Baba wa kiswahili, Shaaban Robert (kuzaliwa 1 January 1909 – kufa 20 June 1962)
Nionacho leo kuhusu kuenzi mchango wako ni USAHAULIFU MKUU, kiukweli UMESAHAULIKA BABA WA KISWAHILI!
Anasimulia
Omar Zongo
Naona aibu kusema kuwa natamani ule utashi wako walau
ungeuacha sehemu kisha ukaniagiza hata ndotoni nikauchukue niutumie kuendeleza
falsafa zako na utamu wa Kiswahili uliopo ndani yako.
Nasikitika ninapogundua kuwa 20 june wakati unafariki
ulikusanya kila kilicho chako nakuelekea nacho kaburini, sitaki kusema kuwa
hilo limetokea kutokana na uchoyo wako laa hasha ila nakulaumu kwanini hukutaka
kumuachia mtu arithi angalau robo ya unguli wako wa kutumia vema hii lugha
Kiswahili katika maandishi.
Ni juzi tu nimemrejea Adili na wasifu wake uliomchora nao
kwenye ile riwaya yako ya adili na nduguze,hakika nafurahishwa sana na jaala ya
mfalme Rai ambaye aliweza kuwa na upendo kwa kila kitu anachokitawala si
mnyama, binaadamu hata mmea, alidiriki kujinyima yeye ili vitu hivyo vineemeke.
Umesahaulika Baba wa Kiswahili na sijui kwanini limewezekana
hilo kwenye ardhi hii ambayo kwa sasa busara zako zingepaswa zitumike zaidi ili
kujenga maudhui sahihi ya utu wema na uongozi bora ndani ya bara letu Afrika.
Naugua maradhi ya kusonona moyo kila nipigapo soga na
mabarobaro rika langu ni wachache kati yao wanaokujua, tena kwa kupapasa papasa. wengi husalia kuuliza “ni nani huyo baba wa
Kiswahili?” nazidi kuamini kuwa umesahaulika nguli wewe ambaye akili yako
nikiitathimini kupitia kazi zako naiona imezidi ukawaida.
Enzi zako upo hai wapo waliodiriki kukufananisha na Wilium
Shakespare lakini vifo vyenu vimedhihirisha kuwa yale yalikuwa maneno tuu,
maana wewe kaburi lako limetelekezwa kule kwenu Tanga, wanaokujali kwa kung’oa walau majani tu kwenye kaburi lako ni wale
waja wenye nasaba nawewena hilo kusema kweli nitofauti na
Yule mwenzio uliyekuwa ukifananaishwa nae bado kaburi lake ni alama
inayosimama kama historia katika anga la waandishi mahiri wa mashairi na riwaya
nchini uingereza na duniani kwa ujumla.
Kinachonifanya niugue maradhi yakusononeka moyo ni kwamba
wewe ni wajuzi tuu labda kama nakosea au sijui mahesabu, lakini ukweli ni
kwamba Willium Shakespare ni wamiaka ya 1564, naomba nirejee
tena elfu 1 mia 5 na sitini na 4 na
akafariki mwaka 1616 ingawa inakisiwa lakini ukweli ni kwamba nguli huyo wa
uingereza ni wa makarne mengi yaliyopita iweje bado anaenziwa na alama yake
bado ni dira kwa vizazi vipya vyote vinavyozaliwa uingereza.
Mwenzangu namimi wewe baba wa
Kiswahili ni wajuzi tuu masikini lakini umesahaulika kwakweli! Kuzaliwa kwako
ni 1909 na kufa kwako 1962 lakini juhudi zako zimezikwa nawe siku ile kule
kwenu mwambani Tanga.
Mwandishi nae ni mtu wa desturi kama walivyo watu wengine
hawezi ishi kwa kunywa upepo nakutafuna mawe, bila shaka nukuu yako hii ulitaka
kudhihirisha mgogoro wako wa nafsi uliokuwa nao katika kupigania mafao yaendane
na kazi zako, kwa maono yangu ni kuwa hapana siku uliyowahi kunufaika na
kuridhishwa na ubaba wa Kiswahili.
Naiona lana kwenye anga hili ulilotokea lana itokanayo na
sononeko lako la tangu ungali hai na hata miaka mingi tangu kufariki kwako.
Umesahaulika Mzee wangu, baba wa Kiswahili!
Niseme nini namimi sina mamlaka yakuamrisha kuwepo siku ya
kuwaenzi ninyi wenye michango yenu katika fani ya ushairi na riwaya.
Nahisi siku hizo zipo lakini kwako wewe ingepaswa kuteuliwe
siku maalumu ya kumbukizi kwa Baba wa Kiswahili lakini bado swali linabaki kuwa
mimi ninani hasa??
Mchango wako si tu mashuleni kukuza bongo za watoto wetu
bali pia ulipigania uhuru kupitia karma yako, zipo sababu zaidi ya bilioni
zakukumbukwa lakini iweje uwe umesahaulika hivi.
Naomba niishie hapa maana niendapo naenda kukufuru,
leo sijaandika barua
kwako bali nimepanda kilimani nikiuagiza upepo ufike na sauti yangu uisikie
nikikwambia habari hii UMESAHAULIKA BABA WA KISWAHILI.
Nilipo naugua maradhi ya kusononeka moyo sababu kama wewe na
utashi wako ule wote umetelekezwa kiasi hicho mimi ninani katika fani ya
uandishi mpaka nije angalau kutajwa tu mdomoni mwa waja wa kesho ambao watakuja
baada ya mimi, kama sisi tulivyokuja baada ya wewe!.
Habari niliyokupa kupitia upepo uvumao kutoka nilipo kufika
huko ulipo bila shaka ni habari mbaya maana hata mimi nisingetabasamu kamwe
kusikia nimesahauliwa licha yakupigania hadhi ya lugha wanayojinasibu nayo watu
hii leo.
Lakini ningefanyaje wakati niwewe ndio uliwahi kuniasa
kuhusu kuwa mkweli, uliwahi sema
Siche kweli kuisema, hata kwa mfalme,
Ingawa inauma, sema kweli atazame,
Kweli ina heshima, wajibu wa mwanamume,
Uongo una lawama, ufukuzeni uhame.
Kweli ina thawabu, wametumia mitume,
Japo wamepata tabu, wamerithi ufalme,
Na waliowaadhibu, hawakumbukwi kamwe,
Kweli ina thawabu, kila mtu aseme.
Hakika sitakuwa mwema kama nikiacha sononeko liendelee
kukusumbua naomba tabasamu sasa kwa uetnzi wako huu!
Wadogo kuwa wakuu, kwa watu ndio tabia,
Na wa chini kuwa juu, ni jambo la mazoea,
Mwenendo wao ni huu, wanao kama sheria,
Watu duni na wakuu, katika hii dunia.
Katika dunia hii, ya machungu na matamu,
Na rafiki na adui, na mepesi na magumu,
Viumbe walio hai, hubadilishana zamu,
Lakini hawatambui, kwa uchache wa fahamu.
Sina shaka utenzi huo umekufanya ukafarijika kuona kuwa kazi
zako bado zingali nasi zikitusuta suto kuu kwa kukusahau baba wa Kiswahili.
Pumzika kwa amani vijana wenye chembechembe za karma aina
yako bado twaendelea pambana ingawa twajua kusahauliwa kwako ni sawa
nakunyolewa hivyo nasi tumetia maji nywele.