SEHEMU YA 1
"Habari hii nilikuwa naisikia sana kwa watu wa Mungu hasa masheikh duniani wakisema kuwa Shetani hufungwa wakati Ramadhani inafika lakini ilikuwa haijanisisimua kama alivyoniambia Rafiki Yangu Ramadhani, chuki dhidi ya huyo kiumbe aitwae Ibilisi ikanivaa, sasa nikawa natamani kumuona"
KIZIMBA cha IBILISI
Na
Omar Zongo
Anaitwa Ramadhani, rafiki yangu asiye na ubaguzi, mpole mnyenyekevu na mwenye kufundisha mema! Hakika sikuwahi kujuta kufahamiana na Mja huyu mwenye kila dalili za utu wema.
Kinachoniuma zaidi ni licha ya kuwa ni mwema na ningependa kuishi
nae milele lakini desturi yake ni kunitembelea mara moja tu kwa mwaka na hakuna namna ambayo naweza fanya kubadili
desturi yake hii.
Miaka yote anakuja naishi nae akinifundisha namna yakuishi
kwa kufanya matendo mema yenye kumpendeza Mungu muumba aliyenifanya mimi nikawa
kwa amri ya neno lake moja tu, miaka yote namfurahia Ramadhani lakini mwaka huu
nimefurahia zaidi ujio wake maana ameweza kunipa fursa namimi nikatembelee
mbinguni, mahala ambako yeye ana uwenyeji napo.
Safari yetu yakufikirika ilianza taratibu nikimuona wazoni
rafiki yangu Ramadhaani akiwa amevalia kanzu nadhifu na baraghashea iliyomkaa
vema kichwani, alivaa viatu vya mikanda na kama kawaida sura yake yenye
tabasamu lakudumu ilikuwa ikinitazama mimi niliye pembeni yake.
Alinishika mkono kwa upendo na wakati mwengine akiweka
mikono yake begani kwangu kuonesha udugu alio nao moyoni mwake, tulikuwa
tunapiga hatua kuelekea mahala Fulani ambako mie sikupajua ila yeye alidai
anapafahamu na akanieleza kuwa ndipo ambako safari yetu ya mbinguni itaanzia
hapo.
Katika muda wote tuliokuwa tukiongozana Ramadhaani hakuacha
kunipa simulizi nzuri kuhusu mahala Fulani paitwapo peponi, alisema ni miongoni
mwa maeneo yaliyo mbinguni ambayo yameumbwa kitaalamu sana na kila kilicho
kizuri duniani basi uzuri wake uliongezeka maradufu peponi.
Alisema akitolea mfano asali, moja ya vitu vitamu mno duniani,
anasema asali ya Mbinguni imetengenezwa kwa utaalamu wake kiasi ambacho kama
ukiionja utabaini kuwa ya duniani si chochote.
Akawagusia walimbwende wanaopatikana peponi, anasema hakuna
mfanowe duniani hapa, alinikosha zaidi alipotaja matunda na vyakula adhimu
vilivyopo huko! Nikajikuta natamani hata leo niende nikaishi huko hasa
aliponiambia kuwa huko hakuna maradhi, kuzeeka wala kuumwa.
Udenda wa tamaa yakuiona pepo ukanitoka, nikajikuta nauliza
kizembe “Nini chakufanya ili mtu uende ukaishi huko?” swali langu hili nasema
nimeliuliza kizembe sababu jibu lake nilikuwa nalijua lakini sijui nini
kikanifanya niulize, uzuri Rafiki yangu Ramdhaani sio mtu wakuchoka kuongea na
mtu wala kukosoa maana yeye hana sifa ya wivu, alinijibu swali langu bila shida
yoyote.
Alisema “pepo hiyo imeumbiwa binaadamu wote lakini
kinachoumiza ni kwamba sio wote wataiona isipokuwa wale wachamungu na wenye
kutenda mema duniani kwa kiwango kinachomridhisha Mungu Muumba vyote” Jibu hili
likanifanya nijitathmini kwa muda nikajikuta natilia shaka matendo yangu, amani
ikatoweka hasa nilipokumbuka kuwa kuswali ni kitu ambacho sikizingatii, Kutoa
sadaka ni kwa hiyari yangu na pia ni bingwa wakuwazini mabinti wa watu bila
kufikiria kuwaoa.
Dah Moyo ulipatwa na joto kuu, nilihisi wazi kuwa naungua
moyoni Mwangu, hata hivyo nikajifariji kuwa nitaendelea kubadilika maana tangu
aje rafiki yangu Ramdhani angalau matendo maovu nimeyaacha kabisa.
“Najua unachohofia” wakati nikiwa nawaza namna gani
yakubadilika kabisa nakuwa mcha Mungu ghafla Rafiki yangu ramadhaan nikamsikia
akisema hivi, nilishtuka nikamgeukia,
“Ndiyo, najua unachokihofia lakini acha nikwambie. Usijali
leo nitaenda kukuonesha Kiumbe mmoja aitwae Ibilisi, ni kiumbe huyu ambaye aliapa
mbele ya Mungu Muumba kuwa atahakikisha anaingia motoni na Binaadamu wote
ikibidi”
Alisema kwa sauti yenye utulivu Ramadhani, ile ilikuwa sio
habari ngeni kwangu lakini wakati inatoka kinywani mwa Ramadhani nikahisi kama
ni habari mpya na nikajikuta naweka utulivu zaidi ili kumsikia Rafiki yangu akizungumza
zaidi kuhusu Ibilisi, Bila shaka Ramadhani aliuona Umakini wangu, akaendelea.
“Ibilisi hutumia mbinu zote kumpotosha mwanadamu ili atende
uovu na amchukize Mungu wake, na hakuna siku ambazo ibilisi anachukia sana kama
siku akisikia mimi nakuja duniani kukutana nanyi…”
Aliendelea kusema Ramadhaani huku mimi nikimsikiliza kwa
makini.
“kwa kawaida Ibilisi hukamatwa nakufungwa minyororo huko juu
mbinguni kipindi ambacho mimi nafika duniani kukutana na wanadamu, na ndio
maana kipindi hiki binadamu wengi mioyo yao huongezeka ucha mungu na wengine
hudiriki kuswali sana maana hakuna anayewazuia kufanya hivyo, suala hili
Ibilisi halipendi sana na huumia akisikia watu wanamcha Mwenyezi Mungu ukweli
wa kumcha, leo nataka nikifika nawewe
mbinguni nikupeleke mahala ambapo ni kizimba anachofungiwa Ibilisi ili
ukamuone…”
Habari hii nilikuwa naisikia sana kwa watu wa Mungu hasa
masheikh duniani wakisema kuwa Shetani hufungwa wakati Ramadhani inafika lakini
ilikuwa haijanisisimua kama alivyoniambia Rafiki Yangu Ramadhani, chuki dhidi
ya huyo kiumbe aitwae Ibilisi ikanivaa, sasa nikawa natamani kumuona.
Muda tunazungumza tulikuwa tunatembea na sasa tayari
tulishafika mahala ambako Ramadhaan akaniambia kuwa ndio mahala pazuri pakupaa
nakuelekea huko mbinguni, mahala ambako sikuwahi dhani kama nitafika hata siku
moja, Ajabu leo nilikuwa safarini nikipelekwa huko kwambaali hofu ilinivagaa maungoni lakini kwa
sababu pembeni yangu alikuwepo Ramadhaani akiniongoza kamwe hofu haikupata
nguvu kubwa.
Kufumba nakufumbua sasa nilikuwa mbinguni, pembeni yangu
alikuwepo Ramadhaani akiniongoza.
“Sasa tumefika” alisema kwa mtindo wakunong’ona na mimi hapa
ndipo nilipogundua kuwa mahala pale hapakuhitaji kelele hata ndogo maana
palikuwa tulivu mno, eneo lile lilikuwa ni mithili ya jumba kuubwa lenye korido
ndefu sana, kwenye korido lile nilikuwa mimi na Ramadhaani tu sikuona mtu
mwengine.
Ramdhani akaniambia kuwa kila chumba katika korida ile kina
kazi yake, ni hapa ndipo nilipogundua kuwa kumbe ile korido ndefu kuna vyumba
vipo pembeni yaani mkono wa kushoto na kulia, wazo la vyumba vya gesti
vinavyokaa duniani likanijia, lakini nikalikemea libaki huko huko ndani maana
nilihisi dhambi kufananisha eneo lile Mbinguni na Vyumba vya nyumba za kawaida
duniani.
Rafiki yangu Ramadhani akaniambia kuwa kila chumba kina
shughuli yake, akasema kuna chumba ambacho mlango wake ni wamotoni, yaani
ukiingia ujue umeingia motoni, akasema pia kipo chumba ambacho wanaishi malaika
na vyengine vingi tu, nilitamani kuona maandishi milangoni yakielekeza chumba
cha hukumu ni kipi lakini sikuona yaani vyumba vyote vilifungwa lakini
haikujulikana chumba kipi kina kazi gani.
“twende kwenye kizimba cha ibilisi” Alisema Ramadhani kama
kawaida kwa mtindo ule wakunong’ona, mie
sikujibu kitu nilikuwa nafata tu maelekezo ya mwenyeji wangu, tukiwa tunatembea
taratibu kwenye korido ile kwambaali nikaanza kusikia sauti za mtu akiongea kwa
nguvu na ukali alisema
“Niachieni, nimesema nifungulieni hapaaaa…” mie sikuelewa
sauti ile inatokea wapi, hofu ikanitanda nikajiuliza ninani huyo, ajabu nikuwa kila tulivyozidi kusogea mahala huko
tulipokwenda ndipo sauti ile ikazidi kuongezeka wakati mwengine mtu huyo alitoa
kabisa lugha chafu akitaka aachiwe.
“Niachieni nimesema nifungilieni hapa, hamuweszi kunifunga
muda wote tuu niachieniiii….” Ilisikika sauti hiyo ikisema.
“Tumefika” Alinong’ona tena Ramadhani na nilipotazama mahala
nilipoambiwa tumefika nikaona tupo nje ya mlango mweusi, mlango ule ulikuwa ni
tofauti kabisa na milango yote niliyoipita mwanzo.
Kilichoniacha hoi zaidi ni sauti ile niliyoisikia ilikuwa
inatokea chumbani mule.
“Huyo ni Ibilisi analilia afunguliwe minyororo ili aende
duniani akaendelee kuwakusanya watu wakuingia nao motoni” Loh!! Habari hii
ilinichosha kwakweli, nilikosa chakusema nikabaki namuangalia Ramadhani, moyoni
nikajiwazia hivi kwa mfano akiniacha pale nitakimbilia wapi au nitatokaje
kurudi duniani, wazo hili liliponijia nikazidi kupatwa na woga lakini
nilipokuja kukumbuka wema wa rafiki niliye nae nikajiambia kamwe hawezi kufanya
hivyo.
sasa nikawa namshuhudia Ramadhani akifungua lango lile la
Kizimba cha Ibilisi…wasiwasi na kihoro vikanivaa sikuamini kuwa ni mimi ndio naenda
kumuona Ibilisi huyo mjaa lana.
Inaendelea….