Barua kwako Mzee wangu Shaaban Robert

                Salaam ama baada ya salaam, Ni matumaini yangu umelala pema peponi, naamini hivo na naendelea kumuomba Mungu aendelee kukupa pepo sababu ya mchango wako mkubwa wakusimamia nakuipa heshima lugha yetu ya kiswahili nakuinyoosha jamii kupitia kipaji chako adhimu ulichokuwa umejaaliwa,          

               Umezaliwa miaka ambayo sio mimi tu hata baba yangu na mama walikuwa hawana dalili yakuzaliwa, lakini nalipa heshima sana tukio lakuzaliwa kwako,ilikuwa ni zamani sana, zamani isiyosemeka, zamani ya mwaka 1909.
nalipa heshima tukio lakuzaliwa kwako sababu zikiwa ni nyingi lakini kubwa ni heshima uliyowahi kuiwekea nchi yangu pamoja na lugha yangu ninayoitumia,

kwa dhati ya moyo wangu kabisa napata muongozo kupitia wewe ingawa sijui ni muongozo gani sababu umefariki kipindi ambacho mimi hata sijawa na dalili yakuiona hii sura ya dunia nimekujua kupitia historia lakini historia hiyo ndio inafanya niseme ulikuwa wa pekee

sina mengi yakukujuza niseme tu kazi zako bado zinaendelea kuishi ingawa tunaamini kuwa asiyekuwepo na lake halipo lakini kwangu mimi licha yakuwa haupo lakini lako bado lipo kichwani mwangu ingawa ni kweli  hatua zakuhifadhi nakuthamini kazi zako zinapigwa lakini zinapigwa kwa mwendo wakinyonga mno,

ile nchi yako uliyoiita yakusadikika, sijui inaendeleaje kwa sasa nimekosa kabisa namna yakufika kule ili kuona namna ambavyo elimu ya sheria ilivyowanyoosha watu, pengine labda ule udhalimu, uonevu na matumizi mabaya ya madaraka umeisha ningeweza kutafuta namna nifike kule nijionee mwenyewe hali ya mambo ilivyo lakini nimejikuta natamani mno ungekuwepo wewe nafikiri ungeniongoza kufika huko au ungenipa ujumbe wa hali ilivyo sababu jicho lako lilikuwa ni pevu mno na mtu wakawaida asingeweza kuiona nchi ile inayoelea angani.

kazi za akili yako zipo bado zinaendelea kuishi, ubora wako haufutiki hata kidogo kichwani mwa mwerevu na mwenye busara yakujua kizuri ni nini,
kwa sasa mambo yamebadilika sana, kuna maghorofa, kuna barabara za kila mtindo na hata mavazi yetu vijana sio kama yale yenu, yale ya balaghashea na kanzu pamoja na bakora, siku izi vijana tunavaa t shirt na jeans, halafu tunashusha kidogo, mtindo wetu maarufu kwa jina la mlegezo, au kata k.
 sipati picha ungekuwepo sasa ingekuwaje sababu kuna mengi yakuyaweka kimaandishi, yenye dhima pana ya migogoro, mauaji, vita, ubaguzi, ukatili, rushwa, tamaa ya madaraka, ubabe na kwakweli haya yote yanahitaji muongozo thabiti, lakini watu kama ninyi hampo tena, tuliopo hatujui utu na thamani ya tamaduni zetu, tunachojali ni masuala mepesi mno ambayo yanaishi kwa muda mchache sana nakufa, mapenzi, starehe na umimi uliomwagika nakusambaa kila kona ya ardhi hii.

Hii ni Barua kwako mzee wangu Shaabani Robert
Naamini tunu yako ya tenzi za mashairi zingetumika kama fimbo kutuchapa vijana wa kiafrika ambao tunaishi katika mawazo ya mzungu, tumekuwa watumwa wa fikra, vyakwetu vyanini vya wageni ndio habari ya mjini,

uliwahi kumuona yule mwanamama siti binti saad ukamuandikia kitabu, lakini mwambie sasa mziki wake ambao ndani yake pia ulibeba ujumbe kuntu kwa jamii, hii leo hakuna kitu kama hicho, hatusikilizi kutikisa kichwa nakutunza, sasa hivi tunaruka kama vichaa, tunavua mashati,tunakanyagana nakupiga kelele hovyo, hatuna muelekeo wa muziki wa akili ambao ndani yake una mafumbo yatafakari na ujumbe wakuona mbali,

naadika barua hii nikiwa nalikumbuka shairi lako la ujana, ujana sio rafiki wakudumu, acha nirejee ubeti wa saba wa shairi lile.

7. Wazuri wenye uturi, na mikono yenye hina,
Kila mtu mashuhuri, alipenda kuniona,
Nilifaa kwa shauri, na sasa kauli sina,
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana 

najaribu kupata mwanga wa nini uliwaza mzee wangu mpaka kuandika shairi hili, lakini utu uzima wako unanipa jibu kuwa ulichoandika ulikuwa unakijua hasa, na ni somo kwa vijana kuhakikisha wanajipa muda wakuutumia vema ujana kwa maana hupita na nyuma haurudi tena,

nina mengi sana yakukuambia ndani ya waraka huu, lakini naamini nitakuchosha sababu MUNGU aliyekuumba alishaamua kukupumizisha, lakini nitakuwa sijatenda haki nisipokupa maendeleo ya lugha uliyokuwa ukiipigania nakuiendeleza sana kupitia karma yako,
hivi sasa vijana wamesoma sana, hawajui kuongea kiswahili moja kwa moja bila kuchanganya na kiingereza, linaniuma sana jambo hili lakini jinsi sina kwa sababu hivi sasa sio kama enzi hizo, siku hizi dunia ni kama kijiji.

uwezo sina wakupata kila ulichokiacha kama zawadi ya kipaji ulichojaaliwa lakini mara zote nimekuwa nikijiambiza kuwa vichache nitakavyokuwa navyo kukuhusu nitavilinda, kuviheshimu na kuvijali sana huku nikivipitia  majira yote ya mawio na machweo.

namaliza kuandika waraka huu, nikiwa na dalili yakulia, natazama huu mgongo wa ardhi nagundua kuwa umehifadhi watu wengi waliokuwa na maana katika dunia hii, napata somo kuwa hata mimi siku moja nitahifadhiwa ndani ya mgongo huu, nauona mkono wa mungu wenye maajabu, ambao unaishi nasi kila siku ukitenda maajabu yake, naukabidhi maisha ya taifa lako, lugha yako, na kazi zako, huku nikiukabidhi waraka huu ukufikie na mwisho kabisa nausindikiza na dua itakayokufanya wewe uendelee kulala salama, tena mahala palipo pema peponi. Amin

           wako mtiifu  katika kuenzi Fasihi simulizi nchini Tanzania
                                              Omar Zongo

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »