KIZIMBA Cha IBILISI



Ilipoishia
sasa Nikawa namshuhudia Ramadhani akifungua lango lile la Kizimba cha Ibilisi…wasiwasi na kihoro vikanivaa sikuamini kuwa ni mimi ndio naenda kumuona Ibilisi huyo mjaa lana.
Sasa endelea

Kidokezo

SEHEMU YA PILI


"Tangu kufika kule juu ambako nilielezwa kuwa ni mbinguni sikio langu lilikuwa linapokea taarifa za ajabu tupu, kama ni somo hakika lile nilibahaika kulisoma pekee yangu duniani, nilizidi kumfurahia Ramadhani, nikajikuta namuuliza “Sasa vipi hapa tulipo hawawezi kutuona?"

Na 
Omar Zongo

Chumba kile kilikuwa kidogo ambacho kilimtosha Ibilisi peke yake, aliviringishiwa minyoror mwili mzima ili kudhibiti vurugu zake zakutaka kutoka kifungoni pale.
Kwa harakaharaka niliyachunguza mazingira ya mule ndani nikabaini kuwa kuna joto kali mno, kiasi cha muda ule mchache tu nikawa tayari nimelowa mwili mzima kwa jasho, nilijiuliza Yule ibilisi anawezaje kukaa mule.
Kama vile Ramadhani alijua nini nawaza akajikuyta ananipa jibu “mahala hapa nikaribu kabisa na ulipo moto mkali wa jehanam, moto ambao ni maalumu kwa watenda dhambi ndio maana chumba hiki kinajoto balaa, fanya tuondoke.”
Niliyasikia maneno ya Rafiki yangu Ramadhani lakini sikuyazingatia sana maana mawazo yangu, akili yangu na macho yangu vyote kwa pamoja vilitulia kwa Ibilisi.
Nilimtazama kwa hasira na Macho yangu yachuki dhidi yake yalikutana na macho yake yenye hila, kiburi na kisasi juu yangu na wenzangu wote wenye haiba kama yangu.
Samahani sana tangu nimeanza simulizi hii sijakutajia jina mimi naitwa Abdi ninayetazamana nae muda huu Ni Ibilisi mjaa lana almaarufu kama shetani, Namshukuru rafiki yangu Ramadhani kwa kunipa fursa yakumuona mshenzi huyu ambaye amefungwa mnyororo muda huu.
Nimeambiwa kuwa hapatani asilani na Ramadhan sababu kila akija shetani hufungwa mnyororo nakuzuiliwa kuvinjari duniani, mkataba wakupotosha wanadamu huvunjwa kila mwezi wa ramadhaan unapofika hivyo hubaki na minyororo yake akiwa amefura hasira.
Kabla sijafika kukutana nae nilikuwa namsikia akipiga kelele eti afunguliwe, nilisikia kinywa chake kikitoa sauti iliyobeba ujumbe wenye maneno machafu yaliyosheheni matusi muda wote analalama akitaka afunguliwe ili je kukusanya watu wake wakuingia nao motoni.
Waqkati nikiwa nimesimama namtazama ghafla nikasikia hatua za watu wakija kuelekea mule ndani tulipokuwepo, Ramadhani akanitaka haraka tuchuchumae, nikafata agizo hilo la Rafiki yangu.
Tukiwa tumechuchumaa nikashuhudia watu wenye mabawa meupe, licha ya kuwa walikuwa na muonekano wa ndege na binaadamu lakini walikuwa wanavutia mno kuwatazama, walikuwa ni wazuri balaa!
Rafiki yangu Ramadhani akaninong’oneza “hao ni malaika kutoka duniani, kazi yao kubwa ni kukusanya taarifa zote za duniani nakuja kuzileta huku mbinguni, wanafanya kazi masaa ishirini nan ne na hupokezana, muda huu bila shaka wengine wapo duniani, wao ndio wamerejea,”
Tangu kufika kule juu ambako nilielezwa kuwa ni mbinguni sikio langu lilikuwa linapokea taarifa za ajabu tupu, kama ni somo hakika lile nilibahaika kulisoma pekee yangu duniani, nilizidi kumfurahia Ramadhani, nikajikuta namuuliza “Sasa vipi hapa tulipo hawawezi kutuona?’’
Ramdhani akanitazama kisha akatabasamu ndipo akanijibu “ Hapana hawa jinsi walivyo huzingatia kazi moja tuu wanayotumwa hawajishughulishi na kluzingatia mambo mengine ingawa ingekuwa ni rahisi kwa wao kuhisi uwepo wetu endapo tungesimama wima, mradi tumefupisha vimo kamwe hawawezi kujua hilo”
Loh ile ilikuwa habari nyengine ngeni kwangu na yakustaajabisha, nilibaini kuwa Malaika wana utofauti pia na binaadamu maana ni ngumu kwa mwanadamu kumuagiza afanye kitu kimoja akakazaznia hicho tu lazima macho yake yatajishughulisha na mengine nachelea kusema labda pengine hii ndio sababu ya wanadamu kutokuwa na ukamilifu katika mambo yao.
Pengine labda dereva angejua kazi yake ya udereva tu bila kufuatilia simu labda ajali zingekuwa adimu, lakini wapi ni wanadamu ndio huongoza kwa kushika mawili nakupuuza ule msemo wao usemao mshika mawili moja humponyoka.
Sasa macho yangu yalifunguka kuona malaika wale wanafanya nini kwenye kizimba cha ibilisi na masikio yakawa wazi pia kusikia ujumbe gani unatoka duniani kaletewa ibilisi.
“Ewe mkaidi Ibilisi, tumekueletea ujumbe kutoka duniani, katika kipindi hiki ambacho umefungiwa humu dunia imekuwa mahala salama, wanawake wanajistiri kwa mavazi makuu kuu, wanaume wanapishana kwa wingi kwenye nyumba za ibada na wazinifu wamekuwa wachamungu na wanbywa pombe wameacha, kwanini hii isiwe habari njema kwako ewe mkaidi Ibilisi”
Malaika wale walizungumza kwa mbwembwe na furaha, dhahiri walionekana kuvutiwa na ujumbe ule wanaompatia Ibilisi, na ilikuwa ni tofauti kabisa na Ibilisi mwenyewe, nilimshuhudia akijibamiza kichwa chake kwenye nondo za kizimba chake.
Eti taarifa ile ilikuwa mbaya kwake! Hakupenda abadani kusikia watu wakiwa wacha Mungu, alinguruma kutoa mlio wa kuogofya uliodhihrisha hasira zake.
Malaika wale wakuvutia walifurahi walionekana wakimdhihaki Ibilisi, na wakaendelea kumonesha kidonda chake kwa kumpa habari ambazo mie zilinishangza zaidi, nasema zilinishangaza maana sikujuwa kabisa kama malaika wale wananijua mimi na marafiki zangu wa duniani. Walinichosha kututaja pale mbele ya ibilisi.
“Abdi kwa sasa anaswali muda wote, ameacha kusikiliza muziki wa duniani anasikiliza mafundisho ya manabii na nyimbo nzuri zinazotaja jina la Mola wetu mtukufu, zaidi rafiki zake wote ni wacha mungu sasa, hawakai tena vijiweni kuzungumzia kuhusu zinaa na wanawake wanaotoka nao, kwa sasa wanamuongelea Mungu na kudhihirhs hofu yao, Ona sasa neema za Mungu zinavyofanya kazi kwa sasa duniani, Abdi anamuomba Mungu ampatie mke aoe nasi tunamlilia MUNGU wetu amuitike Abdi dua yake,
Rafiki yake Abdi aitwae Manji kwa sasa ameoa na hataki kabisa maswala ya zinaa anamuheshimu mke na ndoa yake na pia wanahimizana kuswali kila siku.
Marafiki zake wengine wote kina Madebe, Kurwa na Gidion, Asangama na woote wamesimama katika hofu ya Mungu wanakumbushana kheri na Utukufu Wa Mungu, na wote mioyo yao imediriki kutamani kuoa nakuachana na zinaa”
Loh! Mwenzenu nilishangazwa na kauli za ibilisi wale, walinishangza sana kunitaja nakuwataja watu wangu, na hawakuishia hapo walielezea mambo mengi mema ambayo baadhi ya watu wengine maarufu wanasiasa na wanamuziki wanayafanya kipindi hiki Ibilisi alichofungiwa Kizimbani.
Habari ile ilizidi kumpandisha Jazba Ibilisi, alizidi kupiga kelele, akisema “Ni uonevu huu, haiwezekani watu wangu wote walaghaiwe na ramadhani mpaka washindwe kuetekeleza starehe za dunia nilizowafundisha, haiwezekani Abdi aache kuzini na Yule mwanamke wake niliyemtafutia, haiwezekani aache kusikiliza mziki mzuri wa wasanii wake anaowapenda nimesema nifungulieni nikawachuke watu wangu niwarudishe kundini, ni lazima niingie nao motoni nimesema..”
Aliropoka kwa suati yenye hasira Ibilisi, loh! Nimewahi kuona watu wenye roho mbaya duniani lakini Ibilisi alizidi jamani, yaani alilia kwa uchungu eti kisa kaambiwa watu wamebadilika wanamcha Mungu wao aliyewaumba.
Nilishuhudia Malaika wakimcheka kisha wakaanza kuondoka mule, nikamgeukia Ramadhani mwenye sura ya tabasamu muda wote, nikamuuliza
“Ina maana Ibilisi alikuwa hajatuona, mbona hajawaambia chochote wale malaika kuhusu sisi kuwepo hapa”
Ramadhani alicheka kisha akanijibu “Ibilisi ana roho mbaya kiasi ambacho habari alizoambiwa na malaika zimemfanya asahau kabisa kama sisi  tupo hapa, tayari amechanganyikiwa anatamani niondoke hata sasa ivi pale duniani ili afunguliwe akawapotoshe tena watu.”
Mnh! Kwakweli nilishindwa kuvumilia wala kudhibiti hisia zangu nikaamka bila hata kungoja amri ya mwenyeji wangu, nikasimama wima kwa hasira nikimtazama Ibilisi Yule mjaa lana.
Nilisimama nikimtazama kwa hasira huku nikiwa siamini kuwa macho yangu sasa yanatazamana na  ile sauti yangu ya ndani inayonituma kutamani wanawake niwaonao barabarani bila kujali wengine ni wake za watu,
Aidha huyu ndiye Yule anayenikataza nisisimamishe ibada kumcha mola wangu na pia hunikaa maungoni nakunifanya nivutike zaidi na dunia huku nikiisahau kabisa akhera.
Nilijiambia kuwa nina kila sababu zakumchukia huyu nimuonae mbele yangu mwenye majinywele marefu na machafu, sura baya mithili yake hapana, macho yake ya kiburi yanafanana na ubaya wenye kuogopesha.
Ibilisi alinitazama kwa chuki  sauti yake huku ikiwa na mkwaruzo kwaruzo wa hasira na kiburi aliniambia kuwa  nisiringe maana mwezi ukiisha akiachiwa huru atanisomba tena nirudi kwenye himaya yake  ya starehe dhalili ya ngono, ulevi, wizi, tamaa, magendo, ugomvi, ushirikina na umbeya.
Anasema eti atahakikisha nakuwa tena mfuasi wake na namtumikia kama mwanzo mpaka siku ambayo nitaingia naye motoni, namshangaa anavyojiamini ibilisi huyu mjaa lana! Eti anasema Tamaa yangu ya maisha mazuri itanifanya niende kwake kiulaini kabisa, muoneni jamani anadiriki kutaka kupinga namimi eti tuwekeane dau!!
Vazi lake jeupe lililojaa madoa ya damu za watu waliokufa vitani anajinasibu nalo eti yeye ndiye chanzo kwa kuwashawishi viongozi wawe na tamaa yakuongoza bila kujali mapigano na vita vinavyoathiri watoto na kina mama.
Sauti lake baya linanichefua mno natamani nimsogelee nimpige hata makofi mawili ila jinsi lilivyo linaogopesha kwakwel;i.
Ujasiri wakumtazama nimeupata kwa sababu pembeni yangu yupo rafiki yangu mpole, mwenye haiba ya wema usiomithilika, Rafiki yangu huyu kwa jina Ramadhan ananiuliza kama nina lolote lakumwambia ibilisi, kwa kihoro natikisa kichwa kuitika, wallah tena nilikuwa naitaka hii nafasi nizungumze na hili ibilisi mbele yangu.
Ramadhani  ananisisitiza nifanye haraka maana joto la jehannam linazidi kuongezeka kila muda unavyozidi kwenda mbele maana moto huo huchochewa zaidi, habari ile ilizidi kunipa hofu ya kutenda dhambi niliogopa sana siku moja namimi kuwa ndani ya moto huo, zaidi Ramadhan akanipa habari nyengine iliyoniacha hoi zaidi, eti alisema umbali wa moto ule kutoka mahala pale tulipo ni sawa nakutoka bara moja kwenda jengine lakini joto lake lilikuwa lile, nikajiuliza huo moto una nguvu kiasi gani mpaka mvuke wake uwe vile loh!
Hofu ikaniingia yakuumizwa na moto ule uakapoongezwa ukali nikamgeukia tena ibili ili niseme nae machache yaliyopo moyoni mwangu
sijui Napata wapi ujasiri namsogelea karibu kisha navuta karibu kohozi linasogea mpaka kooni kisha nalivuta kwa kasi kutoka ndani ya kinywa changu ptuu, kohozi lile linatua vema kwenye paji la uso wake! Nafsi yangu inafurahi ingawa bado sijaridhika natamani ningekuwa na basola nimyatulie risasi kummaliza.
Jitu hili ndilo lile lilomuahidi Mola wetu kuwa atahakikisha wanadamu tunaingia nae motoni, silipendi hakika natamani nipasue hiki kifua muuone moyo wangu ulivyofura hasira juu yake.
“Khaa unanitemea uchafu kwenye uso wangu, wallah nakuapia nitaanza nawewe sikukuu ya Eid ikifika! Huo uchamungu wako utaishia muda ule unatoka kuswali swala ya eid, Nitakutuma uende club, nitakutuagiza uzini na mwanamke wako na nitakushawishi unywe pombe, we jishaue muda huu ambao Mungu wako kanifunga minyororo hii mwilini mwangu lakini nakuapia nitaingia nawe motoni…litazame vile binadamu sanamu uliyejengwa kwa udongo wee…!”
Alipaza sauti yake Ibilisi akiongea kwa uchungu baada ya mimi kumtemea kohozi usoni mwake, jazba zinamzidi maradufu…
Namtazama kwa chuki namimi namjibu kwa kiburi kama chake.
“Mwanakharamu mkubwa wee unadhani MUNGU alivyokupa mamlaka ufanye hila zako duniani alikupa na uwezo wakuwashawishi wacha Mungu! Kwa taarifa yako sitamuacha MUNGU wangu majira yote ya usiku na mchana hivyo hautapata nafasi yakusema na moyo wangu, mimi hunipati tena nimezijua hila zako, Motoni utakwenda na wachache sana tena ni wale waliokosa maarifa yakutambua zuri na baya, jema na ovu,
Hii ni vita kati yangu mimi na wewe, kwa taarifa yako watu wangu wote wakaribu na wengine wote wenye sifa ya ubinaadamu nitawahimiza juu ya kumcha Mungu, nitawaeleza nia yako mbaya na nitawaambia mbinu zako zote..
Kwanza nitawaambia kuhusu Ujinga uliouweka kwenye akili za wanawake mpaka wakawa hawathamini maungo yao nakufanya wanaume washawishike kuwazini tu bila kuwaza tena ndoa.
Nitawaambia maumbile makubwa ya wanawake na namna walivyoumbika ni kazi ya MUNGU ila wewe kazi yako ni kutumia sumu ya ujinga uliyopuliza kwa wanawake mpaka kuwafanya waone kutembea uchi ndio urembo.
Nitawaambia kuwa hizo ni mbinu zako na unatumia mitandao ya kijamii kupoteza muda kwa binaadamu wakose hata sekunde chache zakuwaza mema ya MUNGU na Utukufu wake..
Nitawakumbusha watu kuwa Mungu ndiye tajiri ambaye hajawahi kufilisika hivyo wasimnyenyekee mtu yoyote zaidi ya Mungu maana ni yeye ndiye aliyeumba utajiri na ufukara, huzuni na furaha na pia yeye ndiye mwenye mamlaka ya Uzima na Kifo cha kiumbe yoyote duniani.
Nitawapa mbinu yakuwa mbali nawewe, mbinu ambayo hata wewe huna nguvu nayo, mbinu ya wao kuzidisha ibada nakukutanguliza wewe katika kila jambo….
Kinachonifurahisha kwako ni kwamba Unafanya kazi aliyokuagiza MUNGU, Kazi yakupima imani za watu hivyo basi nawe ni mtiifu juu ya Mungu wangu ninayemuabudu hivyo nitawakumbusha watu kuhusu hili na watakuona wewe si lolote mbele ya Mungu, maana kuna wakati utafika nawe utakufa ili kutimiza andiko la kila nafsi itaonja mauti.
Ibilisi wewe fungu lako ni moto tuu na motoni utaingia, binaadamu tumeumbwa kumsujudia Mungu na Nakuhakikishia pepo tutaiona kwa kumkimbilia MUNGU.
Maneno yangu yanaonekana kumdhoofisha mno Ibilisi, sura lake baya linaonekana wazi limekosa amani kwa ukweli huo, tukiwa tunatazamana kwa chuki kila mmoja ghafla nikamsikia Ramadhani akinishauri tuondoke, kwa vile nilikuwa nimeshamaliza kumpa ukweli wote ibilisi mjaa lana. Nikaona ni sahihi kuondoka pale.
Safari yakurudi duniani ilikuwa nyepesi kuliko tulivyoenda, nastaajabishwa na binaadamu wenzangu walivyo na shamrashamra zakupokea idi najisemea kimoyoni laity wangejua eid inakuja kumfukuza ramadhani kamwe wasingeshangilia na pia eid hiyo ibilisi anaachiwa dah roho yaniuma mno.
Nawaza kuwa mchaMungu lakini sitafurahi nikiwa peke yangu natamani kushirikiana na woote duniani tumsaliti shetani, ili ashindwe kutimiza lengo lake.

asante kwa kuifuatilia simulizi hii yakufikirika ambayo usimuliaji wake unakamilika kutokana na kuchora wazoni wasifu wa ramadhan na vitu dhahania kama vile mbingu , pepo na jehanam

sina shaka kuzama wazoni nakuandika simulizi hii ni kukusaidia kifikra na uweze kuona haja yakuaiandaa kesho yako kwa kutenda mema nakuwa na imani thabiti kuhusu Mungu wako aliyekuumba na kuumba kila kilicho kizuri duniani.

Akili fupi ambayo itakufanya uamini uwepo wa MUNGU nikujiuliza kuwa nyumba nzuri, gari zuri au chochote kizuri unachokipenda duniani kinaweza kujitengeneza chenyewe??? kama jibu lake ni hapana basi tambua kuwa yupo ambaye amekutengeneza ukawa wewe binaadamu mzuri wamaajabu  na pia akaitengeneza dunia ikawa kwa namna ambavyo ipo sasa ni wajibu wako kuamini kuwa uzuri wa dunia hii hauwezi kuwa ulijitokea tuu wenyewewe yupo bingwa, Mwenyezi Mungu mimi napenda kumita Jabbari ambaye amefanya haya yote yanayofanya wewe utamani kuishi milele ili uendelee kufaidi utashi wake.

Ishi kwa ukamilifu wa kufuata miongozo yote ya vitabu vinavyoelekeza kuhusu MUNGU muumba mbingu na ardhi kama unavyoenda resi kutafuta kodi ya nyumba unayoishi ndivyo mwenye hii dunia naye anataka kulipwa kwa kumnyenyekea na kumsujudia huku ukimtumainia yeye pekee.

hiyo ndio kodi ya neema zote alizokupa duniani hapa....USIMSAHAU MUNGU WAKO KAMWE!.

TAMATI



Share this

Related Posts

:)
:(
hihi
:-)
:D
=D
:-d
;(
;-(
@-)
:P
:o
:>)
(o)
:p
:-?
(p)
:-s
(m)
8-)
:-t
:-b
b-(
:-#
=p~
$-)
(y)
(f)
x-)
(k)
(h)
cheer