'Watu'

Kwa tabu sana Mzee alijisogeza juu ya kitanda nakulaza shingo yake kwenye mto.

Uchovu wa maradhi ulimdhoofisha vyakutosha, macho yake yaliashiria kukata tamaa, lakini alijikaza kiume.

Alinitazama Na kisha akasema.

"Ilikuwa ni siku ambayo kila mtu alinisema vibaya nakunizungumzia vibaya, lawama za kila rangi nilipakwa,

Hakuna aliyejuwa niwapi nimeelekea nawewe, ulikuwa bado mchanga kabisa.

Nimimi pekee ndio nilijua dhamira yakutoroka nawewe siku ile,

Kwakweli Siku ile nilikuwa naingojea kwa hamu sana ifike sababu nilidhamiria kuzungumza nawewe.

Nilitoroka nawewe nikaenda mbali kidogo Na nyumba yetu,

Ulikuwa una siku 40 tu tangu uzaliwe, nafikiri ndio maana watu walinishangaa sana kuondoka nawewe, tena bila kuwaaga.

Nilienda nawewe mahala nilipopajua mwenyewe, Ninachoshukuru nikwamba nilichodhamiria kilifanikiwa.

Nilizungumza yote na naamini uliyasikia maana hata kawaida yako yakulia siku ile sikuiona kabisa.

Ulinyamaza tuli kana kwamba ulikuwa mkubwa kumbe ni mtoto wa siku 40 tu.

Leo nitakwambia tena maneno yale niliyokwambia miaka ile ukiwa mchanga, naamini utanisikia Na utanielewa maana kipindi kile ulinisikia tu ila  sina hakika kama ulinielewa."

Alizungumza kwa shida Mzee, alilpofika hapa alijikohoza kisha akanyamaza kwa sekunde kadhaa ndipo akaendelea kuzungumza

'WATU'

"Siku ile nilizungumza nawe kuhusu watu, nilikwambia, Watu ni muhimu sana katika maisha yako lakini usiwaamini,

Watakusifia, watasema wanakupenda, watakuita ndugu, rafiki, mtu mwema na kila jina lenye kukupendeza watakuvika lakini endelea Na msimamo wako ' usiwaamini'.

Watacheka nawewe, watakumegea siri zao, watakukumbatia kwa upendo lakini bado mwanangu, sio kigezo chakuwaamini.

Ishi nao kwa akili kubwa, tahadhari iwe muongozo wako, maana ni kawaida yao kupanga njama za kukusaliti hata bila sababu ya msingi.

Hawa watu waone tu hivyo hivyo, lakini wana kawaida yakupenda kuombwa lakini hawana desturi yakutoa,

Ukiwa nacho hawatafurahia sababu wanapenda kusikia shida zako, lakini ajabu siku ukiwa hauna hawatajitokeza kukusaidia, hiyo ndio kawaida ya watu.

Wameumbwa kwa maajabu sana, ishi nao kwa umakini, maana siku zote wanapigana ili ionekane mitazamo yao ndio Bora kuliko wengine.

Dharau ni asili yao, Tazama wasikudhoofishe.

Naomba sana uwe muangalifu Na hiki kitu kinaitwa chuki, ni kawaida ya watu kuwachukia wenzao, asije akakuaminisha mtu kwamba utachukiwa tu bila sababu,

Hapana!!.

Ukiwachunguza sana wanaokuchukia bila sababu, utakuja kubaini kuna kitu wanakihofia kwako,

Ndio,

 lazima kuna kitu utakuwa umewazidi maana hakuna chuki isiyo Na sababu,

Amini nakwambia.

Pia,

Watu hupenda kusujudiwa, mwanangu nakuonya usije kufanya Jambo hili!!

Wakusujudiwa ni MUNGU pekee.

Muheshimu kila mtu, hii sio dhambi, heshima ni jambo tumesisitiziwa,

 Ila sitisha kutoa heshima yako haraka iwezekanavyo kwa mtu asiyekuheshimu.

Halafu ni kawaida kwa watu kujipenda kuliko wanavyowapenda wengine, ukiliona suala hili kemea kwa jina la MUNGU wako maana yeye hakuagiza hivyo.

Naomba sana wapenda wengine, maana kuna hatari kubwa ya anayejipenda mwenyewe kuja kujizika mwenyewe siku za usoni.

Kitu muhimu zingatia, watu siku zote hawana chuki nawewe bali kile ulicho nacho, nilisema mwanzo Jambo hili hapa narudia tena ulichowazidi ndio tatizo hivyo kikumbatie Na ukifanye kwa Utashi zaidi, ipo siku watakuheshimu nacho.

Fahamu kwamba Watu wana akili Na wamepewa ufahamu, wanatambua maovu Na mema lakini wengi wao ni wafuasi wa maovu, sasa akili kichwani mwako, ukemee au uwe miongoni mwao.

Kitu cha mwisho siku ile nilise...."

Kufika hapa Mzee alisita kisha akakohoa "koh ...koh...."

Huruma ilinivaa, nikaongeza umakini kumtazama, kuna maneno alikuwa anayazungumza.

Kwa tabu sana niliyang'amua, alikuwa ananiagiza nimpe maji.

Haraka sana nikalikamata jagi la maji lililokuwa pembeni mwa kitanda chake.

Nilikamata Na glasi kisha nikaanza kumimina maji kwa haraka.

Sikuwahi!!!

Mzee alikuwa anarusha miguu huku Na kule.

Ishara mbaya,

"Baba ndio anakufa!?"

 Nilijiuliza kwa hamaki, glasi ilinidondoka mikononi nakuanguka chini kwa fujo.

Sikujali.

Umakini wangu woote ulihamia kwa Mzee.

Hakika alikuwa kwenye hatua za kifo.

"Toa shahada....baba toa shahada..... Mzee jikaze utoe shahada"

Nilizungumza kwa msisitizo, nikiamini Mzee akitamka shahada basi safari yake ya kuzimu itakuwa nyepesi.

Nashukuru alinielewa, kwa mbali niliona akijitahidi kunyanyua kidole chake cha shahada nikaanza kumtamkisha maneno ya kumpwekesha MUNGU Na kumtambua Muhammad kama mjumbe wake...

Baba akanyamaza.

Izrael akamkabili,
Kifo kikatamalaki,

Wosia wake kuhusu watu bado ungali nami mpaka hii Leo.

Mama yangu pia aliwahi sema kuhusu watu.

Aliniambia 'WATU NI SAWA NA MZIGO WA KINYESI, UKIUWEZA KWA UZITO BASI UTAKUSHINDA KWA HARUFU....'

Samahani sijawatajia jina langu naitwa Adam.

Kwaheri.

Na.
Omar ZONGo
SIMULIZI ZINAISHI

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »