Siku kadhaa zimepita tangu niandike barua kwa marehemu nguli
wa Kiswahili na mtunzi wa mashairi Sheikh Shaabani Robert, Usiku naweweseka
nashtuka nakiona kivuli cha Shaaban
Robet, kinanikabidhi Barua, kisha kinatoweka machoni mwangu , napigwa na
butwaa, nakurupuka kana kwamba nimemwagiwa maji ya baridi naikimbilia taa
naiwasha , mkononi mwangu nauona waraka ule wa barua niliyokabidhiwa, moyo
unaenda mbio, macho yanakimbilia kusoma kilichoandikwa!
Maneo ya juu kabisa yameandikwa.
Shaaban Robert Katabasamu!
Naongeza umakini kusoma zaidi….
iliandikwa hiviii.
Asante sana, kilembwe changu, yumkini baadhi ya kizazi chenu
chatambua niliwahi kuwapo duniani basi najifaghiri sana huku nilipo.
Barua yako nimeipokea, ingawa hukuipa jina barua ile ila
nikaona nisifanye kosa kama ulilofanya wewe yakwangu mie nimeipa jina hilo hapo juu,
Shaaban Katabasamu.
Kwa hakika umenifanya nitabasamuj kwa mara ya kwanza tangu
kufariki kwangu, mwanzoni nilivyoanza kupigania lugha yangu nilianza kwa
masikhara lakini baadae nikaona yapasa nigangamare ili niipatie heshima lugha
hiyo, mchango wangu nilikuja utambua
dakika za mwisho kabisa za uhai wangu, lakini sikuwa na namna yakukwepa rungu
la kifo ambalo liliishukia roho yangu.
Mauti yakanikabili kwa mabavu yake, nikawa mpole nikinyoosha
mikono juu kusalimu amri, tangu hapo nilitaraji kuwapo hata na maadhimisho ya
heshima kwa sisi wapigania hadhi ya lugha hiyo, lakini sikuwahi sikia, angalau
barua yako imenifanya nitabasamu sababu mchango wangu umekuja kuenziwa nawe
ambaye jina langu limekufikia kwa historia tu, naamini labda utakatifu huo
utawashukia na vizazi vyako,pamoja na wenye mamlaka serikalini!
Tabasamu langu lanena maneno ya aina tatu, aina ya kwanza ni
furaha yakupokea barua yako kilembwe changu, aina ya pili ya tabasamu hili
ni huzuni kuu itoakanayo na habari ulizo
nipa kuhusu Fasihi simulizi ilivyo kwa sasa huko duniani, ama hakika ni pigo
kwangu tena pigo takatifu kusikia hii leo duniani hatupo sisi wakina Shaaban
Robert tena, zaidi ule mziki wa kina Bi Siti haupo tena, kimekumbwa na lana
gani kizazi chenu Masikini! Haya huo mziki wakuruka nakuvua mashati ndio mziki
wa aina gani mbona ni khabari ngeni hizi . Tena sio ngeni hivi hivi ni ngeni
zakushangaza.
Ashaakum si matusi Uvaaji wenu huo wakushusha suruali chini
ya makalio, nimeustaajabia mara dufu,
Karima awaponye yasije yakawakuta yalowakuta kizazi cha Nuhu,
Tabasamu langu hili lanena pia kuhusu sononeko langu la kazi
zangu na wanagenzi wenzangu kuthaminiwa kwa mwendo wa kinyonga, lakini usitie
shaka katika hilo, Kusahau ni sifa kuu ya binaadamu dhaifu, na ndio mana
hakamiliki kuumbwa kabla hajafa! Ulizo nazo zitunze ni hadhina kwako na kwa
wale watakaosadiki misemo yetu ya kwamba vyakale ni dhahabu,
Nimeona tamaa yako yakutaka kujua kinachoendela katika nchi
yakusadikika, vizuri sana.
Nchi yakusadikika hii leo angalau imepata kiongozi thabiti,anadhibiti
kweli mianya ya rushwa hatoi hata upenyo kwa mtumishi wa uma kukaa kizembe,
anahimiza kazi, anajenga uzalendo na anafuata sheria kwa maana nchi ile
ilishapoteza kabisa nidhamu yakiungozi. Usitie shaka ipo siku utafika nchini
mule kwa maana hata wageni wanaweza kuingia hivi sasa bila kupata shida sababu,
miundombinu inaendelea kuimarishwa hasa ya usafiri, kuna magari mareefu hivi
sasa yanaingia abiria wengi.
Nakumbuka Niliacha Hati duniani, hati muktasi kwa mabinti, nakumbuka ulikuwa ni wasia wangu
mzuri kwao, hakikisha unaipata hati ile itakusaidia hata kumnyoosha mchumba
wako kimaadili,
Zilikuwa beti 100, nitarejea chache tu hapa,
Taabu zikikukuta waweza nazo kuteta, njia yakupita lazima
zitakwachia.
Lakini zikikuona huwezi nazo pigana,zitakusumbua sana, hati
hii yafunua
Tia katikamoyo nia ya maendeleo hati hii ni cheo kushinda
ovu andaa.
Usishiriki hongo,ijara upate hongo, mtu muongo ni msungo,
masuto mengi hupewa,
Jambo usiloliona haifai kunongona, hiyo ndio fitina mngwana
ya kujitoa.
Hujaniambia katika barua ulonitumia nani hasa amevaa viatu
vyangu katika utenzi wa mashairi, nilipenda sana mashairi, yalinimaliza hasira
iliponikaribia na yalinipa burudani kila nilipoyasikia,
asante sana kwa kuukumbuka uwepo wangu, Ipokee barua hii
Kilembwe changu, nitahakikisha unapata
Baraka zangu, ili uendelee kupigania lugha yangu, vitunze na uvisome vitabu
vyangu angalau utaipata akili yangu. Na ukipata nafasi tembelea kaburi langu, watafute
waliyo na chembe za damu yangu, na usisite kuwapa salamu zangu……
Ni mimi Mwanagenzi Shaaban Robert, Angali bado uhai usisite
kutenda mema, maana Wema hauozi, hudumu huko duniani na huku nilipo akhera,
Wasalaam kilembwe changu Omar Zongo…
Namaliza kusoma barua hiyo Jasho lanitoka, napatwa na woga ghafla
barua hiyo yatoweka mikononi mwangu, nashtuka usingizini loh kumbe nilikuwa
ndotoni
…..ama hakika Mungu Ailaze roho yako mahala pema peponi Shaaban Robert, aamin.
…..ama hakika Mungu Ailaze roho yako mahala pema peponi Shaaban Robert, aamin.