale ile hasa kama hawana sababu za msingi!

ni kunguru na ndege wengine ndio nawaona kwa wingi kwenye misitimu ya umeme wakijibizana kwa sauti zao, kichwani kwangu natafsiri sauti zao kuwa ni kelele za kumtukuza MUNGU muweza vyote! nami kimoyoni namtukuza MUNGU maana nimeambiwa kitabuni kuwa ameniumba kwa ajili hiyo tu.

hatua kadhaa mbele ghafla mwili wangu unanisisimka mno! najiuliza ni kwanini hali hii!? hisia mbaya zanivaa, wazo kuhusu uchawi na hila za majini na binaadamu wabaya lanivaa!

naingiwa na woga kwa mbaali lakini ghafla ndani yangu sauti ya imani kwa MUNGU inanijaa! nakumbuka kukimbilia mikononi kwa mungu kuomba ulinzi wake! napiga dua za kujihami na shari za ubaya wa aina yoyote unaotaka kunidhuru asubuhi ile.

Naam! MUNGU ni mwema ghafla tumaini lanivaa, woga waniepuka sina tena wasiwasi,
imani yangu kwa MUNGU bila shaka imeniweka mbali na mabaya yote yaliyokuwa yananisisimua mwili wangu, kiukweli muda ule sikuona lolote baya lakini waswahili husema kuwa ukihisi mwili wako unakusisimka ujue kuna shari karibu yako, hivyo mie nikaona busara kujikinga kwa MUNGU wangu mlezi.

kama una imani nawe nakushauri kufanya hivyo! kila unaposisimkwa na mwili katika mazingira hatarishi

Hatua zangu Imara hatimaye zikakomea msikitini, Kabla yakuingia ndani ya nyumba hii tukufu namshukuru Mungu kwa kunifikisha salama, maana kutopishana hata na vibaka,wezi au majambazi ni baraka tosha kwakweli.

Jicho langu sasa laangaza msikitini, uzuri ni kwamba tayari nilishachukua udhu nyumbani hivyo nikaingia tuu nakuketi msikitini kusubiria adhana ili niswali sunna!

wakati nimekaa kitako mule msikitini navuta uladu taratabu kumtaja MUNGU wangu kwa wingi ndipo wazo likanijia, wazo muktasi ambalo nikaona si sahihi kuliacha linipite, wazo lakuwatazama watu wachache waliowahi asubuhi ile msikitini kama mimi!

Nikaruhusu jicho langu liangaze kwa kila mmoja, hakika walikuwa sio wengi hata kama ningetaka kuwahesabu ningeibuka na idadi ya watu saba au nane lakini sio zaidi ya kumi, nakiri katika mtazamo wangu kwa waumini wenzangu wale kuna kitu nilikibaini kuwa ni mimi pekee ndiye nilikuwa kijana kati yao!

wengi walikuwa watu wazima, wazee kabisa wenye umri sawa na baba yangu na wengine babu zangu kabisa! wazo langu likakwamia hapa nikajikuta najiuliza kwanini wazee tuu ndio wana muamko wakufanya ibada kwa wingi???

swali langu hili likaibuka na majibu yangu mepesi ambayo naamini kama tukiyatafakari kwa kina labda huenda tukayafanya yawe mazito.

jibu langu kubwa kati ya mengi niliyoyajibu ni kwamba tunapoelekea wazee hawatakuwepo!!
Ni tafakuri yangu ambayo sina shaka itapigwa vita nakuonekana laana kwa vijana lakini kamwe sitaifuta kirahisi na itaendelea kusalia wazoni mwangu labda ikitokea niyaonayo yakibadilika!
huko twendako, siku baada ya hizi nina uhakika wazee watakuwa viumbe adimu kuonekana katika sura ya dunia hii! sababu ni nyingi lakini chache kati ya hizo ndizo nitakazoziwekea mkazo katika andiko langu la leo!

Kwa mahesabu ya haraka haraka yasiyo hitaji akili kubwa kufikiria utabaini kuwa kwa kipindi kirefu sasa misiba mingi tunayoisikia ni ya vijana wadogo ambao bado damu zao zingali mbichi na zenye nguvu yakuzunguka mwilini kwa kasi iliyo kuu.

hali hii ni tofauti na hapo kale, sitashangaa vijana wa leo wakileta mzaha katika neno langu hili wakiniita Mhenga! lakini ukweli nitausimamia daima sitauacha uniponyoke nafsini mwangu.

nahisi sababu ya vijana kufa kwa wingi katika karne hii ni kutokana na dhambi zetu nakuhatarisha maisha yetu kwa kufanya kwa wingi yale ambayo MUNGU ametukataza kuyafanya.

