KWAHERI 2016 ; SHAIRI


Ni mbali ulipotoka
kamili umekamilika
tamati imeshafika
wajibu kukuimbia

safari si lelemama
mengi tumeyaona
mengine yametuuma
ni wewe umetuletea

sifayo sasa ukongwe
ujana hunao tena
yakupasa tu uende
andiko limetimia

wapo wenye simanzi
umewaachia jeraha
uliwatoa machozi
ishawekwa historia

tamu yako na shubiri
vyote tumeviona
umekuwa mashuhuri
jua kupatwa mchana

tetemeko la kagera
tanzia tanzania
umetutia hasara
uendapo salimia

kifo kilifanya yake
mwaka ni mrefu sana
hivyo ni desturi yake
sote twaelekea

furushi lako la rushwa
rudi nalo jeupe
sasa utawala mpya
hauitaji uzembe

Tunza macho ya Side
scopion alikupa
hongera pia kwa ubabe
kumuua rais wa Cuba

Miili ile mtoni
waijua siri yake
na vipi kuhusu John
Faru kufichwa kwake

Afrika ya upinzani
viongozi kushika dola
Uchaguzi Marekani
Trumpel Mr. Hongera.

Mitandao imeonyesha
walimu wagawa dozi
wanafunzi Na shisha
Hawaishi uchokozi

 maisha na mziki
usukuni weka pembeni
dereva kumbe shabiki
Roho zetu mkononi

vazi lako la ugeni
kwasasa halikutoshi
mvike huyo mgeni
mwambie twamngojea

Mhisani naweka nukta
ishara nimeishiwa
nimengi umeyaleta
lakini sijakwambia.
uendapo ukifika
waambie twasalimia.

Mama Mwenye Taadhima ; Shairi

Mama Yangu
Mama malkia,thamani yake sijaona
Mafunzo alonigea, busara na hekima.
nani wakufikia, heshima yake mama,
Salamu hizi pokea, mama mwenye taadhima.

maovu yangu mkuki, hukita moyoni mwako.
Hupigwa taharuki, kusema na mola wako.
yasinifike mauti, iponywe damu yako.
mama wewe  asali, utamu undani yako.

Mama, neno tamu, upendo wake hudumu
najawa na Tabasamu, jinale halishi hamu,
kiumbe maalumu, kaumbwa kitaalamu
ninani asofahamu huyu mama ni adhimu

itachora jina mama, ikimwagika hii damu!
namimi nitalisoma, kwa utashi na nidhamu,
kughilibu nitagoma, laana yake ni sumu
Nikikosa nitasema, Nisamehe sana mama.

Ungali bado wazoni, ingawa u kaburini
ila bado naamini upo mwangu maungoni
mwenginewe simuoni, wafaraja maishani
Penye kosa nakuomba nisamehe sana mama.

kipindi tungali sote, hukunifunza  ujinga
Ilipangwa uondoke, ningewezaje kupinga
si kwamba niadhirike, Mungu bingwa wakupanga
ujumbe wangu ufike, mwanao anakupenda.

mwisho wa huu utenzi unakaribia hapa
sio mwisho wakuenzi,mazuri yako mahaba,
sijayaona mapenzi kama yako na ya baba..
vifo vyenu majonzi, uyatima wanikaba....

THAMANI YA WAZAZI

Naitwa Omar Bin Zongo, wakati mwengine hua napenda kujiita Bin Zongo sababu yakufananisha thamani ya kilichopo ndani yangu na mimi maana mara zote umbile langu halifanani na busara zangu labda pengine nikimtanguliza baba yangu mbele watu watasema amerithi kwa huyo Zongo.

najivunia zaidi na napenda ukiniita Bin Zongo...

leo nina ujumbe maridhawa nataka kukugea.

Baba yangu alifariki dunia mwaka 1995 mimi nikiwa mdogo sana siijui hata sauti ya mzazi wangu huyo wakiume.

mama yangu amefariki mwaka 2014 nikiwa na ufahamu wangu hakika maumivu ya kifo chake bado yangali moyoni mwangu.

kuanzia mwaka huo wa 2014 niliishi bila ile nguvu ya faraja itokanayo na kujua kuwa mama au baba yupo nyuma ya hatua zako.

hakuna faraja inayofariji kwa kiwango kikubwa sana duniani kama faraja ile yakukutana na magumu ukahisi mama au baba yako atasimama kwako kwa ushauri na hata muongozo mwengine wowote utakaokuwa unauhitaji kutoka kwao.

hiyo ndio nguvu itokanayo na tumaini la kujua kuwa wazazi wako wapo duniani.

leo ujumbe wangu unazungumzia thamani na umuhimu wa wazazi hapa duniani.
hakika nakuambia hakuna wivu uumizao kama wivu wakumuona rafiki au jirani yako anakumbatiwa nakufurahi na wazazi wake ilihali wewe wakwako walishapotea katika uso wa dunia hii na hakuna hata bahati mbaya ya wewe kuonana nao tena.
hakuna wivu unaojeruhi ngome ya furaha kama unaposikia mtu amefanyiwa kitu flan na baba au mama yake, au kwenye hafla wewe umeenda mwenyewe lakini wenzako woote waliohuduria kila mmoja ameenda na wazazi wake, wanacheka nakufurahi huku kila mmoja akionekana amepambwa na tumaini la kuwa na wazazi wake maishani.

naamini Mara zote Rabbuka hamtupi mkono mtu mpweke duniani humfariji kwa siri nakumfanya atangamane na wengine bila kuonesha dalili yoyote yakuwakumbuka wazazi wake lkn ni ukweli iliofichika kuwa kumbukumbu za wapendwa wazazi wake lazima zinajirudia nakumtonesha kidonda kisichopona chakuondokewa na watu hao muhimu zaidi duniani.

kuna dawa gani yenye uwezo wakufuta kovu la kuondokewa na wazazi hapa duniani?

jibu ni hakuna na kama ipo basi ni usingizi ambao hukujia kwa muda fulani tu na ukishtuka kovu hilo lingali bado nawe.

nakumbuka nilimwambia rafiki yangu mmoja aitwae Kaijage dakika chache tu baada yakutoka ofisini kwa baba yake Mzee Kabanza.

nilimwambia kwa mtindo wa ujana zaidi utani ukiwa mwingi lakini nilihitaji sana anielewe na azingatie ninachomwambia.

nilimwambia mimi sio mtu wakawaida kaijage nadhani hilo unalijua sasa naomba uzingatie ninachokwambia.

mwenzako mimi sina baba wala pia sina mama, najua madhila ya upweke yatokanayo na kuwakosa watu hawa.
nilimwambia kuwa mimi niko tofauti nayeye sababu mimi nimekosa wazazi yeye anao tena shukrani kwa mola alijaaliwa kuwa nao wote wazazi wenye furaha ambao nilijifaghiri sana kufahamiana nao na nakumbuka niliwaambia nawapenda muda mchache tu nilipoonana nao.

nakumbuka nilimwambia Kaijage asifanye hata kosa la bahati mbaya kuwaudhi wazazi wake.nilimsisitiza kuwapenda sana nakujitoa maisha yake yote kuwatazama wazazi wake kwa jicho lakuwatengenezea furaha na wajivunie kuwa wazazi.

nakumbuka nilimwambia kaijage, ni kijana mwenzangu ambaye tulizoeana sana na urafiki wetu uligeuka kuwa udugu.

na nakumbuka vema kipindi namueleza hayo nilivunja ratiba zangu zote Dar ili kwenda Tanga nyumbani kwao kulikuwa na shughuli ya komunio kwa mdogo wake aitwae Jenifer.

nakumbuka nilipita ardhi ya muheza kama sipajui, ardhi ambayo ulihifadhiwa mwili wa Mama yangu! nakumbuka wakati napita muheza niliumiza sana niliporejea nyuma kimawazo nakukumbuka malezi aliyonipa mama yangu juu ya ardhi nyekundu ya wilaya ile.

nakumbuka vema nilimwambia kaijage na kumkazia sauti hasa pale alipoleta utani wakati me nazungumza kumueleza umuhimu wakuwajali wazazi wake.

nilimsisitiza sana asiuchezee ule muda ambao yeye na wazazi wake wote wana pumzi. nilimwambia achunge ulimi wake anapozungumza nao, matendo yake anapokuwa mbele yao na mara zote apige goti kuwaombea afya n uzima wazazi wake wale.
kaijage nilimwambia haya muda mchache tu kabla yakupanda gari lakurudi dar huku yeye akiahidi kuendelea kuwa tanga kwa siku mbili zaidi.

nilipanda gari nikafunga mkanda nakuanza kuombea safari kabla haijaanza kisha nikaanza kurejea ukarimu ucheshi na upendo wa wazazi wake Kaijage.

hakika nilibaini kuwa wale ni mfano wazazi wote duniani! ni hapa ndipo pia nilipomkumbuka marehemu Mzee Zongo na Mama yangu, ni hapa ndipo kwa mara nyengine nikaumia tena sababu yakubaini mimi sina wazazi.
ona thamani ya wazazi wako rafiki yangu, wapende kwa maisha yako yote, waheshimu kwa akili yako yote na ujitoe kwao kusimamia furaha na amani ya nafsi zao.

ile nukta unayobaini yupo baba na mama yako basi itumie kuwajulia hali hata kama upo mbali nao,

kutwa nzima jiwekee ratiba yakufurahia nao wafanye wahisi upo karibu nao kwa kujadiliana nayo masuala mbalimbali yanayojiri kitaifa na kimataifa.

watanie, waombe ushauri wafanye waione thamani yao, kamwe usifanye kosa hata kwa bahati mbaya kuwaudhi maana nafsi yako itakuja jutia siku moja.

mimi tangu nikose mama duniani, ninapokutana na mama wa mwenzangu namuita mama kwa kumaanisha ili walau niikate kiu yangu yakuita jina hilo.
 hakuna maumivu yanayoumiza kama unapoona mtu anamkaripia mzazi wake, anamdharau nakumpuuza,

unaumia sababu ni wewe pekee ndio unajua kuwa yule hajui atendalo, anachezea muda ambao yatima wanautamani wautumie vizuri kuonesha taadhima yao mbele ya wazazi wao.

tumia vema muda ule ambao unabaini kulia kwako yupo mama na kushoto kwako yupo baba,

pia shukuru Mungu hata kwa kukupa mzazi mmoja wapo kati ya hao muombee mmoja aliyetangulia apumzike kwa amani na uliyebaki naye muoneshe thamani yake na aione furaha unayoitafuta kwa ajili yake.
kwa wewe ambaye una mgogoro wa nafsi kutokana na makosa aliyowahi kukukosea mzazi wako au anayokukosea sasa piga goti muombe MUNGU akupe ujasiri wakumsamehe mzazi wako na huyo huyo mungu muombe amnyooshe mzazi wako,

kwa wewe uliyewakosa wazazi wote piga goti pamoja nami muda huu kwa sauti ya upole na unyenyekevu tuzungumze maneno haya kwa MUNGU wetu
Asante mungu kwa kuwachukua wazazi wangu, nakushukuru sababu haukosei katika mipango yako wewe ni mkamilifu, nina ombi moja mola wangu ambalo hua nalirudia sana hasa ninapowakumbuka wao, ombi lakuwasamehe dhambi zao nakuwahurumia kwa kuwapunguzia adhabu zako, wahurumie sababu ni wao ndio walikuwa wakinihurumia enzi za utoto wangu,
ni wewe ndio mungu unaejua maumivu gani hua nayapata kila nikiwakumbuka wao nakuomba uzidi kunipa faraja niweze ishi bila kufarijiwa na upendo wao.

watunze vema wazazi wa rafiki zangu duniani kote maana kwa sasa ni wao ndio wazazi wangu ninaojivunia nao kwa kuwaita mama nakuwaomba ushauri inapobidi.

ahsante Mungu na nisamehe makosa yangu nami daima niwe mzazi mwema kwa watoto wangu na wa wenzangu! nifanye niwe mzazi ambaye watoto wangu hawatakuja kulilia jina langu kwa mateso ya mama yao.
na kukabidhi amani ya wazazi wote duniani na walinde wewe kwa malaika wakowatukufu amin...

NIMEGHAFIRIKA



Allah mkarimu sana, ana nifanya nahema
Nakushukuru kwa sana, kunijazia neema
Wewe uliye bayana, hutujuza baya  jema
Dunia tambala gani, na nimeghafirika

Sikio lazidi kichwa, wahenga hawapo tena
Vibiongo  vimefichwa, uwazi haupo tena
Vinaliwa tu na mchwa, kwasababu ya  hiyana
Dunia tambala gani, na nimeghafirika

Wanaitana  vyumbani, mda wa kula fikapo
Kwa minong’ono ya chini, wanafungua makopo
Na tena pasipo soni, wanazizuia  pepo
Dunia tambala gani, na nimeghafirika

Dunia sio tambala, halifai hata dekio
Ukizubaa kulala, utabaki na masikio
Pima umri kabla, ni mingapi masalio
Dunia tambala gani, na nimeghafirika

Msikia la mkuu, nini amefaidika
Amevunjika guu, au hakukumbuka
Kuhesabu toka juu, kukwepa kughadhabika
Dunia tambala gani, na nimeghafirika

Hiyari ni ndoto njema, ukiiota mchana
Uking’amua mapema, achana na kubishana
Ya nini ukilema, kwa yasiyo na maana
Dunia tambala gani, na nimeghafirika


By Fulgence Makayula





UMEPATA KILICHO BORA 2016?

 Na Omar Zongo
+255 782181862 (watsap)

Kwa wale marafiki zangu wapya wa mitandao ya kijamii, wasikilizaji wangu wapya wa redio mlimani na wasomaji wangu wapya wa SIMULIZI ZINAISHI naamini ni ninyi pekee ndio mnaweza mkawa hamuijui hulka yangu ya kuongozwa na msemo katika kila mwaka!

wale wandani wangu wakitambo sina shaka hata ukitaka wakumbushie mwaka huu mkongwe wa 2016 tumeongozwa na msemo gani watakwambia tena kwa furaha "tunastahili kilicho bora 2016".

mwaka unaisha bado hulka yangu ingali hai mwaka ujao tutaongozwa na kauli nyengine chanya itakayotufanya tuwe na amani kwa mwaka mzima.

kabla sijaenda kukupasha kwa vipi mwaka huu tulistahili kilicho bora acha nikumbushie misemo ya miaka yanyuma kidogo ili twende sawa kwako wewe damu yangu ngeni. nitaanzia
mwaka 2015 ilikuwa ni CHAGUA KUWA MWEMA na hakika tulikuwa wema haswa nachelea kusema mpaka sasa chembechembe za wema zingali damuni mwangu, hakika nakwambia sijawahi kujutia kuchagua njia ile.

mwaka 2016 ilikuwa ni UNASTAHILI KILICHO BORA 2016 hakika ukiwa mwema zao lake la pekee ni kuishi katika ubora wa kila kitu hakika nakwambia mwaka huu babu unaisha nikiwa na vingi vya ubora.
moja ya faida yakuhitaji kilicho bora mwaka 2016 nikwamba nilipoteza vyote visivyo na ubora nakupata vilivyo bora hakika nakwambia mwaka huu unaisha nikiwa na kitu mpaka watu bora kabisa. ahsante MUNGU wangu.
swali linabaki je mwaka 2017 ni msemo gani kuntu!?????

nitauweka tu acha kwanza tuupe salamu zetu mwaka huu ili ukifika huko uendako ukasalimie miaka mingine iliyokuja kisha ikaondoka kama hivi

kwangu mimi mwaka 2016 ni mwaka ambao nilibahatika kutuma barua ya mwaka kwa nguli wa mashairi na Riwaya. baba wa kiswahili marehemu Sheikh Shaaban Robert.

iliniwia ngumu kuvaa uhusika wa mswahili nitakayeweza kumuandikia barua mwenye kiswahili chake akanielewa, lakini nashukuru barua ile niliituma malaika wema wakamfikishia! Sheikh Shaaban Robert akaisoma na hakika akanijibu tena sio jibu kavu akanijibu huku ametaba
samu.

kama ndani ya mwaka 2016 hujazisoma barua niliyomuandikia na ile aliyonijibu basi fanya hima uzisome kwenye youtube chanel yangu https://www.youtube.com/results?search_query=simulizi+zinaishi

haya ni machache kati ya yale makubwa yenye ubora tuliyoyastahili kwa mwaka huu mkongwe unaotuaga.
watsap simulizi imeuza simulizi za sauti nyingi zaidi kama hujajiunga na group hili nitupie tu namba yako mana utakuwa umekosa kilicho bora pia kwa upande huo.
watsap simulizi namba yake +255 782181862
swali linabaki moja tu vipi tunapaswa tuishi mwaka 2017 baada yakupata kilichobora mwaka 2016.....??

njia nzuri ipo....muongozo upo...muda ukifika tutaachia msemo mpya wa mwaka mpya  2017!

ahsante Mungu kwa kila kitu....makosa yapo lakini ni busara kusameheana jamani tusameheane tulipokwazana!

najua kama mimi nilivyomaliza mwaka 2014 kwa pigo lakuondokewa na mama yangu kipenzi basi hata mwaka huu unaisha akiwepo mtu aliyepoteza mzazi, ndugu, mpenzi au mtu yoyote wakaribu yake nikianza kwangu naipa pole nafsi yangu kisha naipa pole na nafsi yako! MUNGU ana makusudio yake katika maisha inakubidi kuishi kwa furaha tu haijalishi nini umekutana nacho ndani ya mwaka huu

namaliza mwaka huu na ujumbe huu wa neno la kihindi "kal hoo na ho"
ishi kwa ukamilifu na furaha kwenye muda ulio nao sababu HAKUNA AIJUAE KESHO 'Kal hoo na ho'. shar rukh khan

KWAHERI 2016
HAKIKA TULISTAHILI KILICHO BORA!

UTOTO ; SHAIRI

Na. Bin Zongo

utoto upofu,
huyaoni ya dunia,
hupenda  unyoofu,
yakipinda huchukia,
utoto mapungufu,
 wazazi huvumilia.
utoto kumbe ni hivi,
mama yangu nisamehe.

nisamehe mama yangu,
hakika nilikuudhi.
enzi za utoto wangu,
sikuitaka ajizi
nilipotaka jambo langu
ulipaswa kulikidhi,
sikuyajali machungu
 poleni sana wazazi.

poleni sana walezi,
 nyie adha mwazijua
nimekua siku hizi
 namie nayatambua,
mgumu sana ulezi,
 watoto wanasumbua
hasa wasiku hizi,
utajuta kuwajua.

Utajuta kuwajua
 watakacho ndicho hicho
werevu wasotambua
kama huna ama unacho
wataanza kulilia
 ukileta kiinimacho
wamezaliwa wanajua
hawataki danganya toto.

mabingwa wakuchagua
kipikwe chakula gani,
nawewe utaangalia,
wakitazama katuni,
mada zao kuchangia
 itakupasa ukiwa nyumbani.
wao ndio hudatia
nyumba yote nje ndani.

niwao ndio mabosi
wewe kijakazi wao,
kukusaidia kazi
 ni mpaka hiyari yao
haweshi ulalamishi
wakitaka jambo lao
utoto kweli ni ukwasi
ukata umbali nao.

nikama vile wanajua
 ufalme wote niwao.
haweshi kujitanua,
utoto kwao ni ngao.
hutumia kulia lia
kupata walitakalo.
maisha yametimia
kwao siyo hua ndio.


MASIKINI SINA CHANGU ; SHAIRI

Na Bin Zongo.

msimu ndio huu
msimu wa siku kuu
msimu wenye makuu
masikini sina changu.

msimu wa usaliti
msimu watashtiti
msimu wa yakuti
masikini sina changu

msimu flani wa adha
fahari na nyingi bugdha
msimu wakuumiza
masikini sina changu

msimu wakupendeza
msimu wakuchombeza
msimu wakuumiza
masikini sina changu

msimu huu wataka
kula kunywa nakusaza
na pesa zakusakata
masikini sina changu

msimu wanisaliti
wahuba hanitaki
ataka mlimani city
masikini sina changu

mavazi ya kifahari
ataka kupanda meli
visiwani kuvinjari
masikini sina changu

msimu wataka nyama
kama samaki jodari
mfukoni pesa sina
masikini sina changu

mialiko nayo mingi
tatizo langu nauli
hali yangu siipingi
masikini sina changu

gharika limenipiga
katika mifuko yangu
ukata umenizonga
masikini sina changu

msimu huu adimu
wafaa kupokelewa
ila pesa ni muhimu
masikini sina changu

wazuri wote mashem
mie nitawapa nini
sina pakwenda sehem
masikini sina changu

mivinyo yakila aina
clabu yapatikana
tatizo pesa sina
masikini sina changu

melala kama mgonjwa
mialiko nakataa
hali ngumu yaniponza
masikini sina changu

menuniwa na azizi
wahuba wangu mpenzi
kosa langu sina benzi
masikini sina changu

alitaka kuzunguka
viwanja vyote kufika
msimu kufurahika
masikini sina changu

tatizo kukosa vocha
na pesa ya bajaji
mwenzenu yamenifika
masikini sina changu

hii hali kwani vepe
mbona napata mapepe
mie pekee au wote
masikini sina changu

huu upole sio wangu
hali ya uchumi wangu
ndio yanipa machungu
masikini sina changu

Siku kuu shikamoo
masikini umenipatia
nabaki kusema loh!
masikini sina changu.

ANGUKO; SHAIRI



Nina ipata faraja, kwa pendo la maulana
Sina gumizi kutaja, kwa nguvu za Subuhana
Na giza likisha kuja, kimbilio kwa Rabana
Mbishi hana ujanja, kauli yao ya jana

Kumbukumbu sifa njema, sipokupa maumivu
Ukikumbuka kilema, na ukalishika kovu
Mwili utakuzizima, na kupata ukamavu
Mbishi hana ujanja, kauli yao ya jana


Vunjiko kuu la moyo, halinipi majutio
Mengi yavunjikayo, nayaziba masikio
Ninayafuata hayo, kupata mafanikio
Mbishi hana ujanja, kauli yao ya jana

Mimi  wa kuvaa moja,siwezi lilia mbili
Ninavikwepa vioja, wanione  wa akili
Naliuita umoja, wakaja tukajadili
Mbishi hana ujanja, kauli yao ya jana


Tukasemezana kucha, lakini hawaku afiki
Walifunga na mabucha, utii wa kinafiki
Walibaki kula kucha, ni njia za kizandiki
Mbishi hana ujanja, kauli yao ya jana


Wakabomoa daraja, lilo jengwa vitabuni
Na bado wana bwabwaja, hawajui nina  nini
Wananiona buwaja, mzamaji wa ziwani
Mbishi hana ujanja, kauli yao ya jana


Zile ngumi za fahari,na  nyika zikaumia
Kwa yangu tafakari, aridhi zakaukia
Kutulambisha shubiri, huku watupulizia
Mbishi hana ujanja, kauli yao ya jana

By  Fulgence Makayula


CHOZI LAKO ; SHAIRI



Naitafakari siku, ilivyoishia vema
Tena Kwa nyingi shauku, nilitamani kusema
Na hali yangu kapuku, akili ikazizima
Asante kwa chozi lako, nimeijua  thamani

Anililiaye nani, kwa uchungu wa mapendo
Nalijihisi katuni, tena nisiye vishindo
Nitesekae jangwani, nisipate maji fundo
Asante kwa chozi lako, nimeijua  thamani

Kutangatanga msafiri, nisietua mizigo
Ninazipanga safari, zilizo nyingi mitego
Sasa natafakari, ingawa mekupa zogo
Asante kwa chozi lako, nimeijua  thamani
Neno gani nikwambie, huenda ukaelewa
Unisikilize mie, tayari nimechachawa
Ububu nijivikie, usije ona melewa
Asante kwa chozi lako, nimeijua  thamani
Nalikutoa machozi, na wala sikukufuta
Yalidondoka kwe ngozi, hukutaka kupukuta
Nilijifanya ajizi, nisiyejua chakufata
Asante kwa chozi lako, nimeijua  thamani
Asante kwa chozi lako, limeniweka furahani
Najua thamani yako, sitokutoa moyoni
Sikuliliwa mwenzako, wewe wa kwanza amini
Asante kwa chozi lako, nimeijua  thamani
Ujuaye hali yangu, na bado ukathamini
Nakuapia kwa Mungu, sitaitema amini
Sitayasikia majungu, wakitema midomoni
Asante kwa chozi lako, nimeijua  thamani
Sijui nawaza nini, kujibu yaso kichwani
Nashukuru ukibaini, niyasemayo betini
Ndiyo yaliyo moyoni, tena hayo ya sirini
Asante kwa chozi lako, nimeijua  thamani
Huruma  pendo la kweli, hujifichama moyoni
Huna jicho la tapeli, kujisafi tu usoni
Huzuni yako ya kweli, naitazama machoni
Asante kwa chozi lako, nimeijua  thamani

By Fulgence Makayula

JITU ADUI SEHEMU YA 2

 Na Omar Zongo


Walinzi wote walibaki wakimtumbulia macho mtaalamu wa kutambua nyayo, Alionekana kujutia mno kulewa jana yake bila shaka alielewa madhara ya adui aliyepita kuingia duniani.
"Huyu adui aliyeingia atagharimu maisha ya vizazi vyetu vijavyo. Watakuwa watukutu, wavivu na watahadaika na mabadiliko ya kasi ya teknolojia kwa kujidanganya ni maendeleo makubwa, lakini kama atapatikana mwerevu na kuhesabu faida ya maendeleo hayo na kurudi kwenye hasara bila shaka atagundua faida ndogo sana dhidi ya hasara. Makosa yetu ya kujisahau usiku wa jana yatagharimu dunia hii!"
Alizungumza kwa hisia kali yule mtaalamu wa kutambua nyayo alisema ilikuwa ni habari iliyoibua majuto makuu kwa walinzi wale lakini wangefanyaje sasa na adui keshapenya. Hawakuwa na jinsi tena na ndipo hapo na wao pia walipoanza kupoteza umakini katika kazi yao.
Waliendeleza tabia zao za kunywa mvinyo wakijiongopea kuwa wanapoteza mawazo. Maadili ya kazi yao yalishaporwa usiku ule na Jitu Adui.

* * *
Sijui ni utaalamu gani alianza kuutumia Jitu Adui lakini ghafla tu sababu zikaanza kwa wasomaji vitabu, "Kazi nyingi sana sipati hata muda wa kusoma sasa hivi."
Sababu hii ilianza kupenya masikioni mwa Jitu Adui huku ikiibua furaha moyoni mwake kwa kuiona dalili ya ushindi.
Waandishi makini hawakuchoka kuibua dhima zenye tija kwa jamii, na kutoka na upeo waliokuwa nao. Tayari tofauti ya kimaadili wakaiona na kupambana kuiasa jamii katika kusimamia maadili bila kujua kuwa adui wa maadili yupo macho na aliwapinga vikali waandishi.
Jitu Adui akaviona vitabu hivi, alivipenda sana sababu aliziona akili za waandishi na nia zao njema, Alijikuta akitabasamu kwa dharau kabla ya kupuliza sumu ya uvivu wa kutafakari kwa wasomaji vitabu.
Sumu ya uvivu wa kutafakari ilipenya katika mifupa ya binadamu na kuenea miilini mwao, malalamiko ya pili yakapenya masikioni mwa Jitu adui.
"Misamiati migumu na mafumbo, yaani vitabu vinahitaji upate utulivu ndio uvielewe!." Cheko la kejeli na dharau likamtoka Jitu Adui, njia yake  ya kukita mizizi duniani ilikuwa nyeupe sasa.
Bado alikuwa makini na waandishi alitaka sana kusikia wana jipya lipi, Sikio lake likapata kusikia kilio hiki.
" Kazi zetu hazinunuliwi, kipato chetu kinayumba" Furaha ya ajabu ikamfanya ajipige kifua akijinasibu kuwa yeye ndiye JITU ADUI a.k.a ADUI WA MAADILI. Wafanye nini waandishi kama sio kufanya tafiti jamii inavutiwa na nini.
Utafiti ambao haukuchukua muda ulikamilika ukionesha mabadiliko makubwa kwa jamii. Walipenda kusoma vitu vyepesi, na dhima za starehe na mapenzi ndio walihusudu zaidi.
Alijikuta akijisemea Shaaban Robert nguli wa Kiswahili na  mwandishi wa riwaya mashuhuri ukanda wa Afrika Mashariki. "Mwandishi ni mtu wa desturi kama walivyo watu wengine, hawezi kuishi kwa kula ukungu na kunywa hewa"
Ujinga uliwafumba macho binadamu hawakuweza kabisa kufumbua ili wapate nuru ya ufahamu katika vitabu. Kwa pamoja walijikuta wakipiga vita kununua vitabu vya kufundisha na wengi walimiminika dukani kununua machombezo ya mahaba na starehe dhalili ya ngono!
Laiti kama wangelisikia kicheko cha ushindi akicheka Jitu Adui hapana shaka wangemsuta kwa kurejea vitabu vya mafundisho,  mbali na vile vilivyotungwa na watunzi binadamu. Kuna vyingine vilikuja na manabii, navyo vimetelekezwa!
Mbinu yake ya kwanza Jitu Adui imemrahisishia vingi sana, Kwa kutumia mbinu hiyo tu ya kucheza na akili za binaadamu alijikuta akifanikiwa kubadilisha mavazi ya vijana wa kike na kiume.
Tamaduni zao walizihifadhi kwa kiburi kwenye maghala ya kuhifadhia vitu vilivyopitwa na wakati.
Vitabu vyote vilivyoandikwa na waandishi waliotukuka kimaadili havina mahala palipokuwa pakiongelea namna mtu alivyo hodari kitandani wakati akishiriki  mambo ya faragha. Au kuongelea faragha kwa watu wasio na ndoa, hii waliifananisha na laana na adhabu iliyokuwa ikitolewa na waandishi ni mhusika kutengwa na jamii.
Nani leo hii asome dhima hizo zenye mashiko?  Kila mmoja angependa sana kuona kitabu chenye jalada linaloonesha umbo kubwa la mwanamke huku sehemu kubwa ya mwili wake likiwa wazi. Bila kujua ni mafanikio ya Jitu Adui ambaye ameandaliwa karamu kubwa akirejea huko kwao kusipojulikana.
Jamii ya Jitu Adui inajivunia kuwa na kijana aina yake na kwao wanamuita shujaa ambaye amefanya mapinduzi ya kimaadili duniani. Ushindi wake hivi sasa ni pamoja na magonjwa ya zinaa, majanga ya vita, ubaguzi, udini, wivu, uchawi na ukatili wa kila namna.
Waandishi wa kuyanyooshea kidole hayo nao wametekwa na tamaa ya kuuza vitabu vyenye kupotosha maadili, Inashangaza sana dunia hii ni watu wake pekee ndio huwa tayari kukulipa pesa nyingi sana ukiwapotosha.
Jitu Adui lile zigo alilobeba kama zawadi kwa wanadamu amefanikiwa kulipunguza kwa asilmia kubwa amegawa zawadi zake ipasavyo.
Ni nani tena wa kupambana na adui wa maadili, Jitu Adui mwingi wa hila? Swali hili liliponijia ndotoni nilishtuka nikitamka neno "Mimi..."
Ni hakika nilikuwa ndotoni, ndoto ambayo ilinifanya niandike dhima zilizoachwa kuandikwa, na nilipoanza kuandika nilikutana na binadamu walioathiriwa na Jitu Adui wakilalamikia uandishi wangu, eti nina mafumbo na naandika vitu virefu sana wao wanachoka kusoma!
Natikisa kichwa kuwahurumia lakini sikati tamaa sababu bado ningali mapambanoni kummaliza Jitu Adui arudi kwao akiwa dhaifu na ile karamu waliyomwandalia igeuke msiba.
“Sitaacha kuandika ninachoandika sababu nilipenda kusoma aina ya ninachoandika na nilipokikosa ikanibidi kukiandika ili nipate kusoma nilichokikosa

MWISHO.