hata kama ugumu upo wakuyafikia mafanikio lakini kwao ugumu unageuka kuwa ulaini, ulaini ambao unatokana na furaha na amani ya wazazi wao kutokana na kuenziwa kwa juhudi zote nakutangazwa kwa michango yao katika historia ya waliopo sasa na hata wa kesho, lazima wafanikiwe.
najua busara zi pamoja nawe na ndio mana unasadiki kuwa mafanikio yataendelea kuwa kwao sababu hata makazi ya wazazi wao ya milele bado yangali na thamani na wanayaenzi kwa marefu na mapana, sasa kuna kipi kinaweza fanya laana ya umasikini iwe kwao! nasisitiza ni lazima wafanikiwe!
tutaendelea kutamani kutibiwa kwao, kula vyakula wanavyokula wao, kuishi nyumba kama zao na hata tamaduni zao kwetu zitakuwa lulu sababu zetu zimeshasuswa na baraka za wazazi wetu, mababu zetu ambao waliihifadhi heshima yetu mahala wakitaraji tuitafute kwa kuienzi nakuwatunuku joho la heshima katika ukamilifu wote wa maisha yetu, lakini haya ya wapi? ni kinyume na uhalisia wenyewe, kazi zao, damu zao na hata michango yao imepuuzwa huku harakati zikiwa kutafuta maendeleo ya kiuchumi.
hakika haya ni mastaajabio yangu bin Zongo, mastaajabio makuu katika muda wangu huu wa pumzi iliyo hai, mastaajabio ya mafanikio bila baraka za wazazi wetu, wazee wetu na waliowahi kuweka nakshi katika haya tunayojivunia hii leo!
ni nani asiyesadiki ya wahenga waliotukuka kwa misemo na tafakari zakuona mbali ambao walipata muda nakunena kwamba Vyakale Dhahabu, ni nani? jibu ni sisi tuloikuta hii dunia kisha tukawa mbio, tukaharakatia matumbo yetu na vizazi vyetu huku tukisahau utu wa wazee wetu, waliokuwa na michango kwenye tamaduni zetu, nchi yetu na kila kitu kutuhusu
Sehemu ya kumbukumbu ya mwanafasihi | Wilium Shakespear |
Natafakari kwa kina huku nafsi ikilalama naliona tabasamu la maridhio lililo usoni mwa aliyekuwa nguli wa mashairi na mtunzi wa vitabu wa uingereza WILLIUM SHAKESPEAR, naliona kaburi lake linaloenziwa nakutunukiwa Mashada ya pongezi huku taswira chungu yenye sononeko nikiiona kwa Mwanagenzi aliyekuwa mashuhuri ukanda wa Afrika mashariki SHAABANI ROBERT huku kaburi lake likiona aibu kwa kutelekezwa kule Tanga ilhali kazi zake zikiendelea kudumisha utu na uelewa kwa vizazi vyoote tangu na baada ya kifo chake.
Mafanikio Yataendelea kuwa kwao, licha ya mapungufu mengine waliyonayo lakini katika hilo lazima vinara wawe wao! licha ya kwamba inaniuma lakini sitathubutu kusema Mungu wabariki wao na uzidi kutupa laana sie, sitathubutu na hata mdomo ukitaka kusema hivyo nitaukemea kwa sauti kuu na fikra zikianza kuwaza hilo nitazitenga kabisa, sababu nanua laana sio mbaya na daima nitaendelea kusema Mungu simamia imani zetu, tusiendelee kudharau ya wahenga wetu, tuwaenzi kwa yale yakwao yaliyojaa utu ili tuyaone mafanikio yetu.