JUNIOR

 "Sikuwahi kusimulia kisa cha kweli nikakiruhusu kusomwa na watu pengine hii inaweza kuwa simulizi yangu ya kwanza yenye ukweli ndani yake, ni zawadi kwa ndugu yangu Ramadhan Madebe ambaye kwa asilimia kubwa amechangia ukamilifu wa simulizi hii....ni sehemu ndogo pekee ndio yakubuni lakini mengi yana ukweli....."

JUNIOR

SEHEMU YA KWANZA

Niliona wivu sana baada ya rafiki yangu kupewa jina na dada yako, yeye aliitwa mwinjuma lakini alimbeza jina lake hilo na akasema kuwa anapendeza zaidi akiitwa Geminus!

Leo ndio nagundua kuwa aina ya familia bora kama ilivyo ya kwenu ndiyo huwaaribu watoto nakuwafanya wayachukie majina ya Kiswahili kutokana na wao kukesha wakitazama filamu za kizungu na kihispania.
Hata kama muhusika mkuu katika filamu ya kizungu akitokea anaitwa Zongo, mradi ni mzungu na anacheza vizuri kwenye nafasi yake basi jina hilo linaweza kuwa ni jina zuri kuliko yote duniani.

Kiukweli licha ya kuwa akili yangu ndogo lakini imebaini kuwa hili ni tatizo ingawa nakiri sina utaalamu wa kutatua tatizo hilo maana ni tatizo kubwa linalohusu saikolojia zetu waafrika.
Nakumbuka Rafiki yangu Mwinjuma alivyobadilika jina nakuitwa Geminus nilikuja kwenu bila haya nikakulalamikia nikakwambia namimi unitafutie jina.

Sauti ya jibu lako bado inajirudia kichwani mwangu “usijali, acha leo nikeshe nikiomba naamini kesho nitakuja na jina zurii ambalo litakufaa”
Hivi ndivyo ulinijibu, nakumbuka nilifarijika sana na nikarudi nyumbani kwetu kwa furaha nikiiomba kesho ifike nilisikie jina langu ambalo umenichagulia wewe.

Sikujali kuwa mimi nimekupita umri na wewe ni makamo ya mdogo wangu, hilo sikulijali kabisa niliona na kukiri kuwa umenizidi upeo.

Sikujali pia umbali wa kila siku kutoka kwetu uswahilini kuja maneneo ya kwenu uzunguni ambapo hii ni kawaida kwa nchi zetu za kiafrika mitaa kujitenga kutokana na vipato vya watu wake.
Nina uhakika kama familia yako ingekuwa na kiburi kutokana na neema ya utajiri basi mimi na rafiki zangu tusingeweza kabisa kukanyaga nyumbani kwenu lakini nashukuru sana na kila siku nauota ukarimu wa wazazi wako, na ucheshi wa ndugu zako.

Nakiri kuwa hii ni historia ya miaka mingi sana ya nyuma lakini bado inaishi kichwani mwangu zaidi siku hii ambayo uliviweka viganja vya mikono yako usoni mwangu.
Ulitaka kuhakikisha kuwa nimeyafumba macho yangu yaani sioni kitu, uliniambia hilo ndilo sharti la wewe kunitajia jina langu jipya ulililonichagulia.

“kuanzia leo utaitwa Junior” hii ni sauti yako ambayo naisikia mpa
ka leo ikitamka maneno hayo, tangu hapo namimi nikajivunia kuitwa Junior.

JUNIOR
SEHEMU YA PILI


Yote hayo yalikuwa yanajiri tukiwa shule ya msingi, mimi nikiwa nimekupita madarasa matatu, sijui kizazi chetu kimekumbwa na nini masikini yaani tunayajua mapenzi tangu tukiwa wadogo.

Ndio maana mpaka leo muda huu unasoma ujumbe wangu bado mwenzako nastaajabu na hila za mapenzi, ukweli ni kwamba kati yetu kulikuwa na upendo! Lakini utoto wetu ulikuwa chanzo cha sisi kushindwa kuelezana ya kwamba tunapendana tena sio kimasikhara yaani tunapendana sana.

Zaidi tuliishia kucheza pamoja huku kila mmoja akifurahia ukaribu wa mwenzake, kwangu mimi ilikuwa siku mbaya sana ikiisha bila kuiona sura yako sijui kwa upande wako.

Mdogo wangu ambaye ulikuwa unasoma nae darasa moja sijui kwanini alikuwa ananificha kuwa mkiwa pamoja hua unanisifia nakumwambia kuwa mimi ni mstaarabu sana, ndio! mimi ni msataarabu na sijui kwanini nilikuacha mwanamke ambaye uligundua ustaarabu wangu tangu nikiwa mdogo.

Nakumbuka zama zile na natamani zijirudie angalau niwe karibu nawe nikiwa na akili za sasa hivi ili nikwambie neno nililostahili kukwambia kipindi kile nikashindwa.
Ujinga wa utoto ulinifanya nikahadaika na binti mwengine ambaye aliibua wivu wako wa kitoto na ukaanza kujifunza kunichukia tangu hapo.

mwisho wakuiona sura yako ilikuwa ni mimi wakati namaliza kidato cha nne, maisha yalitutenga nakutuwekea mpaka mkubwa uliofanya hadi hii leo sura yako ibaki kuwa kumbukumbu tu.
Asante teknolojia walau sasa nakuona mtandaoni.

Sikuamini kabisa kuwa ungenijibu ujumbe wangu mfupi nilipokusalimia kwa mara ya kwanza Facebook, sikuamini pia uliponijibu kuwa ni wewe ndiye Yule mwanamke wangu wa kwanza kuvutiwa nae duniani hapa.
Ujio wako umekuja siku chache tu baada ya maombi yangu kwa mungu pamoja nakufunga ili anioneshee mke mwema. Sababu nataka kuoa mwenzako.

Kukutana tena kwa mara ya pili nawewe imekuwa ni faraja kwangu nikiamini kuwa umeletwa na Mungu.
Kauli yako ya jana ndio imenitoa kabisa kwenye imani yangu! Siamini kabisa kama ni kweli umeolewa na una watoto wawili.

Masikini mimi nilikuwa wapi! Kwanini sikuwahi kujua kuwa ni wewe ndio nilipaswa nikung’ang’anie.
Unasema hauishi kwa amani na mume wako, ni Malaya na hana kabisa upendo. Amekulaghai kwa pesa zake na sasa haioni thamani yako tena.

Ilikuchukua mud asana kunielezea haya, ulikuwa hutaki kwa sababu ya kuficha maovu ya baba watoto wako, lakini nilipokubembeleza sana ndipo siku moja ukanidokeza japo si kwa undani.
Uliniumiza zaidi uliponiambia kuwa jamaa hakupi haki yako ya ndoa,licha ya kuwa unambembeleza sana.
nafsi yangu ni nzito kukwambia utoroke uje maana najua watoto wako wanapaswa kupata haki ya kulelewa na baba na mama yao.
Naogopa kesho huenda wakanihukumu kuwa nilikuachanisha na baba yao, naogopa pia dhambi maana imani yenu haiwaruhusu kuachana kamwe na mnahitajika mpendane kwenye shida na raha kama mlivyoapa siku ile mnafunga ndoa kanisani.

Lakini kwanini urudi wewe mawazoni baada ya kumuomba Mungu anipe mke mwema! Tafadhali nijibu kama ukipatwa na fahamu maana nimeambiwa na rafiki yako kuwa mume wako amekupiga sana juzi na hivi sasa upo chumba cha wagonjwa mahututi, hali yako ni yakuombewa! Maana humjui aingiaye wala atokaye.
Kwanini wanaume tuko hivi, amewezaje kuutendea maovu mti mbichi namna hii au nikwasababu haijui asili yako,
Nakumbuka kuna siku ulizungumza na baba yangu kwenye simu, mzee wangu ni mtaalamu sana wakugundua tabia ya mtu hata kupitia simu, na nilisubiria maoni yake baada ya kuongea nawewe, sikuongopei alikusifia sana na ajabu alipokutaja kwa mama ndio sifa nzuri juu yako zikazidi, wadogo zangu bado wanakumbuka zawadi na upendo wako kwao, kwa mfano mdogo angu Naa mpaka leo kuna gauni lake ulilomzawadia amelitunza sana licha ya kuwa limemruka na halivai tena lakini anasema ni kumbukumbu ya mdada mkarimu aliyewahi kumjua maishani mwake.

Kiukweli najikaza tu nisilie hasa wazazi wangu wanaponiuliza habari zako ninapoenda kuwatembelea, nashindwa kuwaambia kuwa nilikupoteza.

Sasa nafahamu kuwa kweli mimi ni JUNIOR! Ulikuwa mkubwa kwangu kiupeo na ulijua thamani ya upendo licha ya kuwa umri nilikuzidi na ndio maana uliniambia kuwa “huezi kuendelea kuwa namimi maana nimesoma na wewe unahitaji kusoma” aya maneno yako yalikuja baada yakugundua kuwa mimi nina mwanamke mwengine.

Naomba upone haraka unisaidie kunijibia maswali yangu nini nifanye maana niwewe ndiye nimeonyeshewa baada ya kumuomba mungu lakini ni wewe ndiye ambaye kwa sasa ni mke wamtu.
Tafadhali amka Anna kwa sasa mimi sio Junior Tena mtaani wananiita MR experience, nina uzoefu mkubwa na haya maisha na ninajua pia thamani ya upendo.

Plz Anna amka, nipo na wanao hapa Mumeo amesafiri mchana huu kikazi, ndivyo alivyodai wakati amepigiwa simu kuelezewa hali yako lakini kwenye mtandao wake wa kijamii namuona amepost yuko hoteli flani Arusha na mwanadada mrembo lakini hakuzidi wewe Anna,
Plz naomba uamke unipe dira yangu Katika mapenzi…nahitaji kuoa mwenzako.
Na
Omar Zongo

Inaendelea….
SEHEMU YA TATU

UMESAHAULIKA BABA WA KISWAHILI

Imekuwa ni desturi yangu kuenzi harakati zako kila siku hasa kipindi ambacho ni kumbukizi ya kifo chako mithili yakuzima kwa mshumaa uliokuwa ukimulika fasihi andishi yenye tija na akili kubwa kwa miongo kadhaa sasa yaani tangu na baada ya kifo chako.

Baba wa kiswahili, Shaaban Robert  (kuzaliwa 1 January 1909 – kufa 20 June 1962)

Nionacho leo kuhusu kuenzi mchango wako ni USAHAULIFU MKUU, kiukweli UMESAHAULIKA BABA WA KISWAHILI! 

Anasimulia
Omar Zongo 

Naona aibu kusema kuwa natamani ule utashi wako walau ungeuacha sehemu kisha ukaniagiza hata ndotoni nikauchukue niutumie kuendeleza falsafa zako na utamu wa Kiswahili uliopo ndani yako.
Nasikitika ninapogundua kuwa 20 june wakati unafariki ulikusanya kila kilicho chako nakuelekea nacho kaburini, sitaki kusema kuwa hilo limetokea kutokana na uchoyo wako laa hasha ila nakulaumu kwanini hukutaka kumuachia mtu arithi angalau robo ya unguli wako wa kutumia vema hii lugha Kiswahili katika maandishi.
Ni juzi tu nimemrejea Adili na wasifu wake uliomchora nao kwenye ile riwaya yako ya adili na nduguze,hakika nafurahishwa sana na jaala ya mfalme Rai ambaye aliweza kuwa na upendo kwa kila kitu anachokitawala si mnyama, binaadamu hata mmea, alidiriki kujinyima yeye ili vitu hivyo vineemeke.
Umesahaulika Baba wa Kiswahili na sijui kwanini limewezekana hilo kwenye ardhi hii ambayo kwa sasa busara zako zingepaswa zitumike zaidi ili kujenga maudhui sahihi ya utu wema na uongozi bora ndani ya bara letu Afrika.
Naugua maradhi ya kusonona moyo kila nipigapo soga na mabarobaro rika langu ni wachache kati yao wanaokujua,  tena kwa kupapasa papasa.  wengi husalia kuuliza “ni nani huyo baba wa Kiswahili?” nazidi kuamini kuwa umesahaulika nguli wewe ambaye akili yako nikiitathimini kupitia kazi zako naiona imezidi ukawaida.
Enzi zako upo hai wapo waliodiriki kukufananisha na Wilium Shakespare lakini vifo vyenu vimedhihirisha kuwa yale yalikuwa maneno tuu, maana wewe kaburi lako limetelekezwa kule kwenu Tanga, wanaokujali kwa kung’oa  walau majani tu kwenye kaburi lako ni wale waja wenye nasaba nawewena hilo kusema kweli  nitofauti na  Yule mwenzio uliyekuwa ukifananaishwa nae bado kaburi lake ni alama inayosimama kama historia katika anga la waandishi mahiri wa mashairi na riwaya nchini uingereza na duniani kwa ujumla.
Kinachonifanya niugue maradhi yakusononeka moyo ni kwamba wewe ni wajuzi tuu labda kama nakosea au sijui mahesabu, lakini ukweli ni kwamba Willium Shakespare ni wamiaka ya  1564, naomba nirejee tena  elfu 1 mia 5 na sitini na 4 na akafariki mwaka 1616 ingawa inakisiwa lakini ukweli ni kwamba nguli huyo wa uingereza ni wa makarne mengi yaliyopita iweje bado anaenziwa na alama yake bado ni dira kwa vizazi vipya vyote vinavyozaliwa uingereza.
Mwenzangu namimi wewe baba wa Kiswahili ni wajuzi tuu masikini lakini umesahaulika kwakweli! Kuzaliwa kwako ni 1909 na kufa kwako 1962 lakini juhudi zako zimezikwa nawe siku ile kule kwenu mwambani Tanga.

Mwandishi nae ni mtu wa desturi kama walivyo watu wengine hawezi ishi kwa kunywa upepo nakutafuna mawe, bila shaka nukuu yako hii ulitaka kudhihirisha mgogoro wako wa nafsi uliokuwa nao katika kupigania mafao yaendane na kazi zako, kwa maono yangu ni kuwa hapana siku uliyowahi kunufaika na kuridhishwa na ubaba wa Kiswahili.
Naiona lana kwenye anga hili ulilotokea lana itokanayo na sononeko lako la tangu ungali hai na hata miaka mingi tangu kufariki kwako.
Umesahaulika Mzee wangu, baba wa Kiswahili!
Niseme nini namimi sina mamlaka yakuamrisha kuwepo siku ya kuwaenzi ninyi wenye michango yenu katika fani ya ushairi na riwaya.
Nahisi siku hizo zipo lakini kwako wewe ingepaswa kuteuliwe siku maalumu ya kumbukizi kwa Baba wa Kiswahili lakini bado swali linabaki kuwa mimi ninani hasa??
Mchango wako si tu mashuleni kukuza bongo za watoto wetu bali pia ulipigania uhuru kupitia karma yako, zipo sababu zaidi ya bilioni zakukumbukwa lakini iweje uwe umesahaulika hivi.
Naomba niishie hapa maana niendapo naenda kukufuru,
 leo sijaandika barua kwako bali nimepanda kilimani nikiuagiza upepo ufike na sauti yangu uisikie nikikwambia habari hii UMESAHAULIKA BABA WA KISWAHILI.
Nilipo naugua maradhi ya kusononeka moyo sababu kama wewe na utashi wako ule wote umetelekezwa kiasi hicho mimi ninani katika fani ya uandishi mpaka nije angalau kutajwa tu mdomoni mwa waja wa kesho ambao watakuja baada ya mimi, kama sisi tulivyokuja baada ya wewe!.
Habari niliyokupa kupitia upepo uvumao kutoka nilipo kufika huko ulipo bila shaka ni habari mbaya maana hata mimi nisingetabasamu kamwe kusikia nimesahauliwa licha yakupigania hadhi ya lugha wanayojinasibu nayo watu hii leo.
Lakini ningefanyaje wakati niwewe ndio uliwahi kuniasa kuhusu kuwa mkweli, uliwahi sema
Siche kweli kuisema, hata kwa mfalme,
Ingawa inauma, sema kweli atazame,
Kweli ina heshima, wajibu wa mwanamume,
Uongo una lawama, ufukuzeni uhame.

Kweli ina thawabu, wametumia mitume,
Japo wamepata tabu, wamerithi ufalme,
Na waliowaadhibu, hawakumbukwi kamwe,
Kweli ina thawabu, kila mtu aseme.

Hakika sitakuwa mwema kama nikiacha sononeko liendelee kukusumbua naomba tabasamu sasa kwa uetnzi wako huu!

Wadogo kuwa wakuu, kwa watu ndio tabia,
Na wa chini kuwa juu, ni jambo la mazoea,
Mwenendo wao ni huu, wanao kama sheria,
Watu duni na wakuu, katika hii dunia.

Katika dunia hii, ya machungu na matamu,
Na rafiki na adui, na mepesi na magumu,
Viumbe walio hai, hubadilishana zamu,
Lakini hawatambui, kwa uchache wa fahamu.

Sina shaka utenzi huo umekufanya ukafarijika kuona kuwa kazi zako bado zingali nasi zikitusuta suto kuu kwa kukusahau baba wa Kiswahili.

Pumzika kwa amani vijana wenye chembechembe za karma aina yako bado twaendelea pambana ingawa twajua kusahauliwa kwako ni sawa nakunyolewa hivyo nasi tumetia maji nywele.

KIZIMBA Cha IBILISI



Ilipoishia
sasa Nikawa namshuhudia Ramadhani akifungua lango lile la Kizimba cha Ibilisi…wasiwasi na kihoro vikanivaa sikuamini kuwa ni mimi ndio naenda kumuona Ibilisi huyo mjaa lana.
Sasa endelea

Kidokezo

SEHEMU YA PILI


"Tangu kufika kule juu ambako nilielezwa kuwa ni mbinguni sikio langu lilikuwa linapokea taarifa za ajabu tupu, kama ni somo hakika lile nilibahaika kulisoma pekee yangu duniani, nilizidi kumfurahia Ramadhani, nikajikuta namuuliza “Sasa vipi hapa tulipo hawawezi kutuona?"

Na 
Omar Zongo

Chumba kile kilikuwa kidogo ambacho kilimtosha Ibilisi peke yake, aliviringishiwa minyoror mwili mzima ili kudhibiti vurugu zake zakutaka kutoka kifungoni pale.
Kwa harakaharaka niliyachunguza mazingira ya mule ndani nikabaini kuwa kuna joto kali mno, kiasi cha muda ule mchache tu nikawa tayari nimelowa mwili mzima kwa jasho, nilijiuliza Yule ibilisi anawezaje kukaa mule.
Kama vile Ramadhani alijua nini nawaza akajikuyta ananipa jibu “mahala hapa nikaribu kabisa na ulipo moto mkali wa jehanam, moto ambao ni maalumu kwa watenda dhambi ndio maana chumba hiki kinajoto balaa, fanya tuondoke.”
Niliyasikia maneno ya Rafiki yangu Ramadhani lakini sikuyazingatia sana maana mawazo yangu, akili yangu na macho yangu vyote kwa pamoja vilitulia kwa Ibilisi.
Nilimtazama kwa hasira na Macho yangu yachuki dhidi yake yalikutana na macho yake yenye hila, kiburi na kisasi juu yangu na wenzangu wote wenye haiba kama yangu.
Samahani sana tangu nimeanza simulizi hii sijakutajia jina mimi naitwa Abdi ninayetazamana nae muda huu Ni Ibilisi mjaa lana almaarufu kama shetani, Namshukuru rafiki yangu Ramadhani kwa kunipa fursa yakumuona mshenzi huyu ambaye amefungwa mnyororo muda huu.
Nimeambiwa kuwa hapatani asilani na Ramadhan sababu kila akija shetani hufungwa mnyororo nakuzuiliwa kuvinjari duniani, mkataba wakupotosha wanadamu huvunjwa kila mwezi wa ramadhaan unapofika hivyo hubaki na minyororo yake akiwa amefura hasira.
Kabla sijafika kukutana nae nilikuwa namsikia akipiga kelele eti afunguliwe, nilisikia kinywa chake kikitoa sauti iliyobeba ujumbe wenye maneno machafu yaliyosheheni matusi muda wote analalama akitaka afunguliwe ili je kukusanya watu wake wakuingia nao motoni.
Waqkati nikiwa nimesimama namtazama ghafla nikasikia hatua za watu wakija kuelekea mule ndani tulipokuwepo, Ramadhani akanitaka haraka tuchuchumae, nikafata agizo hilo la Rafiki yangu.
Tukiwa tumechuchumaa nikashuhudia watu wenye mabawa meupe, licha ya kuwa walikuwa na muonekano wa ndege na binaadamu lakini walikuwa wanavutia mno kuwatazama, walikuwa ni wazuri balaa!
Rafiki yangu Ramadhani akaninong’oneza “hao ni malaika kutoka duniani, kazi yao kubwa ni kukusanya taarifa zote za duniani nakuja kuzileta huku mbinguni, wanafanya kazi masaa ishirini nan ne na hupokezana, muda huu bila shaka wengine wapo duniani, wao ndio wamerejea,”
Tangu kufika kule juu ambako nilielezwa kuwa ni mbinguni sikio langu lilikuwa linapokea taarifa za ajabu tupu, kama ni somo hakika lile nilibahaika kulisoma pekee yangu duniani, nilizidi kumfurahia Ramadhani, nikajikuta namuuliza “Sasa vipi hapa tulipo hawawezi kutuona?’’
Ramdhani akanitazama kisha akatabasamu ndipo akanijibu “ Hapana hawa jinsi walivyo huzingatia kazi moja tuu wanayotumwa hawajishughulishi na kluzingatia mambo mengine ingawa ingekuwa ni rahisi kwa wao kuhisi uwepo wetu endapo tungesimama wima, mradi tumefupisha vimo kamwe hawawezi kujua hilo”
Loh ile ilikuwa habari nyengine ngeni kwangu na yakustaajabisha, nilibaini kuwa Malaika wana utofauti pia na binaadamu maana ni ngumu kwa mwanadamu kumuagiza afanye kitu kimoja akakazaznia hicho tu lazima macho yake yatajishughulisha na mengine nachelea kusema labda pengine hii ndio sababu ya wanadamu kutokuwa na ukamilifu katika mambo yao.
Pengine labda dereva angejua kazi yake ya udereva tu bila kufuatilia simu labda ajali zingekuwa adimu, lakini wapi ni wanadamu ndio huongoza kwa kushika mawili nakupuuza ule msemo wao usemao mshika mawili moja humponyoka.
Sasa macho yangu yalifunguka kuona malaika wale wanafanya nini kwenye kizimba cha ibilisi na masikio yakawa wazi pia kusikia ujumbe gani unatoka duniani kaletewa ibilisi.
“Ewe mkaidi Ibilisi, tumekueletea ujumbe kutoka duniani, katika kipindi hiki ambacho umefungiwa humu dunia imekuwa mahala salama, wanawake wanajistiri kwa mavazi makuu kuu, wanaume wanapishana kwa wingi kwenye nyumba za ibada na wazinifu wamekuwa wachamungu na wanbywa pombe wameacha, kwanini hii isiwe habari njema kwako ewe mkaidi Ibilisi”
Malaika wale walizungumza kwa mbwembwe na furaha, dhahiri walionekana kuvutiwa na ujumbe ule wanaompatia Ibilisi, na ilikuwa ni tofauti kabisa na Ibilisi mwenyewe, nilimshuhudia akijibamiza kichwa chake kwenye nondo za kizimba chake.
Eti taarifa ile ilikuwa mbaya kwake! Hakupenda abadani kusikia watu wakiwa wacha Mungu, alinguruma kutoa mlio wa kuogofya uliodhihrisha hasira zake.
Malaika wale wakuvutia walifurahi walionekana wakimdhihaki Ibilisi, na wakaendelea kumonesha kidonda chake kwa kumpa habari ambazo mie zilinishangza zaidi, nasema zilinishangaza maana sikujuwa kabisa kama malaika wale wananijua mimi na marafiki zangu wa duniani. Walinichosha kututaja pale mbele ya ibilisi.
“Abdi kwa sasa anaswali muda wote, ameacha kusikiliza muziki wa duniani anasikiliza mafundisho ya manabii na nyimbo nzuri zinazotaja jina la Mola wetu mtukufu, zaidi rafiki zake wote ni wacha mungu sasa, hawakai tena vijiweni kuzungumzia kuhusu zinaa na wanawake wanaotoka nao, kwa sasa wanamuongelea Mungu na kudhihirhs hofu yao, Ona sasa neema za Mungu zinavyofanya kazi kwa sasa duniani, Abdi anamuomba Mungu ampatie mke aoe nasi tunamlilia MUNGU wetu amuitike Abdi dua yake,
Rafiki yake Abdi aitwae Manji kwa sasa ameoa na hataki kabisa maswala ya zinaa anamuheshimu mke na ndoa yake na pia wanahimizana kuswali kila siku.
Marafiki zake wengine wote kina Madebe, Kurwa na Gidion, Asangama na woote wamesimama katika hofu ya Mungu wanakumbushana kheri na Utukufu Wa Mungu, na wote mioyo yao imediriki kutamani kuoa nakuachana na zinaa”
Loh! Mwenzenu nilishangazwa na kauli za ibilisi wale, walinishangza sana kunitaja nakuwataja watu wangu, na hawakuishia hapo walielezea mambo mengi mema ambayo baadhi ya watu wengine maarufu wanasiasa na wanamuziki wanayafanya kipindi hiki Ibilisi alichofungiwa Kizimbani.
Habari ile ilizidi kumpandisha Jazba Ibilisi, alizidi kupiga kelele, akisema “Ni uonevu huu, haiwezekani watu wangu wote walaghaiwe na ramadhani mpaka washindwe kuetekeleza starehe za dunia nilizowafundisha, haiwezekani Abdi aache kuzini na Yule mwanamke wake niliyemtafutia, haiwezekani aache kusikiliza mziki mzuri wa wasanii wake anaowapenda nimesema nifungulieni nikawachuke watu wangu niwarudishe kundini, ni lazima niingie nao motoni nimesema..”
Aliropoka kwa suati yenye hasira Ibilisi, loh! Nimewahi kuona watu wenye roho mbaya duniani lakini Ibilisi alizidi jamani, yaani alilia kwa uchungu eti kisa kaambiwa watu wamebadilika wanamcha Mungu wao aliyewaumba.
Nilishuhudia Malaika wakimcheka kisha wakaanza kuondoka mule, nikamgeukia Ramadhani mwenye sura ya tabasamu muda wote, nikamuuliza
“Ina maana Ibilisi alikuwa hajatuona, mbona hajawaambia chochote wale malaika kuhusu sisi kuwepo hapa”
Ramadhani alicheka kisha akanijibu “Ibilisi ana roho mbaya kiasi ambacho habari alizoambiwa na malaika zimemfanya asahau kabisa kama sisi  tupo hapa, tayari amechanganyikiwa anatamani niondoke hata sasa ivi pale duniani ili afunguliwe akawapotoshe tena watu.”
Mnh! Kwakweli nilishindwa kuvumilia wala kudhibiti hisia zangu nikaamka bila hata kungoja amri ya mwenyeji wangu, nikasimama wima kwa hasira nikimtazama Ibilisi Yule mjaa lana.
Nilisimama nikimtazama kwa hasira huku nikiwa siamini kuwa macho yangu sasa yanatazamana na  ile sauti yangu ya ndani inayonituma kutamani wanawake niwaonao barabarani bila kujali wengine ni wake za watu,
Aidha huyu ndiye Yule anayenikataza nisisimamishe ibada kumcha mola wangu na pia hunikaa maungoni nakunifanya nivutike zaidi na dunia huku nikiisahau kabisa akhera.
Nilijiambia kuwa nina kila sababu zakumchukia huyu nimuonae mbele yangu mwenye majinywele marefu na machafu, sura baya mithili yake hapana, macho yake ya kiburi yanafanana na ubaya wenye kuogopesha.
Ibilisi alinitazama kwa chuki  sauti yake huku ikiwa na mkwaruzo kwaruzo wa hasira na kiburi aliniambia kuwa  nisiringe maana mwezi ukiisha akiachiwa huru atanisomba tena nirudi kwenye himaya yake  ya starehe dhalili ya ngono, ulevi, wizi, tamaa, magendo, ugomvi, ushirikina na umbeya.
Anasema eti atahakikisha nakuwa tena mfuasi wake na namtumikia kama mwanzo mpaka siku ambayo nitaingia naye motoni, namshangaa anavyojiamini ibilisi huyu mjaa lana! Eti anasema Tamaa yangu ya maisha mazuri itanifanya niende kwake kiulaini kabisa, muoneni jamani anadiriki kutaka kupinga namimi eti tuwekeane dau!!
Vazi lake jeupe lililojaa madoa ya damu za watu waliokufa vitani anajinasibu nalo eti yeye ndiye chanzo kwa kuwashawishi viongozi wawe na tamaa yakuongoza bila kujali mapigano na vita vinavyoathiri watoto na kina mama.
Sauti lake baya linanichefua mno natamani nimsogelee nimpige hata makofi mawili ila jinsi lilivyo linaogopesha kwakwel;i.
Ujasiri wakumtazama nimeupata kwa sababu pembeni yangu yupo rafiki yangu mpole, mwenye haiba ya wema usiomithilika, Rafiki yangu huyu kwa jina Ramadhan ananiuliza kama nina lolote lakumwambia ibilisi, kwa kihoro natikisa kichwa kuitika, wallah tena nilikuwa naitaka hii nafasi nizungumze na hili ibilisi mbele yangu.
Ramadhani  ananisisitiza nifanye haraka maana joto la jehannam linazidi kuongezeka kila muda unavyozidi kwenda mbele maana moto huo huchochewa zaidi, habari ile ilizidi kunipa hofu ya kutenda dhambi niliogopa sana siku moja namimi kuwa ndani ya moto huo, zaidi Ramadhan akanipa habari nyengine iliyoniacha hoi zaidi, eti alisema umbali wa moto ule kutoka mahala pale tulipo ni sawa nakutoka bara moja kwenda jengine lakini joto lake lilikuwa lile, nikajiuliza huo moto una nguvu kiasi gani mpaka mvuke wake uwe vile loh!
Hofu ikaniingia yakuumizwa na moto ule uakapoongezwa ukali nikamgeukia tena ibili ili niseme nae machache yaliyopo moyoni mwangu
sijui Napata wapi ujasiri namsogelea karibu kisha navuta karibu kohozi linasogea mpaka kooni kisha nalivuta kwa kasi kutoka ndani ya kinywa changu ptuu, kohozi lile linatua vema kwenye paji la uso wake! Nafsi yangu inafurahi ingawa bado sijaridhika natamani ningekuwa na basola nimyatulie risasi kummaliza.
Jitu hili ndilo lile lilomuahidi Mola wetu kuwa atahakikisha wanadamu tunaingia nae motoni, silipendi hakika natamani nipasue hiki kifua muuone moyo wangu ulivyofura hasira juu yake.
“Khaa unanitemea uchafu kwenye uso wangu, wallah nakuapia nitaanza nawewe sikukuu ya Eid ikifika! Huo uchamungu wako utaishia muda ule unatoka kuswali swala ya eid, Nitakutuma uende club, nitakutuagiza uzini na mwanamke wako na nitakushawishi unywe pombe, we jishaue muda huu ambao Mungu wako kanifunga minyororo hii mwilini mwangu lakini nakuapia nitaingia nawe motoni…litazame vile binadamu sanamu uliyejengwa kwa udongo wee…!”
Alipaza sauti yake Ibilisi akiongea kwa uchungu baada ya mimi kumtemea kohozi usoni mwake, jazba zinamzidi maradufu…
Namtazama kwa chuki namimi namjibu kwa kiburi kama chake.
“Mwanakharamu mkubwa wee unadhani MUNGU alivyokupa mamlaka ufanye hila zako duniani alikupa na uwezo wakuwashawishi wacha Mungu! Kwa taarifa yako sitamuacha MUNGU wangu majira yote ya usiku na mchana hivyo hautapata nafasi yakusema na moyo wangu, mimi hunipati tena nimezijua hila zako, Motoni utakwenda na wachache sana tena ni wale waliokosa maarifa yakutambua zuri na baya, jema na ovu,
Hii ni vita kati yangu mimi na wewe, kwa taarifa yako watu wangu wote wakaribu na wengine wote wenye sifa ya ubinaadamu nitawahimiza juu ya kumcha Mungu, nitawaeleza nia yako mbaya na nitawaambia mbinu zako zote..
Kwanza nitawaambia kuhusu Ujinga uliouweka kwenye akili za wanawake mpaka wakawa hawathamini maungo yao nakufanya wanaume washawishike kuwazini tu bila kuwaza tena ndoa.
Nitawaambia maumbile makubwa ya wanawake na namna walivyoumbika ni kazi ya MUNGU ila wewe kazi yako ni kutumia sumu ya ujinga uliyopuliza kwa wanawake mpaka kuwafanya waone kutembea uchi ndio urembo.
Nitawaambia kuwa hizo ni mbinu zako na unatumia mitandao ya kijamii kupoteza muda kwa binaadamu wakose hata sekunde chache zakuwaza mema ya MUNGU na Utukufu wake..
Nitawakumbusha watu kuwa Mungu ndiye tajiri ambaye hajawahi kufilisika hivyo wasimnyenyekee mtu yoyote zaidi ya Mungu maana ni yeye ndiye aliyeumba utajiri na ufukara, huzuni na furaha na pia yeye ndiye mwenye mamlaka ya Uzima na Kifo cha kiumbe yoyote duniani.
Nitawapa mbinu yakuwa mbali nawewe, mbinu ambayo hata wewe huna nguvu nayo, mbinu ya wao kuzidisha ibada nakukutanguliza wewe katika kila jambo….
Kinachonifurahisha kwako ni kwamba Unafanya kazi aliyokuagiza MUNGU, Kazi yakupima imani za watu hivyo basi nawe ni mtiifu juu ya Mungu wangu ninayemuabudu hivyo nitawakumbusha watu kuhusu hili na watakuona wewe si lolote mbele ya Mungu, maana kuna wakati utafika nawe utakufa ili kutimiza andiko la kila nafsi itaonja mauti.
Ibilisi wewe fungu lako ni moto tuu na motoni utaingia, binaadamu tumeumbwa kumsujudia Mungu na Nakuhakikishia pepo tutaiona kwa kumkimbilia MUNGU.
Maneno yangu yanaonekana kumdhoofisha mno Ibilisi, sura lake baya linaonekana wazi limekosa amani kwa ukweli huo, tukiwa tunatazamana kwa chuki kila mmoja ghafla nikamsikia Ramadhani akinishauri tuondoke, kwa vile nilikuwa nimeshamaliza kumpa ukweli wote ibilisi mjaa lana. Nikaona ni sahihi kuondoka pale.
Safari yakurudi duniani ilikuwa nyepesi kuliko tulivyoenda, nastaajabishwa na binaadamu wenzangu walivyo na shamrashamra zakupokea idi najisemea kimoyoni laity wangejua eid inakuja kumfukuza ramadhani kamwe wasingeshangilia na pia eid hiyo ibilisi anaachiwa dah roho yaniuma mno.
Nawaza kuwa mchaMungu lakini sitafurahi nikiwa peke yangu natamani kushirikiana na woote duniani tumsaliti shetani, ili ashindwe kutimiza lengo lake.

asante kwa kuifuatilia simulizi hii yakufikirika ambayo usimuliaji wake unakamilika kutokana na kuchora wazoni wasifu wa ramadhan na vitu dhahania kama vile mbingu , pepo na jehanam

sina shaka kuzama wazoni nakuandika simulizi hii ni kukusaidia kifikra na uweze kuona haja yakuaiandaa kesho yako kwa kutenda mema nakuwa na imani thabiti kuhusu Mungu wako aliyekuumba na kuumba kila kilicho kizuri duniani.

Akili fupi ambayo itakufanya uamini uwepo wa MUNGU nikujiuliza kuwa nyumba nzuri, gari zuri au chochote kizuri unachokipenda duniani kinaweza kujitengeneza chenyewe??? kama jibu lake ni hapana basi tambua kuwa yupo ambaye amekutengeneza ukawa wewe binaadamu mzuri wamaajabu  na pia akaitengeneza dunia ikawa kwa namna ambavyo ipo sasa ni wajibu wako kuamini kuwa uzuri wa dunia hii hauwezi kuwa ulijitokea tuu wenyewewe yupo bingwa, Mwenyezi Mungu mimi napenda kumita Jabbari ambaye amefanya haya yote yanayofanya wewe utamani kuishi milele ili uendelee kufaidi utashi wake.

Ishi kwa ukamilifu wa kufuata miongozo yote ya vitabu vinavyoelekeza kuhusu MUNGU muumba mbingu na ardhi kama unavyoenda resi kutafuta kodi ya nyumba unayoishi ndivyo mwenye hii dunia naye anataka kulipwa kwa kumnyenyekea na kumsujudia huku ukimtumainia yeye pekee.

hiyo ndio kodi ya neema zote alizokupa duniani hapa....USIMSAHAU MUNGU WAKO KAMWE!.

TAMATI



KIZIMBA Cha IBILISI


SEHEMU YA 1

"Habari hii nilikuwa naisikia sana kwa watu wa Mungu hasa masheikh duniani wakisema kuwa Shetani hufungwa wakati Ramadhani inafika lakini ilikuwa haijanisisimua kama alivyoniambia Rafiki Yangu Ramadhani, chuki dhidi ya huyo kiumbe aitwae Ibilisi ikanivaa, sasa nikawa natamani kumuona"


 KIZIMBA cha IBILISI

Na
Omar Zongo


Anaitwa Ramadhani, rafiki yangu asiye na ubaguzi, mpole mnyenyekevu na mwenye kufundisha mema! Hakika sikuwahi kujuta kufahamiana na Mja huyu mwenye kila dalili za utu wema.

Kinachoniuma zaidi ni licha ya kuwa ni mwema na ningependa kuishi nae milele lakini desturi yake ni kunitembelea mara moja tu kwa mwaka na  hakuna namna ambayo naweza fanya kubadili desturi yake hii.
Miaka yote anakuja naishi nae akinifundisha namna yakuishi kwa kufanya matendo mema yenye kumpendeza Mungu muumba aliyenifanya mimi nikawa kwa amri ya neno lake moja tu, miaka yote namfurahia Ramadhani lakini mwaka huu nimefurahia zaidi ujio wake maana ameweza kunipa fursa namimi nikatembelee mbinguni, mahala ambako yeye ana uwenyeji napo.

Safari yetu yakufikirika ilianza taratibu nikimuona wazoni rafiki yangu Ramadhaani akiwa amevalia kanzu nadhifu na baraghashea iliyomkaa vema kichwani, alivaa viatu vya mikanda na kama kawaida sura yake yenye tabasamu lakudumu ilikuwa ikinitazama mimi niliye pembeni yake. 

Alinishika mkono kwa upendo na wakati mwengine akiweka mikono yake begani kwangu kuonesha udugu alio nao moyoni mwake, tulikuwa tunapiga hatua kuelekea mahala Fulani ambako mie sikupajua ila yeye alidai anapafahamu na akanieleza kuwa ndipo ambako safari yetu ya mbinguni itaanzia hapo.
 
Katika muda wote tuliokuwa tukiongozana Ramadhaani hakuacha kunipa simulizi nzuri kuhusu mahala Fulani paitwapo peponi, alisema ni miongoni mwa maeneo yaliyo mbinguni ambayo yameumbwa kitaalamu sana na kila kilicho kizuri duniani basi uzuri wake uliongezeka maradufu peponi.

Alisema akitolea mfano asali, moja ya vitu vitamu mno duniani, anasema asali ya Mbinguni imetengenezwa kwa utaalamu wake kiasi ambacho kama ukiionja utabaini kuwa ya duniani si chochote.
Akawagusia walimbwende wanaopatikana peponi, anasema hakuna mfanowe duniani hapa, alinikosha zaidi alipotaja matunda na vyakula adhimu vilivyopo huko! Nikajikuta natamani hata leo niende nikaishi huko hasa aliponiambia kuwa huko hakuna maradhi, kuzeeka wala kuumwa.

Udenda wa tamaa yakuiona pepo ukanitoka, nikajikuta nauliza kizembe “Nini chakufanya ili mtu uende ukaishi huko?” swali langu hili nasema nimeliuliza kizembe sababu jibu lake nilikuwa nalijua lakini sijui nini kikanifanya niulize, uzuri Rafiki yangu Ramdhaani sio mtu wakuchoka kuongea na mtu wala kukosoa maana yeye hana sifa ya wivu, alinijibu swali langu bila shida yoyote.

Alisema “pepo hiyo imeumbiwa binaadamu wote lakini kinachoumiza ni kwamba sio wote wataiona isipokuwa wale wachamungu na wenye kutenda mema duniani kwa kiwango kinachomridhisha Mungu Muumba vyote” Jibu hili likanifanya nijitathmini kwa muda nikajikuta natilia shaka matendo yangu, amani ikatoweka hasa nilipokumbuka kuwa kuswali ni kitu ambacho sikizingatii, Kutoa sadaka ni kwa hiyari yangu na pia ni bingwa wakuwazini mabinti wa watu bila kufikiria kuwaoa.

Dah Moyo ulipatwa na joto kuu, nilihisi wazi kuwa naungua moyoni Mwangu, hata hivyo nikajifariji kuwa nitaendelea kubadilika maana tangu aje rafiki yangu Ramdhani angalau matendo maovu nimeyaacha kabisa.
“Najua unachohofia” wakati nikiwa nawaza namna gani yakubadilika kabisa nakuwa mcha Mungu ghafla Rafiki yangu ramadhaan nikamsikia akisema hivi, nilishtuka nikamgeukia,

“Ndiyo, najua unachokihofia lakini acha nikwambie. Usijali leo nitaenda kukuonesha Kiumbe mmoja aitwae Ibilisi, ni kiumbe huyu ambaye aliapa mbele ya Mungu Muumba kuwa atahakikisha anaingia motoni na Binaadamu wote ikibidi”
Alisema kwa sauti yenye utulivu Ramadhani, ile ilikuwa sio habari ngeni kwangu lakini wakati inatoka kinywani mwa Ramadhani nikahisi kama ni habari mpya na nikajikuta naweka utulivu zaidi ili kumsikia Rafiki yangu akizungumza zaidi kuhusu Ibilisi, Bila shaka Ramadhani aliuona Umakini wangu, akaendelea.
“Ibilisi hutumia mbinu zote kumpotosha mwanadamu ili atende uovu na amchukize Mungu wake, na hakuna siku ambazo ibilisi anachukia sana kama siku akisikia mimi nakuja duniani kukutana nanyi…”
Aliendelea kusema Ramadhaani huku mimi nikimsikiliza kwa makini.

“kwa kawaida Ibilisi hukamatwa nakufungwa minyororo huko juu mbinguni kipindi ambacho mimi nafika duniani kukutana na wanadamu, na ndio maana kipindi hiki binadamu wengi mioyo yao huongezeka ucha mungu na wengine hudiriki kuswali sana maana hakuna anayewazuia kufanya hivyo, suala hili Ibilisi halipendi sana na huumia akisikia watu wanamcha Mwenyezi Mungu ukweli wa kumcha,  leo nataka nikifika nawewe mbinguni nikupeleke mahala ambapo ni kizimba anachofungiwa Ibilisi ili ukamuone…”

Habari hii nilikuwa naisikia sana kwa watu wa Mungu hasa masheikh duniani wakisema kuwa Shetani hufungwa wakati Ramadhani inafika lakini ilikuwa haijanisisimua kama alivyoniambia Rafiki Yangu Ramadhani, chuki dhidi ya huyo kiumbe aitwae Ibilisi ikanivaa, sasa nikawa natamani kumuona.

Muda tunazungumza tulikuwa tunatembea na sasa tayari tulishafika mahala ambako Ramadhaan akaniambia kuwa ndio mahala pazuri pakupaa nakuelekea huko mbinguni, mahala ambako sikuwahi dhani kama nitafika hata siku moja, Ajabu leo nilikuwa safarini nikipelekwa huko  kwambaali hofu ilinivagaa maungoni lakini kwa sababu pembeni yangu alikuwepo Ramadhaani akiniongoza kamwe hofu haikupata nguvu kubwa.

Kufumba nakufumbua sasa nilikuwa mbinguni, pembeni yangu alikuwepo Ramadhaani akiniongoza.
“Sasa tumefika” alisema kwa mtindo wakunong’ona na mimi hapa ndipo nilipogundua kuwa mahala pale hapakuhitaji kelele hata ndogo maana palikuwa tulivu mno, eneo lile lilikuwa ni mithili ya jumba kuubwa lenye korido ndefu sana, kwenye korido lile nilikuwa mimi na Ramadhaani tu sikuona mtu mwengine.

Ramdhani akaniambia kuwa kila chumba katika korida ile kina kazi yake, ni hapa ndipo nilipogundua kuwa kumbe ile korido ndefu kuna vyumba vipo pembeni yaani mkono wa kushoto na kulia, wazo la vyumba vya gesti vinavyokaa duniani likanijia, lakini nikalikemea libaki huko huko ndani maana nilihisi dhambi kufananisha eneo lile Mbinguni na Vyumba vya nyumba za kawaida duniani.

Rafiki yangu Ramadhani akaniambia kuwa kila chumba kina shughuli yake, akasema kuna chumba ambacho mlango wake ni wamotoni, yaani ukiingia ujue umeingia motoni, akasema pia kipo chumba ambacho wanaishi malaika na vyengine vingi tu, nilitamani kuona maandishi milangoni yakielekeza chumba cha hukumu ni kipi lakini sikuona yaani vyumba vyote vilifungwa lakini haikujulikana chumba kipi kina kazi gani.

“twende kwenye kizimba cha ibilisi” Alisema Ramadhani kama kawaida kwa mtindo ule  wakunong’ona, mie sikujibu kitu nilikuwa nafata tu maelekezo ya mwenyeji wangu, tukiwa tunatembea taratibu kwenye korido ile kwambaali nikaanza kusikia sauti za mtu akiongea kwa nguvu na ukali alisema

“Niachieni, nimesema nifungulieni hapaaaa…” mie sikuelewa sauti ile inatokea wapi, hofu ikanitanda nikajiuliza ninani huyo, ajabu  nikuwa kila tulivyozidi kusogea mahala huko tulipokwenda ndipo sauti ile ikazidi kuongezeka wakati mwengine mtu huyo alitoa kabisa lugha chafu akitaka aachiwe.

“Niachieni nimesema nifungilieni hapa, hamuweszi kunifunga muda wote tuu niachieniiii….” Ilisikika sauti hiyo ikisema.
“Tumefika” Alinong’ona tena Ramadhani na nilipotazama mahala nilipoambiwa tumefika nikaona tupo nje ya mlango mweusi, mlango ule ulikuwa ni tofauti kabisa na milango yote niliyoipita mwanzo.
Kilichoniacha hoi zaidi ni sauti ile niliyoisikia ilikuwa inatokea chumbani mule.

“Huyo ni Ibilisi analilia afunguliwe minyororo ili aende duniani akaendelee kuwakusanya watu wakuingia nao motoni” Loh!!  Habari hii ilinichosha kwakweli, nilikosa chakusema nikabaki namuangalia Ramadhani, moyoni nikajiwazia hivi kwa mfano akiniacha pale nitakimbilia wapi au nitatokaje kurudi duniani, wazo hili liliponijia nikazidi kupatwa na woga lakini nilipokuja kukumbuka wema wa rafiki niliye nae nikajiambia kamwe hawezi kufanya hivyo.

sasa nikawa namshuhudia Ramadhani akifungua lango lile la Kizimba cha Ibilisi…wasiwasi na kihoro vikanivaa sikuamini kuwa ni mimi ndio naenda kumuona Ibilisi huyo mjaa lana.

Inaendelea….


EL PERDEDOR

“Wanaume ni watashi sana katika kutumia nguvu na mabavu yao kuwanyanyasa wanawake, lakini sijui kwanini wanashindwa kutumia utashi wao huo kutambua thamani na upendo wa mwanamke anayempenda kwa dhati.
 


Kuzidisha drugs watu wanaweza sema ndio chanzo cha kifo chako shoga angu lakini mimi nasema mapenzi ndio chanzo...naamini nafsi yako itawaadhibu wanaume wote wenye moyo kama wa aliyekufanya uwe marehemu leo hii, Rest In Peace shoga angu, nitamiss kukuita hivi madia...”

 EL PERDEDOR
Na
Omar Zongo

Uliniumiza kichwa sana nilipoona mchoro wako ulioonesha mwanamke amejiinamia kisha ukiambatanisha na neno hilo El Perdedor.
Niliwaza nikawazua nikijiuliza unamaanisha nini, nilijihoji je ni jamaa mwengine umempata ambaye amekalia kiti cha huba kilichopo moyoni mwako ndio anaitwa jina hilo?? Lakini nilijikosoa maana kama ni jamaa mwengine kwanini uliweka picha yako ukiwa umeinama, kulalia magoti.
Nikajiuliza tena neon lile linatoka kwenye lugha gani  maana kwenye kabila lenu wazanaki hamna msamiati wenye maandishi kama hayo ingawa nilikuwa sina uhakika n]maana sio maneno yote ya kizanaki ninayajua.
“El perdedor.. El Perdedo” kila mara neno hili lilikuwa likijirudia kwenye kichwa changu, tangu nilipoliona kwenye picha yako uliyoituma instagram.
Kuhusu Picha iliyoamabatana na neno hilo haikunisumbua maana hata wewe  uwe wapi kamwe siwezi kukusahau, lakini namna ambavyo mchoraji amekuchora umejiinamia kisha akaweka na maneno hayo ndipo nilipopata mashaka sana.
Kama mashaka yangu ni dalili ya kuwa bado nakupenda basi nakiri upendo wangu kwako hautakuja kuchuja licha ya kuwa mimi ndio nilikuacha.
Sababu zangu zilikuwa dhaifu tu eti kwanini ulienda club usiku na marafiki zako bila kuniaga, nafikiri ilishapangwa tuachane maana hata uliponililia machozi ya huruma mie sikudhania wala kufikiri kurudisha huba kwako.
Nilikuacha kiukweli na haukuamini macho yako! ilikuuma sana ulipobaini kuwa ni kweli ulivyodhani nakuacha sababu nimepata mwanamke mwengine, maana haikuchukua muda ukaona mtandaoni nikituma picha za msichana mwengine, kwa ulimbukeni wangu nikihisi nakurusha roho.
laiti kama ningejua maumivu ya mapenzi yanafananaje kamwe nisingefanya ujinga huo, yaani sikuwaza kabisa kama nakuumiza kwa kiwango kikubwa mno.
Najuta sana sababu nimechelewa hata kusema nisamehe maana hali yako haina utayari wowote wakunielewa hata ikitokea nakutamkia neno hilo.
Ile siku niliyokuomba tukutane ni siku ambayo jana yake nilitoka kumfumania mwanamke yule niliyemfata baada ya kukuacha wewe.
laiti ningejua kuwa mwanamke yule ni kijiko cha hoteli kamwe nisingethubutu ulimi wangu utamke tuachane.
masikini wewe hukuwa na hiyana kukutana namimi na pia hukusita kunieleza maana ya neno uliloambatanisha na mchoro wako kwenye bega, sauti yako bado inajirudia nakumbuka ulisema
"mimi ni mkosaji, nimekosa vingi vizuri maishani mwangu akiwemo mama angu, na pia nimekosa upendo wa baba maana alinikana tangu niko tumboni, lakini sijui kwanini sikuumia sana kama nilivyokukosa wewe mwanaume wangu niliyekupenda kwa dhati, najiona mkosaji maana nikweli nilikukosea lakini ilikuwaje kosa lile linihukumu kuishi bila pendo langu...."
ulishindwa kuendelea kuongea, ukaanza kulia.
Huruma iliniingia sana, nikajutia kukuacha na Zaidi iliniuma maana niliiona hali yako na ikaniambia wazi kuwa siwezi tena kuwa nawewe! ulikuwa umekonda, sio nadhifu tena, mchafu na mikono yako ilikuwa imetoboka toboka matundu madogo ya sindano..
hali yako ilinidhirishia kuwa X wangu umekuwa Teja! uliniumiza sana uliposema kuwa ulichagua maisha hayo sababu ndio faraja pekee uliyoona inafaa kukufariji.
Nilipokubembeleza unieleze maana ya neno ulilochora kwa ufafanuzi ukarudia kwa unyonge huku ukijikaza kibandidu kuonesha kuwa uhuni umekuvaa, ulisema kwa sauti ya kike lakini iliyotawaliwa na uteja "wee sinishakwambia maana yake ni Mkosaji, mimi ni Loser, ndio mimi ni El Perdedor  hilo ni neon la kihispania nimechora mwili wangu kukiri kuwa mimi ni loser lakini wewe ndio chanzo...."
Ulisema tena ukashindwa kuendelea ukaanza kulia, siku ile ulinielezea maisha yako ya sasa unayoishi, uliniambia wahuni wanakubaka mtaani ukishazidiwa na dawa za kulevya, uliniambia kuwa nyumbani wamekutenga na sasa unalala popote penye maficho au palipo wazi, mradi kukuche.
Kauli zako ziliniumiza! ule urembo wako sikuuona tena! macho yangu yalipata nafasi kwa mara nyengine kuutazama tena mchoro wako begani, safari hii nikijua sasa maana yake.
Mchoraji alikuwa mtashi kwelikweli, aliweza kukuchora ukiwa umejiinamia na kisha aliyaweka maneno hayo kwa weledi wa hali ya juu.
El perdedor nikalisoma tena kimya kimya neno hilo, huku nikilitafsiri kwa kiingereza Loser, na nikafasiri kwa lugha yetu Kiswahili nikapata neno, mtu aliyepoteza, hana dira, mkosaji!
Kichwa changu kiliugua huzuni maneno yako yalipojirudia kichwani mwangu "wee sinishakwambia maana yake ni Mkosaji, mimi ni Loser, ndio mimi ni El Perdedor lakini wewe ndio chanzo...."
Maisha yangu niliyaona kabisa yakiingia mkosi wa laana yako, dhambi ya hali uliyokuwa nayo haikuweza kuniepuka kamwe, nafsi ilinisuta suto kuu, majuto yangu yalishavaa vazi la ujukuu.
Wakati nawaza nini chakufanya au nini chakukwambia, nakumbuka uliniambia unaomba shilingi elfu mbili, bila kufikiri mara mbili nikakutolea noti ya elfu tano nakukukabidhi, ukapokea na ajabu ulipoitia mkononi tuu, ukaniaga.
Hapa ndio nilikiri kuwa kweli sio wewe tena! Nakumbuka uliniaga kihuni sana eti ulisema
“kama vipi tutakutana siku nyengine acha mimi niingie chimbo”
Sikukuelewa, na hata nilipotaka kukuzuia sababu nilikuwa sijamaliza kuongea nawewe ukanikatalia kabisa na ukaondoka zako, nilibaki nakutazama bila kukumaliza mpaka ulipopotea kabisa machoni kwangu ndipo namimi nikaondoka eneo lile la makutano yetu.
Siku ile ilikuwa ni siku ya hukumu yangu ya matendo maovu yakukuacha bila huruma, hakika ningejua kama ungechagua maisha yale baada ya kunikosa kamwe nisingethubutu kukuacha,
Niliumia kumpoteza mwanamke aliyekuwa ananipenda kupita kiasi, sikujua kwa siku ile nani wakumlaumu, nafsi yangu au shetani au nilaumu ujana ambao ulinivaa na kutamani mwanamke mwengine huku nikukuacha wewe ambaye ulikuwa na upendo wa dhati kwangu.
Siku ile ilikuwa chungu kwangu, na uchungu wake ukaongezeka makali ilipofika usiku baada yakuona picha mitandaoni zikitumwa na ndugu na marafiki zako, wengi wakiandika kifupi cha maneno matatu ya kiingereza Rest In Peace (RIP) huku wakiambatanisha na picha zako.
Nilipoona picha ya kwanza nilidhani macho yananidanganya lakini baadae nikagundua kila mtu anayekujua ameandika neno hilo kuashiria kuwa wewe sio miongoni mwa tulio hai, yaani sikuamini kabisa kama umetutoka duniani.
Rafiki yako Devotha aliyekuwa akiniita shem Darling enzi nipo nawe ndio aliandika maneno makali, ingawa yalinipa chanzo cha kifo chako lakini pia yaliniongezea hukumu ya nafsi yangu ovu, hakika nilijiona muuaji, hakika mimi ndio nilikuua  rafiki yako Devotha hakukosea kuandika hivi.

“Wanaume ni watashi sana katika kutumia nguvu na mabavu yao kuwanyanyasa wanawake, lakini sijui kwanini wanashindwa kutumia utashi wao huo kutambua thamani na upendo wa mwanamke anayempenda kwa dhati.
Kuzidisha drugs watu wanaweza sema ndio chanzo cha kifo chako shoga angu lakini mimi nasema mapenzi ndio chanzo...naamini nafsi yako itawaadhibu wanaume wote wenye moyo kama wa aliyekufanya uwe marehemu leo hii, Rest In Peace shoga angu, nitamiss kukuita hivi madia...”
Ujumbe huu ulinigusa kabisa mimi, niliusoma mara mbilimbili huku nikiona kabisa Devotha alivyonishambulia shambulio lile kubwa lililobeba silaha kali za tuhuma dhidi yangu, japo hakunitaja lakini dhahiri niliona ule ni ujumbe wangu, nawezaje kupinga.
“Hii ndio sababu ya mimi leo hii kuchora maneno haya kifuani kwangu upande wa moyo wangu, sijawahi kumwambia mtu suala hili wala mchoro huu haujawahi kuonekana na mtu yoyote zaidi yako, ilinichukua muda sana kuamua kuwa na msichana mwengine kimahusiano baada ya kifo chake.
Muda wote nilikuwa nautumia kutubu dhambi zangu, na nilimuomba pia Mungu anipe mwanamke mwengine yeye mwenyewe huku nikimuahidi kuwa sitapuuza tena upendo wa mwanamke atakayenipa.
Hiyo ndiyo sababu ya kuwepo huu mchoro kifuani kwangu na ndio sababu pia ya kwanini nakupenda sana, nakuheshimu na najali maumivu yako..naomba nisamehe kwa makosa niliyowahi kuyafanya kwa mwanamke mwenzako hadi kusababisha awe teja na baadae marehemu.
Samahani jamani sijawatajia jina, mimi naitwa Prince Jocha, na hii ni simulizi yangu fupi ya maisha yangu yakimahusiano ambayo nilikuwa na msimulia mke wangu!
tayari nimejiomba msamaha, nikawaomba pia msamaha wanawake wote na nikatubu kwa mungu hivyo akanisamehe nakunijaalia  familia nzuri yenye afya na wanamjua Mungu! Kwasasa Mimi ni baba wa watoto wawili! Devis na Dayana.
Dayana ndio jina la Yule mwanamke niliyemsababishia kifo!
Kwasasa nachukia sana kuona mtu akipuuza upendo wa anayempenda laiti kama ningekuwa upepo ningevuma na utenzi huu, kutambulisha duniani thamani ya upendo.

Upendo sio bidhaa, kupatikana dukani,
Wala sio chokaa, pambo la ukutani,
Upendo labda sanaa, ipendezayo moyoni
Tena ikisambaa, furaha kote nyumbani.

Upendo ni mshumaa, nuru yake gizani,
Tamati yake balaa, totoro giza machoni,
Kama nikitambaa, hufuta chozi jichoni
Dhambi kumhadaa, mwenye upendo moyoni.
INATOSHA

Na,

Omar Zongo