BURIANI BI SHAKILA

Hakika kila mmoja anaweza sema lake kuhusu ujumbe huu!

ila mimi sitajibu hayo yote nitajibu kuhusu huyu atakayesema kwanini nimechelewa kuomboleza na hata kutia neno kuhusu kifo chako mpaka siku kadhaa sasa zimepita.

Burian Bi Shakila na hakika wanazidi kuniliza hawa waja kwa swali hili na kabla sijaendelea kukuaga acha nisemezane nao

hivi Ningewazaje kutia neno katika msiba mzito kama huu, msiba uliogonga moyo wangu nakunipa ganzi katika viungo vyote hasa ulimi unaomfanya mtu atamke.

ni mikono hii ndiyo iliyoshindwa kabisa hata kunyanyuka nakuipungia mkono wa kwaheri nafsi ya Nguli huyu wa Muziki wa taarab iliyokuwa inapaa angani taratiibu huku ikisonona kuona Taarab asilia waasisi wake wanaisha katika ulimwengu huu.

ni macho haya yakwangu Bin Zongo ambayo yalishindwa hata kudondosha chozi ilhali moyo ukiwa umetota kwa huzuni ya msiba ule, hakika yalikuwa maajabu mpk jicho kushindwa kulia kwa mshtuko wa habari hii yatanzia.

kama viungo vyangu vilishtushwa na msiba ule ningewezaje kuushawishi mdomo wangu unyanyuke ilihali wenyewe ulijawa na dukuduku la majonzi nakushindwa hata kutoa kilio kwa sauti.

hakika imenichukua muda kiasi kuweza kustahimili pigo la kifo chako na kuweza pia kutamka neno Buriani.

Nakuaga Bi Shakila huku nikishindwa kuamini kabisa kuwa ile sauti yako nzuri yakumtoa nyoka pangoni imeshindwa kushawishi mauti yakuache!

Nikisema Buriani muda huu mawazo ya yale mahojiano yako uliyoyafanya na mwandishi wa habari wa gazeti maarufu nchini Tanzania yananirejea.

ni kupitia mahojiano yale ndio nilijua pia kuwa zamani mama zetu mlikuwa mnaozeshwa mapema sana, sidhani kama alikosea yule aliyeona tamaduni ile haitufai waafrika.

mahojiano yale pia yalinigusa hasa lilipokuja swali la kazi zako nzuri ulizowahi kufanya zimekunufaisha vipi kimaisha.

ulinihuzunisha sana ulipotanabaisha kuwa ulikuwa unapata kiasi kilichokokuwa kinakidhi nauli ya kwenda kwenye kutumbuiza nakurudi nyumbani tu.

Ni mahojiano yale ndio ambayo bado yananifanya niamini wenzetu MAFANIKIO YATABAKI KWAO, maana ni wao ndio ambao huthamini wazazi wao hasa wale waliojaaliwa talanta kubwa yakutangaza nchi zao.

Burian bi shakila, umeondoka huku nyuma umeniachia fundisho lakuzingatia na kupambana kutimiza unachokipanga maana nakumbuka niliwahi kupanga nakutamani kukutafuta ili nikufanyie mahojiano kupendezesha kipindi fulani pale redio mlimani kipindi hicho nilikuwa nami ni mtayarishajj wa kipindi cha muziki uufanyao, lakini ngojangoja imenifanya mkono uondoke duniani bila hata kupeana mkono nami.

burian bi shakila mradi sasa nimeweza sema acha nikuombee kwa mola akupumzishe kwa amani.

Hakika kifo chako maumivu yake kwetu wazalendo na tunaojua thamani ya ulichokuwa unakifanya ni zaidi ya yale maumivu uliyowahi kuyaongelea yatokanayo na kifo cha mahaba.

Burian bi shakila uendapo naomba sana unisalimie Fatma bint Baraka, Siti Bint Saad na wengine lukuki walomezwa na ardhi hii.

Burian Bi shakila Mungu akupumzishe kwa Amani.

uliwahi sema macho yanacheka moyo unalia hakika nakuambia kifo chako kimenipiga ganzi kiasi kwamba hakuna kinachocheka ndani yangu, vyote yaani vyote vinalia.

UNATAKA KUJA DAR?


Natoka zangu mihangaikoni, mwili umechoka akili haifanyi kazi ipasavyo nahitaji kuoga nakupumzika, nawaza ningekuwa na mke nyumbani angalau ingekuwa afadhali nipate tulizo walau lakupokelewa furushi langu zito lenye vifaa muhimu vya ujenzi. kazi yangu mie ni ujenzi wa nyumba. sikusomea kazi hiyo bali nilijifunza tu kwa wataalamu wa fani hiyo, nakutokana na utundu wangu nikawa fundi mzuri wa nyumba. ingawa ilikuwa yaniuma sana ninapobaini kila nyumba nzuri inayosifiwa jijini dar es salaam ni kazi ya mkono wangu ilhali mwenyewe bado naishi nyumba yakupanga.

 niliwahi jaribu kununua kiwanja maeneo ya chanika nijenge lakini sunami la dhulma na dhoruba kali ya utapeli ikanirudisha nyuma sana.

mpaka leo mimi ni mdau wakupanga huku tabata matumbi,

maombi yangu siku zote ni mvua isinyeshe maana adha ya maeneo haya aijuae ni MUNGU.
unataka kuja??

hatua zangu za kichovu hatimaye zikagota katika mlango wa chumba changu..

naufungua naingia ndani, chumba chanizomea maana tangu nilivyokurupuka alfajiri ndio narudi mishale ile ya saa sita usiku, huku taswira ya chumba changu ikinieleza kuwa haina matunzo na mpangilio unaoridhisha, chandarua hakijakunjwa, kitanda hakijatandikwa yaani ndani kulikuwa ni shaghalabaghala.

kwa mara nyengine tena wazo la kuoa lanirudi kichwani mwangu, namkumbuka Mwanaidi mpenzi wangu niliyeachana nae Tanga muheza miaka mitatu sasa.

mchana alikuwa akinipigia simu sana lakini kutokana na kubeba zege nakulisambaza hata simu niliiona adui sikuwa na muda wakuongea nae, na sio yeye tu ni wengi walikuwa wakifanya juhudi kunitafuta majira ya mchana waliambulia kutokupokelewa simu.

 maisha haya,! kweli wanaume tuliambiwa tutatafuta kwa jasho!.

muda ule sasa licha ya kwamba ni usiku sikuwa na jinsi ilinipasa kuwajulia hali watu wenye umuhimu kwangu akiwemo mwanaidi mchumba angu.

nakaa kitandani kizembe nikiubwaga mzigo wangu sakafuni, navua shati na suruali bahati nzuri nilishaoga kazini hivyo kilichobaki nikumtafuta mwanaidi nakumpoza hasira zake zakutompokelea simu kutwa nzima.

nachukua simu yangu ya bei rahisi, mwenzenu situmii simu za kisasa muda wakuwasiliana huko facebook na watsap sina.

nashukuru na nafurahi kupiga nakupokea tu na mara chache sana kutuma ujumbe mfupi.

simu sasa ilikuwa sikioni na nilisikia ikiita huku nikiomba mungu mwanaidi awe hajalala.

nakumbuka niliuona ujumbe wake mfupi alioniandikia asubuhi eti aliniambia anahitaji kuja Dar es salaam.

ni mara ya tatu sasa mwanaidi alikuwa akirudia kuniambia suala hili...anataka kuja dar.

sekunde chache ya simu ya mwanaidi kuita hatimaye sauti nzuri yenye uchovu wa usingizi ikapokea, dah mwanaidi mwenyewe alikuwa kalala wakati mie ndio narudi...maisha haya!

niliwaza hayo huku pia sauti ya mwanaidi ikinituliza kabisa uchovu nakunisahaulisha adha za kutwa nzima.

nilianza kuzungumza kwa furaha kiasi

haloo....habari mpenzi wangu, pole kwa upweke wa kutwa nzima ni matumaini yangu ulishanisamehe kabla ya muda huu, kwa kutokupokea simu yako ni dhahiri wajua sifanyi kusudi bali ni kutingwa tu na majukumu mazito yakupambania tonge,

asante kwa kunikumbuka laazizi wangu, meseji yako nimeipokea na imenifariji ikinipa sababu zakuendelea kupambana ili nikutunze ua langu.

nimeona pia umesema kuwa unataka kuja dar es salaam eti mchumba ni kweli unataka kuja dar?

mwanaidi: Ndio me nataka kuja dar, nataka kukufata tuishi wote, nahisi wanisaliti ulipo...nimechoshwa na huu umbali...

alinijibu hivi Mwanaidi kwa sauti iliyo na lafudhi ya kipwani.

nilipoteza sekunde kadhaa nikitafakari ombi lake, na nikajikuta namjibu

ni wewe ndio uwaridi wangu, tulizo la moyo wangu, ni wewe mwanaidi pekee ndio ambaye unastahili kuitwa mama na watoto wangu, ni wewe mchumba ndio ambaye mawazo yangu yametawaliwa nawe.

nitawezaje kukataa utakalo, lakini naomba mpenzi wangu kabla hujaja dar nisikilize basi kwanza.

unajua maisha ya dar yanaongopa sana hasa kwa mtu anayeyafikiria akiwa mbali, ukiitaja dar bila shaka kichwani mwako unayaona maghorofa, wasichana waliojipamba na magari yaliofuatana barabarani yakishindana uzuri.

kwa kuifikiria dar utaiona pesa ikipatikana kwa urahisi kazi zipo tu bila shida tena nyingi zakumwaga, na kila kitu kizuri unakipata.

hiyo ndio dar ya kuifikiria mwanaidi wangu, dar ambayo hata mimi kabla yakutoroka nyumbani muheza na gari la machungwa nilikuwa nafikiria nikifika dar nitafanikiwa kwa urahisi.

ukweli sio huo laazizi wangu, dar ni chungu ni ngumu na ina kila aina ya sababu za mtu kuendelea kuishi mkoani asikimbilie kuja dar.

dar haitamaniki, pengine unajiuliza kama dar ni hivyo kwanini bado mie ningali huku? ni swali zuri Mwanaidi wangu!

mie naona aibu kurudi huko sababu nilipotoroka nakuunga magari kufika huku niliapa kutokujutia kosa hili kwa kupambana tu sababu maji niyaogayo nilishayavulia nguo.

nikirudi Mbwana atanicheka, Sudi atanicheka na hata mashoga zako watakucheka sababu kwasasa wanakuonea wivu kuwa mchumba ako niko dar na niliahidi kuja kukuchukua.

ugumu wa maisha sio tatizo tutapambana lakini hii dar ina ushawishi sana, na uzuri wako ukija nikishindwa kukupa wanachopewa wengine utahadaika na mabosi wa huku ambao wao pesa zao zipo tu kwa ajili ya kulaghai wachumba wa watu.

naujua uzuri wako na haiba yako ukija dar nina mashaka sana na uhai wa penzi letu.

mwenzio huku dar wakati mwengine nalala na njaa natembea kwa miguu na ni uhakika ili kutaka kunionesha kuwa una mapenzi ya dhati namimi utataka kuja ili tuishi wote kwa shida na raha.

ni wengi waliambizana hivyo lakini tamati yake haikuwa hivyo, huku dar mioyo yenye majeraha yakuumizwa na mapenzi ipo mingi sana barabarani.

mpaka dakika hii naongea nawe yupo mmoja analia kwa kutendwa.

hii ndio dar unayotaka kuja. gharama za maisha zipo juu sana lakini sitaki uendelee kujisikia vibaya nipe wiki hii ninunue sukari niweke ndani, unga niweke ndani.

mchele nitaweka ndani na hata mafuta ili ukija tuwe na mwanzo mzuri.

jiandae mpendwa mwishoni mwa juma hili nitaminyana nikutumie nauli mana nikisema kesho nitaongopa kwakweli.

nimefurahi kuongea nawe usiku huu, sauti yako ni tiba ya kazi ngumu niliyoifanya leo hii. naomba nikuache ulale
pumzika waridi langu malaika wema wakulinde na shari za usiku huu.

jiandae nitapambana uje dar!

JIANDAE KISAIKOLOJIA

Nina uhakika wenzio yalivyowakuta walihangaika sana nakuteseka sababu hawakujiandaa kisaikolojia.

nakuasa mapema sana ujiandae kisaikolojia ndugu yangu maana dunia hii huzunguka kwa usiri katika muhimili wake.

mzunguko wake mmoja ni mengi yanajiri na katika hayo mengi naamini kuna moja ambalo linakupasa ujiandae nalo kisaikolojia.

we jiandae tu usichoke kufanya hivyo maana muda sio mrefu nimetoka kumbembeleza rafiki yangu aliyeumizwa vibaya na mpenzi wake.

anasema "alikuwa akinipenda sana, alinijali mno, hakuwa tayari hata siku moja kuona nasononeka, nateseka wala kuhangaika. mara zote aliniambia hataki kuliona chozi langu, nilimuamini na sikuwahi kudhani kama angenifanyia haya"

huyu ni mfano wa mamilioni ya watu duniani ambaye anaumia nakulia sababu hakujiandaa kabisa kisaikolojia yeye aliamini mapenzi aliyopewa hayatakuja kubadilika.

nina uhakika angejiandaa mapema kwa kujua kuwa mapenzi ni kama majira ya mwaka hii leo asingelia maana tahadhali tayari angekuwa ameichukua mapema tu.

jiandae kisaikolojia lolote linaweza kutokea kwa huyo umpendae, usijisahau maana mjuzi wa mapenzi hakuwahi kuzaliwa katika dunia hii unachojivunia anakupenda nacho ni mapito tu ipo siku atakudharau nacho.

Jiandae kisaikolojia!

unae mama hii leo unacheka nae! unampenda anakupenda na kila siku unavuna busara na muongozo wake hivi umeshajiuliza kuna siku unaweza ukawa haupo nae??

najua kufika hapo umeshtuka kidogo na hata ukatamani kuacha kuendelea kusoma, najua kuwa huo ni ukweli ambao wengi hatupendi kuuota, kuusikia na hata kuufikiria, ni ukweli unaoumiza.

lakini mpaka lini tutakataa ukweli huu!? chamsingi nikujiandaa tu kisaikolojia, nautafanya jambo la msingi sana kama ukigundua kuwa duniani hapa mkubwa anaenda na mdogo anaenda hivyo mpende na mama kwa kumwambia naye ajiandae kisaikolojia ikitokea umemuacha wewe.

Jiandae kila siku iitwayo leo maana kuna nafasi ya kesho ambayo wewe hujaijua itakufikia kwa mtindo gani.

tafakari wakimbizi wanaokimbia nchi zao, watoto wadogo kinamama na wazee, tafakari adha wanazokumbana nazo porini yote ni sababu ya mapigano na vita katika nchi zao.

wewe kama una amani jiandae kisaikolojia maana wao hawapendi na wala hawajawahi kutamani hiyo adha.

jiandae tu kisaikolojia maana wamezaliwa wengi sana wenye uchu wa madaraka wanaopenda uongozi bila kujali matokeo hasi ya tamaa zao, na namna ambavyo watu wao wanaumia.

jiandae kisaikolojia hata kwa kusema tu MUNGU TUBARIKI WAAFRIKA MUNGU TUBARIKI WATANZANIA!

Jiandae kisaikolojia rafiki yangu tajiri kumbuka wapo matajiri ambao hii leo wanasugua gaga kitaa ni mtihani kwao hata kubadili nguo zakuvaa, wewe ni nani mpaka uamini kuwa utadumu milele na huo utajiri wako? we jiandae tu maana huijui saa wala dakika iweke poa tu saikolojia yako.

janga lakufilisika likikukumba naamini ukiwa tayari umejiandaa ni rahisi kujiweka imara zaidi na usiadhirike sana.

Jiandae tu ndugu yangu mzima huwezi jua ni lini utaumwa, lini utaumbwa kwa namna nyengine na lini utapatwa na janga lolote likafanya uitwe mlemavu, mgonjwa mahututi, marehemu nk.

we jiandae tu kisaikolojia, piga goti mshukuru MUNGU ulivyo leo na mpe nafasi akuongoze kwa jinsi utakavyokuwa kesho.

Jiandae tu
ndio kujiandaa kwenyewe huko, we jiandae iwekee utayari akili yako itambue kuwa maisha haya barabara yake imeumbwa kwa kona, milima, mabonde na kila aina ya tofauti kwa mpita njia.

wewe mwenye chuki jiandae kupokea taarifa nzuri za unaemchukia, maana chuki yako haina uwezo wakupindua alichopangiwa mwenzio na Mola wake.

wewe MZEE MPUMBAVU unaeruka viwanja na watoto wa wenzio unaechezea miili yao kama mwanamuziki afanyavyo kwenye gitaa lake jiandae ipo siku binti yako nae atafanyiwa hivyo na yule kijana uliyemvurugia penzi lake nakumtekea mpenzi wake kisa pesa zako.

enzi hizo kijana huyo atakuwa fataki kama ulivyo wewe nae anatumia pesa kama fimbo kuwachapia mabinti zako wapenda pesa ambazo baba yao ulizichezea kwa kuhonga.

jiandae kisaikolojia mzee usiendelee kuwa MZEE MPUMBAVU.

Jiandae kisaikolojia wewe unaechukia post zenye ukweli kama huu, ambaye hutaki kukubali eti kisa muandishi havutiwi nawe! au sababu tu una chuki zako binafsi jiandae kisaikolojia maana ipo siku SIMULIZI hizi zitamfundishia mwanao.

"Kama nilivyokuaminisha kuwa SIMULIZI ZINAISHI ipo siku nitakuaminisha kuwa SIMULIZI ZINAKUFA"

 Bin Zongo

AHSANTE MWANA KUJA


Nakushukuru Karima, umpendevu ajabu
Unanifanya nahema, kunipa nyingi thawabu
Ninaipata salama, sia yakutu bawabu
 Ahsante mwanakuja, salamu nimezipata

Ikarima ya Imamu, shauku  tunu amini
Ulinipatia salamu, kwa mikonoko kichwani
Ukaniita binamu, na majina ya utani
 Ahsante mwanakuja, salamu nimezipata

Umenialika kwako, nakuja nafamilia
Nabeba yangu  mifuko, na vibwende navalia
Usije pata shituko, mi sina cha kulalia
 Ahsante mwanakuja, salamu nimezipata

Una nyumba kubwa sana, tarifa nimepata
Yenye viwanja vipana, na kwa kufugia bata
Nina kuweka bayana, usipike vya mafuta
 Ahsante mwanakuja, salamu nimezipata

situmii vya dukani vinanitoa malenge
Sijapona na  madonda, nilopata mwaka jana
Hapa nipo nimekonda, mzee kama kijana
Pika ninavyo vipenda, vya enzi zetu za jana
 Ahsante mwanakuja, salamu nimezipata

Situmii vya dukani, vinanitoa malenge
Andaa na vya zamani, kama vya kwa mama bonge
Ule mkeka wa utani, ulosukwa kwa mkonge
 Ahsante mwanakuja, salamu nimezipata

Unitandikie chini, nikila na kulalia
Na kiti cha makondeni, sebuleni ntakalia
Zile nyimbo za zamani, nitafurahi kusikia
 Ahsante mwanakuja, salamu nimezipata

Nimesikia tetesi, kwa chombo ki onaona
Wabomoa mkakasi, alojengea Sabuna
Yeye ni fundi wa nyasi, aliyejifunza kushona
 Ahsante mwanakuja, salamu nimezipata


Hakika juhudi nzuri, wembamba wakupongeza
Nina yaona dhahiri, na wala sitakubeza
Nakutambua Amiri, usiyejua teleza
 Ahsante mwanakuja, salamu nimezipata

Mimi sipendi kasuku, nasikia unafuga
Uwafukuze na huku, wanaiba zetu soga
Uzifute na shabuku, usije nipe mizoga
 Ahsante mwanakuja, salamu nimezipata



Na, Fulgence Makayula

Waandishi Wanaandika


sijui hata wanakuwa wapo wapi muda huo wakiandika!

wanaandika kwa utashi na weledi wa hali ya juu, huandika kila aina ya jumbe tena kwa mpangilia kuntu unaoeleweka na usio msumbua msomaji..

Mwanzo wa maandishi yao hupamba kwa maneno yenye mvuto yanayompa kila sababu msomaji aendelee kusoma.

kwa hakika watu wanaandika!

navutiwa kusoma maandishi yao na hua natenga muda wangu kuyasoma maana hunipa maarifa maandishi yao!

kila niendeleapo kusoma nagundua kuwa utashi wa watu kuandika kuhusu KUTOKUKATA TAMAA YA MAISHA unaongezeka.

kila mmoja huvaa uhusika wa mueleweshaji wa wengine kuhusu kutokukata tamaa na magumu tuyapitiayo!

nafarijika sana kuona aina hii ya maandishi sababu saikolojia za wasomaji zinazidi kuamini kuwa kukata tamaa ni sumu ya mafanikio, nami nisisitize TUSIKATE TAMAA!.

Maandishi haya zaidi nayaona kwenye mitandao ya kijamii na watu wanashare kwa nguvu kuonesha nia yakusaidia wengine wasome.

Maandishi mengine ni kuhusu MAHUSIANO utakuta maandishi mareefu yameandikwa yakishiba hoja za namna gani uwe mama au baba bora kwa familia yako.

Siku hizi haina nguvu tena elimu ya unyago watu wanafundishana mitandaoni kupitia maandishi huku wakishare kwa kasi isiyoelezeka.

wakati mwengine muandishi husisitiza kabisa mwisho kwa maneno haya SHARE NA WENGINE WAPATE KUJUA.

inapendeza sana, maana ni heri jumbe hizi zina faida chanya kuliko zile zenye kuigusa hasira ya sheria ya mtandaoni.

watu wanaandika bwana! muda mwengine mtu hutumia hata njia ya kueleza kisa ama chakubuni au chakweli na mwisho huelezea fundisho lake alilokusudia.
Waandishi Wanaandika

kwa tafiti yangu ndogo ambayo sio rasmi nimegundua aina hii ya uandishi hupendwa sana na watu.

Hongera sana kwa waadishi! hongera kwenu sababu licha ya juhudi zenu hizo zakuandika ujira wenu siku zote umekuwa ni watu kushare, kulike na Kucoment mimi naamini Mnastahili ujira zaidi ya huo lakini simaanishi muache endeleeni sababu SIMULIZI ZINAISHI hata ikitokea ninyi mmekufa kizazi kijacho watanufaika na jumbe zenu na hata kwa MUNGU mtalipwa kwa utashi wenu wakuiasa jamii.

Hofu yangu ni moja tu, haya maandishi yenu huwa yanaishia wapi?

mnawapa moyo vijana wasikate tamaa kwa mifano hai lakini wao ndio wamekuwa wakwanza kukata tamaa nakudondoka kwenye dimbwi la dawa haramu za kulevya, wakiamini eti ndio faraja ya maisha magumu!

kama hiyo haitoshi ona na hili, mabinti wa sasa huaelezwa namna yakuheshimu waume zao kupitia maandishi kadhalika na vijana wakiume pia lakini ni kizazi hikihiki ndicho ambacho huathiriwa na jinamizi linalovunja ndoa nyingi duniani.

huwa najiuliza yale yanayoandikwa yanaishia wapi? au ni fahari tu kushare nakupongeza waandishi kuwa wameandika vizuri huku ujumbe ukiingia sikio la kulia nakutokea kushoto kabla halijasombwa na upepo wa kus kuelekea kas....

eti waungwana waandishi maandishi yao yanaelelekea wapi nijibuni tafadhali!?

ona, kuwalipa hamuwalipi mifuko yao imetoboka lakini hata kazi zao pia mnazipuuza hamzifanyii kazi....!

ona masikini ya Mungu yalosemwa vitabuni na manabii yana jidhihiri kwa maringo katika dunia hii...

ni wao ndio waliwahi sema kizazi hiki kitaangamia kwa kukosa maarifa, ndugu zangu,
maarifa yapo vitabuni kupitia maandishi yaloandikwa kwa utashi na waandishi ambao siachi kuwaombea heri duniani na mbinguni.

KUMBUKUMBU YA PENZI


Nilikuita jina gani, kwanza nilipo kuona
Nilianza kwa utani, au nilijua jina
Hivi ilikuwa sokoni, au kwa kina Safina
Moyo wangu umetuwa, kumbukumbu we rejea

Nilianzaje kusema, kwa binti wewe mrembo
Ni kweli sijatetema, kwa mvuto wako wa umbo
Ni vipi je nilihema, kwa tenzi zangu za fumbo
Moyo wangu umetuwa, kumbukumbu we rejea

Jicho lipi shahadia, jasiri kwa babu babu
Nilijawa na hisia, kisio lenye sababu
Nilianza simulia,  ni kipi kilinisibu
Moyo wangu umetuwa, kumbukumbu we rejea

Au nilikusifia, pasipo kunjo aibu
Hivi nilikurukia, tena pasipo adabu
Wewe uliye malkia, mrembo usiye gubu
Moyo wangu umetuwa, kumbukumbu we rejea

Sikumbuki ilikuwa lini, na jibu gani ulinipa
Ila nipo furahani, nisiye penda kwa pupa
Nimekuweka moyoni, nihifadhi kwenye chupa
Moyo wangu umetuwa, kumbukumbu we rejea


Penzi hili si kasiri, Kaharu kalipangia
Tena halina tafsiri, kwa jina kulipatia
Tuijenge tafakuri, magumu tukipitia
Moyo wangu umetuwa, kumbukumbu we rejea

Tusije kujihasiri, tupatapo  maanguko
Tujivike ujasiri, kuepuka masumbuko
Habibi tusikariri, kila chozi  bubujiko
Moyo wangu umetuwa, kumbukumbu we rejea


Na, Fulgence Makayula

ZIMETOSHA SIFA ZENU



Nimesema Sitaki Misifa
Ndio sizitaki sifa zenu na kwa kauli nyengine ningesema Sitaki tena kusifiwa,

kama ninyi ni mahodari wakusifia mpeni sifa jogoo ambaye ana juhudi kubwa yakuwaamsha alfajiri ili mkatafute riziki.

mimi sitaki kabisaa sababu MUNGU wangu alinipa upeo na busara yakutambua jema na baya.

kuhusu sifa mnazotoa sioni wema hapo nauona ubaya, naomba msinisifie tafadhali.

kama mna nia nzuri na mnataka mema kwangu fanyeni maombi ili bendera ya SIMULIZI ZINAISHI iendelee kupepea vema.

mkifanyacho sasa mnarusha mawe yalio na mfano wa mkate yanatua sawia kichwani mwangu maumivu na kuvimba kichwa hiki yatasababisha nisiwe msanifu na mwenye kujiongeza tena.

kwani ni wangapi walioanza vema wakasifiwa kwa nderemo na vifijo na matokeo yake wakapotea mithili ya jua majira ya jioni.

Sitaki tena sifa zenu! naamini kuwa sifa hizo ndizo zitakazonifanya nifanane na wengine waliowika Tanzania hii.

wale ambao waliweza kusahau utamu wa lugha yetu wakaweza kuhadaika na kuandika simulizi pendwa wakawa mabingwa wa kusisimua bila kufikiri walio nyuma yao wanafaidika na nini.

hakika ni hizi sifa ndizo zinazomaliza kabisa ufanisi wa kijana wa kitanzania na akachoka mapema kufikiria jukumu lakuipa hadhi nchi yake kupitia alichojaaliwa.

nasema tena safari hii bila kunong'ona SIZITAKI SIFA ZENU. nisubirini nife mnisifie malaika wangu wataniambia kaburini.

hivi mnawezaje kuusifia mti huu mchanga usionufaika na matunda yake!? hivi kwanini mnajipatia dhambi za bure?

kwanini mnashindwa kubaini kuwa SIMULIZI ZINAISHI ni kioo cha kesho ambacho mnapaswa kukiombea dua leo na kutafuta njia ya kusaidia simulizi hizi zifike mbali na sio kuzitemea sumu ya sifa.

kwanza me mwenzenu ni mshamba kutoka TANGA misifa sijazoea, na wasichana baadhi wa leo huona fahari kubwa kuwa na bwana mwenye kusifiwa, hujirahisisha kwake wakidhani ndio njia ya wao kufaidika na pepo ya dunia hii.

akili zao fupi na sijui kwanini hawaoni mfano wa kina mama mashuhuri Tanzania hii, ambao sauti zao walipozitoa ziliweza kutetemesha hata masikio  ya wanaume, na hata siku moja hawajahadaika na maisha ya ganda la ndizi kutegemea mteremko.

sizitaki sifa zenu kuwaepuka watu hawa mabinti waso haya,  watanichafulia sifa na heshima niliyofunzwa, watanifanya nami nianguke kwenye tope la ujinga wa kutafuta njia yakusikika redioni hata nisipokuwa na sababu ya msingi ya kusikika huko, wakileo wanaita kutafuta kiki.

Sitaki sifa hizo sababu mama yangu marehemu nafsi yake inaishi ndani yangu na kila siku ananiambia kuwa bado sana sijatimiza hata robo ya ninachokiota hivyo nisidhani ni lelemama.

baba yangu marehemu nae hunisisitiza sana kuhusu kupigania heshima ya jina lake, asije akazungumziwa Zongo kijana mwenye maringo, mchepukaji na mwenye kudharau wengine.

na sio siri yote haya hutokea kutokana na sifa za wanadamu wanazozitoa wengine wakidhani ni vizuri au wananipa moyo kumbe wananiua kisaikolojia.

kimbilio langu ni MUNGU na namaliza kwa kusema nae,

yaarab nijaalie upeo wakuona zaidi kama nilivyoona sifa kuwa ni sumu immalizayo mtu, nipe staha na kiu yakuhitaji kufika unaponielekeza wewe na sio shetani, nipe upendo na uzalendo wa kipaji changu na nchi yangu.
niondoe mimi na wengine katika upofu wa kutoona baya katika zuri. nakabidhi uhai wa milele wa simulizi katika mikono yako salama.

nami najificha katika ubavu wako nikiepuka hadaa za ibilisi na wabaya wenye kufitini na kufalakanisha.

nasema ahsante Mungu baada yakujiridhisha kuwa sasa nipo salama na nimeepuka mshale wa misifa isiyo na tija.

amin....

MIMI NI NANI?

Mimi Ni nani
"hii simu nani kaiwasha!?" maneno haya yalijisema yenyewe ndani yangu huku uchovu wa usingizi unaomalizikia ukiwa umenizingira kote maungoni mwangu.

ilikuwa ni asubuhi, dirisha lilipenyeza miale ya jua la asubuhi, jua ambalo liliwika kama jogoo likiwataka watu waamke kuutafuta mkate wa kila siku.

ilikuwa ni jumaapili tarehe sikumbuki wala mwezi pia kwa hili nakiri kuwa kweli mimi ni kilaza!

sauti iliyojisemeza ndani yangu ikiilalamikia simu ilitokana na mlio wa simu hiyo kunitoa katika ladha taaamu ya usingizi wa mwisho wa wiki.

huku nikijigalagaza kivivu kwenye uwanja wa fundi seremala nikaurusha mkono wakulia ambao uliifikia simu ile lkn bado swali lilikuwa ninani ameiwasha maana sikuwa na kawaida yakulala nikiwa nimewasha simu.

lakini sikuendelea kuumiza kichwa kuwazia hilo sababu pia sikua na uhakika kama jana yake nilikumbuka kuizima.

kono langu la kulia lililofura uvivu tayari liliikamata ile simu kibabe na kuisogeza usawa wa uso wangu sasa nilikuwa nalazimisha macho yatazame kwenye kioo kujua nani ananipigia simu.

sikuweza kung'amua kabisa namba iliyokuwa ikinipigia ni yanani sababu ilikuwa ngeni kwenye simu yangu.

sekunde chache zakujishauri kama nipokee au la zilinipa jibu la nipokee na bahati nzuri dole gomba linatambua kazi yake tayari lilishabofya kitufe chakupokelea.

ilikuwa ni sauti ya kike.

MPIGAJI; Hallow

MIMI; Hallow

MPIGAJI; Naitwa Mzalendo kutoka Tanzania, mimi ni mfuatiliaji mzuri wa simulizi zako katika blog ya ommyzongo.blogspot.com bila shaka naongea na mwandishi mwenyewe wa blog ile Bin Zongo?

MIMI; Rabbeka bibie hujakosea

MZALENDO; waoh! najifaghiri sana kuzungumza nawe..

MIMI; Karibu sana!

MZALENDO; naomba kujua kitu kutoka kwako.

MIMI; ikiwa MUNGU hakatai maombi yetu wanadamu mimi ni nani hasa mpaka nikatae ombi lako...karibu!

MZALENDO; Wapo wanaosema kuwa wewe ni mtangazaji na muandishi wa habari huku wengine wakisema unafaa zaidi kuwa mtunzi wa hadith na wengine wakitanabaisha kuwa unafaa kujikita kwenye filamu.....nataka kujua kwa kukusikia wewe mwenyewe.....wewe ni nani hasa?

MIMI; (kimya nikitafakari chakujibu, na nikijiweka vizuri kitandani)

MZALENDO; Hallow ( akihakikisha kama nipo hewani)

MIMI; Hallow nakupata uzuri kabisa ndugu yangu mzalendo. umesema watu wanasema hivyo wewe nae kwa upande wako unasema mimi ni nani?

MZALENDO; nani mimi..? (huku akionekana kutotegemea swali hilo)

MIMI; Ndio nazungumza nawe.....

MZALENDO; Mimi naona wewe ndiye mrithi wakina Willy Gamba...Amri Bawj...Yusuph Ulenge na Baba etu wa kiswahili Shaaban Robert.

MIMI: Basi nenda kwenye mitandao yote ya kijamii, vyombo vya habari ufikishe taarifa kuwa SIMULIZI ZINAISHI, lugha ya kiswahili inaongelewa na watu wengi zaidi duniani, mapenzi ya waafrika kusoma sasa yameongezeka na wasijiongopee kuficha pesa vitabuni tutaziona. sambaza ujumbe kuwa Willium ShakesPare mfano wale umezaliwa ukanda wa afrika mashariki na Simulizi Zitaendelea Kuishi daima, waambie....(Simu inakata)

Mimi ni Nani
naitoa sikioni simu naitazama maneno ya mwisho yananiaga yakisomeka BATTERY LOW sasa nakumbuka kuwa jana nilijilaza kizembe huku nikijiambiza kuwa simu itazima yenyewe sababu haikuwa na chaji na umeme ulikuwa umekata.

natazama kiwashia umeme ukutani bado kimewashwa ni dhahiri umeme haujarudi.. saa ukutani inaonesha sura ya marehemu mama angu ikinikumbusha namna ilivyokuwa ikitembea kwenye ukuta wa chumba chake kabla yakukumbwa na mauti nami kujirithisha saa ile, Sindano ya moto inapenya kifuani ikiniletea maumivu lkn ghafla mawazo hayo yanapotezwa na mishale ile ya saa, niliduwaa kuona imesimama ikiniambia batery zake zimeisha. kwahivyo nilishindwa kung'amua ni saa ngapi

kitu pekee nilichoona ni sahihi ni kuendelea tu kulala maana siku za mwisho wa wiki kama zile nakuwa tu nyumbani sina ratiba ngumu ya siku za wiki yakudamka saa tisa kila siku kusaka shilingi.

Nililala tena huku nilijifariji kuwa nimemuelewesha MZALENDO kuwa mimi ni nani..