Uzinzi, Uasherati, Ulevi, Utovu wa Nidhamu na Starehe zilizo kinyume kabisa na maandiko kutoka kwake Jabbar.

Uzinzi huo niliyoutaja matokeo yeke mengi ni sambamba na Maradhi yanayosababisha kifo.

Uasherati pia nimeujumuisha ingawa hauna tofauti na uzinzi lakini nahisi huu umepita mipaka ndipo tunapoona hata matendo yaliyoangamiza kizazi cha Nuhu, hakika hili nalo matokeo yake ni kifo.

Ulevi nao huchangia kwa asilimia kubwa Ajali na mengine mengi yanayokatisha maisha ya vijana, kama vile matumizi ya dawa za kulevya yanayonyonya nguvu na ushababi wa mamia kwa maelfu ya vijana duniani kote.

Utovu wa nidhamu na starehe zilizo kinyume na maandiko haya yote kwa ujumla na mengine yanayofanana na haya huzalisha wivu, visasi, tamaa na mabalaa yanayosababisha wenyewe kwa wenyewe kuuana.

Vijana kwasasa tunaisha kwa kasi inayoogopesha ni nadra sasa mtu kufika umri walau wa miaka 40, yaani thelathini na tano yenyewe mtu amekwepa mengi yaliyotaka kummaliza au kama sio hivyo ndio yuko mbioni kufa aidha kwa virusi vilivyo mwilini mwake au kwa visasi alivyowekewa na wenzake kutokana na kuiba mwanamke wa watu au kuzulumu mali ya mtu.

Nionavyo Mimi miaka ijayo Dunia haitakuwa na wazee au kama watakuwepo basi wachache sana! hawa tulio naso sasa masikini ya Mungu wanadondoka taratiibu sana ukilinganisha na vijana lakini utaratibu huo nina uhakika utawamaliza wote na hakutakuwa na wazee tena maana tunaotakiwa tukawe wazee ndio hivyo tena tumezongwa na vikwazo vyakukanyaga anga hilo la uzee.

Masikini ya Mungu bila shaka wazee wana ile hofu ya kuwa umri wao umeenda mbele, nguvu zao zinawaisha mauongoni mwao kwa hivyo wameamua kujikurubisha kwa MUNGU wao walau watubu dhulma walizozifanya kipindi chote cha ujana wao.

dhana hii inawasaidia wazee wengi kufanya ibada na natamani vijana nao tungekuwa tunajijengea hofu hii kwamba sasa izrael anatuwinda sisi kwa hiyo tuanze kumrudia MUNGU, maana hatuijua saa wala dakika.

lakini Masikini vijana sisi tupo tofauti kabisa na dhana ya wazee, daima tunajiona wenye nguvu na tunaweza kufanya lolote kwa kipidi hiki, mbaya zaidi wakati mwengine tukidiriki kusema kuwa "Muda wakutumia ndio huu, kutubu tutaanza uzee ukitufikia"

Hakika kizazi hiki kinapotea kwa kukosa maarifa! uvivu wakufikiri na kuzifuata hadaa za mpumbavu, mjaa lana, maaluni ibilisi, shetani kiumbe ninayemchukia kuliko wote duniani! MUNGU anilinde na kuniepusha na shari zake mjinga huyu.

Tafakari sasa na unipe jibu jee unadhani TUENDAKO WAZEE WATAKUWEPO??? baada ya hawa waliopo kuisha!

MUNGU atujaalie mwisho mzuri! atuondoe gizani na atufanye tuwe wenye kumtukuza kwa kufuata amri zake!

amen!!!

Muda wa swala umefika, acha nisimame na waumini wachache waliofika msikitini leo, vijana nao tupo ila wengi wazee.

nakuahidi nitakutaja katika swala yangu hasa muda wakusujudi ili uwe mwenye kukumbuka kuwa duniani Tunapita!

SAUTI YA MUNGU


 Anaandika 
Omar Zongo

wakati mwengine ukiwaza sanaaaa utagundua kuwa hauna faida yoyote kwa mwenzio wala yeye hana faida yoyote kwako!

ukiendelea kuwaza sanaa utagundua ni MUNGU pekee ndio mwenye faida kwenu wote, na ukiendelea kuwaza sanaa utagundua mnashobokeana, kufuatiliana kujuliana hali na kujaliana kutokana na Amri ya huyo  MUNGU ambaye ametuamrisha tupendane na ni dhambi kuchukiana.

ukiwa unaendelea kuwaza sanaa utazidi kubaini kuwa anaekupuuza kutojali uwepo wako na kukupotezea hauna sababu yoyote yakumshobokea, kumfutalia nakumjali lakini ajabu ukiendelea kuwaza sanaa utagundua kuwa kufanya hivyo nikumuudhi MUNGU wako ambaye anakujali wewe kwa ukarimu mkuu! na niyeye ndiye aliyekuamrisha umpende adui yako!

ukiwa hujachoka kuwaza utagundua kuwa kuna kitu kinaitwa uvumilivu kinahitajika sana ili uwende sawa na watu wote maana wameumbwa kwa mitihani usipoangalia unaweza ukaamka asubuhi moja nakuwatukana wote kwa kuwa hawana faida kwako!

ukiwa unaendelea kuumiza kichwa kuwaza utagundua kuwa hata uvumilivu wenyewe kwa sasa haupo bali ni maigizo ya uvumilivu kuchekeana kinafki na upendo wenye joho la fitina ndani yake!
ukiwa unaendelea na juhudi yako yakuwaza utagundua kuwa hata wewe umeshaanza kurithi kajiunafki hako ambako kanakufanya ucheke wakati moyoni una jiduku duku! huo ni mwanzo wake mwisho wake unakuwa na jiroho jikubwa kama bara la afrika!

Utajiona hakika ukiwa unaendelea kuwaza na utabaini kuwa wakati mwengine kile unachokisema moyoni mwako sicho kabisa kinachotoka mdomoni mwako, lakini kutokana na kuwa hutaki vita na kuchukiwa ndio maana unajitahidi kujichekesha na kujifanya uko karibu na watu!

endelea kuwaza na kama hutaki mimi nitakuwazisha ili ujione kuwa kuna kajiunafki umeumbwa nako na kanakufanya wakati mwengine umchukie mtu bila sababu lakini kutokana na kuwa hutaki wengine wajue unajifanya unabaki na siri yako moyoni!

naitamani ile siku ya dhahiri ifike! siku ambayo mioyo ya watu itafunguliwa nakuwekwa wazi kilichojificha humo, naamini siku hiyo itashibisha mawazo yangu ya leo ya kwamba sura unazozioana zikikuchekea nakutabasamu ukikutana nazo sio sura zinazokufurahia kwa dhati kabisa kwa kile ulichojaaliwa!

usichoke kuwaza rafiki angu endelea ili uone kuwa Binaadamu ukiwepo wewe pia namimi tumeumbwa na siri na wakati mwengine tunasingizia eti damu yangu na yake haijaendana! nani kasema kumchukia mtu kunasababishwa na damu, huu ni ufinyu wa fikra ambao unakufanya uhisi kuwa una haki yakutafuta sababu zakumchukia mja mwenzako!

laiti kama ungekuwa unajua kuwa kuna wakati mwili wako utaishiwa nguvu, utasikia lakini hutaweza kujibu, utaona lakini hutaweza kuamka na utabebwa lakini hutaweza kujisogeza! naamini ungejua kuwa huna thamani na wewe ni kitu kidogo sana katika dunia hii na unapaswa kutokuwa mnafki na kuizulumu nafsi yako kwa kumchukia mwenzako hata kwa siri.

hakuna mkubwa wala mwenye hadhi kuliko mwenzake duniani wote ni sawa! kuna vitu tuu vidogo sana ndio vimetufanya leo hii tuone fulani ni wa muhimu na fulani ni dhalili na hana thamani!

nikivitaja naamini vitakufanya uendelee kuwaza nakugundua kuwa binaadamu tuna ujinga ambao unatufanya fikra zetu chanya tulizoumbwa nazo tusizitumie maana haiwezekani, Muonekano wa mtu uwe ni tija katika kumtukuza huyu na kumdunisha yule.

au utajiri uwe ni chanzo chakumuona huyu ni wa maana na yule ni dhalili aso na tija! haiwezekani hata ukiniamsha usiku nikiwa na miusingizi nitakijubu haiwezekani, na nitasisitiza tena haiwezekani kumfanya fulani awe chini kisa ana kitu unahisi kitamnufaisha nawe kitakuangusha nasema HAIWEZEKANI!
Sikuwa MREXPERIENCE kabla, nilikuwa Zongo wakawaida lakini ukubwa, malezi na kuishi na waja wenzangu vyote vinanipa maneno yanayoshibisha andiko langu hili leo ambalo naamini ni SAUTI YA MUNGU!
ingepata shida nafsi yangu kama siku ingedondoka bila kuonya kuhusu maisha haya yenye utabaka,  maisha yenye umimi na ubaguzi wa hali ya juu! maisha yaliyojaa wivu, husda, uchawi na kila aina ya takataka!
hayana faida maisha haya kama waja wasiposhtuka nakugundua kuwa shetani ametutawala katika fikra zetu, anatuendesha katika maamuzi yetu na anayasimamia vema mawazo na maamuzi yetu, ni huyu mpumbavu shetani ndiye ambaye aliapa kutuingiza motoni sisi binaadamu na mungu alituamrisha tumchukie na tujikinge naye maana ni ADUI YETU.

Ukiwa bado hujachoka kuwaza utamuona huyu mjaa lana shetani anavyokupa wivu kwa kilicho bora kinachopatikana kwa mwenzako, niyeye ndiye ambaye anakupa nguvu yakumchukia kimoyomoyo na muda mwengine hukushinda nakukufanya mpaka ushiriki shirki na udiriki kuroga!

laiti kama ningekuwa sijachoka kuwaza ningeendelea kukufanya nawewe uwaze sema nahisi nimechoka na kichwa kinaniuma kwa kuwaza udhalili wetu binadamu, fikra hasi na matendo yakinafki tuliyojigubika nayo mithili ya vazi zito kwenye msimu wa baridi.

laiti kama ningekuwa sijachoka kuwaza ningeendelea kukufanya nawewe uwaze sema nahisi nimechoka na kichwa kinaniuma kwa kuwaza udhalili wetu binadamu, fikra hasi, husda na matendo yakinafki tuliyojigubika nayo mithili ya vazi zito kwenye msimu wa baridi.

Imefika muda sasa tugundue kuwa waliokufa kuwapata ni ngumu na mazuri yao, upekee wao na kila kitu kilichowafanya wawe wao wameenda navyo, hivyo sisi tuliobaki tupendane na kufurahia vizuri vilivyopo ndani yetu, maana hatutaweza kuvitoa tena andiko likitimia.

IGIZI UKAMILIFU2017

NIHESHIMU MKE WANGU

Unakumbuka maisha yako kabla sijakuoa??

ulikuwa hauna tofauti na bidhaa yakukodiwa ambayo ilikuwa ikitumiwa nakurudishwa ili mwengine aje aikodi tena.

maisha yako yalikuwa na uhuru wakukudharaulisha.
wapo wanaume wengi kama mimi walikufata nakukutumia bila hata kuwaza kuwa unastahili kuolewa.
kitendo cha mimi leo kutimiza ahadi yangu nakukuoa kinatosha kabisa kufanya wewe uniheshimu.
sio kama sijaona mapungufu yako au wewe ndio mwanamke mkalimilifu kuliko wote laa hasha! nimekuoa kwasababu nimeamua kukupokea kwa jinsi ulivyo so inatosha kabisa wewe kuniheshimu.
kwani hujasikia fununu kuwa duniani wanawake mpo wengi kuliko wanaume sasa kwanini usione bahati kubwa kwako kuchaguliwa namimi nakuolewa eti huoni kuwa nastahili kuheshimiwa nawewe??
Niheshimu mke wangu sababu nahisi kuwa nimekuvisha stara nakukutofautisha na wanawake wengine wahuni wanaotumiwa nakuachwa kila siku, naamini kuwa hayo sio maisha mazuri yanayompendeza binti yeyote hivyo niheshimu mume wako maana ni mimi ndiye niliyekukinga na mwamvuli ili usinyeshewe na mvua ya dharau wala usichomwe na jua la uhuni.

niheshimu mke wangu maana nimimj ndiye niliyewahifadhi wanao kwenye mgongo wangu bila mimi usingepata jina la heshima nakutambulika kama mama duniani hapa hivyo wakati unamshukuru Mungu kwahilo naomba unifurahishe pia kwa kuniheshimu mume wako.

ni mimi ndiye ambaye nikilala nawaza kesho niamkie wapi na nikafanye nini ili wewe ule, uvae na upendeze, tafadhali mke wangu niheshimu basi hata kwa sababu hii nitaridhika.

ndio wakati mwengine huenda nakukwaza kwa mapungufu yangu, lakini sio sababu yakunishusha thamani nakunidharau nakusihi niheshimu maana mimi sifanani na mwanaume yoyote unae na uliyewahi kumjua.

ni mimi ndiye niliyeshinda ndumba za vimada nikaruka vizuizi vyakukuoa nikafumba masikio ili nisisikie maneno ya wanafki wasiopenda nikuoea jee hii haitoshi wewe kuniheshimu mke wangu??
niheshimu mke wangu tafadhali maana wakati mwengine sina hamu yakula dona lakini kila ninapowaza natakiwa nijenge nguvu mwilini zakukulinda nakukuridhisha haja zako basi nafakamia vyote vinavyosaidia afya yangu nanguvu kuimarika.

