Kwaheri 2021

 Wakati unakuja tulikupokea kwa Matumaini makubwa na imani yetu ni kwamba nuru ya mafanikio itatuangazia kwa wingi ndani ya siku zako.


Matokeo ya tulichoamini na tulichokitumaini ni siri yetu maana ndani yako tumejifunza kuwa kinywa kinachonyamaza kinaiacha na uzima shingo.


Walioshindwa kuficha hasadi zao na kutuonyesha wazi chuki walizo nazo juu yetu ni wengi.


Kinachoshangaza majina yao ni ya watu ambao mwanzo tuliamini ni majirani wema.


Walioacha kutuamini kwa kuhisi ni wazembe na hatujielewi ni wengi pia.


Waliongoja tuanguke ili watucheke hawakukosekana na waliotabasamu kinafki kila tuliponana nao tuliwabaini tukakosa cha kuwafanya.


Walioacha kupokea simu zetu kwa kuhisi tutawapiga vizinga ni wengi kama idadi ya waliokataa kujibu meseji zetu kwa kujua kuwa tuna shida.


Matendo yetu ya wema yaliyopokelewa kama ni shobo na kujionesha ni mengi kama yalivyo malipo ya dhuluma na chuki tulizoambulia.


Mifuko yetu iliposhindwa kununua upendo tukaambulia dharau na kupuuzwa.


Juhudi zetu za kuonesha talanta na tunu tulizojaaliwa zilitafsiriwa kama ujinga usio na tija yeyote.


Waliokataa kutupa pesa za matibabu ili tupone ndio waliohidi kutoa eneo la kuzikia tukifa.


Waliopendekeza majina yetu yakatwe kwenye mahojiano ya kazi ndio waliokuwa wa kwanza kutupa pole tulipotolewa vitu vyetu nje kwa kushindwa kulipa kodi.


Unaenda ukiwa na taarifa za majeraha yetu ya kutendwa na tuliowapenda na kuwaamini zaidi.


Unatuacha tukiwa na kumbukumbu ya zile siku tulizoomba tukanyimwa na kunyenyekea tukapuuzwa.


Mahangaiko yetu ya bure yamekuwa na tafsiri za wivu kwa watu ambao hata hawatujui vizuri na wala hatujawahi kuwakosea.


Uthubutu wa kujaribu kila siku kubadili historia ya tulipotoka umechochea vita hata na watu tusioweza kupigana nao.


Ukubwa wa silaha zao na uzoefu wa maangamizi unatulenga sisi tusio na lengo lolote baya kuwahusu isipokuwa tamaa ya kuhudumia walio nyuma yetu.


Purukushani za kujikomboa na maisha zinatuongezea idadi kubwa ya maadui wanaoamini tunashindana nao wakati kweli haipo jirani hata kidogo na hizo fikra zao.


Kwa kuwa hujaja kuamulia wanyonge na wenye haki unaondoka hali ya mambo kuwahusu ikiwa ni shaghala baghala.


Hata bahati inapoamua kuja kwetu hukumbana na vizuizi vingi vya watu wetu wanaotujua.


Idadu ya watu wanaopimia mafanikio yako ni kubwa kama ilivyo idadi ya watu ambao hawatataka ufanikiwe kuwapita.


Mchezo wa kuvutana mashati ili ubaki nyuma umekuwa na umaarufu mkubwa katika ulimwengu wa giza.


Kila anayethubutu kuwasha taa ili kumulika mchezo huo sio tu anauliwa bali pia anachomwa moto na majivu yake yanafichwa kusikojulikana.


Zaidi ya kutufariji tuendelee kupambana haukuwa na neno jengine, ukaribu wako na sisi umetuachia funzo kubwa sana.


Ajenda zilizokuwa chukizo kuongelewa na wazazi wetu zama za kale zimekuwa ajenda kubwa katika siku zako lakini umejitoa hatiani kwa kusema kuwa MTU WA MWISHO ATAJIZIKA MWENYEWE.


nilipoamua kuzima simu baada ya kukutana na mtu mtandaoni anajiita Juma utam nikawasha redio na kusikiliza wimbo unatusishi tupeleke moto as much as we can.


Niliporudi vitabuni kutathmini labda tupo zama za mwisho nikakutana na wewe ukisema Nyuki hakumbatiwi.


Mafumbo yako sijayapatia jibu mpaka sasa unaondoka.


Uendako salimia kama ukipata nafasi ya kutaja majina yetu huko basi ukifikia kwenye jina langu weka kando mapungufu yangu na uwaambie sishindani na yoyote chini ya jua isipokuwa mimi mwenyewe!!


Kumuona mimi bora wa leo niliye na utofauti mkubwa na wa jana ndio dhamira halisi ya jitihada zangu.


Zaidi ya pesa sina kingine nitakachotafuta mwakani, nyayo zangu zipo tayari kukanyaga chochote cha hovyo ili kuruhusu akili yangu ifikiri sawa sawa namna ya kupata pesa.


Kwaheri 2021, karibu 2022...


WEMA UENDELEE.....

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »