Kuanzishwa, kuishi na kuanguka kwa Taifa Daladala!


Taifa lenye kila aina ya sifa lakuitwa taifa lenye maendeleo, ajabu haliishi mtu ndani yake, limeumbwa kwa mvuto wa hali ya juu, linavutia ndani na nje, kwa upande wa nje limechorwa maandishi makubwa mbele, maandishi yaliyonakshiwa kwa rangi za bendera ya tiafa hilo, maandishi hayo yanasomeka DALADALA.
Watu wawili wanaonekana wakishangaa uzuri wa taifa hilo, wanastaajabu kwanini taifa zuri kama hilo haliishi watu, wanalisogelea, wanalikagua mwisho wanaambizana
Daladala
            ''tunaweza kuwa viongozi wa taifa hili, tutawakusanya wananchi mbalimbali kutoka maeneo tofauti ya dunia nakuwafanya wawe raia ambao wataishi ndani ya Taifa hili kwa kulipa kodi maalumu, inapoisha wanaachana na taifa letu tunatafuta raia wengine, hii itasaidia kuongoza nchi hii sababu ikitokea hata tunatakiwa tukarabati miundombinu na makaazi ya watu inakuwa ni rahisi kutumia kodi zao''

wanaweka mikakati, kanuni yakuendesha Taifa hilo, wanaridhika mmoja anajipa madaraka ya urais mwengine waziri mkuu, waziri mkuu anasimama mlangoni nakuanza kuita watu, huku aliyejipa cheo cha urais akikalia kiti chake cha enzi, mbele kabisa akizingatia usukani wake na namna atakavyoutumia kuongozea nchi ile, usukani unakuwa ndio katiba yake yakuongoza taifa lile liitwalo daladala.
shughuli yakuwapata raia, wananchi waje kulipia kodi kwenye taifa ile inakuwa ngumu kidogo, waziri mkuu mlangoni anatumia lugha nzuri, kuwalaghai wananchi waweze kuingia kwenye taifa hilo linalotembea. wengi wanahadaika nakuzama ndani kuwa raia halali kwa kulipa kodi zao.

Raia wanaanza kuingia wale wamwanzo, wanawahi makaazi yao na rafiki zao, wengine wanaochelewa wanakosa mahala pakukaa wanasimama kinyonge huku wakimtazama Rais wao wakikosa namna yakumwambia kuwa anawasaidiaje. waziri mkuu mlangoni anaonekana akiwanyanyasa vijana wadogo ambao wamevaa sare wakijitambulisha kuwa wao ni wanafunzi, anawaambia wanatosha hataki wengine.

vijana wale wanajipima nguvu zao na waziri yule aliye mlangoni wanabaini hawamuwezi hata kidogo kwani yeye amewazidi nguvu. kwa unyonge wanamuacha kwa siri kubwa laana ya wanafunzi wale inadokndoka kwenye taifa lile hasa rais wake na waziri wake, lakini wao hawajui wanaendelea kujaza watu...

sababu ya kuwakataa wanafunzi ni kwamba wametosha watu na hakuna nafasi nyengine lakini bado anaonekana akiwaita watu wengine waingie ndani ya Taifa lile, hajali namna ambavyo wamebanana mule ndani mpaka kelele zinaanza kusikika ndani ya taifa hilo HAKUNA NAFASI, JAMANI SITUMETOSHA... BASI SOGEA HUKO, JAMANI WE KAKA UNANIKANYAGA........DEREVA TWENDE.

Raisi wa taifa lile akiwa amekamata katiba yake hajali wala hageuki nyuma kuwatazama raia wake kazi hiyo kamuachia waziri wake ambaye sasa ameanza kuwa na lugha chafu  akiwatukana raia bila kujali aliwaita mwenyewe, rais yeye hasemi kitu lakini kichwanii mwake anajua kuwa taifa lake lina changamoto za sehemu za kukaa watu wakajinafasi bila kubanana na kukanyagana, kichwa chake kinarudi katika historia za mataifa mbalimbali yanayopiganis ardhi lakini hatilii maanani sana anaendelea kunyonganyonga katiba yake ikiwa kama ndio namna yakuendesha nchi ile masikio yake yanafuata sana muongozo kutoka kwa waziri wake, mara kadhaa akiambiwa waache hapo Anaruhusu taifa lile linalozunguka kutafuta abiria lisimame ili liwaache abiria waliokwisha lipa kodi ili kupandisha wengine ambao hawajalipa.

anawaza namna yakuboresha taifa lake ili angalau makaazi yawe mengi raia wake wasipate shida yakukanyagana lakini anakosa hivyo anaona kile anachokifanya waziri wake ni sahihi, bila kujua Masikini ya Mungu wamekusanya laana ya kwanza kutoka kwa wanafunzi ambao wanakosa namna yakufika shuleni kupata haki elimu sababu taifa lile halitaki wanafunzi kisa wanalipa kodi ndogo.

Hapa rais wa taifa hili DALADALA hafikirii kuwa wale ndio marais wa kesho wa kuongoza taifa lile lakini pia wataweza kutumika kubuni mataifa mengine yenye eneo kubwa ambalo raia hawatapata shida kukanyagana nakugombea makaazi kwa kutumia elimu zao.
waziri mkuu mwenye kiburi anawatukana kina mama wafanyabiashara wenye mizigo yao anawaambia kwa kejeli ''hakuna nafasi ya mizigo hiyo''.

kina mama wajasiriamali wengine wajane waume zao wamefariki wanakosa namna yakufanya wanazidi kuchelewa kufika waendako, taifa lile limewakataa, wanazidi kusubiria hifadhi kutoka kwenye taifa lenye waziri mkuu mwenye imani ambalo ni nadra sana kutokea.

ndani ya taifa hili ambalo raia wanachaguliwa mlangoni na waziri mkuu, kuna watu wa ajabu mno, wao wanajiita staff..watu ambao wana ukaribu na rais, wamepata makao huku wazee watu wazima wakiwa wamening'inia, nakukanyagwa bila huruma. hakuna anaewajali taifa linaangalia kodi tu!
hewa nzito, watu ni wengi wapo wajawazito ambao hawapewi haki zao, waziri mkuu bila huruma anachangisha kodi zake huku akiwaambia sogea huko nipite.

Laana inazidi kulikumba taifa hili, laana kutoka kwa wamama watu wazima, watoto, na wazee ambao walihitaji wapishwe kukaa ikibidi hata waishi bure mule lakini matokeo yake wananufaika wachache tu kisa wanajuana na mwenye nchi, mara kadhaa wana usalama wa kimataifa walipojaribu kuisimamisha nakuiwekea vikwazo kwa kufuatilia uhalali na haki pamoja usalama wa wananchi katika nchi hiyo daladala waliambulia kuzungumza kwa siri kubwa na waziri mkuu, halafu hakuna hatua zinazochukuliwa, udhalimu unaendelea, huku sasa jasho la mbanano

likifukuta, na taratibu hofu ya maradhi ya mlipuko kwa kuambukizana ikiianza kutanda miongoni mwa wananchi wa taifa lile.

Daladala
Maisha ndani ya taifa hili lenye waziri mkuu aso na nidhamu yanazidi kuwa magumu kutokana na laana, ghafla kunaibuka mgogoro ndani ya Nchi, raia mmoja kalipa kodi yake waziri mkuu anasema hajalipa, wanajibizana machafuko yanatokea huku waziri mkuu akijinasibu kuwa anaweza kumshusha katika taifa lile, raia anasema nina haki yakuishi humu nakufika niendako sababu nimelipia kodi yangu,

Rais anaona kero vurugu zinazoibuka katika nchi yake anaamua kusimamisha shughuli ya uendeshaji nchi kwa kufuata katiba, raia wanashangaa kwanini Rais asimamishe Taifa lile lisitembee kufika waendako, wote wanadhani labda Mheshimiwa Rais  amekerwa na mivutano ndani ya taifa lake kumbe la hasa! anaonekana akimgeukia Waziri wake " Naomba Buku", rais anaomba pesa watu wote wananyamaza mzozo unasimama kwa muda, moja ya abiria anajisemea " pesa zetu hizi, sijui anaenda kununua nini'' sauti hii inasikika moyoni mwake tu, na hata hivyo anajisemea hivyo huku wazi akijua kuwa hana tena mamlaka na zile pesa sababu alilipia kuishi mule ndani nakufika aendako, waziri mkuu anamkabidhi rais wake noti ya shilingi elfu moja, rais kauzu hacheki hata kidogo, anashuka kukiacha kiti chake cha urais, raia mmoja anatamani kukikalia akiendeshe yeye lakini anahofia watu watamuona fisadi na mwizi.

laana zitokanazo na uonevu na ubabe wa waziri wake mkuu mtendaji wake langoni ndio zimempata hadi yeye, na pale aliamua kwenda kununua na  kunywa kinywaji cha laana Maarufu kwa jina la Kiroba, eti alijiambiza kuwa huenda akinywa kinywaji kile ndio hataona bughda yale makelele ya Wananchi wake.

Raia wake nyuma wanapiga kelele kila mmoja akidai anacheleweshwa kufika aendako. Dereva hajali anapotelea kwenye duka moja lililo pembezoni mwa ramani ya taifa lake. anatumia dakika saba dukani pale,anarudi akiwa ameshika chupa ya maji safi ndani inaonekana ni maji lakini ukweli sio huo, ile  ni pombe kali yenye rangi ya maji lakini ladha ya dawa chungu kama vile muarobaini,
anarudi anakaa kwenye kiti chake cha enzi anakamata tena katiba yake maarufu kwa jina la Usukani, anainyonga nyonga Taifa lile liitwalo Daladala linaanza kuondoka.

Laana  walioachiwa na wazee waliokosa kukirimiwa kwa kupishwa wakae linawakumba Dereva anaanza kuyumba yumba, Abiria wanaanza kupayukwa " hujabeba makopa humu ndani tafadhali bwana endesha taratibu".

Dereva haelewi taratibu kilevi kilishaanza kupenya kwenye mifupa yake ya fahamu, raia walio kaa jirani yake ndio wanagundua kuwa kiongozi wao yule anatumia kilevi, wana patwa na mashaka na uhai wao, hata uendeshaji wa Taifa lile umebadilika, Wanapitisha maamuzi ya busara. wanaambizana washuke.
mmoja anasimama anapaza sauti yake " jamani hawa wanacheza na akili zetu, daladala lenyewe konda hana ustaarabu, dereva wake ndio chizi kabisa amelewa, watoto wadogo kule amewakatalia kupanda wazee hawawathamini wananing'inia kwenye mabomba huku siti zikiwa zimekaliwa na mastaf wao, tushukeni atatuua huyu bwege!'"

Maneno haya yanapokelewa kwa hisia tofauti na raia wote, lakini wote wanaunga mkono hoja ile mwengine anasimama nakusema '' hatuwezi shuka hivihivi lazima waturudishie pesa zetu, wapumbavu hawa, la sivyo tuwapeleke mbele ya sheria,"

Daladala
Umoja huo wa abiria ndani ya Nchi ile Daladala unajenga hofu kwa Waziri mkuu Konda kama vile anashtuka kutoka usingizini, ghafla Daladala inasimama, konda anafungua mlango anataka kukimbia, abiria wanamkamata wanamvuta ndani, wanamshambulia wakitaka awarudishie pesa, wanamkalia kooni nakufanikiwa kumpokonya pesa zote,wale awananchi waliokuwa wakijita mastaf wanashindwa kutetea kutokana na umoja wa raia wale wenye hasira kali. zoezi la dakika chache tu wanafanikiwa kumpokonya pesa zote yule waziri mkuu, mjeuri.
wanashuka,kwenye gari wanabaki konda na Dereva wake na vijana wawili waliojiita mastaf, Konda anajikagua anagundua sare zake za uwaziri mkuu zimechanwa chanwa, akijikagua zaidi anagundua hakuachwa hata na shilingi hamsini, anamtazama Dereva wake, hana habari, anasinzia kutokana na viroba anavyoendelea kujidunga navyo.

"umeyataka wewe, ona sasa! tumetumia mafuta ya bure kuendeshea daladala, hatujarudisha kitu, wamechukua pesa zao, acha mimi niendeshe hii gari, wewe kaa mlangoni,"
 dereva hajielewi anakubaliana na hoja hiyo, huku akipepesuka anasoge mlangoni, yule waziri mkuu mjeuri, anakalia kiti cha kuendeshea taifa lile, sio mzoefu na masuala ya uongozi, anajipa moyo kwamba ataweza, anafanikiwa kuwasha gari, linawaka, anaanza safari, wanafanikiwa kutembea kidogo tu, abiria wanakataa kupanda gari linayumba muendeshaji sio mzoefu, konda amelewa hawaiti kistaarabu, Dereva ambaye alikuwa waziri mkuu anaamua kurudisha Daladala walipotoka lakini wakati akijaribu kukunja kona arudi alipotoka anakumbana uso kwa uso na gari kubwa, ajali isiyoesemeka, wanagongana uso kwa uso,  Daladala lao linaminywa hakuna anaefanikiwa kutoka mzima,

 wengi wanaoshuhudia ajali ile wanasema kosa lilikuwa kwa dereva hakustahuili kugeuzia pale kwa maana sio mahala pakugeuzia,

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »