WARAKA WA JPM

 Huu ni waraka wa kufikirika wa Hayati John Pombe Magufuli, Rais awamu ya tano wa Tanzania ambaye alifariki dunia usiku wa tarehe 17 march mwaka 2021...


Muandishi wa waraka huu ni Omar Zongo

Kutokea Eneo ambalo wanaenda waliokufa tumepokea waraka huu.

Waraka wa JPM.

Anasema....

Ndugu zangu watanzania,    ile siku ambayo roho yangu iliusaliti mwili wangu, ilikuwa ndio siku ya kwanza ya mimi na ninyi kutenganishwa katika ulimwengu huu wa Roho na Mwili.

Sikuwa na namna yoyote ya kupinga rungu la malaika mtoa roho, ninachoshukuru ni kwamba udongo umeudhibiti mwili wangu lakini Roho yangu ingali hai hata kupata uwezo wa kuyaona yanayoendelea Duniani, lakini zaidi kuwaandikia waraka huu.

Nimelazimika kuuandika waraka huu kwa sababu nyingi lakini kubwa ni hili tendo linalotarajiwa kujiri hivi karibuni 

Tendo la kuuaga mwaka uliogharimu maisha yangu.

Najua nimesaliti kiapo cha Uongozi, kwa kuwaacha kabla ya muda, lakini ningewezaje kupinga mapenzi yake Mungu.

Katika waraka wangu huu wa leo sitaongelea kwa kukosoa hata kimoja kuhusu uongozi wa Samia Suluhu kwa sababu kila nabii na zama zake hivyo, KAZI NA IENDELEE.

Kama nyani mzee tu nilikwepa mishale mingi enzi niko hai lakini ule mshale ulionitandika ndani ya mwezi wa tatu wa mwaka 2021 sikuweza kabisa kuukwepa.

Ulikuwa ni mshale wa mauti yangu na hata mbinu zote ningetumia kuukabili isingewezekana abadani.

Hiyo inatokana na kweli wa kwamba sikuwa wa kwanza kunyanga'anywa roho na wala sitakuwa wa mwisho.

kesho yako na wewe inakuja!!

Jiandae!

Kuna nukuu zangu nyingi kwenu zimebaki kama ushuhuda wa kuwa nilijua kuna siku nitakuja mahali nilipo kama ambavyo nafahamu kuwa na wewe utakuja, suala la nani atangulie ni siri ya Mungu.

Sikutaka kutenda hovyo katika wakati wangu ndio maana nilijitahidi sana kuacha alama.

Kama katika juhudi zangu hizo kuna mtu alikwazika basi aruhusu moyo wake usamehe maana maisha ya mwanadamu duniani huambatana na mapungufu yake.

Zile Siku chache baada ya kifo cha mzee mkapa zilikuwa ni siku za maandalizi ya kifo changu.

Balozi kijazi alilazimika kunitangulia ikawa simanzi kwangu hata udhaifu wa afya yangu ukawa maradufu.

Mfululizo wa vifo vya watu wazito waliokuwa chini yangu katika taifa langu ulikuwa ni ishara mbaya kwangu lakini sikupata mfasiri akanipa maana ya mambo yale tanzia yaliyojiri kwa kufuatana.

Maalim Seif niko nae huku, Anna Mghwira niko nae huku Jaji Ramadhami niko nae huku na jambo la kufariji ni kwamba naandika waraka huu ukiwa umepata baraka zao wote watu niliowataja.

Watanzania msiache kumtanguliza Mungu katika kila jambo, vikwazo na majaribu ya Dunia havishindwi na maarifa ya mwanadamu peke yake.

Kesheni mkisali kuliombea Taifa lenu, amani iendelee kudumu na raslimali za nchi yenu ziwanufaishe watu wote.

Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere anawasalimia sana huku tulipo tunakesha tukiwaombea mzidi kustawi na kuwa taifa kubwa na lenye nguvu ulimwenguni.

Nitumie nafasi hii kuwatakia heri ya mwaka mpya na kila jema liwafikie ndani ya mwaka 2022.

2021 imeondoka na zigo kubwa ambalo ndani yake ipo roho yangu ila isiwe chanzo cha kuuchukia huo mwaka Mungu apangalo halijawahi kushindwa.

Poleni wafanyabiashara wa kariakoo mlio unguliwa na soko lenu, ujenzi ukikamlika nina imani mtarudi kuchapa kazi.

Kuanguka na kusimama ndio ladha halisi ya maisha ya duniani hivyo miskate tamaa ba hasara iliyojitokeza.

Ndugu zangu machinga kuweni na moyo mkuu na mfuate maagizo ya mamlaka maana mamlaka zote duniani zinawekwa na MUNGU hivyo fuateni utaratibu ili kudumisha mshkamano na amani.

Niwatakie kila la kheri ndugu zangu watanzania msisahau ya kwamba Huu ndio msimu wa kufanya biashara na SIMULIZI ZINAISHI GROUP ni sehemu sahihi ya kubrand biashara yako..

Wasiliana nasi 0788777658

Ili kupata maandishi yetu kwa sauti Usiache kutembelea youtube channel yetu SIMULIZI ZINAISHI kwa kjubofya link hii hapa chini

 https://www.youtube.com/results?search_query=simulizi+zinaishi

Kwaheri 2021

Kwaheri 2021

 Wakati unakuja tulikupokea kwa Matumaini makubwa na imani yetu ni kwamba nuru ya mafanikio itatuangazia kwa wingi ndani ya siku zako.


Matokeo ya tulichoamini na tulichokitumaini ni siri yetu maana ndani yako tumejifunza kuwa kinywa kinachonyamaza kinaiacha na uzima shingo.


Walioshindwa kuficha hasadi zao na kutuonyesha wazi chuki walizo nazo juu yetu ni wengi.


Kinachoshangaza majina yao ni ya watu ambao mwanzo tuliamini ni majirani wema.


Walioacha kutuamini kwa kuhisi ni wazembe na hatujielewi ni wengi pia.


Waliongoja tuanguke ili watucheke hawakukosekana na waliotabasamu kinafki kila tuliponana nao tuliwabaini tukakosa cha kuwafanya.


Walioacha kupokea simu zetu kwa kuhisi tutawapiga vizinga ni wengi kama idadi ya waliokataa kujibu meseji zetu kwa kujua kuwa tuna shida.


Matendo yetu ya wema yaliyopokelewa kama ni shobo na kujionesha ni mengi kama yalivyo malipo ya dhuluma na chuki tulizoambulia.


Mifuko yetu iliposhindwa kununua upendo tukaambulia dharau na kupuuzwa.


Juhudi zetu za kuonesha talanta na tunu tulizojaaliwa zilitafsiriwa kama ujinga usio na tija yeyote.


Waliokataa kutupa pesa za matibabu ili tupone ndio waliohidi kutoa eneo la kuzikia tukifa.


Waliopendekeza majina yetu yakatwe kwenye mahojiano ya kazi ndio waliokuwa wa kwanza kutupa pole tulipotolewa vitu vyetu nje kwa kushindwa kulipa kodi.


Unaenda ukiwa na taarifa za majeraha yetu ya kutendwa na tuliowapenda na kuwaamini zaidi.


Unatuacha tukiwa na kumbukumbu ya zile siku tulizoomba tukanyimwa na kunyenyekea tukapuuzwa.


Mahangaiko yetu ya bure yamekuwa na tafsiri za wivu kwa watu ambao hata hawatujui vizuri na wala hatujawahi kuwakosea.


Uthubutu wa kujaribu kila siku kubadili historia ya tulipotoka umechochea vita hata na watu tusioweza kupigana nao.


Ukubwa wa silaha zao na uzoefu wa maangamizi unatulenga sisi tusio na lengo lolote baya kuwahusu isipokuwa tamaa ya kuhudumia walio nyuma yetu.


Purukushani za kujikomboa na maisha zinatuongezea idadi kubwa ya maadui wanaoamini tunashindana nao wakati kweli haipo jirani hata kidogo na hizo fikra zao.


Kwa kuwa hujaja kuamulia wanyonge na wenye haki unaondoka hali ya mambo kuwahusu ikiwa ni shaghala baghala.


Hata bahati inapoamua kuja kwetu hukumbana na vizuizi vingi vya watu wetu wanaotujua.


Idadu ya watu wanaopimia mafanikio yako ni kubwa kama ilivyo idadi ya watu ambao hawatataka ufanikiwe kuwapita.


Mchezo wa kuvutana mashati ili ubaki nyuma umekuwa na umaarufu mkubwa katika ulimwengu wa giza.


Kila anayethubutu kuwasha taa ili kumulika mchezo huo sio tu anauliwa bali pia anachomwa moto na majivu yake yanafichwa kusikojulikana.


Zaidi ya kutufariji tuendelee kupambana haukuwa na neno jengine, ukaribu wako na sisi umetuachia funzo kubwa sana.


Ajenda zilizokuwa chukizo kuongelewa na wazazi wetu zama za kale zimekuwa ajenda kubwa katika siku zako lakini umejitoa hatiani kwa kusema kuwa MTU WA MWISHO ATAJIZIKA MWENYEWE.


nilipoamua kuzima simu baada ya kukutana na mtu mtandaoni anajiita Juma utam nikawasha redio na kusikiliza wimbo unatusishi tupeleke moto as much as we can.


Niliporudi vitabuni kutathmini labda tupo zama za mwisho nikakutana na wewe ukisema Nyuki hakumbatiwi.


Mafumbo yako sijayapatia jibu mpaka sasa unaondoka.


Uendako salimia kama ukipata nafasi ya kutaja majina yetu huko basi ukifikia kwenye jina langu weka kando mapungufu yangu na uwaambie sishindani na yoyote chini ya jua isipokuwa mimi mwenyewe!!


Kumuona mimi bora wa leo niliye na utofauti mkubwa na wa jana ndio dhamira halisi ya jitihada zangu.


Zaidi ya pesa sina kingine nitakachotafuta mwakani, nyayo zangu zipo tayari kukanyaga chochote cha hovyo ili kuruhusu akili yangu ifikiri sawa sawa namna ya kupata pesa.


Kwaheri 2021, karibu 2022...


WEMA UENDELEE.....

ACHA!! USING'ANG'ANIE MAHUSIANO YALIYOISHA MUDA WAKE.

ACHA!! USING'ANG'ANIE MAHUSIANO YALIYOISHA MUDA WAKE.

 Kuanzisha mahusiano ya mapenzi sio dhambi wala jambo baya katika akili ya yeyote aliye timamu.

Lakini ubaya unakuja jitokeza pale ambapo mnashindwana na kushindwa kuamini kama mmeshindwana hivyo kubaki mnavumiliana, mkikondeshana, kudharauliana, kutukanana, kupigana na wakati mwengine hata kuuana.

Jifunze leo hapa kumuacha aende zake, kuitambua,kuiheshimu na kuitumia vizuri siku.

Siku ya kuachana.

Na.

Omar zongo.

Hakikisha muda wa kuachana ukifika unafanya hima muachane.

Using'ang'anie bidhaa ambayo  imefika tamati Yake ya matumizi.

Hiyo tayari ni sumu kukuua si ajabu!

Muda wa kuachana una dalili na upo dhahiri.

Ukiona tu mambo yamebadilika, upendo umechujuka, taa imezimika, nakusihi ondoka.

Hakuna Tena zile 'baby' na 'sweetheart' unaitwa kwa jina lako, au 'Apple' na 'Chocolate' ujue ndio mwisho wako.

Kitendo cha 'text' kupungua, zile 'I miss you' kupotea na hakuna kujishtukia ujue muda umewadia.

Muda wa kuchokana una nyingi tashtiti kwanza kugombana, pili kuchuniana tatu kudharauliana na mwisho kutukanana.

Isifike kupigana haraka Sana fanya hima, ni Bora ya kuachana kuliko kuumizana.

Ulipomuona mara ya kwanza alikuvutia, ukajiambia yeye ndiye ule ubavu wako uliomegwa akaumbwa, ukatabasamu ulipomtazama, ukamwambia maneno yote mazuri.

Ukatoa maneno matamu katoka kwenye wimbo ulio bora wa Suleiman, ukamsifia kwa sifa zote, ukamridhia kwa moyo wote na ukamuahidi ahadi zote.

 ziko wapi zile siku?, uko wapi wema wako?, yako wapi maneno yako, matendo yako, furaha yako na.... ya mwenzako?

Leo hii kawa mjinga, mpumbavu, havutii, hapendezi na anakera ukimuona!!

Mabadiliko sio mwiko, hutokea na ni kawaida hivyo usiumie unapochokwa au kuchoka.

Ni kosa kulazimisha  hasa muda ukishafika, utajitia mashaka na homa Kali ya simanzi.

Tambua Hakuumbwa peke Yake, muache aende zake, yashike mazuri Yake, sahau ubaya wake.

Haukupoteza muda, umejifunza kuwa nae, Kuna Elimu kubwa kaitumie kwengine.

Mwengine kwa ajili yako yupo mahali katulia, kumng'ang'ania yeye ni kupoteza bahati, kumsubirisha wasahihi 'asisogee karibu yako.

Mahusiano wakati mwengine ni kama vile chakula kizuri ukipendacho, kikiwa pale mezani kinapendezea macho.

Lakini ukisha kula, hugeuka matapishi na baadaye kinyesi kinachoumiza tumbo.

Ukishaenda chooni sakata limeishia, Maisha yanaendelea kwa kuhitaji chakula kingine.

Huu ni muda sahihi, muda wa kuacha, nyuki hakumbatiwi wala miba haitafunwi.

Utambue huu muda.

Muda wa kuachana ni muhimu hasa ukifikia, Ni muhimu kuujua na kuutendea haki.

Kuendelea kumkumbatia mtu aliyekuchoka ni hatari matokeo yake ni vifo na ukatili, mume kamuua mke au mke kumchoma moto mume.

Zamani ulikuwa thamani Sasa wa kazi gani, usijipe jaka rohoni, muepuke shetani.

Nenda anakusubiri, yule mwengine wa kweli, penzi lenye shubiri ni dhambi kulivumili.

Kwani yeye ni nani mpaka usimuache achana na hayawani siku za kuishi ni chache.

Hajabandua kiungo kisafishe ukihifadhi mwenye matumizi nacho akikute kipo safi.

Usivumilie karaha zisizo na marekebisho, Leo kosa kesho kosa,hapa kosa kule kosa, makosa ya makusudi.

Makosa mfululizo Usaliti na Dharau, Kiburi na ushubwada amua kutupa Kule, muache aende zake.

Thamani yako adimu hayuko nayo mwengine usiruhusu dhalimu akaitupa kwengine, Furaha yako muhimu anaijua mwengine, achana nae wazimu moyo wako upone.

Nakusihi umuache usingoje akuache yeye, muoneshe nguvu yako abaki ajute yeye.

Utampata mwengine mkarimu na mwenye upeo, mpole na mnyenyekevu aliyeumbwa kwa ajili yako.

Tena mwenye taaluma, na  hodari wa mapenzi, mwenye moyo wa kuchuma na bingwa wa kuenzi.

Heshimu muda ndugu yangu, usisubiri matokeo mabaya ukaweka historia mbaya, ukayatenda mabaya ya jinai na aibu.

Muache aende kwa amani ya bwana.

Leo nipo hapa kukusihi Usihuzunike bali  usheherekee ukiziona dalili za siku.

Siku ya kuachana...

Kama umevutiwa na Andiko hilo Unaweza kulisikiliza na kulidownload pia kwa njia ya Sauti kwa kuBofya Link hii hapa https://youtu.be/rz6fJhfpirk

Kifo chako kikitokea


Kifo chako kikitokea, kitawashtua wanaokujua Na wengi watakulilia lakini zaidi watakaoumia ni wale walio karibu na wewe!

Pia kwasasa upo hai,Wapo ambao unawakera nakuwaudhi lakini kwa unafki wao siku hiyo watasema kuwa wewe ni mtu mwema sana.

Moja ya fikra zako muda huu upo hai ni labda siku ukifa mzigo wa majukumu yako ataubeba ndugu yako flani, kisa anakuchekea, anawafurahia watoto wako, mke au mume wako.

Labda kisa mnasaidiana sana na ushamtendea mema mengi! Unajifariji huenda yeye atavaa viatu vyako, atawasomesha kwa moyo mmoja, atawaongoza nakuwafariji bila Tatizo.

Sipingi hisia zako inawezekana zipo sahihi, lakini acha nikufikirishe tofauti kidogo!

Tambua kuwa binaadamu tumeumbwa Na unafiki wa asili!

Wengi wao waliokufa walijifariji kama wewe lakini matokeo yake watoto wao wanadhalilika, ni ombaomba Na wengine hawana ndoto tena.

Au wengine walibahatika kulelewa lakini kwa dhiki Na masimango makubwa, makovu ya mateso waliyopitia wanayakumbuka hadi Leo.

Ipo hivyo rafiki yangu, hivyo

Siku ukifa wakati unalilia dhambi Na matendo yako uliyoyafanya usiache kulilia watoto na majukumu yako unayoyaacha.

Lia ukijiuliza ninani atawafariji nakuwatimizia ndoto zao.

Je yupo ambaye utu Na thamani yako ataendelea kuvienzi kwa kuwafariji wanao nakuwafuta machozi daima.

Je yupo ambaye atataja sifa zako kwa wema hata baada ya mwaka mmoja wa kifo chako.

Je yupo ambaye atalipa fadhila kwa kuwatendea wema wanao ambapo Pengine ulikuwa ukifanya wema ili siku moja nao waje watendewe wema.

Naogopa kusema moja kwa moja kwamba siku ukifa itakuaje lakini historia inaonesha wengi walipofariki waliacha mwanya wa familia zao kuonekana takataka Na hata kuwatenga wakati mwengine.

Nachelea kusema.

Wapo watakaojaribu kuzulumu jasho lako ili lisiwafikie uliowachumia.

Wapo ambao hawatajali maumivu ya wale uliokuwa unawajali nakuwapigania furaha zao.

Amini nakwambia siku ukifa ndio mwisho wa kuthaminika kwa ndoto zako.

Ipo siku utakufa!

Ipo hivyo!

Sijui Kati ya mimi au wewe nani atatangulia lakini naomba nikukumbushe kuwaandaa uwapendao kisaikolojia

Waambie kuwa ni muhimu kujitambua, wajue namna gani wanaweza kusimama hata wewe ukiwa haupo.

Waambie siku ukifa wasitegemee tena kupata mazuri uliyoahidi utawapa katika maisha yako.

Waambie wajiandae kupata changamoto mpya Na wakuenzi kwa mapenzi yao nasio kuongozwa Na wengine.

Waoneshe vitu vyakuvishika siku ukifa, kama ni Mali hakikisha wanaijua Na hatatokea mtu akawanyang'anya.

Kama ni tabia waelekeze utu Na uchamungu, waambie wasimlaumu mtu yakishindikana uliyopanga kuyafanya wewe.

Waambie duniani kila mtu ana Mipango yake ni jukumu Lao kuendeleza Mipango yako nasio kwakutegemea mtu awaongoze.

Waambie washukuru nakumuomba MUNGU kila wanapoguswa Na kutokuwepo kwako.

Waambie wasimdai mtu fadhila ulizowafanyia Na kama ikitokea mtu akaamua kuwalipa basi wapokee kwa kumshukuru.

Wape wosia kabla hujafa!

Waambie bamkubwa yupo lakini huenda akawa Na mzigo mkubwa hivyo akashindwa kuwajali nakuwahudumia mahitaji yao.

Kama ikitokea hivyo wasisitize wasimchukie, wampende nakumuombea huku wakipigania kujikomboa wenyewe kwani ipo siku nawao watakuwa mabamkubwa.

Mwambie mke wako, zilipo hazina zako! Muoneshe viwanja vyako mwambie ni Mali zako, umetafuta kwa jasho lako kwa ajili ya watoto wako.

Msisitize aache uhuni, asije akazihonga! Mtafute mwanasheria kuziwekea hati miliki.

La kama huachi kitu, fukara mwenzangu na mimi! Waambie wanaokuhusu mapambano yaendelee.

Tena uwape Ari watafute kwa juhudi, wasitegemee cha mtu watakumbushwa msiba.

Upendo wasipopewa wasilazimishe kwa kuuomba, cha msingi wajitambue upendo wajipe wenyewe.

Tena washirikiane, kamwe wasiachane, kama wapo wawili faraja wagaiane.

Kama yupo mdogo useme Na mama ake, mwambie awe imara apigane peke yake.

Mueleze ukitakacho, ampe mtoto wako! Mpatie baraka zako uende kwa tabasamu.

Mwambie asilaumu ndugu zako wakimuacha, alee watoto wake kwa shida Na raha zote.

Mkiondoka pamoja mkamuacha mtoto, wala hiki si kioja MUNGU atamkuza.

Atayapata mateso au raha kama ipo, ila mwisho atakuwa maisha ndivyo yalivyo.

Siku ukifa shukuru kama umeacha wosia, waambie wasiutupe radhi itawazuru.

KILA HATUA UNAYOIPIGA WAZA UTAKAOWAACHA BAADA YA KIFO CHAKO.

MUDA NI HUU WAAMULIE WAISHI VIPI BAADA YA KIFO CHAKO.

SOTE TUTAKUFA ILA MKUBWA ANATAZAMIWA ZAIDI....

IPO HIVYO..



RUDI KWA MAMA

Na.
Omar Zongo

Wino huu uliomwagika umeandikwa Na yatima asiye Na baba wala mama!

Mwenye machungu ya kumbukumbu kila atazamapo picha za wazazi wake!

Mwenye tamaa yakuzungumza Na mama kumwambia anampenda! Nakushauriana na baba jinsi dunia inavyokwenda.

Leo wino wangu umebeba dhamira yakukumbusha urudi kwa Mama.

Usiseme hakuna sababu yamsingi yakwenda kumsalimia mama!

Ukifanyacho kinakupa riziki, mafanikio na utajiri lakini vitu hivyo ni vichungu siku utakapokuwa huwaoni wazazi wako.

Siku watakapokuwa mbali Na upeo wa macho yako!

Siku nawewe utakapokuwa yatima.

Rudi kwamama!

Nenda kamwambie unampenda sana! Kaseme nae yote yakwako naumsikilize yote yakwake.

Hakikisha anafarijika kwa uwepo wako!

Usitoe hata dakika akahisi upweke! Akahisi umemtenga nakuzipa thamani kazi zako au watu wako wengine ulionao.

Kumbuka wao wanakuona wamuhimu, mwenye nguvu Na wathamani! Kwasababu ya juhudi za wazazi wako.

Walikesha nawewe ulipokuwa unawasumbua ukilia usiku kucha enzi za uchanga wako.

Walihakikisha unanyamaza haraka pindi uliponyanyua kinywa chako kulia kwa nguvu.

Muone MUNGU rafiki yangu naleo urudi kwa Mama!

Mwenzako natamani sana ule muda wakutafuta walau namba ya mama angu niipige nimsalimie.

Lakini kwenye simu yangu haipo!

Nimeifuta!

Ndio, nimeifuta tangu nilipotoka kuweka dongo la mwisho kwenye nyumba yake ya milele.

Rudi nyumbani Leo! Kama haiwezekani panga hata kesho, mama Na baba wanakusubiri!

Nafsi zao zinatafakari mauti!

Wanaona namna umri wao unavyokwenda mbele, hisia zao nikwamba wanakaribia kufa.

Nenda Leo! Utawafariji nakuwaondoa hofu walio nayo,

Watajiona wenye nguvu na wanasababu zakuendelea kuishi.

Mimi mama yangu alivyokuwepo sikuwahi kupata nafasi yakumkumbatia nakumbusu kwa upendo.

Leo hii najuta natamani siku zirudi nyuma, nimkumbatie kisha nimbusu kwenye paji lake la uso Na mwisho nimwambie nampenda sana.

Nasikitika kuwa siwezi tena kufanya hivyo ndio maana Leo nakwambia rudi kwamama.

Ukifika kule utamkuta nababa.

Wape ruhusa wakutume kama watapenda! Waambie wasiogope maana kwao hujawahi kukua.

Cheo chako kazi yako! Pesa zako vyote viache getini, ingia kwenu ukiwa mtoto kabisa.

Waazime sikio lako! Waambie nini shida Na pia wangependa wakuone vipi kwenye maisha yao yote yaliyobaki.

Fanyia kazi mawazo yao!

Hakika watahisi ni wenye kuheshimiwa sana Na wewe.

Wino wangu umeisha!

Naomba niishie hapa kwa kukwambia kuwa NINA SABABU YAKUNENA HAYA KWAKO.

SABABU YENYEWE NI UKIWA NILIO NAO KWAKUKOSA KABISA WATU WAKUWALIPA FADHILA YA KUNIZAA, KUNILEA NA KUNIONGOZA ENZI ZOTE ZA UTOTO.

Mungu awasamehe wazazi wetu waliotangulia mbele ya haki Na awape afya njema walio hai ili tuendelee kuchuma upendo halisi na muongozo thabiti.

"Hofu, wasiwasi Na mashaka niliyonayo, vinanipa sababu niseme kumbe hata Jasiri kuna vitu anaviogopa"

BinZongo...

'Watu'

Kwa tabu sana Mzee alijisogeza juu ya kitanda nakulaza shingo yake kwenye mto.

Uchovu wa maradhi ulimdhoofisha vyakutosha, macho yake yaliashiria kukata tamaa, lakini alijikaza kiume.

Alinitazama Na kisha akasema.

"Ilikuwa ni siku ambayo kila mtu alinisema vibaya nakunizungumzia vibaya, lawama za kila rangi nilipakwa,

Hakuna aliyejuwa niwapi nimeelekea nawewe, ulikuwa bado mchanga kabisa.

Nimimi pekee ndio nilijua dhamira yakutoroka nawewe siku ile,

Kwakweli Siku ile nilikuwa naingojea kwa hamu sana ifike sababu nilidhamiria kuzungumza nawewe.

Nilitoroka nawewe nikaenda mbali kidogo Na nyumba yetu,

Ulikuwa una siku 40 tu tangu uzaliwe, nafikiri ndio maana watu walinishangaa sana kuondoka nawewe, tena bila kuwaaga.

Nilienda nawewe mahala nilipopajua mwenyewe, Ninachoshukuru nikwamba nilichodhamiria kilifanikiwa.

Nilizungumza yote na naamini uliyasikia maana hata kawaida yako yakulia siku ile sikuiona kabisa.

Ulinyamaza tuli kana kwamba ulikuwa mkubwa kumbe ni mtoto wa siku 40 tu.

Leo nitakwambia tena maneno yale niliyokwambia miaka ile ukiwa mchanga, naamini utanisikia Na utanielewa maana kipindi kile ulinisikia tu ila  sina hakika kama ulinielewa."

Alizungumza kwa shida Mzee, alilpofika hapa alijikohoza kisha akanyamaza kwa sekunde kadhaa ndipo akaendelea kuzungumza

'WATU'

"Siku ile nilizungumza nawe kuhusu watu, nilikwambia, Watu ni muhimu sana katika maisha yako lakini usiwaamini,

Watakusifia, watasema wanakupenda, watakuita ndugu, rafiki, mtu mwema na kila jina lenye kukupendeza watakuvika lakini endelea Na msimamo wako ' usiwaamini'.

Watacheka nawewe, watakumegea siri zao, watakukumbatia kwa upendo lakini bado mwanangu, sio kigezo chakuwaamini.

Ishi nao kwa akili kubwa, tahadhari iwe muongozo wako, maana ni kawaida yao kupanga njama za kukusaliti hata bila sababu ya msingi.

Hawa watu waone tu hivyo hivyo, lakini wana kawaida yakupenda kuombwa lakini hawana desturi yakutoa,

Ukiwa nacho hawatafurahia sababu wanapenda kusikia shida zako, lakini ajabu siku ukiwa hauna hawatajitokeza kukusaidia, hiyo ndio kawaida ya watu.

Wameumbwa kwa maajabu sana, ishi nao kwa umakini, maana siku zote wanapigana ili ionekane mitazamo yao ndio Bora kuliko wengine.

Dharau ni asili yao, Tazama wasikudhoofishe.

Naomba sana uwe muangalifu Na hiki kitu kinaitwa chuki, ni kawaida ya watu kuwachukia wenzao, asije akakuaminisha mtu kwamba utachukiwa tu bila sababu,

Hapana!!.

Ukiwachunguza sana wanaokuchukia bila sababu, utakuja kubaini kuna kitu wanakihofia kwako,

Ndio,

 lazima kuna kitu utakuwa umewazidi maana hakuna chuki isiyo Na sababu,

Amini nakwambia.

Pia,

Watu hupenda kusujudiwa, mwanangu nakuonya usije kufanya Jambo hili!!

Wakusujudiwa ni MUNGU pekee.

Muheshimu kila mtu, hii sio dhambi, heshima ni jambo tumesisitiziwa,

 Ila sitisha kutoa heshima yako haraka iwezekanavyo kwa mtu asiyekuheshimu.

Halafu ni kawaida kwa watu kujipenda kuliko wanavyowapenda wengine, ukiliona suala hili kemea kwa jina la MUNGU wako maana yeye hakuagiza hivyo.

Naomba sana wapenda wengine, maana kuna hatari kubwa ya anayejipenda mwenyewe kuja kujizika mwenyewe siku za usoni.

Kitu muhimu zingatia, watu siku zote hawana chuki nawewe bali kile ulicho nacho, nilisema mwanzo Jambo hili hapa narudia tena ulichowazidi ndio tatizo hivyo kikumbatie Na ukifanye kwa Utashi zaidi, ipo siku watakuheshimu nacho.

Fahamu kwamba Watu wana akili Na wamepewa ufahamu, wanatambua maovu Na mema lakini wengi wao ni wafuasi wa maovu, sasa akili kichwani mwako, ukemee au uwe miongoni mwao.

Kitu cha mwisho siku ile nilise...."

Kufika hapa Mzee alisita kisha akakohoa "koh ...koh...."

Huruma ilinivaa, nikaongeza umakini kumtazama, kuna maneno alikuwa anayazungumza.

Kwa tabu sana niliyang'amua, alikuwa ananiagiza nimpe maji.

Haraka sana nikalikamata jagi la maji lililokuwa pembeni mwa kitanda chake.

Nilikamata Na glasi kisha nikaanza kumimina maji kwa haraka.

Sikuwahi!!!

Mzee alikuwa anarusha miguu huku Na kule.

Ishara mbaya,

"Baba ndio anakufa!?"

 Nilijiuliza kwa hamaki, glasi ilinidondoka mikononi nakuanguka chini kwa fujo.

Sikujali.

Umakini wangu woote ulihamia kwa Mzee.

Hakika alikuwa kwenye hatua za kifo.

"Toa shahada....baba toa shahada..... Mzee jikaze utoe shahada"

Nilizungumza kwa msisitizo, nikiamini Mzee akitamka shahada basi safari yake ya kuzimu itakuwa nyepesi.

Nashukuru alinielewa, kwa mbali niliona akijitahidi kunyanyua kidole chake cha shahada nikaanza kumtamkisha maneno ya kumpwekesha MUNGU Na kumtambua Muhammad kama mjumbe wake...

Baba akanyamaza.

Izrael akamkabili,
Kifo kikatamalaki,

Wosia wake kuhusu watu bado ungali nami mpaka hii Leo.

Mama yangu pia aliwahi sema kuhusu watu.

Aliniambia 'WATU NI SAWA NA MZIGO WA KINYESI, UKIUWEZA KWA UZITO BASI UTAKUSHINDA KWA HARUFU....'

Samahani sijawatajia jina langu naitwa Adam.

Kwaheri.

Na.
Omar ZONGo
SIMULIZI ZINAISHI

Tafakari Wengine

Muda mwingi hua unautumia kutafakari mazuri yako huku ukihitaji kusifiwa, hua unatamani kuongelewa wewe tu, unatamani kuonekana  Na wote wanaokuzunguka wasifu nakukuheshimu.

 Ni nadra sana mtu kutoa nafasi yakutafakari wengine, hivi ndivyo tulivyoumbwa, tumeumbwa na umimi.

Unajiona Bora kuliko wengine, wewe ndio unajiona mwenye akili, busara Na ushauri mzuri unaweza kutokea kwako.

Ni ajabu sana tabia hii Na kwa vile ni asili ya kuumbwa kwako sina lawama katika hilo

Ila leo nataka utenge muda kutafakari wengine, kuona vipawa vyao, nafasi yao, akili zao Na tamaa zao.

Ndio,

Anza sasa kumfikiria mtu wako wakaribu, ana umuhimu gani kwako.

Acha kuwaza wewe tu ndio mwenye umuhimu kwake.

Jiulize maswali ya Je ni vipi ingekuwa kama yeye asingekuwepo.

Tuanze Na msaidizi wako wa kazi za ndani.

Yeye anafua nguo zako, anakupikia, anakufanyia usafi wa nyumba n.k.

Acha kiburi chakusema hata kama asingekuwepo ungetafuta mwengine fikiria kuna watu duniani wanatafuta msaada kama huo lakini hawaupati.

Hivi unadhani fedha yako unayomlipa inazidi wema wakukutunzia nyumba yako, vitu vyako Na wakati mwengine hata watoto wako??

Tafakari wengine!

Kila mtu aliyekuzunguka anamchango mkubwa kwenye saikolojia yako.

Hebu pata picha unaamka asubuhi halafu kila unayekutana nae unamsalimia halafu anakujibu hovyo nakukudhalilisha au wengine hawakujibu wanakutema mate.

Unadhani saikolojia yako itakuwa nzuri hali hiyo ikiendelea mpaka unafika kazini kwako?

Wafanyakazi wenzako wote hawakupi ushirikiano hata wasalamu, kila mmoja anakuchunia nakukuona silolote.

Shtuka rafiki!

Kila mmoja unayekutana naye barabarani ana Faida kwako, ukijiheshimu atakuheshimu Na wewe utajisikia vizuri kuheshimiwa.

Leo nataka utafakari umuhimu wa kila aliyekuzunguka hata yule jamaa mtaani ambaye huna mazoea nae, husalimiani nae wala humkubali.

Nayeye ni sehemu ya maisha yako, anza sasa kuwaza umuhimu wake.

Paulo Coelho kwenye kitabu chake cha the alchemist kuna mahali anasema katika maisha yako yakawaida yule unayekutana nae kila siku ujue ni sehemu ya historia ya maisha yako, ni muhimu kumthamini sababu ana mchango mkubwa kwako.

Ni sahihi mtazamo wa bwana Coelho namimi nipigilie msumari hakuna ambaye hana mchango kwako, hata adui.

Wanasema wataalamu wa mambo ili ufanikiwe unahitaji marafiki lakini ili ufanikiwe zaidi unahitaji maadui.

Nakamilisha Na mfano wakubuni ambao naamini utaona Faida za maadui kwenye maisha yako.

Bosi mmoja alikuwa anapata malalamiko kila siku kuhusu mfanyakazi wake, alikuwa anaambiwa hafai, mla rushwa mara ooh hathamini wateja.

Ilifika mahali maneno kuhusu mfanyakazi wake yalimkera akataka kumfukuza kazi ila kabla hajafanya ivo akaenda kuomba ushauri kwa Mzee wake ambaye ndiye aliyemkabidhi ofisi.

Mzee akashtuka sana kusikia maneno anayoambiwa mwanae kuhusu mfanyakazi yule.

Alishtuka sababu yeye alimfahamu vema mfanyakazi yule.

Mara kadhaa wakati wa uongozi wake alishapata barua kutoka kwa wateja wa kampuni wakisifu huduma za mfanyakazi yule.

Wengine walidiriki hadi kumuomba akafanye kazi kwenye kampuni yao, lakini Mzee alikataa.

Mzee kwavile alimuachia mwanae ofisi akamwambia hatampa mbinu yoyote ya uongozi kwasababu anaamini kijana wake atakuwa mbunifu Na atakuwa Na mbinu mpya kwa maendeleo ya kampuni hivyo alivyotakiwa kutoa ushauri akatabasamu tu kisha akamwambia mwanae.

"Ni vema ukasikiliza maneno ya watu sababu lisemwalo lipo lakini vilevile ni vema ukachuja unayoambiwa maana Mti mwema mara zote ndio huandamwa kwa mawe"

Bosi alipoyatafakari maneno ya Mzee wake akayaelewa nakuona kuna haja yakuanza kufatilia utendaji kazi wa yule mfanyakazi kabla yakumfukuza.

Loh alipoanza kumfatili ndipo alipoanza kukutana Na sifa lukuki kuhusu utendaji kazi wa mfanyakazi yule.

Bosi akamuweka karibu zaidi nakumuongezea mshahara.

Maadui waliokuwa wanamchonganisha walisababisha jamaa ijulikane thamani yake.

Mwisho wa mfano huo.

Naomba uruhusu milango yako yote ya fahamu itafakari umuhimu wa yeyote uliye naye karibu kisha mthamini, muheshimu Na umjali.

Tambua yakwamba binaadamu tunategemeana katika kukamilisha tamaa zetu zote.

 Na
Omar ZONGo
SIMULIZI ZINAISHI