KUMBUKUMBU YA PENZI


Nilikuita jina gani, kwanza nilipo kuona
Nilianza kwa utani, au nilijua jina
Hivi ilikuwa sokoni, au kwa kina Safina
Moyo wangu umetuwa, kumbukumbu we rejea

Nilianzaje kusema, kwa binti wewe mrembo
Ni kweli sijatetema, kwa mvuto wako wa umbo
Ni vipi je nilihema, kwa tenzi zangu za fumbo
Moyo wangu umetuwa, kumbukumbu we rejea

Jicho lipi shahadia, jasiri kwa babu babu
Nilijawa na hisia, kisio lenye sababu
Nilianza simulia,  ni kipi kilinisibu
Moyo wangu umetuwa, kumbukumbu we rejea

Au nilikusifia, pasipo kunjo aibu
Hivi nilikurukia, tena pasipo adabu
Wewe uliye malkia, mrembo usiye gubu
Moyo wangu umetuwa, kumbukumbu we rejea

Sikumbuki ilikuwa lini, na jibu gani ulinipa
Ila nipo furahani, nisiye penda kwa pupa
Nimekuweka moyoni, nihifadhi kwenye chupa
Moyo wangu umetuwa, kumbukumbu we rejea


Penzi hili si kasiri, Kaharu kalipangia
Tena halina tafsiri, kwa jina kulipatia
Tuijenge tafakuri, magumu tukipitia
Moyo wangu umetuwa, kumbukumbu we rejea

Tusije kujihasiri, tupatapo  maanguko
Tujivike ujasiri, kuepuka masumbuko
Habibi tusikariri, kila chozi  bubujiko
Moyo wangu umetuwa, kumbukumbu we rejea


Na, Fulgence Makayula

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »