sio rahisi hata kidogo
na inahitaji moyo na sio mradi moyo tu, moyo wenye ujasiri na usio mwepesi
kutiririkwa na machozi, moyo wenye kustahimili na wenye kuelewa kuwa haya mambo
ndivyo yalivyo na yanahitaji utashi na busara ili yaweze kukupa heshima kwa
vizazi vyote vya sasa na vijavyo,
Waswahili walitukuka kwa
misemo na walimaanisha waliposema ukiona vyaelea ujue vimeundwa, au ukitaka
uzuri sharti uzurike.
Inataka Moyo |
walikuwa na maana pana
sana waliposema hayo lakini maana hiyo ililenga hasa maisha yetu ya kawaida.
Umezaliwa Kijijini
hakuna nyezo za aina yoyote ile, shule ipo mbali sana inasababisha hata viatu
vya shule visidumu nakufanya muda wote vionekane kama vinacheka mbele na soli
ikiwa ina upara wa lazima unaotokana na kiguu na njia kila uchwao.
unajikuta una uwezo
mkubwa wakuimba lakini kipaza sauti hujawahi hata siku moja kukiona, wenzako
mjini wanatunga mashairi huku ala ikiwa inasikika aidha kwenye kinukulishi, au
simu lakini wewe huna hata redio, baba mkali sana ukiikaribia redio yake hivyo
unakuwa mpole tu ukiendelea kujifariji kuwa lazima siku moja utatoka.
mara moja moja tena kwa
tabu sana huwa unawasiliana na rafiki zako kadhaa ambao tayari angalau wapo
mjini, na zamani mlikuwa mnadanganyana kuwa wote lazima mtatoka, lakini wewe
kwa sababu huna hata ndugu mjini wenzio wamekuacha ukiendelea kupalilia shamba
la familia nakusaga dona ili wadogo zake wasikose ugali watakaporudi nyumbani.
Mara moja ulishawahi
kukutana na rafiki yako mmoja kati ya wengi walioenda mjini alirudi mara moja
kwenye msiba wa mama wa bibi yake anakwambia habari za mjini, unamsikiliza kwa
makini sana licha ya kwamba pia unamshangaa jinsi alivyobadilika , nywele
amenyoa kote katikati ameacha, shati limekatwa mikono yote na suruali
imechanika chanika magotini, ana kitu ambacho mara zote unawaona Wanawake
wanakiweka masikioni. Unajiuliza maswali mengi kwanini avae yeye puani na
kwenye sikio lake moja lakulia,
Kutokana nawewe una
kipaji sawa na chakwake na mlikuwa mnaimba sana shuleni kwenu kwenye sherehe za
shule basi unajiweka nae karibu huku ukitaka sana kujua habari za mjini, dakika
kumi tu za mwanzo unabaini kuwa ili kuendana na kipaji chako lazima uwe kama
jamaa,
Unajikuta unachukia
lakini huna jinsi nawe taratibu unaanza kujitengenezea picha ya baadae utakuwa
kama vile, wazee wote wa kijiji wanalaani uvaaji na muonekano wa rafiki yako
lakini wewe tayari ulishakolea na simulizi za mjini umeshadanganyika unatamani
kwenda mjini nawe ukawe vile,
Masikini ya mungu una
kiu kweli kweli, kiu yakuonesha uwezo wako uliojaaliwa na Mungu, bila kuwa
karibu na jamaa utakosa njia yakutangaza kipaji chako mjini. Jamaa anakwambia
kuwa mjini tayari anafahamiana na watangazaji kadhaa na madj maarufu ambao
wanaweza kumtoa mtu kimuziki.
Unazidi kuchizika,
lakini kutokana na busara za mzee wako baadae unakaa na echini ya mti
anakurejesha kwenye utimamu wako, anakwambia busara tupu, zinazokufanya ujione
mjinga kwa kumpa muda wako jamaa kumsikiliza nakutamani kuwa kama yeye…mzee
anakwambia kwa upole na umakini huku akionekana kujua zaidi saikolojia yako
inawaza nini
“Mwanangu, najua uwezo
wako, kipaji chako na karma yako uliyopewa, miaka mingi ya nyuma niliwahi
kuishi mjini, nilibahatika kukutana na watu wenye kipaji aina yako,
nilibahatika kuzungumza nao sababu hawakuwa kama alivyo rafiki yako.
walikuwa wastaarabu, sio
wahuni, walikuwa wasikivu waelewa na katika maneno yao Ishirini kumi na tano
yote wanaelezea kiu yao yakutaka kujulikana, kutangaza kipaji chao nakutumia
kalamu zao kukosoa, kuelimisha na kurekebisha jamii, niliwafanya rafiki na
nikawaazima sikio lao pia kuwasikiliza wanachoimba,mashallah nyimbo zao
zilifunza, zikanipa muongozo na zikanijengea uzalendo wa nchi yangu, tamaduni
yangu na kila kitu kuhusu asili yangu.
nyimbo zao zilinyooshea
vidole maadili ya kiafrika yanayomomonyoka mithili ya mvua inayomomomnyosha
udongo mabondeni, nyimbo zao zilibeba ujumbe thabiti uliokosoa viongozi
walafi, lakini zaidi nyimbo zao ziliburudisha nakukukonga nyoyo sababu ya ala
safi ya muziki uliopangiliwa ukapangika.
Sikuona kama walisuka
nywele au walikata nywele kama rafiki yako, sikuona kama walikuwa na ufinyu wa
akili nakuvaa nguo zinazobana na zilizochanika magotini kama alivyokuja nazo
huyu mwenzio, lakini pia sikumbuki kama walitoboa pua zao sababu ni wao ndio
walihimiza jamii kusimama imara katika tamaduni za kiafrika, na waafrika hawana
maelekezo ya wanaume kuvaa urembo katika pua wala kwenye masikio,
Nakupa Baraka upambane
kutangaza kipaji chako lakini mara zote jiulize nini unakifanya kwa jamii yako
kupitia kipaji chako. Kumbuka kuwa Kesho lazima utaulizwa!”
Baba huyu ni miongoni
mwa wazee ambao huamini kuongea sana ni dalili yakutojiamini, hivyo alipomaliza
kusema hivyo alimuacha mwanae, na somo moja lililopita kama muhtasari kichwani
kwake, UWEZO ULIO ZALIWA NAO NI JAMBO LA KWANZA, NAMNA YAKUITUMIKIA JAMII YAKO
KUPITIA UWEZO HUO NI JAMBO LA PILI NA LA MUHIMU ZAIDI.
Maneno ya baba yake
yalisimama kama muongozo tangu hapo lakini swali gumu likabaki kwake ni vipi
atapata pesa, na wakati Aina ya muziki aliomuelekeza baba yake ni mziki ambao
vijana abadani hawauelewi, wanapenda mapenzi, starehe na dhima nyengine nyingi
rahisi kama vile majivuno na sifa.
Inataka moyo, kusimamia
uzalendo wakati mfuko upo hoehae, inataka moyo zaidi kuielimisha jamii ambayo
yenyewe inataka kukulipa ukiipotosha, Inataka moyo sana kuchagua Kulipwa kesho
na Mungu wako kupitia alichokuzawadia kwa kuisadia jamii kuzinduka kutoka
katika kiza cha ujinga, uonewaji, ukatili na kunyimwa haki zao au kulipwa leo
kwa kuwapa chakula ulichokiandaa chenye dhima waipendayo lakini sumu
iwamalizayo
Inataka moyo….