Kwa sasa ni zaidi ya miaka 40 tangu kujiri kwa mauaji ya watoto hawa wa afrika kusini, watoto ambao damu zao zingali puani mwetu hadi hivi leo, sauti zao za kilio chakupigania roho zao bado zimetanda katika anga la afrika nakufanya kila ifikapo tarehe 16 mwezi wa sita tusimame nakuenzi Kilio cha mtoto wa afrika!
Naomba nikurejeshe nyuma kimawazo, naomba nikukumbushe sababu rahisi za watoto hawa wa shule wapatao 600 miili yao kugaragazwa chini kwa risasi za kaburu mjaa lana!
eti ni kwasababu damu hii changa ya mtoto wa afrika ilikuwa barabarani ikifanya maandamano ya amani kupinga mtaala mpya na lugha ya Afrikaan kutumika katika kufundishia..
hiyo ndiyo sababu naamini sasa utaniunga mkono kauli yangu ya kuwa ni sababu rahisi ukilinganisha na adhabu ya kifo iliyowashukia!
Ninani angezuia risasi ya Kaburu na wakati muda huo kina nelson Mandela walikuwa jela??? Afrika yote iligubikwa na simanzi..
Mungu awalaze pema watoto hawa wa afrika! damu zao bado zinalilinda bara la afrika na kila aina ya baya kutoka kwa maadui wake...
Nataka kukamilisha Ripoti yangu kwa ukamilifu wakukujulisha dhima yakuandika ujumbe huu katika siku hii ya kukumbuka mauaji ya Soweto!
Mosi, uzalendo wangu kwa watoto wa Afrika na bara langu la Afrika kukumbuka tukio hilo la kikatili lililotokea miaka 39 iliyopita, bado lina simanzi na makiwa moyoni wangu.
Pili, kuonesha enzi hizo umoja, msimamo, mshikamano na uzalendo ulivyowajaa, si watu wazima tu bali hata watoto shuleni, walivyokuwa na hamasa na ari kupinga utawala uliojaa ubaguzi wa rangi, dhuluma, mateso na manyanyaso, uliofanywa na walowezi makaburu dhidi ya wenye mali na nchi – Waafrika.
Tatu, kusisitiza umuhimu wa elimu shuleni. Masomo ndiyo shule. Walimu, vitabu, madawati, majengo na kadhalika ni njenzo za kufundishia na kujifunzia kupata elimu bora. Kuweka mitaala na lugha isiyofahamika ya kufundishia, ukweli ni kubagua utaratibu mzuri wa utoaji elimu bora na hatimaye kuua elimu na kuwafanya watoto kuwa wajinga. Elimu ni hazina kubwa na urithi wa uhakika usio na mtetereko.
Nne, kukumbusha na kufahamisha daima adui ni nduguyo na kikulacho kimo maungoni mwako. Watoto wale walifyatuliwa risasi na askari 48 waliopangwa kutekeleza operesheni ile. Kati ya askari wale Wazungu walikuwa wanane na Waafrika walikuwa 40.
Sababu hizo zimenifanya leo kushika kalamu kuandika na kutia ubani kuwaombea rehema kwa Mwenyezi Mungu. Laiti watoto wale wasingenyang’anywa uhai wao hapana shaka baadhi yao leo wangekuwa walimu, viongozi wa serikali au siasa, waganga na wauguzi, manahodha na marubani, madereva na mafundi mchundo. Achilia mbali wahandisi na wataalamu. Bila kusahau viongozi wa dini, wanamichezo na wasanii, polisi na askari jeshi na waandishi wa habari wangepatikana.
Leo hatunao tena watu hawa, uwepo wao umebaki katika historia vichwani mwetu na wengi wao wakizisoma vitabuni..
wazalendo wabara letu hatutaacha kuenzi kwa kilio kila linalosababisha machozi kwa waafrika na tutaendelea kuenzi kwa tenzi.....
Muafrika amka, simama imara
muda ushafika, Muafrika ni Bora
Mja alo tukuka, Bara letu Dira
Soweto maafa, twawezaje sahau.
Haki yao, kosa lao,
kifo chao, lana kwao,
Damu zao, dhambi yao
kaburu mjaa lana, hatutokusahau.
Na.
Omar Zongo