EL PERDEDOR

“Wanaume ni watashi sana katika kutumia nguvu na mabavu yao kuwanyanyasa wanawake, lakini sijui kwanini wanashindwa kutumia utashi wao huo kutambua thamani na upendo wa mwanamke anayempenda kwa dhati.
 


Kuzidisha drugs watu wanaweza sema ndio chanzo cha kifo chako shoga angu lakini mimi nasema mapenzi ndio chanzo...naamini nafsi yako itawaadhibu wanaume wote wenye moyo kama wa aliyekufanya uwe marehemu leo hii, Rest In Peace shoga angu, nitamiss kukuita hivi madia...”

 EL PERDEDOR
Na
Omar Zongo

Uliniumiza kichwa sana nilipoona mchoro wako ulioonesha mwanamke amejiinamia kisha ukiambatanisha na neno hilo El Perdedor.
Niliwaza nikawazua nikijiuliza unamaanisha nini, nilijihoji je ni jamaa mwengine umempata ambaye amekalia kiti cha huba kilichopo moyoni mwako ndio anaitwa jina hilo?? Lakini nilijikosoa maana kama ni jamaa mwengine kwanini uliweka picha yako ukiwa umeinama, kulalia magoti.
Nikajiuliza tena neon lile linatoka kwenye lugha gani  maana kwenye kabila lenu wazanaki hamna msamiati wenye maandishi kama hayo ingawa nilikuwa sina uhakika n]maana sio maneno yote ya kizanaki ninayajua.
“El perdedor.. El Perdedo” kila mara neno hili lilikuwa likijirudia kwenye kichwa changu, tangu nilipoliona kwenye picha yako uliyoituma instagram.
Kuhusu Picha iliyoamabatana na neno hilo haikunisumbua maana hata wewe  uwe wapi kamwe siwezi kukusahau, lakini namna ambavyo mchoraji amekuchora umejiinamia kisha akaweka na maneno hayo ndipo nilipopata mashaka sana.
Kama mashaka yangu ni dalili ya kuwa bado nakupenda basi nakiri upendo wangu kwako hautakuja kuchuja licha ya kuwa mimi ndio nilikuacha.
Sababu zangu zilikuwa dhaifu tu eti kwanini ulienda club usiku na marafiki zako bila kuniaga, nafikiri ilishapangwa tuachane maana hata uliponililia machozi ya huruma mie sikudhania wala kufikiri kurudisha huba kwako.
Nilikuacha kiukweli na haukuamini macho yako! ilikuuma sana ulipobaini kuwa ni kweli ulivyodhani nakuacha sababu nimepata mwanamke mwengine, maana haikuchukua muda ukaona mtandaoni nikituma picha za msichana mwengine, kwa ulimbukeni wangu nikihisi nakurusha roho.
laiti kama ningejua maumivu ya mapenzi yanafananaje kamwe nisingefanya ujinga huo, yaani sikuwaza kabisa kama nakuumiza kwa kiwango kikubwa mno.
Najuta sana sababu nimechelewa hata kusema nisamehe maana hali yako haina utayari wowote wakunielewa hata ikitokea nakutamkia neno hilo.
Ile siku niliyokuomba tukutane ni siku ambayo jana yake nilitoka kumfumania mwanamke yule niliyemfata baada ya kukuacha wewe.
laiti ningejua kuwa mwanamke yule ni kijiko cha hoteli kamwe nisingethubutu ulimi wangu utamke tuachane.
masikini wewe hukuwa na hiyana kukutana namimi na pia hukusita kunieleza maana ya neno uliloambatanisha na mchoro wako kwenye bega, sauti yako bado inajirudia nakumbuka ulisema
"mimi ni mkosaji, nimekosa vingi vizuri maishani mwangu akiwemo mama angu, na pia nimekosa upendo wa baba maana alinikana tangu niko tumboni, lakini sijui kwanini sikuumia sana kama nilivyokukosa wewe mwanaume wangu niliyekupenda kwa dhati, najiona mkosaji maana nikweli nilikukosea lakini ilikuwaje kosa lile linihukumu kuishi bila pendo langu...."
ulishindwa kuendelea kuongea, ukaanza kulia.
Huruma iliniingia sana, nikajutia kukuacha na Zaidi iliniuma maana niliiona hali yako na ikaniambia wazi kuwa siwezi tena kuwa nawewe! ulikuwa umekonda, sio nadhifu tena, mchafu na mikono yako ilikuwa imetoboka toboka matundu madogo ya sindano..
hali yako ilinidhirishia kuwa X wangu umekuwa Teja! uliniumiza sana uliposema kuwa ulichagua maisha hayo sababu ndio faraja pekee uliyoona inafaa kukufariji.
Nilipokubembeleza unieleze maana ya neno ulilochora kwa ufafanuzi ukarudia kwa unyonge huku ukijikaza kibandidu kuonesha kuwa uhuni umekuvaa, ulisema kwa sauti ya kike lakini iliyotawaliwa na uteja "wee sinishakwambia maana yake ni Mkosaji, mimi ni Loser, ndio mimi ni El Perdedor  hilo ni neon la kihispania nimechora mwili wangu kukiri kuwa mimi ni loser lakini wewe ndio chanzo...."
Ulisema tena ukashindwa kuendelea ukaanza kulia, siku ile ulinielezea maisha yako ya sasa unayoishi, uliniambia wahuni wanakubaka mtaani ukishazidiwa na dawa za kulevya, uliniambia kuwa nyumbani wamekutenga na sasa unalala popote penye maficho au palipo wazi, mradi kukuche.
Kauli zako ziliniumiza! ule urembo wako sikuuona tena! macho yangu yalipata nafasi kwa mara nyengine kuutazama tena mchoro wako begani, safari hii nikijua sasa maana yake.
Mchoraji alikuwa mtashi kwelikweli, aliweza kukuchora ukiwa umejiinamia na kisha aliyaweka maneno hayo kwa weledi wa hali ya juu.
El perdedor nikalisoma tena kimya kimya neno hilo, huku nikilitafsiri kwa kiingereza Loser, na nikafasiri kwa lugha yetu Kiswahili nikapata neno, mtu aliyepoteza, hana dira, mkosaji!
Kichwa changu kiliugua huzuni maneno yako yalipojirudia kichwani mwangu "wee sinishakwambia maana yake ni Mkosaji, mimi ni Loser, ndio mimi ni El Perdedor lakini wewe ndio chanzo...."
Maisha yangu niliyaona kabisa yakiingia mkosi wa laana yako, dhambi ya hali uliyokuwa nayo haikuweza kuniepuka kamwe, nafsi ilinisuta suto kuu, majuto yangu yalishavaa vazi la ujukuu.
Wakati nawaza nini chakufanya au nini chakukwambia, nakumbuka uliniambia unaomba shilingi elfu mbili, bila kufikiri mara mbili nikakutolea noti ya elfu tano nakukukabidhi, ukapokea na ajabu ulipoitia mkononi tuu, ukaniaga.
Hapa ndio nilikiri kuwa kweli sio wewe tena! Nakumbuka uliniaga kihuni sana eti ulisema
“kama vipi tutakutana siku nyengine acha mimi niingie chimbo”
Sikukuelewa, na hata nilipotaka kukuzuia sababu nilikuwa sijamaliza kuongea nawewe ukanikatalia kabisa na ukaondoka zako, nilibaki nakutazama bila kukumaliza mpaka ulipopotea kabisa machoni kwangu ndipo namimi nikaondoka eneo lile la makutano yetu.
Siku ile ilikuwa ni siku ya hukumu yangu ya matendo maovu yakukuacha bila huruma, hakika ningejua kama ungechagua maisha yale baada ya kunikosa kamwe nisingethubutu kukuacha,
Niliumia kumpoteza mwanamke aliyekuwa ananipenda kupita kiasi, sikujua kwa siku ile nani wakumlaumu, nafsi yangu au shetani au nilaumu ujana ambao ulinivaa na kutamani mwanamke mwengine huku nikukuacha wewe ambaye ulikuwa na upendo wa dhati kwangu.
Siku ile ilikuwa chungu kwangu, na uchungu wake ukaongezeka makali ilipofika usiku baada yakuona picha mitandaoni zikitumwa na ndugu na marafiki zako, wengi wakiandika kifupi cha maneno matatu ya kiingereza Rest In Peace (RIP) huku wakiambatanisha na picha zako.
Nilipoona picha ya kwanza nilidhani macho yananidanganya lakini baadae nikagundua kila mtu anayekujua ameandika neno hilo kuashiria kuwa wewe sio miongoni mwa tulio hai, yaani sikuamini kabisa kama umetutoka duniani.
Rafiki yako Devotha aliyekuwa akiniita shem Darling enzi nipo nawe ndio aliandika maneno makali, ingawa yalinipa chanzo cha kifo chako lakini pia yaliniongezea hukumu ya nafsi yangu ovu, hakika nilijiona muuaji, hakika mimi ndio nilikuua  rafiki yako Devotha hakukosea kuandika hivi.

“Wanaume ni watashi sana katika kutumia nguvu na mabavu yao kuwanyanyasa wanawake, lakini sijui kwanini wanashindwa kutumia utashi wao huo kutambua thamani na upendo wa mwanamke anayempenda kwa dhati.
Kuzidisha drugs watu wanaweza sema ndio chanzo cha kifo chako shoga angu lakini mimi nasema mapenzi ndio chanzo...naamini nafsi yako itawaadhibu wanaume wote wenye moyo kama wa aliyekufanya uwe marehemu leo hii, Rest In Peace shoga angu, nitamiss kukuita hivi madia...”
Ujumbe huu ulinigusa kabisa mimi, niliusoma mara mbilimbili huku nikiona kabisa Devotha alivyonishambulia shambulio lile kubwa lililobeba silaha kali za tuhuma dhidi yangu, japo hakunitaja lakini dhahiri niliona ule ni ujumbe wangu, nawezaje kupinga.
“Hii ndio sababu ya mimi leo hii kuchora maneno haya kifuani kwangu upande wa moyo wangu, sijawahi kumwambia mtu suala hili wala mchoro huu haujawahi kuonekana na mtu yoyote zaidi yako, ilinichukua muda sana kuamua kuwa na msichana mwengine kimahusiano baada ya kifo chake.
Muda wote nilikuwa nautumia kutubu dhambi zangu, na nilimuomba pia Mungu anipe mwanamke mwengine yeye mwenyewe huku nikimuahidi kuwa sitapuuza tena upendo wa mwanamke atakayenipa.
Hiyo ndiyo sababu ya kuwepo huu mchoro kifuani kwangu na ndio sababu pia ya kwanini nakupenda sana, nakuheshimu na najali maumivu yako..naomba nisamehe kwa makosa niliyowahi kuyafanya kwa mwanamke mwenzako hadi kusababisha awe teja na baadae marehemu.
Samahani jamani sijawatajia jina, mimi naitwa Prince Jocha, na hii ni simulizi yangu fupi ya maisha yangu yakimahusiano ambayo nilikuwa na msimulia mke wangu!
tayari nimejiomba msamaha, nikawaomba pia msamaha wanawake wote na nikatubu kwa mungu hivyo akanisamehe nakunijaalia  familia nzuri yenye afya na wanamjua Mungu! Kwasasa Mimi ni baba wa watoto wawili! Devis na Dayana.
Dayana ndio jina la Yule mwanamke niliyemsababishia kifo!
Kwasasa nachukia sana kuona mtu akipuuza upendo wa anayempenda laiti kama ningekuwa upepo ningevuma na utenzi huu, kutambulisha duniani thamani ya upendo.

Upendo sio bidhaa, kupatikana dukani,
Wala sio chokaa, pambo la ukutani,
Upendo labda sanaa, ipendezayo moyoni
Tena ikisambaa, furaha kote nyumbani.

Upendo ni mshumaa, nuru yake gizani,
Tamati yake balaa, totoro giza machoni,
Kama nikitambaa, hufuta chozi jichoni
Dhambi kumhadaa, mwenye upendo moyoni.
INATOSHA

Na,

Omar Zongo

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »