Mchamungu Maskani


leo mcha Mungu
nimekuja maskani
umenizidi uchungu
namkemea shetani
enyi vijana wenzangu
twendeni ibadani

kwani wewe ninani
mbona anaturushia
stimu zipo kichwani
wewe unatuzingua
Ibada ndio kitu gani
mbona sijakuelewa

 Hili kweli nijanga
vijana mwateketea
Mungu anamipenda
ndio mana mewajia
punguzeni Maujinga
shetani anawaponzea

masela hili balaa
maskani limeingia
jamaa sijui ni njaa
msikie anachoongea
oyah hebu ambaa
tusije kukuchengua

huruma nawaonea
enyi vijana wenzangu
nawaomba zingatia
nasaa hizi zakwangu
nyakati zimewadia
anawahitaji Mungu

Mungu ndio kitu gani
lini ulimuona akija
mambo ya kizamani
maskani toa kioja
Mungu wetu mjani
kamatia pafu piga

Mungu awasamehe
hamjui mlisemalo
shetani tumkemee
hatapata atakalo
acheni niwaombe
enyi mabarobaro

shika adabu yako
muombee mama ako
hatutaki sera zako
ni hora uende zako
sura ka mbwa koko
fanya usepe zako.

maarifa ndio hamna
basi pokeeni yangu
nafanya kila namna
kuwaokoa wenzangu
shetani hana maana
rejeeni kwa MUNGU.

Ila masela kweli
hebu tumsikilize
pengine hili zali
wahuni tusipuuze
mbingunu ujue mbali
ubishi siendekeze

haya sema haraka
skani umefata nini
kama huwezi ondoka
kahubiri kanisani
laa hujaokoka
kaswali msikitini

Asanteni kwa muda
enyi kizazi potofu
achaneni na wida
rejeeni uongofu
msiupoteze muda
leo hai kesho mfu

Anzeni sasa ibada
dunia kuti chakavu
uchaMungu si ukuda
ni njia ya uwokovu
jivunieni faida
hamtabaki na kovu

walikuja manabii
werevu na watukufu
wakaiweka bidii
kutangaza uongofu
ajabu dunia hii
yaongoza kwa uovu

kuna maisha baada
tazama nyendo zako
uzima upo kwa muda
uchunge ulimi wako
na uheshimu ibada
ina manufaa kwako

wekeni chini sigara
mibange mihadarati
iepukeni hasara
madawa sio rafiki
maombi kwenu ni bora
shetani ana unafiki

eh baba wa mbinguni
mfalme wa vitu vyote
nakuleta masikani
uondoe dhambi zote
vijana hawa makini
ibadani tuwe wote

waondoke leo nami
nikasali nao wote
waondoshe dhambini
usimuache yeyote
zile bange za kichwani
Mungu ziondoshe zote

ndugu semeni amin
maombi yapokelewe
kisha ondokeni nami
twendeni mkaokolewe
yoyote mwenye imani
naomba anyookewe


blaza asante sana
wokovu tumeuona
bange sasa hapana
ni ibada kwa sana
chars mshtue kombe
ili ibadani twende

mwana umetisha sana
hizi tano pokea
masikani sikai tena
ibadani naelekea
kauli yangu nasema
Shetani kapungukiwa.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »