BABA


....Faraja kwa mara ya kwanza tangu kuanza Shule ile alisimama mbele ya wanafunzi wenzake, akijaribu kuelezea kitu ambacho yeye hakukijua vizuri lakini mradi mama yake alimuelezea na kilimuhusu baba yake aliona kuna haja yakuwaleza wenzake.....

Na
Omar Zongo 

Ilikuwa ni asubuhi tulivu mishale ya saa ikimuelezea mtazamaji kuwa ni saa tatu na dakika kumi na saba.
Ilikuwa ni katikati ya wiki siku ya jumaatano, wanafunzi wa shule ya msingi Mdote wakiwa darasani kufuatilia ratiba zao za kawaida za masomo hali ilikuwa ni tofauti kidogo kwa upande wa wanafunzi wadogo wa darasa la tat
u ambao wao walikuwa wakipiga kelele mfululizo kana kwamba wako kwenye gulio.
Idadi kubwa ya wanafunzi waliomo kwenye darasa lile ilitosha kufanya madawati yawe kidogo hivyo wanafunzi wengi kulazimika kukaa chini huku wenyewe wakionekana hawajali kabisa suala lile na waliendelea kukimbizana kucheza nakuzungumza kwa sauti kubwa bila maelewano hali iliyofanya kuwe na kelele kubwa ndani ya darasa lile, hakika walidhihirisha utoto wao, hawakujua watendalo.
laiti wangejua kuwa ukubwa ndio utafuata baada ya udogo ule wakupiga kelele darasani nina uhakika wangetulia wenyewe kisha wakajisomea ili kujiandaa vema nakummaliza adui ujinga ambaye huchangia maisha ya wengi kuwa duni na dhalili.
Kelele za wanafunzi wa darasa lile zilikuja zimwa na mwalimu wao wa darasa, mama mtu mzima kwa makadirio miaka yake ilikaribia 43, alikuwa mfupi kiasi rangi maji ya kunde.
machoni alivaa mawani yake inayomsaidia kuona, nywele zake alizichana vizuri kabisa kisha akazibana kwa nyuma na banio, pale shuleni alitambulika kama Mwalimu Betty.
Nina uhakika alikuwa ni mkali mwalimu Yule na hili lilidhihirika alipoingia tu darasani, ghafla ukimya ukashika hatamu na zile vurugu zote zikatoweka kabisa kiasi kwamba mtu asingeamini kabisa kuwa sekunde chache darasa lile lilikuwa ni zaidi ya soko.
“Heeeeeeshima..” ghafla ilisikika sauti hii ya kijana mmoja mdogo ambaye alikuwa ni kiongozi wa darasa lile, na punde tu baada yakusema neno hilo darasa zima likalipuka kwa kutoa salamu kwa mwalimu wao, walisikika wakijibu.
“Eeelimu ni ufunguo wa maisha shkaaamooo mwaaaalim” walitoa salamu hii wanafunzi wale kwa mtindo kama wanaimba kwa pamoja.
ilipendeza sababu maneno hayo waliyatoa huku wote wakiwa wamesimama, kudhirisha heshima kwa mwalimu wao.
mwalimu Betty aliwajibu huku akisjipenyeza katikatia ya wanafunzi waliokuwa wamekaa chini, alionekana akijitahidi kupita kwa umakini ili asije kuwakanyaga maana walishonana vyakutosha!
dakika chache mbele baada ya mwalimu Yule kuwemo mule darasani ndipo nabaini kuwa ni Tofauti kabisa na ile dhana yangu ya mwanzo kumbe mwalimu huyu alikuwa ni mcheshi, mpole na anayependwa mno na wanafunzi wake kutokana na haiba yake.
“Wanangu, hamjui kuwa kelele zenu mnazopiga zinafika mpaka kwenye ofisi ya mwalimu mkuu, hamuogopi kuchapwa fimbo za mgongo asubuhi yote hii???” Alizungumza kwa upole na upendo mwalimu Yule huku akizungusha macho kutazama wanafunzi wake wote waliomo mule darasani, akaendelea
“Muda ambao darasani hakuna mwalimu, msiwe mnapiga kelele, hakikisheni mnajisomea tunakaribia kuanza mitihani hivyo mkiwa hamsomi mtafeli, sawa watoto eee?” Alisema tena kwa kuwabembeleza wanafunzi wale ambao wengi wao walionekana na sura za kudeka kana kwamba wamemuona mzazi wao anayewapenda.
Hakika kwa mja yeyote mtafiti bila shaka angeweza kubaini kuwa kuwanyamazisha watoto watukutu sio lazima kuwafokea, kuwa mkali au kuwapiga.
Watoto kumbe huweza kunyamaza tu wenyewe wanapoona kitu wanachofanya hakimvutii mtu wanayempenda na pia ni rahisi mtoto kunyamaza anapoiona sura ya mtu anayemfariji maana hutaraji kumbatio lenye tulizo.
hii ilijidhihiri kupitia mwalimu Betty, yaani kitendo cha watoto kumuona tuu mwalimu wao mpendwa wote walijikuta wananyamaza nakutega sikio kumsikiliza anachowaambia.
“nimekuja kuwaambia kuwa mwalimu wenu wa hesabu leo hayupo, hivyo nataka kuwapa fursa ninyi muelezee kitu chochote kuhusu Baba zenu, lakini kabla mtu hajasimama kunieleza kuhusu Baba yake nataka mtoto mzuri yoyote aanze kusimama nakunieleza kwanini leo tumuongelee baba na sio mama, atakayenijibu vizuri nitamnunulia visheti wakati wa mapumziko..”
Alisema Mwalimu Batty na alipomaliza tu watoto baadhi walionekana kunyoosha mikono juu lakini idadi yao ilikuwa ndogo sana ukilinganisha na watoto wote waliopo kwenye darasa lile, hii ilidhihirisha kuwa wengi walikuwa hawajui kwanini mwalimu wao amewataka wazungumze kitu chochote kuhusu baba.
Mwalimu Betty alichagua watoto wanne mfululizo lakini hakuna aliyetoa jibu la swali lake mpaka aliposema anamchagua wa mwisho ndipo akamchagua binti mdogo aitwae Asha.
binti huyu alijibu kwa uzuri kabisa ingawa alionesha kuwa hajiamini alisema huku aking’ata vidole vyake kwa aibu “Leo ni siku ya Baba Duniani”
Alijibu Yule mtoto kwa aibu ingawa jibu lake lilisikika na hata hakungojea kusikia kama amepata au amekosa aliwahi kukaa nakujificha kwenye dawati kwa aibu, Asha akiwa amejificha akashangaa kumsikia mwalimu akiwaamuru wenzake wampigie makofi maana amepatia.
akili yake ikarudi nyuma asubuhi alipomsikia mama yake akisema kuhusu siku ya baba duniani, yeye alibahatisha tu kujibu wala hakujua kama angepatia.
Hata Mwalimu Betty hakutaraji kupata jibu sahihi la swali lile tena mbaya zaidi kwa watoto wa darasa la tatu, alimpongeza Asha kisha akawataka watoto walio tayari kuongelea kitu kuhusu baba zao.
Kila mtoto alikuwa na namna ambavyo alilipokea swali la mwalimu Betty, wapo ambao vichwa vyao vilivuta kumbukumbu ya baba zao nyumbani, wengi waliona ukali, ulevi na ubabe, na hata mwalimu Betty alipowagusa baadhi yao walielezea baadhi ya sentensi zao ni “Baba yangu mlevi” wapo waliosema “Baba yangu ni mkali huyo” mwengine akasimama nakuwavunja mbavu wenzake akisema “Baba yangu ni Mwanaume anaendesha pikipiki prupruuupruuuu” huku akionesha kwa vitendo.
Pia wapo ambao walikosa kabisa chochote chakuzungumzia kuhusu Mtu Baba miongoni mwao ni Faraja, Kijana mdogo haiba yake ni upole na hakuwa mtoto mgomvi kama walivyo watoto wengi darasani mwao.
wakati mwalimu anauliza swali hili Faraja akili yake ilijikuta kwa mara ya kwanza anauona utofauti wake na wenzake, ni hapa ndipo alipogundua kuwa duniani kuna mtu anaitwa baba, nae ni mzazi tena ana umuhimu na zaidi wenzake walio wengi darasani kwao wana baba.
sio kwamba Faraja alikuwa hajui kitu chochote kuhusu baba laa hasha ila hakuwahi kuzingatia kuhusu yeye kuwa na baba na umuhimu wake na athari zake, kwa mara ya kwanza akili yake changa ikaanza kumtafakari upya mtu huyo baba ndipo alipokumbuka kisa kimoja ambacho mama yake alimuelezea kuhusu baba yake.
Muda ambao anakumbuka kisa hiki kuhusu Baba yake ndio muda ambao Mwalimu Betty alimtaja Faraja aende mbele akazungumze kitu chochote kuhusu Baba.
Mwalimu Betty akiwa ametuliza macho yake kwa Faraja ndipo alipogundua Faraja ametuliza macho yake kwenye mkono wake wa kushoto, Faraja alionekana anatazama kwenye mkono huo ambapo palionekana kovu moja kubwa sana jeusi.
Faraja alionekana akitazama kovu lile na ghafla machozi yakaanza kumtoka! ajabu hakuweza kujizuia kutokwa na machozi na pia hakuweza kujizuia kwenda mbele alipoitwa na mwalimu wake.
Watoto wenzake wote walijikuta wanamshangaa Faraja, walishangazwa na kitendo chake chakufuta machozi wakati wala hajapigwa, wao walizoea kuona mtu akilia baada yakutoka kucharazwa bakora.
Mwalimu Betty huruma ikamuingia, alijikuta anamwambia Faraja apumzike atazungumza nae baada ya muda ule bila shaka alihisi labda amemkumbusha tukio la kuhuzunisha kuhusu baba yake hivyo hakutaka kuendelea kumuumiza lakini ajabu Faraja alikataa na akamwambia kwa upole mwalimu “Hapana Mwalimu namimi nataka kuelezea kitu kuhusu Baba....”
Mwalimu Betty alishangazwa na ombi lile na hakujua nini anataka kuzungumza Faraja kuhusu Baba yake ghafla akajikuta nayeye anatamani kujua, akatafakari kwa sekunde kadhaa kisha akaamua amruhusu.
Faraja kwa mara ya kwanza tangu kuanza Shule ile alisimama mbele ya wanafunzi wenzake, akijaribu kuelezea kitu ambacho yeye hakukijua vizuri lakini mradi mama yake alimuelezea na kilimuhusu baba yake aliona kuna haja yakuwaleza wenzake.
Darasa lote sasa likawa kimya kumsikiliza Faraja...

INAENDELEA.......

Na

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »