BABA : SEHEMU YA PILI

Muhtasari

  “....alitokwa na machozi kwa uchungu, pili aliwafokea nakuwanunia wooote nyumba nzima na zaidi alimkataza mtu yoyote asinishike wala kunikaribia alisema anataka kunihudumia mwenyewe mpaka nipone ....”

Ilipoishia

Mwalimu betty anajaribu kumzuia Faraja lakini Faraja anakataa nakuomba aelezee nayeye kuhusu Baba yake, Mwalimu anakosa namna anaamua kumruhusu na sasa Faraja kwa mara ya kwanza anasimama mbele ya darasa kueleza kitu kuhusu baba yake ambaye hakuwahi kumjua ila alihadithiwa na mama yake....
Sasa Endelea....

“Nilikuwa mnene sana, nilikuwa nawachosha ndugu zangu hivyo kama mtoto sikuwa nafaidi kubebwa maana uzito wangu ulikuwa adhabu kwao.
katika nyumba yetu ni Baba na mama tu ndio waliweza kunibeba bila kulalamikia uzito wangu au kusema kuwa nawachosha.

Kuna siku dada yangu ambaye ndiye aliniachia mimi ziwa aliambiwa akae na mimi huku dada yangu mkubwa akiwa ananiandalia uji wangu wa ulezi.

Dada angu mdogo alinibeba kidogo tu akachoka ikabidi aniweke chini ili apumzike, bahati mbaya nayeye akanogewa na michezo yake yakuchezesha akanisahau kabisa na wala hakujua kuwa mimi aliponiweka chini nilikaa kidogo kisha nikaanza kutambaa kumfata dada angu mkubwa ambaye alikuwa anapika.

nilifika jikoni, dada mkubwa alikuwa hayupo! uji tayari ulikuwa umeiva na ameuweka kwenye chupa sasa jikoni ilikuwa ni zamu yakuchemsha maziwa.

Mimi nikiwa sielewi chochote kuhusu moto nikajikuta navutiwa na namna ambavyo moto ule unawaka, nasemea akili zangu zile za utoto bila shaka zilivutiwa na rangi ya moto au pengine namna ambavyo maziwa yanachemka nikajikuta najivuta karibu na jiko nakupeleka mkono wangu,
masikini mimi nilivuta sufuria ile ya maziwa ambayo tayari yalishaanza kuchemka, nahisi Ile ilikuwa ni siku yangu yakufa lakini naamini kutokana na udogo wangu malaika wa huruma waliweza kunitetea ili adhabu ya maziwa ya moto isinimalizikie mwilini.

nilipiga kelele za maumivu baada ya maziwa yale ya moto kunimwagikia mkononi mwangu, kwqa akili zangu za utoto nilihisi moto unanichokoza maana sikuelewa kabisa kama moto hauna akili wala kujua kama mimi ni mtoto.

kelele zangu ndiyo zilimtoa dada chumbani haraka na wakati anafika tayari nilishamwagikiwa na maziwa.
Dada alilia sana ajabu alilia huku akisema kuwa atakuja kumwambia nini baba angu! woote nyumbani kwetu walikuwa wanasema eti nilikuwa napendwa mno na baba tangu nikiwa mtoto mchanga nina siku moja.

muda janga lile linanitokea wazazi wetu walikuwa wameenda mjini kwenye mihangaiko yao, waliporudi jioni looh! mama yangu alihuzunika sana lakini hakulia wala kuwafokea sana dada zangu kwa kutokuwa waangalifu lakini baba yeye aliyafanya hayo yote.

Kwanza alitokwa na machozi kwa uchungu, pili aliwafokea nakuwanunia wooote nyumba nzima na zaidi alimkataza mtu yoyote asinishike wala kunikaribia alisema anataka kunihudumia mwenyewe mpaka nipone.
kila siku baada ya siku ile alikuwa haishi kuwalaani dada zangu kuwa wana roho mbaya yaani alikuwa ameumizwa mno namimi kuungua wakati nikiwa sijui lolote la dunia hii alijilaumu yeye na kuwalaumu wote akisema kuwa wana roho mbaya na mimi malaika mdogo ambaye sijui lolote.

mpaka muda huu naelezea kuhusu baba yangu nasikitika sana kuwa sina vitu vingi sana vyakuelezea kuhusu yeye kwa sababu sijui lolote tena kuhusu baba yangu, maana ni katika kipindi kilekile baada yakupona yale majeraha yakuungua mwaka mmoja mbele Baba yangu huyu akafariki dunia.

Tangu hapo sikuwahi kumuona baba mwengine zaidi ya mama kuniambia baba yangu alikuwa na upendo mkubwa na familia yake na kunielezea baadhi ya matendo yake hayo mazuri yenye utu, mie sikumbuki kitu wala sijui kama niliwahi kuishi na mtu wa waina hii, wakati mwengine mama  akinisimulia hua nahisi kama ananipigia tu hadithi za kale.

Kinywa change hakina mazoea yakutamka Baba na hata kama nikilinganisha idadi ya kutamka neno baba na mama bila shaka Neno Mama linaweza kuongozwa kwa kutajwa sana namimi kuliko Baba, na siku ya leo naomba nitumie nafasi hii kusema kuwa  Nampenda sana Marehemu  baba yangu, japo simjui na najisikia vibaya leo kugundua kuwa wenzangu wengi kumbe mna baba zenu!
wapendeni msiwatenge kumbukeni kuwa nao ni wazazi wenye huruma kubwa kwetu na upendo pia....”
Kufika hapa Faraja alishindwa kuendelea, kwa mara ya kwanza alihisi upweke wakulelewa na mama yake pekee, kwa mara ya kwanza alijihisi ana mapungufu jambo ambalo mama yake mzazi alilipigania siku zote lisijitokeze kwa mwanae.

alihakikisha anampa kila kitu ambacho watoto wengine wenye baba zao wanapewa ili mwanae asijione mnyonge lakini juhudi zake ziliishia siku hii...kwa mara ya kwanza Faraja akatamani baba yake naye angekuwepo lakini aliumia zaidi kugundua kuwa hakiwekezekani kitu hicho.

MWISHO....

“wakati mwengine ni busara kuigiza ukamilifu ili uwe mbali na makosa, Igiza ukamilifu ili wengine wasione udhaifu wako, Igiza ukamilifu kwa namna yoyote ile”

IgizaUkamilifu2017

Na

Omar Zongo

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »