Natoka zangu mihangaikoni, mwili umechoka akili haifanyi kazi ipasavyo nahitaji kuoga nakupumzika, nawaza ningekuwa na mke nyumbani angalau ingekuwa afadhali nipate tulizo walau lakupokelewa furushi langu zito lenye vifaa muhimu vya ujenzi. kazi yangu mie ni ujenzi wa nyumba. sikusomea kazi hiyo bali nilijifunza tu kwa wataalamu wa fani hiyo, nakutokana na utundu wangu nikawa fundi mzuri wa nyumba. ingawa ilikuwa yaniuma sana ninapobaini kila nyumba nzuri inayosifiwa jijini dar es salaam ni kazi ya mkono wangu ilhali mwenyewe bado naishi nyumba yakupanga.
niliwahi jaribu kununua kiwanja maeneo ya chanika nijenge lakini sunami la dhulma na dhoruba kali ya utapeli ikanirudisha nyuma sana.
mpaka leo mimi ni mdau wakupanga huku tabata matumbi,
maombi yangu siku zote ni mvua isinyeshe maana adha ya maeneo haya aijuae ni MUNGU.
unataka kuja?? |
hatua zangu za kichovu hatimaye zikagota katika mlango wa chumba changu..
naufungua naingia ndani, chumba chanizomea maana tangu nilivyokurupuka alfajiri ndio narudi mishale ile ya saa sita usiku, huku taswira ya chumba changu ikinieleza kuwa haina matunzo na mpangilio unaoridhisha, chandarua hakijakunjwa, kitanda hakijatandikwa yaani ndani kulikuwa ni shaghalabaghala.
kwa mara nyengine tena wazo la kuoa lanirudi kichwani mwangu, namkumbuka Mwanaidi mpenzi wangu niliyeachana nae Tanga muheza miaka mitatu sasa.
mchana alikuwa akinipigia simu sana lakini kutokana na kubeba zege nakulisambaza hata simu niliiona adui sikuwa na muda wakuongea nae, na sio yeye tu ni wengi walikuwa wakifanya juhudi kunitafuta majira ya mchana waliambulia kutokupokelewa simu.
maisha haya,! kweli wanaume tuliambiwa tutatafuta kwa jasho!.
muda ule sasa licha ya kwamba ni usiku sikuwa na jinsi ilinipasa kuwajulia hali watu wenye umuhimu kwangu akiwemo mwanaidi mchumba angu.
nakaa kitandani kizembe nikiubwaga mzigo wangu sakafuni, navua shati na suruali bahati nzuri nilishaoga kazini hivyo kilichobaki nikumtafuta mwanaidi nakumpoza hasira zake zakutompokelea simu kutwa nzima.
nachukua simu yangu ya bei rahisi, mwenzenu situmii simu za kisasa muda wakuwasiliana huko facebook na watsap sina.
nashukuru na nafurahi kupiga nakupokea tu na mara chache sana kutuma ujumbe mfupi.
simu sasa ilikuwa sikioni na nilisikia ikiita huku nikiomba mungu mwanaidi awe hajalala.
nakumbuka niliuona ujumbe wake mfupi alioniandikia asubuhi eti aliniambia anahitaji kuja Dar es salaam.
ni mara ya tatu sasa mwanaidi alikuwa akirudia kuniambia suala hili...anataka kuja dar.
sekunde chache ya simu ya mwanaidi kuita hatimaye sauti nzuri yenye uchovu wa usingizi ikapokea, dah mwanaidi mwenyewe alikuwa kalala wakati mie ndio narudi...maisha haya!
niliwaza hayo huku pia sauti ya mwanaidi ikinituliza kabisa uchovu nakunisahaulisha adha za kutwa nzima.
nilianza kuzungumza kwa furaha kiasi
haloo....habari mpenzi wangu, pole kwa upweke wa kutwa nzima ni matumaini yangu ulishanisamehe kabla ya muda huu, kwa kutokupokea simu yako ni dhahiri wajua sifanyi kusudi bali ni kutingwa tu na majukumu mazito yakupambania tonge,
asante kwa kunikumbuka laazizi wangu, meseji yako nimeipokea na imenifariji ikinipa sababu zakuendelea kupambana ili nikutunze ua langu.
nimeona pia umesema kuwa unataka kuja dar es salaam eti mchumba ni kweli unataka kuja dar?
mwanaidi: Ndio me nataka kuja dar, nataka kukufata tuishi wote, nahisi wanisaliti ulipo...nimechoshwa na huu umbali...
alinijibu hivi Mwanaidi kwa sauti iliyo na lafudhi ya kipwani.
nilipoteza sekunde kadhaa nikitafakari ombi lake, na nikajikuta namjibu
ni wewe ndio uwaridi wangu, tulizo la moyo wangu, ni wewe mwanaidi pekee ndio ambaye unastahili kuitwa mama na watoto wangu, ni wewe mchumba ndio ambaye mawazo yangu yametawaliwa nawe.
nitawezaje kukataa utakalo, lakini naomba mpenzi wangu kabla hujaja dar nisikilize basi kwanza.
unajua maisha ya dar yanaongopa sana hasa kwa mtu anayeyafikiria akiwa mbali, ukiitaja dar bila shaka kichwani mwako unayaona maghorofa, wasichana waliojipamba na magari yaliofuatana barabarani yakishindana uzuri.
kwa kuifikiria dar utaiona pesa ikipatikana kwa urahisi kazi zipo tu bila shida tena nyingi zakumwaga, na kila kitu kizuri unakipata.
hiyo ndio dar ya kuifikiria mwanaidi wangu, dar ambayo hata mimi kabla yakutoroka nyumbani muheza na gari la machungwa nilikuwa nafikiria nikifika dar nitafanikiwa kwa urahisi.
ukweli sio huo laazizi wangu, dar ni chungu ni ngumu na ina kila aina ya sababu za mtu kuendelea kuishi mkoani asikimbilie kuja dar.
dar haitamaniki, pengine unajiuliza kama dar ni hivyo kwanini bado mie ningali huku? ni swali zuri Mwanaidi wangu!
mie naona aibu kurudi huko sababu nilipotoroka nakuunga magari kufika huku niliapa kutokujutia kosa hili kwa kupambana tu sababu maji niyaogayo nilishayavulia nguo.
nikirudi Mbwana atanicheka, Sudi atanicheka na hata mashoga zako watakucheka sababu kwasasa wanakuonea wivu kuwa mchumba ako niko dar na niliahidi kuja kukuchukua.
ugumu wa maisha sio tatizo tutapambana lakini hii dar ina ushawishi sana, na uzuri wako ukija nikishindwa kukupa wanachopewa wengine utahadaika na mabosi wa huku ambao wao pesa zao zipo tu kwa ajili ya kulaghai wachumba wa watu.
naujua uzuri wako na haiba yako ukija dar nina mashaka sana na uhai wa penzi letu.
mwenzio huku dar wakati mwengine nalala na njaa natembea kwa miguu na ni uhakika ili kutaka kunionesha kuwa una mapenzi ya dhati namimi utataka kuja ili tuishi wote kwa shida na raha.
ni wengi waliambizana hivyo lakini tamati yake haikuwa hivyo, huku dar mioyo yenye majeraha yakuumizwa na mapenzi ipo mingi sana barabarani.
mpaka dakika hii naongea nawe yupo mmoja analia kwa kutendwa.
hii ndio dar unayotaka kuja. gharama za maisha zipo juu sana lakini sitaki uendelee kujisikia vibaya nipe wiki hii ninunue sukari niweke ndani, unga niweke ndani.
mchele nitaweka ndani na hata mafuta ili ukija tuwe na mwanzo mzuri.
jiandae mpendwa mwishoni mwa juma hili nitaminyana nikutumie nauli mana nikisema kesho nitaongopa kwakweli.
nimefurahi kuongea nawe usiku huu, sauti yako ni tiba ya kazi ngumu niliyoifanya leo hii. naomba nikuache ulale
pumzika waridi langu malaika wema wakulinde na shari za usiku huu.
jiandae nitapambana uje dar!
1 comments:
commentsnyc one
Reply