Ni Kama Nyota

Majira yanabadilika, kuna muda anga linameremeta kwa uangavu wa jua, huku likiwa na matokeo ya joto kali na mvuke wa moto utokanao na hasira za kuwaka kwa jua hilo!

sijui lakini naamini kuna maana ya jua kuwaka mchana na watu kuhitajika wafanye kazi mchana ili kukamilisha ule msemo usemao, mtatafuta kwa jasho, ikiwa na mantiki ya kwamba hata kama kazi yako itakuwa ya kukaa tu, lakini kutokana na ukali wa jua lazima jasho likutoke labda kwa wale wenye viyoyozi katika maeneo yao ya kazi, lakini muda wote jua halitishwi wala kubabaishwa lenyewe linawaka tu na ukithubutu utoke nje utakutana nalo!.

lengo sikulisakama jua, la hasha!

lengo langu nikuzungumzia majira yanavyobadilika, kuna muda ukitazama anga utagundua kuwa halipo tena jua, giza linakuwa limetanda kote na anga lote linapambwa na vimeremeta vyenye kupendeza na huwa vingi sana angani, na kama ukivitazama kwa hisia kali lazima neno litakutoka, neno lakupongeza kazi ya MUNGU. kazi ambayo hufanyika kwa siri kubwa hivyo kuongeza maajabu katika tafakuri yako.

lakini ukiwa unatazama zaidi angani muda huo utagundua kuwa vimeremeta hivyo vinavyotambulika kama nyota vinatofautiana kwa kuwaka, ukipata muda tazama kwa umakini utaona zipo nyota ambazo huwaka zaidi na mwanga wake huonekana kuwa na nguvu kuliko nyota nyengine ya jirani yake, lakini utofauti huo wakuwaka haubadilishi jina la nyota zote zinaitwa nyota,

Ni kama Nyota
safari ya maelezo yangu inaelekea mwisho kwa kusadiki kichwa cha habari ya maelezo haya 'Ni kama Nyota' ndiyo wala hakuna tofauti maisha yetu sisi binadamu ni kama nyota angani, wapo ambao wanang'ara na wala hupati shida kubaini hilo pindi tu unapomuona unahisi ni rafiki, unatamani kuongea nae, unamuamini kwa haraka unamdhamini na hata unaweza kumpa chochote akiongea nawe na akaonesha nia thabiti ya kuhitaji kitu hicho. 

huyu hana tofauti na nyota zile zinazong'aa angani, na yupo tofauti kabisa na ambaye  hajengi mvuto wa aina yoyote kwa mtu, hata ukikutana nae haraka unajikuta unamdharau, kwa kujipa majibu ya hawezi, sio rafiki, wakazi gani na mengine mengi tu yakumshusha sababu tu hajajenga mvuto katika macho yako wala hajang'ara.

unaweza kumuona mbaya, havutii, mwizi, hana ushawishi wala hawezi kukusaidia chochote, hata ikitokea amekufanyia kitu kizuri, unahisi hastahili kupongezwa nawe, ni dhalili, fakiri na anakushusha kuwa nawe karibu, unamuona yupo chini yako, wewe una thamani kubwa kuliko yeye, unamuona anafaa kuwa mtumishi wako, NI KAMA NYOTA, huyu ni aina ya nyota isiyong'aa!

lakini suala la msingi zote ni nyota, na anga inapendezeshwa zaidi na nyota za aina mbili, zenye kung'aa sana, na zenye kung'aa kwa kufifia, nyota hizi ndizo zinakamilisha anga la nyota ambalo hukumbatwa na usiku wa kiza wenye kujenga ladha ya usingizi kwa wanadamu.

najaribu kulitathimi  Anga lenye nyota zooote zenye kung'aa, nikiri kwamba sijawahi kuliona, na kama siku likitokea usiku huo utakuwa wa ajabu na una upekee ndani yake, sitaki kusema kama anga hilo litapendeza ama la! labda siku ikitokea tutajionea,

Ni kama nyota, unapaswa kutambua hili, unapaswa kujijua wewe ni aina gani ya nyota, na hata kama ukibaini kuwa wewe ni dhalili mbele ya wengine, huna thamani wala hujengi mvuto kwa yoyote, hupongezwi wala ile thamani yako ambayo wewe mwenyewe unaamini ipo ndani yako lakini wengine hawaitambua usijisikie hovyo, tambua kuwa macho yanatofautiana,

Naamini mimi na wewe tukisimama usiku kutazama angani, nyota ambayo itajenga mvuto kwako pengine mimi inaweza isinijengee mvuto huo, hivyo tambua kuwa hatua zako unazopiga katika maisha unaweza usikutane na mtu akakupokea kwa shangwe, lakini amini kadiri unavyoendelea kupiga hatua utajikuta anajitokeza mtu tena mwenye thamani kubwa kuliko uliowahi kukutana nao, atakupokea, atakukirimu, atakukaribisha kwa tabasamu linaloimba shairi lenye kupendeza, lenye maneno yanayofariji na atakupamba kwa marashi yakunukia, atakufuta dharau zote uliozopakwa,
atakupangusa mikosi yote yakupuuzwa na atakukalisha kwenye kiti cha enzi,

Ni kama nyota lakini macho yetu yanatofautiana, wapo wenye uwezo wakuona mbali, na wapo wenye uwezo wakuona karibu, wakijitokeza wengi wasiione thamani yako, tambua atajitokeza mmoja tu mwenye thamani kuwazidi wote na akakupa vyeo vyote vinavyopita heshima ya ufalme,
umeumbwa kwa sababu, usiache kuiamni sauti inayokwambia kuwa wewe ni wapekee, na wewe ni mbora, amini hivyo mitazamo ya watu kamwe isikurudishe nyuma, macho yao ndio yana matatizo wewe umeumbwa vizuri, ni kweli hakuna mkamilifu, lakini mapungufu yako wewe sio sababu ya wao kuendelea kukushusha...uliumbwa hivyo ulivyo kwa sababu, 

usichoke kuitafuta sababu hiyo.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »