'Watu'

Kwa tabu sana Mzee alijisogeza juu ya kitanda nakulaza shingo yake kwenye mto.

Uchovu wa maradhi ulimdhoofisha vyakutosha, macho yake yaliashiria kukata tamaa, lakini alijikaza kiume.

Alinitazama Na kisha akasema.

"Ilikuwa ni siku ambayo kila mtu alinisema vibaya nakunizungumzia vibaya, lawama za kila rangi nilipakwa,

Hakuna aliyejuwa niwapi nimeelekea nawewe, ulikuwa bado mchanga kabisa.

Nimimi pekee ndio nilijua dhamira yakutoroka nawewe siku ile,

Kwakweli Siku ile nilikuwa naingojea kwa hamu sana ifike sababu nilidhamiria kuzungumza nawewe.

Nilitoroka nawewe nikaenda mbali kidogo Na nyumba yetu,

Ulikuwa una siku 40 tu tangu uzaliwe, nafikiri ndio maana watu walinishangaa sana kuondoka nawewe, tena bila kuwaaga.

Nilienda nawewe mahala nilipopajua mwenyewe, Ninachoshukuru nikwamba nilichodhamiria kilifanikiwa.

Nilizungumza yote na naamini uliyasikia maana hata kawaida yako yakulia siku ile sikuiona kabisa.

Ulinyamaza tuli kana kwamba ulikuwa mkubwa kumbe ni mtoto wa siku 40 tu.

Leo nitakwambia tena maneno yale niliyokwambia miaka ile ukiwa mchanga, naamini utanisikia Na utanielewa maana kipindi kile ulinisikia tu ila  sina hakika kama ulinielewa."

Alizungumza kwa shida Mzee, alilpofika hapa alijikohoza kisha akanyamaza kwa sekunde kadhaa ndipo akaendelea kuzungumza

'WATU'

"Siku ile nilizungumza nawe kuhusu watu, nilikwambia, Watu ni muhimu sana katika maisha yako lakini usiwaamini,

Watakusifia, watasema wanakupenda, watakuita ndugu, rafiki, mtu mwema na kila jina lenye kukupendeza watakuvika lakini endelea Na msimamo wako ' usiwaamini'.

Watacheka nawewe, watakumegea siri zao, watakukumbatia kwa upendo lakini bado mwanangu, sio kigezo chakuwaamini.

Ishi nao kwa akili kubwa, tahadhari iwe muongozo wako, maana ni kawaida yao kupanga njama za kukusaliti hata bila sababu ya msingi.

Hawa watu waone tu hivyo hivyo, lakini wana kawaida yakupenda kuombwa lakini hawana desturi yakutoa,

Ukiwa nacho hawatafurahia sababu wanapenda kusikia shida zako, lakini ajabu siku ukiwa hauna hawatajitokeza kukusaidia, hiyo ndio kawaida ya watu.

Wameumbwa kwa maajabu sana, ishi nao kwa umakini, maana siku zote wanapigana ili ionekane mitazamo yao ndio Bora kuliko wengine.

Dharau ni asili yao, Tazama wasikudhoofishe.

Naomba sana uwe muangalifu Na hiki kitu kinaitwa chuki, ni kawaida ya watu kuwachukia wenzao, asije akakuaminisha mtu kwamba utachukiwa tu bila sababu,

Hapana!!.

Ukiwachunguza sana wanaokuchukia bila sababu, utakuja kubaini kuna kitu wanakihofia kwako,

Ndio,

 lazima kuna kitu utakuwa umewazidi maana hakuna chuki isiyo Na sababu,

Amini nakwambia.

Pia,

Watu hupenda kusujudiwa, mwanangu nakuonya usije kufanya Jambo hili!!

Wakusujudiwa ni MUNGU pekee.

Muheshimu kila mtu, hii sio dhambi, heshima ni jambo tumesisitiziwa,

 Ila sitisha kutoa heshima yako haraka iwezekanavyo kwa mtu asiyekuheshimu.

Halafu ni kawaida kwa watu kujipenda kuliko wanavyowapenda wengine, ukiliona suala hili kemea kwa jina la MUNGU wako maana yeye hakuagiza hivyo.

Naomba sana wapenda wengine, maana kuna hatari kubwa ya anayejipenda mwenyewe kuja kujizika mwenyewe siku za usoni.

Kitu muhimu zingatia, watu siku zote hawana chuki nawewe bali kile ulicho nacho, nilisema mwanzo Jambo hili hapa narudia tena ulichowazidi ndio tatizo hivyo kikumbatie Na ukifanye kwa Utashi zaidi, ipo siku watakuheshimu nacho.

Fahamu kwamba Watu wana akili Na wamepewa ufahamu, wanatambua maovu Na mema lakini wengi wao ni wafuasi wa maovu, sasa akili kichwani mwako, ukemee au uwe miongoni mwao.

Kitu cha mwisho siku ile nilise...."

Kufika hapa Mzee alisita kisha akakohoa "koh ...koh...."

Huruma ilinivaa, nikaongeza umakini kumtazama, kuna maneno alikuwa anayazungumza.

Kwa tabu sana niliyang'amua, alikuwa ananiagiza nimpe maji.

Haraka sana nikalikamata jagi la maji lililokuwa pembeni mwa kitanda chake.

Nilikamata Na glasi kisha nikaanza kumimina maji kwa haraka.

Sikuwahi!!!

Mzee alikuwa anarusha miguu huku Na kule.

Ishara mbaya,

"Baba ndio anakufa!?"

 Nilijiuliza kwa hamaki, glasi ilinidondoka mikononi nakuanguka chini kwa fujo.

Sikujali.

Umakini wangu woote ulihamia kwa Mzee.

Hakika alikuwa kwenye hatua za kifo.

"Toa shahada....baba toa shahada..... Mzee jikaze utoe shahada"

Nilizungumza kwa msisitizo, nikiamini Mzee akitamka shahada basi safari yake ya kuzimu itakuwa nyepesi.

Nashukuru alinielewa, kwa mbali niliona akijitahidi kunyanyua kidole chake cha shahada nikaanza kumtamkisha maneno ya kumpwekesha MUNGU Na kumtambua Muhammad kama mjumbe wake...

Baba akanyamaza.

Izrael akamkabili,
Kifo kikatamalaki,

Wosia wake kuhusu watu bado ungali nami mpaka hii Leo.

Mama yangu pia aliwahi sema kuhusu watu.

Aliniambia 'WATU NI SAWA NA MZIGO WA KINYESI, UKIUWEZA KWA UZITO BASI UTAKUSHINDA KWA HARUFU....'

Samahani sijawatajia jina langu naitwa Adam.

Kwaheri.

Na.
Omar ZONGo
SIMULIZI ZINAISHI

Tafakari Wengine

Muda mwingi hua unautumia kutafakari mazuri yako huku ukihitaji kusifiwa, hua unatamani kuongelewa wewe tu, unatamani kuonekana  Na wote wanaokuzunguka wasifu nakukuheshimu.

 Ni nadra sana mtu kutoa nafasi yakutafakari wengine, hivi ndivyo tulivyoumbwa, tumeumbwa na umimi.

Unajiona Bora kuliko wengine, wewe ndio unajiona mwenye akili, busara Na ushauri mzuri unaweza kutokea kwako.

Ni ajabu sana tabia hii Na kwa vile ni asili ya kuumbwa kwako sina lawama katika hilo

Ila leo nataka utenge muda kutafakari wengine, kuona vipawa vyao, nafasi yao, akili zao Na tamaa zao.

Ndio,

Anza sasa kumfikiria mtu wako wakaribu, ana umuhimu gani kwako.

Acha kuwaza wewe tu ndio mwenye umuhimu kwake.

Jiulize maswali ya Je ni vipi ingekuwa kama yeye asingekuwepo.

Tuanze Na msaidizi wako wa kazi za ndani.

Yeye anafua nguo zako, anakupikia, anakufanyia usafi wa nyumba n.k.

Acha kiburi chakusema hata kama asingekuwepo ungetafuta mwengine fikiria kuna watu duniani wanatafuta msaada kama huo lakini hawaupati.

Hivi unadhani fedha yako unayomlipa inazidi wema wakukutunzia nyumba yako, vitu vyako Na wakati mwengine hata watoto wako??

Tafakari wengine!

Kila mtu aliyekuzunguka anamchango mkubwa kwenye saikolojia yako.

Hebu pata picha unaamka asubuhi halafu kila unayekutana nae unamsalimia halafu anakujibu hovyo nakukudhalilisha au wengine hawakujibu wanakutema mate.

Unadhani saikolojia yako itakuwa nzuri hali hiyo ikiendelea mpaka unafika kazini kwako?

Wafanyakazi wenzako wote hawakupi ushirikiano hata wasalamu, kila mmoja anakuchunia nakukuona silolote.

Shtuka rafiki!

Kila mmoja unayekutana naye barabarani ana Faida kwako, ukijiheshimu atakuheshimu Na wewe utajisikia vizuri kuheshimiwa.

Leo nataka utafakari umuhimu wa kila aliyekuzunguka hata yule jamaa mtaani ambaye huna mazoea nae, husalimiani nae wala humkubali.

Nayeye ni sehemu ya maisha yako, anza sasa kuwaza umuhimu wake.

Paulo Coelho kwenye kitabu chake cha the alchemist kuna mahali anasema katika maisha yako yakawaida yule unayekutana nae kila siku ujue ni sehemu ya historia ya maisha yako, ni muhimu kumthamini sababu ana mchango mkubwa kwako.

Ni sahihi mtazamo wa bwana Coelho namimi nipigilie msumari hakuna ambaye hana mchango kwako, hata adui.

Wanasema wataalamu wa mambo ili ufanikiwe unahitaji marafiki lakini ili ufanikiwe zaidi unahitaji maadui.

Nakamilisha Na mfano wakubuni ambao naamini utaona Faida za maadui kwenye maisha yako.

Bosi mmoja alikuwa anapata malalamiko kila siku kuhusu mfanyakazi wake, alikuwa anaambiwa hafai, mla rushwa mara ooh hathamini wateja.

Ilifika mahali maneno kuhusu mfanyakazi wake yalimkera akataka kumfukuza kazi ila kabla hajafanya ivo akaenda kuomba ushauri kwa Mzee wake ambaye ndiye aliyemkabidhi ofisi.

Mzee akashtuka sana kusikia maneno anayoambiwa mwanae kuhusu mfanyakazi yule.

Alishtuka sababu yeye alimfahamu vema mfanyakazi yule.

Mara kadhaa wakati wa uongozi wake alishapata barua kutoka kwa wateja wa kampuni wakisifu huduma za mfanyakazi yule.

Wengine walidiriki hadi kumuomba akafanye kazi kwenye kampuni yao, lakini Mzee alikataa.

Mzee kwavile alimuachia mwanae ofisi akamwambia hatampa mbinu yoyote ya uongozi kwasababu anaamini kijana wake atakuwa mbunifu Na atakuwa Na mbinu mpya kwa maendeleo ya kampuni hivyo alivyotakiwa kutoa ushauri akatabasamu tu kisha akamwambia mwanae.

"Ni vema ukasikiliza maneno ya watu sababu lisemwalo lipo lakini vilevile ni vema ukachuja unayoambiwa maana Mti mwema mara zote ndio huandamwa kwa mawe"

Bosi alipoyatafakari maneno ya Mzee wake akayaelewa nakuona kuna haja yakuanza kufatilia utendaji kazi wa yule mfanyakazi kabla yakumfukuza.

Loh alipoanza kumfatili ndipo alipoanza kukutana Na sifa lukuki kuhusu utendaji kazi wa mfanyakazi yule.

Bosi akamuweka karibu zaidi nakumuongezea mshahara.

Maadui waliokuwa wanamchonganisha walisababisha jamaa ijulikane thamani yake.

Mwisho wa mfano huo.

Naomba uruhusu milango yako yote ya fahamu itafakari umuhimu wa yeyote uliye naye karibu kisha mthamini, muheshimu Na umjali.

Tambua yakwamba binaadamu tunategemeana katika kukamilisha tamaa zetu zote.

 Na
Omar ZONGo
SIMULIZI ZINAISHI

Mpumbavu 'Shida'

Huna stara, vazi lako ni fedheha, aibu hata huna waadhirisha wazee.

Mpumbavu shida.

Wafanya mtu awe lofa penye sio aseme ndio, mjinga baradhuli huna utu ata chembe.

Ujio wako ni waghafla, hodi kwenu hujafunzwa, harufu yako inatesa pua zote ni madonda.

Mpumbavu shida.

Kwani kwenu wapi!?? Bosi wako wewe nani, ujio wako washetani ama una baraka za Mungu!?

Eti!!, wapendelea nini kwenye maisha ya watu, mbona king'ang'anizi kwenye majumba ya watu!!.

Ujira wako upi, kumdhalilisha baba, umefaidika nini kumuandama mama!??

Eti mpumbavu shida!! Nani kakuagiza kwangu, ina maana umeshamalizana na mke wa jirani yangu??

Nani kakupa kiburi,  Shida kuandama watu, hata laana za wahenga shida hazijakupata!!

Acha ya mbaraka mwishehe kuna laana ya babu yangu, ulimuandama mpaka kifo shida kweli baradhuli.

Okey shida! Keti chini puuza maneno yangu.

Zungumza nami Leo nani kakuagiza!?? Kama rushwa nikupe uwaache watu huru!

Waache watoto wetu, waache wazazi wetu, waache viongozi wetu, liache Na bara letu.

Kama maneno yangu makali basi naomba niyafute sikuiti tena mpumbavu  nitakuita Jirani.

Ila sasa kabla ya hayo!! Badilisha tabia zako, usitiandame waja unatutesa wenzako.

Dah mpumba......oh sorry Jirani Shida.

Tunaomba huruma yako.

Na
Omar ZONGo
SIMULIZI ZINAISHI

Nachora Picha

Hata kama sio mzuri kwenye kuchora lakini Leo naanza rasmi kuchora picha.

Picha ya kusisimua,

Picha yenye kupendeza,
Picha niipendayo, Leo rasmi naichora.

Kwanza ile nyumba yangu nnayoiota kila siku.

Naanza kuchora kiwanja eneo flani tulivu, upepo flani mwanana, uwanja wake mkubwa.

Nachora eneo la kuogelea, eneo lakupumzikia, eneo lakuchezea Na eneo la hifadhi ya ndege Na wanyama

Nawachora wanyama, ndege na miti mingi nawaweka humu ndani katika eneo Lao maalum.

Nauchora uzio mrefu wa nyumba yangu, nauwekea umeme kuilinda nyumba yangu.

Nachora mageti mengi nawaweka Na walinzi nayachora Na magari mazuri ya kila aina nayaweka kwenye 'parking' ya kwenye hii nyumba yangu.

Nachora picha ya ndani ya vyumba vya nyumba yangu, kila chumba choo ndani ni nzuri picha yangu..

Rangi flani za amani zinapamba nyumba yangu, ukumbi mkubwa ndani yapendeza nyumba yangu.

Nachora samani zote zifaazo ndani, tena zile zakisasa zenye mvuto wa juu.

Naichora bahari eneo la mbele ya nyumba, fukwe yakifahari ubaridi wenye raha.

Bustani ndani ya uzio, maua yote ya mvuto, eneo la kucheza watoto mabembea Na maringi, napenda mpira wakikapu, uwanja wake nauchora.

Napenda sana riadha nitakimbia ufukweni, mapenzi yangu yakusoma nitayakidhi kwa maktaba, nitavichora vitabu vingi vyakila ladha.

Riwaya, machombezo, hamasa Na mauchawi, ngonjera nayo mashairi, vitabu aina zote.

Chumba hiki chasinema chasumbua kukichora, naweka mikanda yote ya kihindi nakichina, nawapenda wakorea wa mapanga Na mishale.

Sinema za Tanzania namuenzi kanumba, nawatazama wakali siwaachi Nigeria.

Nachora club ndani, wapenda muziki karibuni, ukumbi kamili vinywaji Na vilaji.

Nahisi hisi kuchoka mchoro bado kabisa,

Acha nimalizie watu wakuishi nyumba hii.

Namchora mwanadada mpole muadilifu, mkimya asiye na tamaa namfanya mke wangu.

Jina nampa la kibantu namuita Sijali, namchora umbo la namba, kifuani wastani, rangi nyeusi adhimu, mvuto wa chocolate.

Mie namuita SIJa namfupisha mwandani,
Huyu ndio mama watoto namchora kwa makini.

Naichora imani yake, mchamungu mashallah, stara mavazi yake, ndani msafi balaa.

Naichora tabia mpole, mnyenyekevu, mcheshi kwa wageni moyoni si mkorofi.

Naichora familia watoto flani wadadisi, watundu wa kujaribu, wenye akili balaa.

Najichora mie baba, baraghashea kichwani, msuli wangu kiunoni Na mustachi mdomoni.

Najichora nimekaa nje bustanini, mezani kikombe cha kahawa kitabu cha historia namsoma bunuasi Na mawazo kama yangu.

Hahahahaaaa....

Nitaendelea kuchora siku nyengine.

Na
Omar ZONGo
SIMULIZI ZINAISHI

USIJIELEZEE SAAANA!

We jamaa!!

Umerudi home mapema kabla ya mpenzi wako, umekuta nguo zako Na za mkeo zimeanikwa nje!!

Umeamua kuanua ili uziingize ndani!!

Bila kujua unaanua nguo ya ndani ya jirani yako(wakike), unaingiza ndani.

Dakika chache tu jirani yako anagonga mlango, unamkaribisha anaingia,

Anaulizia nguo yake kama umeondoa kwenye kamba bahati mbaya,

Unamwambia asubiri umuangalize,

Ametoka kuoga yuko Na khanga moja tu.

Unamlaani shetani, unaingia chumbani nakuanza kuchangua manguo uliyoanua!

Unaiona nguo ya ndani ya rangi ya pinki.

Unatoka nayo fasta, ili isiwe msala, unamkabidhi.

Anatoka nje mara paaap, uso kwa uso na mwanamke wako anatoka kazini.

Wivu wa mapenzi unamvaa mkeo, anatazama jirani alivyonona Na khanga moja, anajiaminisha kabisa kuwa ametoka kutenda dhambi Na wewe!!

Khanga moja, imeloa!! Mbaya zaidi mkononi kashika nguo ya ndani!!

Hata ni mimi nisingeelewa!!

Mkeo analianzisha pale nje, anamshukia Na mineno mikali jirani yenu.

Jirani mpole,  hajibu kitu anaingia ndani kwake.

Balaa linakugeukia wewe!!

"Malaya mkubwa wewe, mwanaume huridhiki, unafanya ushenzi chumbani kwangu!!"

Mineno ya shombo inamtoka, unamtuliza wapi, unajaribu kumuelezea ukweli, wapi!!

Ngoma imekufia!!

Sasa Leo nina ushauri BROH!!

Usijielezee saana!, muache aamue anachoamini.

Lengo nikurahisisha maisha!

Hakuna haja yakujielezea saana, kwasababu watu sasa hivi wanaamini zaidi mawazo yao kuliko ya wengine.

Kuwa Na desturi yakujielezea sana ili ueleweke ni kupoteza muda!

Elezea ukweli kuhusu wewe!! Kama bado hawaelewi achana nao hakuna Faida yoyote yakujielezea zaidi.

We Mdada!!

Jamaa hulijui limekosea meseji ikaja kwako.

Imeandikwa hivi.

' Jana sijaridhika kabisa, ulikuwa Na haraka kumuwahi uyo boya wako, yani bado nina hamu nawewe kinyama...'

Bahati mbaya meseji hiyo kaisoma jamaa ako,

Amevimba kwa hasira, mineno inamtoka!!

Kila unavyomuelewesha haelewi.

Muache.

Usiendelee kujieleza, mradi ukweli unaujua Na yeye hataki kuusadiki basi usiendelee kupoteza muda.

Muache aamue anachoamini.

Sio rahisi saaana, kama unavyosoma, sababu mapenzi ni ujinga! Watu huomba msamaha hata kwa kosa ambalo silo.

Ila jitahidi uweze! Achana Na Habari zakujilezea saaana.

Zimepitwa Na wakati Habari hizo.

Namalizia kukwambia kwanini nataka uache Habari zakujielezea saana.

Kwanza! Watu siku izi wanauliza maswali ilhali kichwani wana majibu yao Na maamuzi pia.

Pili, dunia siku hizi inajali ushahidi Na haina mpango wakutafuta ukweli.

Dunia imeshindwa kabisa kutambua kuwa ushahidi sio ukweli, hivi vitu vina utofauti mkubwa.

Kwamfano, Nguo ya ndani kuwa mkononi Mwa jirani, ni ushahidi tosha kuwa ametoka ndani kufanya dhambi Na mume wa mtu lakini ukweli sio huo.

Nyengine
Meseji ya mapenzi kutoka kwa jizi la wake za watu ni ushahidi tosha lakini sio ukweli kwamba dada wawatu amesaliti.

Dunia inathamini ushahidi kuliko maelezo yenye ukweli.

Mkweli ni mwenye ushahidi, kinyume Na hapo wewe ni Muongo tu.

Usijielezee saana waache waamue wanachoamini.

Agh!! Acha namimi niishie hapa nisikuelezee saaaana.

Acha niache uelewe ulivyoelewa.

Na
Omar Zongo
SIMULIZI ZINAISHI

This Iz My Sister


Na.
OMAr ZONGo

Hey niaje, naitwa Jayvny, kwetu tumezaliwa wawili tu, mimi na dada 'angu, yeye anaitwa Jackline.

Tumepishana miaka sita mimi nayeye!!, tunapendana sana mimi na dada angu licha ya yakwamba tumetofautiana baba.

Nataka kukupa kitu chakujifunza Leo kutoka kwa dada 'angu.

Sitakwambia amepitia mangapi mpaka kumuita shujaa kwenye Andiko hili ila nitakwambia kuhusu Moyo wake wa chuma.

2014 terehe 01, mwezi wa 11, ndio siku tulimpoteza mama etu, nikiwa Na umri wa miaka 16.

Mama aliondoka ghafla duniani, hakupata hata nafasi yakusema 'kwaherini wanangu'.

Alituacha mimi Na dada 'angu tukiwa wakiwa, tena wapweke wenye donda kubwa la maumivu ya kifo cha mama etu mpendwa.

Nakumbuka kifo cha bimkubwa kilinifanya nilie sana, nilipoteza fahamu.

Nakumbuka nilipozinduka nikajikuta nimelala chumbani, kichwa changu kikiwa juu ya mapaja ya dada.

Nilifumbua macho kuangaza humu ndani, vilio vya chini chini vilisikika kutoka kwa watu wengi waliomo humu.

Niliwatambua,

Wengi walikuwa ndugu zetu.

Ndio, ndugu zetu,

 Walikuwa hapa kuomboleza msiba wa mama 'etu.

Dah!! Akili ilinirudi!!

Masikini mimi nilikuwa kwenye siku za msiba wa mama angu, siku za majonzi makuu!.

"Pole Jayvny" sauti ya dada ilisema.

Niligeuka kumtazama, ni wa ajabu dada angu, alikuwa anatabasamu.

Kwa siku hii kwakweli sikumuelewa, nilidhani hakuwa Na uchungu na kifo cha mama.

Lakini sivyo!!! Ni dada ndio alikuwa ameguswa Na msiba ule pengine kuliko mie niliyezimia.

Ndio!!

dada ndio aliguswa zaidi, maana alijua kuwa majukumu ya mama yooote sasa yalimgeukia yeye.

Ule mkopo wa benki ambao mama aliuchukua ili afungue Biashara iliyovunjwa Na mgambo kisa iko barabarani, sasa ulimngoja yeye.

Kodi ya nyumba tuliopanga ambayo mwenye nyumba siku zake ziliisha zakusubiri, ilikuwa yakwake.

Ada yangu ya shule ya gharama ninayosoma, tayari muhula ulishakaribia kuanza.

Hayo Na mengine mengi sasa yalikuwa yanamngoja da' Jackline.

Lakini kwenye msiba wa mama alikuwa ameniweka mapajani kwake akinifariji nakunisihi ninyamaze kulia!!

Nakumbuka alisema "mama yupo nasi, ataendelea kua nasi, anatupenda na hapendi kuona tukisononeka maana ameenda kupumzika kwa MUNGU aliye hai"

Maskini dada!!

 Sikumuelewa, kumbe alikuwa anasimama imara yeye ili kunifanya kunifariji mimi.

Kumbe alikuwa anasimamia falsafa ya 'magumu hupita'

Hata baada ya mtihani ule, maisha yaliendelea.

Hakuwa Na kazi lakini alihakikisha nyumbani pengo la mama halionekani.

Mara zote alimtaja Kristo akisema ndio kimbilio letu.

Alisema kamwe hatutaanguka tukimtumainia bwana.

Hata aliyempa ujauzito alipokataa kulea mtoto dada hakuacha kujipa sababu zakulea nakumpenda mwanae.

Siku zote alisema maisha ni mazuri sana, alisema kila kitu kinapangwa na Bwana, alisimama imara Na lile tabasamu lake alilonionesha siku ile kwenye msiba wa mama.

Leo hii nakusimulia kuhusu dada angu imepita miezi sita tangu nisimame kwenye kitanda chake, maumivu makali ya maradhi yakiwa yamemdhoofisha.

Nakumbuka siku zile mara zote nilizokuwa nikimuona kitandani amelala hoi, machozi yalikuwa hayaachi kunitoka lakini yeye bado aliendelea kunifariji kwa sauti yake ya uchovu wa maradhi.

Alisema "Jayvny nitapona tu hivi karibuni, kila siku afya yangu Inaendelea kuimarika"

Maneno yake haya alikuwa haachi kuyasema, ingawa ukweli haukuwa huo kabisa.

Kila siku dada alikuwa akizidi kuwa hoi kitandani.

Hata siku ambayo alikutana na daktari wa kiroho, akampa tiba ya matumaini nilishindwa kuamini kama atapona.

Lakini hatimaye kweli dada akapona, afya yake iliporejea akasema "nilikwambia Jayvny, hatupaswi kulia magumu yakitufikia, ni mapito tu, ona sasa niko mzima."

Huyu ndio dada angu ambaye hivi sasa naongea nawewe niko nae kwenye chumba cha mauti.

Tumetekwa Na watu wasiojulikana, watesi wetu hawachoki kutupa adhabu bila sababu ya msingi.

Wanaionea miili yetu kwa vitu vyenye ncha Kali, wanatuadhibu kwa chakula kidogo nakutulazimisha kufanya yaliyo kinyume Na utu wetu.

Mwisho wa maisha yangu nauona, hali ya kukata tamaa imenitawala lakini bado dada angu haachi kusema "MUNGU ameruhusu haya yatufike, ana maana iliyo nzuri wala tusilaumu, endelea kuamini kuwa maisha yetu yabaadae tukitoka hapa ni Bora na mazuri mno"

Nashindwa kumuamini dada maana mateso yametuzidi kwakweli lakini namshangaa uso wake wenye damu kila mahali bado una lile tabasamu lake la faraja..

Anaitwa Jackline,
Ni jasiri, hakati tamaa, mpambanaji Na mwingi wa imani.

THISI IS MY SISTER.
Naamini tutatoka hapa.

To be cont....    


SiMUlizi ZinAishI

Dunia ni jinsia Gani??

Nawaza natafakari, kichwani hoja lukuki!!!
Naugua na maswali dunia jinsia gani??

Yakike au kiume, dunia ni dini gani?? Kabila lake mchaga, mnyamwezi au mhehe?? Dunia asili Ipi Iraq ama brazil?? Mwenyeji wa bara lipi afrika ama ulaya??

Dunia yajua nini swahili ama Arab?? Chakula chake ni kipi ni wanga au mafuta??

Yote Mie nayawaza ila kubwa ni hili.

DUNIA JINSIA GANI???

Jinsia yake ni KE au ni ME semeni!!

Ina hila za kike wakati mwengine huringa!

Lakini msimamo
wake ni dume, umeikuta na utaiacha.

Dunia ina magumu, harakati za kibabe! Tabia hii ni dume, ila utamu wakike.

Imehifadhi mengi viumbe aina zote, sifa hii yakike twaitambua wote lakini mbona ni kali yatesa viumbe wake, mwanaume baradhuli hii ni sifa yake..

Dunia kama ni kike kwanini yapendelea, upendo wa mwanamke kotekote waenea.

Au tuseme kidume ndio yake jinsia ila mbona pakashume yalea mpaka wambea.

Dunia kama ni mama mbona huruma haina, haya tuseme ni baba matunzo yake yawapi??

Kama ni mke iseme wahuni tupite nayo!! Kama ni dume ropoka warembo wakutunuku.

Jamani basi semeni dunia ni dada duu, au ni kaka flani mwenye hulka kuu kuu!!

Dunia ina unafiki tabia za wanawake lakini  na usaliti wanafanya wanaume.

Wahenga walishasema mengi kuhusu hii dunia, waliita tambara lenye viraka chakavu.

Lakini hawakuweza kutanabaisha jinsia, walibaki tu kusema eti dunia hadaa.

Swali langu watafiti, wasomi, wataaalamu nijibuni himahima dunia jinsia gani??

Na.
Omar ZONGo
SIMULIZI ZINAISHI

Dear tomorrow

Mambo vipi?? Nataka kusema nawewe, imenilazimu kufanya ivo sababu ya hofu uliyoijenga kwa mdogo wangu Sam!

Maneno yake mengi kukuhusu ameyaelezea acha nimnukuu "bro, natamani kujua vipi itakuwa kesho yangu, natamani kuona mahali nitakapoanguka, Na jee nitasimama kuendelea Na safari au ndio basi tena, kipi kitajiri kesho nijiandae nacho...nawaza sana!!"

Mwisho wakunukuu!!

Dear tomorrow!!

 Kipi nikupe ili unimegee siri, Je ukifika yatanitokea yaliyonitokea Jana au wewe utakuja namengine mapya!?

Je utakuja Na vazi liitwalo huzuni au utaniletea zawadi ya furaha?

utasimamia ndoto yangu vema au utaiacha iende Na maji.

Nataka dawa ya wanafiki, wazandiki, wachawi waliojificha kwenye mwamvuli wa wema, sasa niambie utakuja Na ufumbuzi wa kuwajua au ndio bado nitaendelea kuishi nao nikidhani ni watu kumbe majitu.

Dear tomorrow, nakuwaza mpaka nakonda! Je utakuja Na maradhi yakunilaza au uzima wakuniimarisha??

Utasema namimi kwa upole au utanikemea kwa jazba!

Ukija utaambatana na mke mwema au kizabi zabina, katili wa moyo wangu??

Nasikia yupo kiumbe ambaye hajawahi kufa tangu kuumbwa kwake, nasikia anaitwa Melchizedek, nasikia eti yeye husaidia wanadamu wenye dhiki kuu!!

Niambie basi utakuja nae huyu?, kama yawezekana basi njoo nae maana mbele yetu kuna maradhi ya ajabu yanatungoja, pembeni yetu ajali zinatumendea, nyuma yetu tunasindikizwa Na kifo Na juu yetu tunatazamwa Na Mashaka.

Njoo nae mkombozi, mwambie MUNGU amemweka ili awe nusura yetu.

Dear tomorrow!

Kama yawezekana njoo Na dawa ya kusahau ya Jana!! Hasa yale yanayoumiza.

Natamani kujua nini nifanye ili uje Na tabasamu, uwe mfariji Na usimamie vema malengo yangu.

Nakusubiria tomorrow, hisia zangu zimetawaliwa Na vitu aina tatu.

Kwanza hofu sababu sjui utakuja kwa mtindo gani.

Pili Tumaini sababu ya maandalizi niliyoyafanya yakukupokea.

Tatu maswali mengi, juu ya nini utapenda nikuandalie ili ukija niwe rafiki yako daima Na usiniache mkiwa siku utapoondoka.

Welcome tomorrow!!!!

Na
Omar ZONGo
Simulizi Zinaishi

MASWALI Unayojiuliza

 NA
Majibu niliyokuandalia!!

No1.
Nimesoma, nimemaliza nina vyeti smart sana!! Sasa kwanini sina kazi!??

Jibu lake:

Kwasababu ulibweteka ukategemea elimu ikufanyie makubwa, ukasahau ulichosomea wenzako mamia wapo mtaani wamesomea!!!

Hutaki kujiajiri wala kujitolea kufanya kazi bure, unaamini katika muujiza wakuitwa Na bosi uliyemtumia barua ya kazi!! Unahisi siku moja utakua meneja, kiongozi katika kampuni hiyo, unamuamini mganga aliyekutuma kuku, akakupa hirizi nakukuaminisha utapata kazi hivi karibuni.

Shtuka, tafuta njia ya kujiajiri hiyo nafasi unayoitaka kuna mwenzako kaikalia Na amejizatiti kwelikweli mpaka umng'oe basi lazima uwe mzoefu zaidi yake, uwe Na ushawishi zaidi yake lakini zaidi uwe mchawi zaidi yake.

Usiendelee kujiuliza swali hili acha sasa Na ubadili mtazamo.

No2.
Kwanini msichana akiwa Na mvuto sana nakosa ujasiri wakumtongoza!??

Jibu lake!!

Kwasababu haujiamini, uzuri wake umefanikiwa kudhoofisha akili yako Na mara zote unajiambia "atakutoa nishai" sauti hii ya ndani yako ina kufanya uzidi kuwa muoga Na ujione hauendani nae,

Kitu usichokijua nikwamba yeye pia ana shida kama wewe, ameumbwa kama wewe, Na huenda ni fukara kama wewe Na pia hajiamini kama wewe,

Usichokijua zaidi huenda anatamani mwanaume kama wewe, mwenye sifa kama zako.

Tatizo ni hujiamini tu, unaishi kwa story za vijiweni na vimaneno vya kukatishana tamaa, kwa taarifa yako mwanamke ni kiumbe dhaifu hasa akikutana na mwanaume wa shoka, akamtuliza nakumuimbisha kiume.

Kumbuka kabla ya pesa alikuwepo adam ambaye hakuwa hata Na senti yakununua nguo, Na walipendana na Hawa kindakindaki,

Usijipe sababu zakushindwa chief nenda ukamng'oe yule mtoto.

No.3
Sioni wakumuoa!!?

Jibu lake!!
Khaaa!! Haupo serious chief,

Wadada wote hawa tena wengine mpaka wanajiuza unakosaje wakumuoa!??

Jibu lake ni fupi tu!! Haupo tayari kuoa!

Skia popote penye nia, njia haiwezi jificha, wanawake wengi wapo ambao wanatamani kutamkiwa ndoa, wewe uko wapi!! Au unataka mzuri wa tabia, haiba yakuvutia, mpole na atakayekupenda kwa dhati!??

Amini au usiamini sifa hizo zote zinategemea Na wewe utakuwa mume wa aina gani!! Kama utaweza kusimamia majukumu yako, basi mwanamke wako atakuwa Na sifa hizo tena Na yaziada iitwayo KUKUHESHIMU.

Oa kisha simamia matunzo, mtosheleze kitandani, muonee huruma, msikilize Na mshirikishe mambo yako, mjali na umpe kipaumbele.

Kama bado hatatulia oa mwengine kisha mfanyie mambo hayo, kama nae hatatulia waache wote kisha baki mwenyewe!!!

No 4.
Nifanyeje kutimiza ndoto zangu??, broh nina kipaji ujue!!???

Jibu lake:

Ni simpo tu!! Jiamini, kuwa tofauti Na wenye kipaji kama chako, usikate tamaa!

Nikisema uwe tofauti Namaanisha usiige kufanya kama waliokutangulia wanavyofanya, jipambanue kwa ubunifu mpya ili watu wapate kiu yakukusikiliza wewe nakuthamini ulicho nacho!!!.

No. 5

Natamani kufanya kitu, tatizo mtaji tu!! Sjui nifanyeje!??

Jibu lake:

Point yakushindwa kufanya kitu unayo ila ni dhaifu sana,

Mbuyu kabla yakuwa mti mkubwa wenye heshima zake, ulikuwa kadomfyo mno.

Enzi za udogo mbuyu ulikumbana Na adha yakukanyagwa, kulimwa Na kubaki mzizi tu lakini haukukata tamaa, kwa kudra za mvua ulinyeshewa, ukamea Na ukapata nafasi ukakuwa Na hadi sasa kuunyanyasa mbuyu itakupasa ujizatiti kwelikweli.

Anza Na ulicho nacho! Usikidharau, kiheshimu, kitunze na unapopata nafasi yakuzungumza na mwenye kuweza kukusaidia muombe akusaidie, usimuombe kikubwa we msihi akupe kidogo tu ili ukijumlishe Na ulichoanza nacho naamini utafanikiwa tu....

Kama una swali endelea kuuliza me ntakujibu tu!!!

SIMULIZI ZINAISHI
Na.
Zongo Omar

Mchamungu Maskani


leo mcha Mungu
nimekuja maskani
umenizidi uchungu
namkemea shetani
enyi vijana wenzangu
twendeni ibadani

kwani wewe ninani
mbona anaturushia
stimu zipo kichwani
wewe unatuzingua
Ibada ndio kitu gani
mbona sijakuelewa

 Hili kweli nijanga
vijana mwateketea
Mungu anamipenda
ndio mana mewajia
punguzeni Maujinga
shetani anawaponzea

masela hili balaa
maskani limeingia
jamaa sijui ni njaa
msikie anachoongea
oyah hebu ambaa
tusije kukuchengua

huruma nawaonea
enyi vijana wenzangu
nawaomba zingatia
nasaa hizi zakwangu
nyakati zimewadia
anawahitaji Mungu

Mungu ndio kitu gani
lini ulimuona akija
mambo ya kizamani
maskani toa kioja
Mungu wetu mjani
kamatia pafu piga

Mungu awasamehe
hamjui mlisemalo
shetani tumkemee
hatapata atakalo
acheni niwaombe
enyi mabarobaro

shika adabu yako
muombee mama ako
hatutaki sera zako
ni hora uende zako
sura ka mbwa koko
fanya usepe zako.

maarifa ndio hamna
basi pokeeni yangu
nafanya kila namna
kuwaokoa wenzangu
shetani hana maana
rejeeni kwa MUNGU.

Ila masela kweli
hebu tumsikilize
pengine hili zali
wahuni tusipuuze
mbingunu ujue mbali
ubishi siendekeze

haya sema haraka
skani umefata nini
kama huwezi ondoka
kahubiri kanisani
laa hujaokoka
kaswali msikitini

Asanteni kwa muda
enyi kizazi potofu
achaneni na wida
rejeeni uongofu
msiupoteze muda
leo hai kesho mfu

Anzeni sasa ibada
dunia kuti chakavu
uchaMungu si ukuda
ni njia ya uwokovu
jivunieni faida
hamtabaki na kovu

walikuja manabii
werevu na watukufu
wakaiweka bidii
kutangaza uongofu
ajabu dunia hii
yaongoza kwa uovu

kuna maisha baada
tazama nyendo zako
uzima upo kwa muda
uchunge ulimi wako
na uheshimu ibada
ina manufaa kwako

wekeni chini sigara
mibange mihadarati
iepukeni hasara
madawa sio rafiki
maombi kwenu ni bora
shetani ana unafiki

eh baba wa mbinguni
mfalme wa vitu vyote
nakuleta masikani
uondoe dhambi zote
vijana hawa makini
ibadani tuwe wote

waondoke leo nami
nikasali nao wote
waondoshe dhambini
usimuache yeyote
zile bange za kichwani
Mungu ziondoshe zote

ndugu semeni amin
maombi yapokelewe
kisha ondokeni nami
twendeni mkaokolewe
yoyote mwenye imani
naomba anyookewe


blaza asante sana
wokovu tumeuona
bange sasa hapana
ni ibada kwa sana
chars mshtue kombe
ili ibadani twende

mwana umetisha sana
hizi tano pokea
masikani sikai tena
ibadani naelekea
kauli yangu nasema
Shetani kapungukiwa.