Jicho Vumilia

Jicho Vumilia
Jicho langu mwenzio naamini kuwa wewe ndio kipimo cha utu wangu usipokuwa mvumilivu  utanifanya niwe mtu wa ajabu sana, nilo jisitiri kwa vazi zuuri la staha lakini nanuka uvundo wa fedheha.

Jicho langu wewe, ni wewe ambaye huona kwanza kabla unachokiona hakijajadiliwa na ubongo nakupenya moyoni.

Jana nilipita barabarani nikaona Gari, kwa hakika nisingejua kama ni zuri gari lile bila wewe kulitazama, jicho siunakumbuka vizuri kama ulikiponza kidole changu cha mguu sababu nilijikwaa kwa kushangaa gari lile.

basi sawa nilifurahi wewe kutenda uwezo uliopewa na mola wako lakini ilikuwaje mpaka ukatazama sana mpaka akili ikajenga mvuto wa hali ya juu wa gari lile,nikabaki naumia moyoni sababu sina hata shilingi moja yakuweza kununua gari lile.

nikapiga moyo konde nakuendelea na safari huku nikifariji moyo kwamba ipo siku nitakuja kumiliki gari lile.
hatua si chini ya kumi na Tano, mbele nikiwa nimeongozana nawe jicho ukisimama kama bakora inayoniongoza niendapo ghafla ukatulia kumtazama msichana wa haiba, mwenye mvuto usio semeka..nakumbuka vema shingo yake uliiona wewe kama ni ndefu mithili ya twiga, mpole kama mnyama huyo na hata mwendo wake ulikuwa ni kama mnyama huyo pia.

rangi yake yakiafrika ambayo uliiona wewe ilifanya mpaka moyo uende mbio ukijiambiza kuwa yule ni malkia wa kiafrika.

alivaa mavazi ya asili na nywele zake zilionekana kuwa na chuki na madawa yakuunguza nywele, sababu alikuwa amesuka kawaida sana, alisuka mnyoosho lakini nywele zake zilishiba rangi nyeusi na ziliniwiri kichwani.

Jicho wewe, jicho wewe! ulisita kabisa kuhama nakutazama kwengine, ulituwama kwa binti wa watu mpaka alipokuja jamaa ambaye dhahiri alionekana ni mchumba wake, ni wewe ndio uliona namna ambavyo jamaa yule alimtandika bakora za mabusu na kumkumbatia kwa hisia, huku nafsi za wote zikionekana kufurahia kukutana kwao.

ni wewe jicho ndio ulinifanya nione wivu nakutonesha kidonda cha moyo wangu ambacho kiliwekwa na mpenzi aliyenighilibu nakuniacha mpweke huku akienda kwa vijana wenzangu wenye kuvaa chepeo na nguo mlegezo,huku masikioni wakijipamba kwa hereni na kuzungumza kwa kupindisha mdomo wenyewe wakiita swagg.

Ni wewe jicho, ambaye licha ya kuona madhara uliyoyakabidhi kwa nafsi yangu kwa kukumbushia upweke bado ukaenda kushuhudia chumba cha mwenyeji wangu niliyekuwa namfata.

Jicho wewe!
ni kweli kile chumba kilikuwa kizuri mashaallah! lakini haikuwa vema wewe kutazama kwa hisia hadi kujenga tamaa ndani ya moyo wangu, niwewe ndiye ambaye ulifanya nikashusha thamani chumba changu kwa kukiona si lolote!
Jicho kuwa na ustahimilivu, tazama kidogo utosheke, utaendelea kunipa maumivu hadi lini, mwenzio sio vyote uvionavyo nina uwezo navyo. Kuwa na Uvumilivu tafadhali


Share this

Related Posts

Previous
Next Post »