Nimesema Sitaki Misifa |
kama ninyi ni mahodari wakusifia mpeni sifa jogoo ambaye ana juhudi kubwa yakuwaamsha alfajiri ili mkatafute riziki.
mimi sitaki kabisaa sababu MUNGU wangu alinipa upeo na busara yakutambua jema na baya.
kuhusu sifa mnazotoa sioni wema hapo nauona ubaya, naomba msinisifie tafadhali.
kama mna nia nzuri na mnataka mema kwangu fanyeni maombi ili bendera ya SIMULIZI ZINAISHI iendelee kupepea vema.
mkifanyacho sasa mnarusha mawe yalio na mfano wa mkate yanatua sawia kichwani mwangu maumivu na kuvimba kichwa hiki yatasababisha nisiwe msanifu na mwenye kujiongeza tena.
kwani ni wangapi walioanza vema wakasifiwa kwa nderemo na vifijo na matokeo yake wakapotea mithili ya jua majira ya jioni.
Sitaki tena sifa zenu! naamini kuwa sifa hizo ndizo zitakazonifanya nifanane na wengine waliowika Tanzania hii.
wale ambao waliweza kusahau utamu wa lugha yetu wakaweza kuhadaika na kuandika simulizi pendwa wakawa mabingwa wa kusisimua bila kufikiri walio nyuma yao wanafaidika na nini.
hakika ni hizi sifa ndizo zinazomaliza kabisa ufanisi wa kijana wa kitanzania na akachoka mapema kufikiria jukumu lakuipa hadhi nchi yake kupitia alichojaaliwa.
nasema tena safari hii bila kunong'ona SIZITAKI SIFA ZENU. nisubirini nife mnisifie malaika wangu wataniambia kaburini.
hivi mnawezaje kuusifia mti huu mchanga usionufaika na matunda yake!? hivi kwanini mnajipatia dhambi za bure?
kwanini mnashindwa kubaini kuwa SIMULIZI ZINAISHI ni kioo cha kesho ambacho mnapaswa kukiombea dua leo na kutafuta njia ya kusaidia simulizi hizi zifike mbali na sio kuzitemea sumu ya sifa.
kwanza me mwenzenu ni mshamba kutoka TANGA misifa sijazoea, na wasichana baadhi wa leo huona fahari kubwa kuwa na bwana mwenye kusifiwa, hujirahisisha kwake wakidhani ndio njia ya wao kufaidika na pepo ya dunia hii.
akili zao fupi na sijui kwanini hawaoni mfano wa kina mama mashuhuri Tanzania hii, ambao sauti zao walipozitoa ziliweza kutetemesha hata masikio ya wanaume, na hata siku moja hawajahadaika na maisha ya ganda la ndizi kutegemea mteremko.
sizitaki sifa zenu kuwaepuka watu hawa mabinti waso haya, watanichafulia sifa na heshima niliyofunzwa, watanifanya nami nianguke kwenye tope la ujinga wa kutafuta njia yakusikika redioni hata nisipokuwa na sababu ya msingi ya kusikika huko, wakileo wanaita kutafuta kiki.
Sitaki sifa hizo sababu mama yangu marehemu nafsi yake inaishi ndani yangu na kila siku ananiambia kuwa bado sana sijatimiza hata robo ya ninachokiota hivyo nisidhani ni lelemama.
baba yangu marehemu nae hunisisitiza sana kuhusu kupigania heshima ya jina lake, asije akazungumziwa Zongo kijana mwenye maringo, mchepukaji na mwenye kudharau wengine.
na sio siri yote haya hutokea kutokana na sifa za wanadamu wanazozitoa wengine wakidhani ni vizuri au wananipa moyo kumbe wananiua kisaikolojia.
kimbilio langu ni MUNGU na namaliza kwa kusema nae,
yaarab nijaalie upeo wakuona zaidi kama nilivyoona sifa kuwa ni sumu immalizayo mtu, nipe staha na kiu yakuhitaji kufika unaponielekeza wewe na sio shetani, nipe upendo na uzalendo wa kipaji changu na nchi yangu.
niondoe mimi na wengine katika upofu wa kutoona baya katika zuri. nakabidhi uhai wa milele wa simulizi katika mikono yako salama.
nami najificha katika ubavu wako nikiepuka hadaa za ibilisi na wabaya wenye kufitini na kufalakanisha.
nasema ahsante Mungu baada yakujiridhisha kuwa sasa nipo salama na nimeepuka mshale wa misifa isiyo na tija.
amin....