Na Omar Zongo
Walinzi wote walibaki wakimtumbulia
macho mtaalamu wa kutambua nyayo, Alionekana kujutia mno kulewa jana
yake bila shaka alielewa madhara ya adui aliyepita kuingia duniani.
"Huyu
adui aliyeingia atagharimu maisha ya vizazi vyetu vijavyo. Watakuwa
watukutu, wavivu na watahadaika na mabadiliko ya kasi ya teknolojia kwa
kujidanganya ni maendeleo makubwa, lakini kama atapatikana mwerevu na
kuhesabu faida ya maendeleo hayo na kurudi kwenye hasara bila shaka
atagundua faida ndogo sana dhidi ya hasara. Makosa yetu ya kujisahau
usiku wa jana yatagharimu dunia hii!"
Alizungumza
kwa hisia kali yule mtaalamu wa kutambua nyayo alisema ilikuwa ni
habari iliyoibua majuto makuu kwa walinzi wale lakini wangefanyaje sasa
na adui keshapenya. Hawakuwa na jinsi tena na ndipo hapo na wao pia
walipoanza kupoteza umakini katika kazi yao.
Waliendeleza
tabia zao za kunywa mvinyo wakijiongopea kuwa wanapoteza mawazo.
Maadili ya kazi yao yalishaporwa usiku ule na Jitu Adui.
* * *
Sijui
ni utaalamu gani alianza kuutumia Jitu Adui lakini ghafla tu sababu
zikaanza kwa wasomaji vitabu, "Kazi nyingi sana sipati hata muda wa
kusoma sasa hivi."
Sababu hii ilianza kupenya masikioni mwa Jitu Adui huku ikiibua furaha moyoni mwake kwa kuiona dalili ya ushindi.
Waandishi
makini hawakuchoka kuibua dhima zenye tija kwa jamii, na kutoka na upeo
waliokuwa nao. Tayari tofauti ya kimaadili wakaiona na kupambana kuiasa
jamii katika kusimamia maadili bila kujua kuwa adui wa maadili yupo
macho na aliwapinga vikali waandishi.
Jitu
Adui akaviona vitabu hivi, alivipenda sana sababu aliziona akili za
waandishi na nia zao njema, Alijikuta akitabasamu kwa dharau kabla ya
kupuliza sumu ya uvivu wa kutafakari kwa wasomaji vitabu.
Sumu
ya uvivu wa kutafakari ilipenya katika mifupa ya binadamu na kuenea
miilini mwao, malalamiko ya pili yakapenya masikioni mwa Jitu adui.
"Misamiati
migumu na mafumbo, yaani vitabu vinahitaji upate utulivu ndio
uvielewe!." Cheko la kejeli na dharau likamtoka Jitu Adui, njia yake ya
kukita mizizi duniani ilikuwa nyeupe sasa.
Bado alikuwa makini na waandishi alitaka sana kusikia wana jipya lipi, Sikio lake likapata kusikia kilio hiki.
"
Kazi zetu hazinunuliwi, kipato chetu kinayumba" Furaha ya ajabu
ikamfanya ajipige kifua akijinasibu kuwa yeye ndiye JITU ADUI a.k.a ADUI
WA MAADILI. Wafanye nini waandishi kama sio kufanya tafiti jamii
inavutiwa na nini.
Utafiti ambao
haukuchukua muda ulikamilika ukionesha mabadiliko makubwa kwa jamii.
Walipenda kusoma vitu vyepesi, na dhima za starehe na mapenzi ndio
walihusudu zaidi.
Alijikuta
akijisemea Shaaban Robert nguli wa Kiswahili na mwandishi wa riwaya
mashuhuri ukanda wa Afrika Mashariki. "Mwandishi ni mtu wa desturi kama
walivyo watu wengine, hawezi kuishi kwa kula ukungu na kunywa hewa"
Ujinga
uliwafumba macho binadamu hawakuweza kabisa kufumbua ili wapate nuru ya
ufahamu katika vitabu. Kwa pamoja walijikuta wakipiga vita kununua
vitabu vya kufundisha na wengi walimiminika dukani kununua machombezo ya
mahaba na starehe dhalili ya ngono!
Laiti
kama wangelisikia kicheko cha ushindi akicheka Jitu Adui hapana shaka
wangemsuta kwa kurejea vitabu vya mafundisho, mbali na vile
vilivyotungwa na watunzi binadamu. Kuna vyingine vilikuja na manabii,
navyo vimetelekezwa!
Mbinu yake ya
kwanza Jitu Adui imemrahisishia vingi sana, Kwa kutumia mbinu hiyo tu
ya kucheza na akili za binaadamu alijikuta akifanikiwa kubadilisha
mavazi ya vijana wa kike na kiume.
Tamaduni zao walizihifadhi kwa kiburi kwenye maghala ya kuhifadhia vitu vilivyopitwa na wakati.
Vitabu
vyote vilivyoandikwa na waandishi waliotukuka kimaadili havina mahala
palipokuwa pakiongelea namna mtu alivyo hodari kitandani wakati
akishiriki mambo ya faragha. Au kuongelea faragha kwa watu wasio na
ndoa, hii waliifananisha na laana na adhabu iliyokuwa ikitolewa na
waandishi ni mhusika kutengwa na jamii.
Nani
leo hii asome dhima hizo zenye mashiko? Kila mmoja angependa sana
kuona kitabu chenye jalada linaloonesha umbo kubwa la mwanamke huku
sehemu kubwa ya mwili wake likiwa wazi. Bila kujua ni mafanikio ya Jitu
Adui ambaye ameandaliwa karamu kubwa akirejea huko kwao kusipojulikana.
Jamii
ya Jitu Adui inajivunia kuwa na kijana aina yake na kwao wanamuita
shujaa ambaye amefanya mapinduzi ya kimaadili duniani. Ushindi wake hivi
sasa ni pamoja na magonjwa ya zinaa, majanga ya vita, ubaguzi, udini,
wivu, uchawi na ukatili wa kila namna.
Waandishi
wa kuyanyooshea kidole hayo nao wametekwa na tamaa ya kuuza vitabu
vyenye kupotosha maadili, Inashangaza sana dunia hii ni watu wake pekee
ndio huwa tayari kukulipa pesa nyingi sana ukiwapotosha.
Jitu Adui lile zigo alilobeba kama zawadi kwa wanadamu amefanikiwa kulipunguza kwa asilmia kubwa amegawa zawadi zake ipasavyo.
Ni
nani tena wa kupambana na adui wa maadili, Jitu Adui mwingi wa hila?
Swali hili liliponijia ndotoni nilishtuka nikitamka neno "Mimi..."
Ni
hakika nilikuwa ndotoni, ndoto ambayo ilinifanya niandike dhima
zilizoachwa kuandikwa, na nilipoanza kuandika nilikutana na binadamu
walioathiriwa na Jitu Adui wakilalamikia uandishi wangu, eti nina
mafumbo na naandika vitu virefu sana wao wanachoka kusoma!
Natikisa
kichwa kuwahurumia lakini sikati tamaa sababu bado ningali mapambanoni
kummaliza Jitu Adui arudi kwao akiwa dhaifu na ile karamu
waliyomwandalia igeuke msiba.
“Sitaacha
kuandika ninachoandika sababu nilipenda kusoma aina ya ninachoandika na
nilipokikosa ikanibidi kukiandika ili nipate kusoma nilichokikosa"
MWISHO.