Niheshimu mumeo maana nimeumbwa na nyama zisizopenda dharau abadan na tena dharau kutoka kwa wewe mwanamke wangu niliyejitoa kwako kwahali na mali.

Niheshimu tu kwakweli maana nafanya juhudi kubwa mwenzio ili kushinda vishawishi vya wanawake wengine wanaojipamba makusudi ili kuiba waume za watu, wanaojidai kunijali kushinda wewe na wanaokesha kwenda na wakati kwa nguo za wazi zinazonijengea ushawishi wa tamaa sababu ya miili yao wazi isiyostirika.
nipatie heshima yangu mke wangu maana kushinda mitego ya shetani mtaani ninakopita sio wanaume wote wanaweza! huoni tu kuwa unapaswa kuniheshimu na kujizuia kunidharau hata kwa sekunde moja.

usiseme eti ukali wangu wakiume ndio sababu ya wewe kunibyedulia midomo, kama mumeo wakati mwengine napaswa kukufokea ninapohisi umenikosea na sio vema kunijibu kwa kiburi utanipandisha jazba halafu nikose chakufanya maana mkono wangu mimi ulipewa tahadhari na mama yakutomgusa kwa kibao mwanamke wangu.

niheshimu tu mke wangu nami nitakuheshimu maana heshima ndio kila kitu katika ujenzi wa utulivu wa familia yetu.
tena niheshimu si kwa maigizo niheshimu kwa dhati ya moyo wako maana akili zangu zina jicho lakutambua maigizo na uhalisia hivyo tafadhali mke wangu usinifanyie maigizo katika kunipa heshima yangu.
naongea nawewe mke wangu sasa kama usasa umekuzidi kiasi kwamba kila kitu wataka ushauri kutoka mitandaoni nenda kawaambie na hili najua wapo watakaosema kuwa nina mfumo dume hivyo kukujaza umaaluni kisha ukaanza kunipuuza haki vile nakwambia NITAKUFIKIRIA UPYA NA KURUDI KWA MUNGU WANGU NAKUMUULIZA NIKWELI NDIYE WEWE NILIYEMUOMBA AU ULILETWA NA SHETWANI MJAA LANA.

Tusifike huko mke wangu naomba NIHESHIMU MKE WANGU!

MWENYE SIFA HIZI AJE!!!

Awe na kinywa tulivu chenye ulimi asali, neno lake tulizo sauti yake gitaa.
umbo lake pambo, mvuto kwa jicho langu, rangi ladha tamu si mweupe si mweusi!
lafudhi yake wimbo lahaja iwe ya pwani, sikio lipumbazike aniitapo jina.

aniduwaze na mwendo mithili yake hapana kaumbwa kwa mapambo na Mungu wa sifa njema.
upole tabia yake si binti wa pekepeke imani vazi lake hofu kwa Mungu wake.

kajaaliwa midomo unene wa kitumbua jicho lake legevu MUNGU kalipaka kungu.
nijione Adamu naye ndiye Hawa Wangu tena anipe faraja tabasamu lake afya.

Ngozi yake mboga wala sio yakughushi mchicha na matembele si maji wala mchina.
kauli yake dira, upole ndo vazi lake wala hawezi kuzira subira tabia yake.

roho yake imani, uchamungu matendo yake, adui yake shetani tumaini lake MUNGU.
mwenye sifa hizi nani namgojea afike simtaki hayawani akija nifilisike.

sitaki jibu dhalili eti nimuumbe mwenyewe naahidi kumsubiri hata kama yu tumboni.
akijue kiswahili maneno yake matamu, kizungu sistahili mie sio lugha yangu.

usomi uwepo kwake tena umsaidie kunitunza mume wake sio anikimbie.
ugumu wa hali hii aje anipe msaada kazini iwe bidii ndio ngao sio mwili.

yeyote mwenye adili akili ilo kamili mtambuzi wa neno hili afike namsubiri.