Hasira zilinipanda kiasi chakunivimbisha koo, pale chini niliendelea kumburuza kwa mateke sikujali hata sauti yake iliyokuwa inaniomba msamaha, kwangu nilimuona muuaji,iweje wivu wake tu wa mapenzi anishikie kisu, eti kisa kaona ujumbe mfupi wa mwanamke kwenye simu yangu akiniita ‘bae’.
nilifululiza kumshushia mvua ya kipigo mpaka nilipokuja kugundua baadae kuwa nimemzimisha.
Hapa ndipo akili iliponirudi nikabaini kuwa nilitumia nguvu kwa mwanamke, sikuona chakujisifu zaidi nilijidharau sana kwa kujiona si lolote maana kama ningekuwa mkamilifu nisingeweza kumshambulia vile mwanamke kama vile napambana na mwanaume mwenzangu,
Nafikiri kama ningekuwa na hata chembe ya ubinaadamu ingetosha tu kumnyang’anya kile kisu nakumpiga vibao viwili tu kumuonya kisha nikaachana nae, lakini loh! Jazba ilinipanda mtoto wa kiume nikamshambulia kama mbogo na sasa nimemzimisha kwa kipigo ndipo nabaini kuwa sina ubinaadamu ndani yangu, nasijui nipo kwenye fungu gani maana hata wanyama wenyewe kwa wenyewe wakati mwengine huoneana huruma.
Akilini mwangu chanijia kisa cha nabii Muhammad (S.W.A) Katika shughuli yake yakusambaza dini ya kiislamu alifika sehemu makafiri wakamshambulia kwa mawe mpaka kumtoboa mwili wake damu zikawa zinammiminika, kwa vile ni Nabii kipenzi cha Rahman, akashushiwa malaika kiongozi wa miamba akamuuliza mtume vipi tulete Jabari liwabane watu hawa???
Nafkiri kutokana na unabii wake na uchamungu Mtume Mohammad (S.W.A) akakataa nakumwambia Mungu awasamehe watu wale maana yeye alichokipenda ni Ukaribu wake na Mungu pekee, hivyo mradi Mungu yupo pamoja nae inatosha.
Kilinirudia kisa hiki kichwani nikabaini kuwa Ubinaadamu sinao hata chembe na kamwe siwezi kuwa na sifa hata ndogo tuu ya unabii.
Akili yangu ikakumbuka mafunzo yakwake Issah Bin Mariam almaarufu kama YESU, aliwahi kusisitiza kumgeuzia adui yako shavu lakulia pindi akikuchapa kibao kwenye shavu la kushoto Afanaleki!! Hiki nacho ni kitu kidogo tuu lakini kwa kukiwaza tuu mwenzenu sikiwezi bado naendelea kusema Ubinaadamu sinao na Unabii ndio sifanani nao hata chembe.
Kama haitoshi huyuhuyu Nabii Issah aliwaombea msamaha kwa MUNGU waliomsulubu akisema kuwa ‘hawajui watendalo’!!!!!.
Hakika Itikadi za watu kama hawa tumewazika nazo maana hazijawahi kuonekana mahala popote katika dunia ya leo.
Nina uhakika si mimi tu niliyemzimisha mwanamke wangu wengi duniani pia wamenyimwa ubinaadamu na unabii pia hawafanani nao, mfano mdogo ni wewe unapopata nafasi yakuombea wabaya wako, je ni kweli unawaombea mema kama ambavyo vinaelekeza vitabu au ndio unawaombea mabaya wanayokufanyia yawarudie..
Walijisemea waswahili wakale mabingwa wa hekima ‘Ubinaadamu kazi’, Uhakika ninao namimi nikiwa shahidi katika maombi yangu sijawahi kukumbuka hata siku moja kumuombea kwa MUNGU msamaha mbaya wangu, zaidi hua namuombea njaa ili apotee kwangu iwe furaha.
Ni hapa ndipo nabaini pia MUNGU ana kazi kubwa sana katika dunia hii! Nilishapata wazo siku moja kwa mfano ningepewa mamlaka yake, naona kabisa namna ambavyo watu wa ukoo wangu wangenufaika, marafiki zangu na jamaa wote wa karibu yangu wangepata yote wayatakayo tena kwa wakati bila kuchelewa.
Ingekuwa ni pigo na maumivu makubwa kwa wale wasio nihusu au wenye mgogoro namimi wa aina yoyote ile, na hili ni tofauti na MUNGU yeye huwabariki hata wanaomkosea.
Umimi huo ndio unazidi kunifanya nimtukuze Rabbuka, hakika yeye ametukuka, Bingwa wa kusamehe na hajawahi kuwa na upendeleo kwa waja wake…kupitia ubinaadamu aliouumba nakuelezea sifa zake kwenye vitabu vya dini nakiri kuwa mimi sina ubinaadamu na namna ambavyo amewafanya manabii wake wakawa, nakubali wazi kuwa unabii ndio kitu sikiwezi kabisa, yaani ubinaadamu kwangu kazi na unabii ndio mzigo mzito kabisa.
Hebu ona Nabii Ayoub alivyopata jaribio la Shetani, ibilisi mjaa lana!.
Nabii Ayoub alikuwa tajiri aliyegeuka fukara kwa kupoteza watoto wake wote na mali zake zote. kama haitoshi Akagaa gaa na maradhi kwa miongo kadhaa lakini bado hakuingia katika mitego ya shetani iliyomtaka amkane Mungu.
Nabii Ayoub aliugua nakuoza mwili wake woote, maradhi yake hayajawahi kupata kufanana na maradhi ya aina yoyote katika dunia hii lakini hakuwahi kufikiria kuwa MUNGU amemtenga licha ya kuwa Ibilisi alimwambia hivyo.
Na hata siku ambayo MUNGU anamshushia tena malaika jibril baada ya kitambo kirefu Ayoub alisita kuitikia salamu ya malaika huyo sababu kuna funza alikuwa anatafuna mnofu wa ulimi wake hivyo kuitikia salamu ile alihisi atamsumbua mdudu Yule ambaye alikuwa anajipatia mlo wake, Laa haulla wala akwat! Ninani mwenye kuweza haya jamani!!
Yote haya tisa kumi muone kiumbe huyu ambaye amepewa na MUNGU nusu ya uzuri wa mwanadamu, yaani nusu iliyobaki ndio tumegawana sisi ambao leo tunajiona mahandsome boy na mapretty girl, si mwengine bali ni Nabii Yusuph radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie.
Ni yeye ndiye ambaye alilaghaiwa na mke wa mfalme mwanamama aliyeumbika haswa, tena mbaya zaidi chumbani wawili mwanamke huyu akamvulia Nguo Yusuph akimshawishi wazame hubani, lakini Yusuph kwa hofu Ya Mungu alikataa kwa kujiziba ukutani akiyaonya macho yake yasitalii uzuri wa mwanamke Yule, labda nahisi alidhani akiruhusu kuona angeweza kujikuta anamparamia mithili ya fisi aonapo mfupa, Yusuph alinusurika na dhambi hii na hakushiriki kamwe tendo hilo ulipendalo mwanadamu wa sasa!
Tabia hii Ya Yusuph naona alikuja nayo kwa dharula tu duniani na alipoondoka kaondoka nayo maana sina uhakika kama katika kundi kumi la vijana wakileo kuna wawili ambao wanaweza kushinda kishawishi cha aina hii.
Nasema kwa kujiamini maana jicho hilo linajionea mengi na kubaini kuwa dunia hii ndio ambayo mwanamke hushawishi mwanaume hata bila yakuvua.
Kipimo kidogo ni wewe ukiugua kidole tu kwa muda mrefu bila kupona imani yako kwa MUNGU inalega lega na unaelekeza matumaini kwa dokta, kana kwamba Dokta ndiyo kakuumba, Dokta akishindwa unahamia kwa kalumanzira, huko ndio unafanya shirki yakufa mtu, unadiriki hata kuwaekea ubaya ndugu zako sababu umeambiwa na mganga wako kuwa wao ndio wanahusika na kuumwa kwako, Shabash naamini sasa nawewe unasadiki kuwa Ubinaadamu hauna na Unabii ndio haufanani nao kabisa.
Ukubali ukatae..!
Na..
Omar Zongo