NIONE KABLA SIJAZIKWA @Sauti ya Akwi

Ijumaa tarehe 16 mwezi wa pili, 2018 Mpaka saa tatu usiku muda naenda kulala bado nilikuwa sijapata taarifa zozote kuhusu msichana aliyepigwa risasi Na polisi.

Hii ni ajabu kwakweli!!!

Ni kawaida yangu kabla yakulala kuvinjari mtandaoni kujua matukio muhimu yaliyo Na yanayoendea kujiri nchini kwangu Na kwengineko.

Nashangaa kwanini sikuliona tukio hili Tanzia.

Anyway namshukuru MUNGU huenda alitaka iwe hivyo ili usingizi wangu usiwe wa mang'am ng'am.

Lakini inawezekana vipi mpaka saa nane usiku nashtuka naingia mitandaoni kuona yaliyojiri usiku bado nisione hili tukio!!

Mpaka kesho nitaendelea kujiuliza kwanini tukio hili lilichelewa kunifikia.

Nakumbuka usiku ule nilivinjari mtandaoni kutazama zaidi maandalizi ya uchaguzi mdogo kwenye jimbo la kinondoni, Dar es salaam na lile la Siha, Kilimanjaro pamoja na kata nane ambazo nazo zilikuwa na pengo la madiwani.

Nakumbuka usiku ule zaidi nilifuatilia maagizo ya mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Jaji Kaijage.

Alikuwa anaelezea Mipango yote Na taratibu zote zinazopaswa kufuatwa kwenye uchaguzi ule.

Ni kawaida yangu saa nane usiku nikiamka silali tena mpaka kunapambazuka.
Lakini huezi amini mpaka kunapambazuka sikuwa nimeiona taarifa ya kifo cha Akwilina

Habari za Akwi zikanifikia kulipokucha kabisa tena mishale ya saa sita sita hivi kama sikosei.

Tayari ilikuwa ni siku nyengine ya jumaamosi tarehe 17 febr.

Nakumbuka Habari za kifo hiki Tata cha Akwilini zilinipa maswali kwasababu aliyenipa taarifa nae alinipa kwa mfumo wa swali.

Alisema "inawezekana vipi?"

Nami nikamuuliza "kivipi"

Akanijibu "risasi ipigwe juu af imuue mtu aliye chini??"

Nikanyamaza kwasababu sikuwa na jibu maana sikuwepo kwenye eneo la tukio.

Ila jamaa kama alidhamiria hivi kunitesa kwa maswali magumu kana kwamba mie ndiye  muhisika niliyetenda jinai ile.

Akauliza "kwanini mpaka sasa hivi kimyaaa ?? "(kwamuda ule bado hakukuwa Na tamko lolote)

Mnh! Swali hili likanifikirisha zaidi nikajikuta namuuliza "kwani ulitaka nani azungumze"

Jamaa akajibu tena "mamlaka zilipaswa kutoa tamko!"

Baadae ndio niligundua kuwa jamaa ndani yake Ana uzalendo na mwanafunzi, Mtanzania, binti mrembo ambaye ndoto yake ilizimwa ghafla na kipande cha chuma cha moto kilichopenya kichwani kwake.

Ndio! Nilibaini kuwa mtu ninayezungumza nae ana utu, ubinaadamu na ameguswa na tukio lile.

MUNGU awabariki watanzania wote walioguswa na tukio la Akwilina.

Nasikitika kuwa hayo mazungumzo yangu hapo juu sio lengo la Andiko hili.

Naomba niende sasa kwenye dhima halisi ya kunyanyua kalamu nakuumba maneno yenye kichwa kitambulishi kiitwacho NIONE KABLA SIJAZIKWA @Sauti ya Akwi.

Usiku wa siku ile ya uchaguzi nakumbuka nililala mapema sana nahisi ilikuwa ni saa moja tu tayari nilikuwa niko bed.

Sio kawaida yangu lakini naamini marehemu Akwi    alikuwa ananiita ili tukutane ndotoni.

Samahani jamani namuita Akwi nikimaanisha Akwilina, ni mapenzi yangu tu kumfupisha, naamini hakuna atakayekwazika.

Enzi za uhai wake sikuwahi kumjua, kumuona wala kuhisi kama nitakutana nae ila siku moja tu baada ya kifo chake chakupigwa risasi ameweza kunijia ndotoni!!

Ujio wake ulikuwa wa ajabu! Mavazi yake meupe juu mpaka chini! Ni machozi Na damu pekee ndio vilifanya sehemu ndogo ya vazi lake hilo ibadilike hasa eneo la mgongoni Na begani.

Eneo moja la kuchwa chake linaonekana tundu la risasi likisibabisha damu kumiminika kama bomba, machozi Na jasho la mauti yalilowesha kifua chake.

Mazingira haya ya ndoto namuona Akwilina
Akinitaka nimuone kabla hajazikwa.
 "Hakikisha unanitia machoni kabla sijazikwa"

Masikio yangu yalisikia sauti yake yenye mwangwi.

Kihoro kikanipata nikajiuliza kwanini ndoto hii!!! Kwanini akwi anataka nimuone.

Nilijua mtihani anaonipa ni mgumu hivyo nikawahi kupiga magoti mbele yake nikimsihi aniambie tu muda ule kile anachotaka kuniambia.

Akwi alisita akabaki Na msisitizo wake wa nimuone kabla hajazikwa.

Sikuchoka kumlilia nakumsihi abadilishe msimamo wake Na anieleze alichodhamiria kunieleza huo muda nikimuona.

Kwa shingo upande Akwi akaniambia " ungenitafuta kabla sijazikwa ningepata muda mwingi wakukueleza vingi ila kwavile umelazimisha nikuelewe sasa hivi nitakwambia kwa ufupi wake."

Nilishukuru akwi kukubali ombi langu nikaongeza umakini..

Akaanza kwabkuniita jina langu kifupi 'Ommy' niksataajabu nikajiuliza amenijuaje, lakini sikuwa na namna nikatuliza ubongo Na umakini ukaongezeka pia.

Akwi akaendelea kusema
"siamini kama Ndoto zangu zimezima ghafla namna hii!, uhai wangu umegeuka kafara, damu yangu ndio sadaka.

Siamini kama nimekufa kwa risasi kwenye taifa langu tulivu ambalo watu wake wengi miaka ya nyuma walikufa kwa maleria tuu Na sio mtutu.

Sikuwahi dhani kama kifo changu kingefanana Na hiki maana hata siku moja sikuwahi kutamani kwenda Kongo, Somalia wala afrika ya kati ukiachilia mbali Syria Na palestina.

Nimetamani kuonana nawewe kabla sijazikwa uiweke kumbukumbu yangu kwenye moja ya maandishi yako.

Uwaambie watoto wako kuwa Akwi ninani na kifo chake kilikuwaje.

Uwakumbushe watu kuwa kifo ni popote Na chochote huweza kutamatisha uhai wako hivyo wajiandae maana malaika wa mauti hana muda wala siku saa zote anakutazama kwa matamanio huku akingoja agizo tu kutoka kwa MUNGU aliye hai.

Nilikuwa nimekusanya coursework yangu chuo, nimemaliza napeleka barua ya field,

 kituoni nikiwa nasubiria gari simu yangu iliita nikapokea nikawa naongea kwenye simu na ndugu zangu wako mkoani.

Niliwaambia najiandaa na UE (University Examination) jumaatatu.

Nikiwa nazungumza ghafla gari la ninapoeleka likaja kituoni! Lilikuwa limejaza lakini kwavile nilitaka kuwahi kupumzika nikapanda hivyohivyo.

Masikini mimi, safari yangu ilikuwa nusu kama sio robo!

Maisha yangu yakazimwa kama mshumaa Na risasi ambayo sijui hata ilikifikiaje kichwa changu.

Uwaambie Ommy, waambie binaadamu wajue kuwa wakati mwengine binaadamu mwenzio ndio aliyepangwa aidhulumu nafsi yako bila sababu ya msingi Na hakuna wakupinga hilo maana Andiko limeshaandikwa ni ngumu kufutika, hivyo wakeshe wakiomba.

Waambie amani ya kweli, utulivu wa nafsi haupo mahali popote duniani ila mbinguni pekee kwa MUNGU mfalme wa haki.

Nina mengi lakini kwahayo machache naamini utaelewa chakuwaambia watu kupitia maandiko yako.

Mengi zaidi kama utayahitaji usisite kuniona kabla sijazikwa."

Maneno haya mkuki yalichoma kifua changu yakapasua nafsi yangu nikakurupuka kutoka usingizini,

Hammadi nipo kitandani kwangu!!!

Wanasema ndoto ni tafsiri ya yale uliyokuwa unayafikiria mchana lakini pia ni ndoto hizi hizi ndizo alizotumiwa Nabii Yusuph kujulishwa yeye ninani chini ya jua.

Acha niamini tu kuwa hii ni ndoto tu iliyokamilisha usiku wangu wa siku ile.

Ila acha nifatilie zaidi nikufahamu Akwi, nifahamu ilikuaje siku hiyo nijue pia ni katika mazingira gani risasi ikakupata kichwani, maana haukuwa miongoni mwa wanaharakati.

sitafanya uchunguzi wakiintelijensia maana tayari wapo wenye dhamana hiyo ila nitajiuliza tu maswali yangu ya kawaida huku nikingoja majibu ya ripoti kutoka kwa wataalamu wa uchunguzi.

Sina Shaka nao maana ni jaala yao, sasa kama wataficha ukweli laana ya Mungu pekee ndio itakuwa vazi Lao.

Yote ya yote MUNGU akupokee kwa tabasamu Akwi.

Nyuma yako ni vilio vya watanzania, wakililia damu yako, Rais wetu mpendwa ameguswa na kifo chako, waziri mwenye dhamana ya elimu, wanafunzi wenzako na hata vyama viongozi wa Siasa wanakulilia.

Malaika wakufikishie salamu zetu!

Tutaonana baadae Akwilina!!!!!


Note.
BAADHI YA VITU KWENYE ANDIKO HILO HAPO JUU NI VYAKUBUNI TU HAVINA UKWELI WOWOTE!