NILIWAHI

Niko ndani chumbani, ugenini,gizani, najihisi mpweke, aliyezima taa sijakua nae, simjui nimekutana nae ukubwani, nakumbuka utotoni niliwahi kuzoeana na mtu kama yeye lakini sio yeye, nabaini kuwa kila siku iitwayo leo hili neno niliwahi linaendelea kunizoea sababu naweka historia ya mambo mengi ambayo nayapitia
Nakumbuka vizuri kabisa kuwa niliwahi kuwa na wazazi, baba na mama yangu, alianza kufariki baba nikabaki na mama na mara zote nilikuwa najiambia kuwa niliwahi kuwa na baba, maisha yameenda sana hii leo sina mama, najiambia tena kuwa niliwahi kuwa na mama sababu sipo nae tena,
Niliwahi kulia nakubembelezwa kwa upendo huku nikiulizwa unataka nini mtoto, lakini sasa hivi imebaki simulizi tu na huku nikijiwazia mwenyewe kwa kusema kuwa niliwahi kupitia maisha hayo,
Niliwahi kuwa na ndugu zangu walinijali kama mdogo wao, kipindi hicho nasoma walihakikisha sikosi kitu na walinitetea pale nilipokuwa naonewa, lakini sasa hivi imebaki kumbukumbu tu  na nakubali kuwa kipindi kile familia ile iliunganishwa na wazazi wetu na sasa hivi kila mmoja ana familia yake yaani kaka zangu sasa ivi wameshakuwa mababa wa familia zao, na dada zangu wameshakuwa wake wa mtu Fulani na pia ni ma mama wa familia zao,
Nakumbuka sana kuwa niliwahi kuwa nanunuliwa nguo, chakula na kupewa hata mahala pakulala, lakini sasa hivi naita ni mapito na hata sikumbuki tena mambo hayo kufanyiwa mara ya mwisho ni lini,
Niliwahi kuwa na shida nikamlilia mama yangu, niliwahi kukosa nauli nikawaomba ndugu zangu, na niliwahi kutamani ukubwa bila kujua kuwa siku moja nitakuja kuukumbuka udogo.
Dah siamini kabisa kuwa niliwahi kuwa na marafiki wengi ambao tulikuwa tukifuatana kila mahali, lakini wako wapi sasa, kila mmoja ana familia yake, niliwahi kulaumu sana wazazi walipokuwa wananiambia kuwa nisubirie wakipata pesa wataninunulia kitu flani, nilihisi wanafanya makusudi , nakiri sasa sikuwa najua,niliwahi kuwa mjinga!
Niliwahi kutamani kuyaanza maisha nikiamnini kuwa  nimepesi mno, nakiri sasa kuwa nilipotea sana, nilikuwa mfupi mno, mfupi wa fikra!
Nakumbuka niliwahi kuwa na mpenzi wangu wakwanza kabisa katika mapenzi, nikamuona yeye ni wamuhimu kuliko hata elimu yangu, nikawa natumia muda mwingi kuwa nae huku wenzangu wakiwa darasani,  niliwahi kujidanganya kuwa huyu ndie waubavu wangu, nikadharau wazazi na ushauri wao, nikapuuzia masomo nakuyavalia njuga mapenzi nikiyaona ndio kitu pekee cha faraja duniani, nakumbuka mwisho wake niliambulia kuvunjika guu, sababu sikusikia ya mkuu, hivi sasa yeye ana maisha yake na wapenzi wake na mimi niko na maisha yangu huku muda huu nikikumbuka kuwa niliwahi kuhadaika kipindi Fulani na huyu kiumbe hatari aitwae  Balehe, niliwahi kuwa mtumwa, mtumwa wa mapenzi!
Niliwahi kuwaza maisha bila Mama yangu, maisha ambayo nayaishi hivi sasa wakati nilikuwa naamini kuwa hayawezekani, kwakweli nimewahi mambo mengi sana ambayo yananiimarisha ili niwe nyani mzee niliyekwepa mishale mingi, na niweze kuja kuwasimulia wajukuu zangu kuwa Niliwahi kitu Fulani aidha kwa kuwaza au kutenda, lakini niliwahi!
Naumia sana muda huu nikiwaza hayo niliyowahi kuyatenda , nakuyawaza, yote yamebaki story, niko mpweke sina rafiki niliyekuwa nae, mpenzi niliyeanzana nae wala mzazi niliyempenda kwa dhati, sina yeyote ambaye nilikuwa nae muda mwingi nikijadili nae masuala mengi ya mbele, najiona mimi pekee kwenye safari hii, wengi ni wapya ambao nao naamini nitakuja kuwafikiria kuwa niliwahi kukutana nao…
Simulizi ya maisha ina ladha mbili, chungu na tamu, ulimi wako unapaswa kujiandaa kuonja ladha hizo zote huku ukitambua kuwa maisha ni hatua inayojipiga yenyewe huku ikikuachia alama ya kumbukumbu, wako wapi uliokuwa nao mwanzo, yako wapi ulioyawaza mwanzo, na kwanini kila siku wanajitokeza watu wapya katika maisha yako na mambo mapya katika maisha yako, maisha yana maana kubwa na ni wajibu wa kila mtu kuishi kwa akili, wema na upendo ili ukiwaza yote uliyowahi kuyapitia ujikute unatabasamu, huku ukiamini kuwa uliyewahi kukutana nae pia huko aliko anatabasamu kila anapokukumbuka…

MIMI NILIWAHI KUWAZA IPO SIKU UTAYAAMINI MAWAZO YANGU  NAKUYAISHI SABABU YALISHAWEKEWE BARAKA NA TUNU YA PEKEE NA MUNGU MUWEZA!
NILIWAHI
ZONGO

MREXPERIENCE

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »