TWENDAPO WAZEE HAWATAKUWEPO!!!

"Huko twendako, siku baada ya hizi nina uhakika wazee watakuwa viumbe adimu kuonekana katika sura ya dunia hii! sababu ni nyingi lakini chache kati ya hizo ndizo nitakazoziwekea mkazo katika andiko langu la leo!"

Na
Omar Zongo

Baridi kali inayopuliza mwilini inasababisha mwili usisimke kwa woga vinyweleo visimame, hali hii ya hewa ni sababu tosha kwa wavivu kuvuta shuka hasa mishale hii ya asubuhi lakini kwangu ni tofauti, saa kumi kamili za alfajiri niko macho natafakari utashi wa MUNGU.

tafakuri yangu hiyo inaenda sambamba na vitendo vyangu takatifu vyakujiandaa kwenda masjid kumsujudia mwenye dunia hii, mwenzenu imani yangu ni muislamu lakini namshukuru MUNGU sijawahi kukashifu imani za wengine.

vitendo vyangu vya maandalizi yakujiweka safi kimwili na kiimani vinachukua kama dakika kumi na tano hivi, najipuliza marashi, navaa msuli wangu kwa kuukunja vema mkwiji, shati langu safi nililoliandaa kwa ajili ya swala ile kisha nalisindikizia na koti kubwa ili angalau kuzuia ubaridi usiendelee kunipa adhabu!

Sasa nimekalimika kwenda kumsujudia aliyeniumba mimi na kuumba kila unachokifahamu ulimwenguni hapa! msikiti uko mbali kidogo hivyo nina kama mwendo wa hatua elfu mbili mia tano ili kuufikia lakini nitafanyaje na wakati nina nia yakuswali na waumini wenzangu, Njiani nipitapo waja wachache mno.

ndio, lazima wawe wachache maana sio wote wenye ujasiri wakudamka mishale ile hasa kama hawana sababu za msingi!

ni kunguru na ndege wengine ndio nawaona kwa wingi kwenye misitimu ya umeme wakijibizana kwa sauti zao, kichwani kwangu natafsiri sauti zao kuwa ni kelele za kumtukuza MUNGU muweza vyote! nami kimoyoni namtukuza MUNGU maana nimeambiwa kitabuni kuwa ameniumba kwa ajili hiyo tu.

hatua kadhaa mbele ghafla mwili wangu unanisisimka mno! najiuliza ni kwanini hali hii!? hisia mbaya zanivaa, wazo kuhusu uchawi na hila za majini na binaadamu wabaya lanivaa!

naingiwa na woga kwa mbaali lakini ghafla ndani yangu sauti ya imani kwa MUNGU inanijaa! nakumbuka kukimbilia mikononi kwa mungu kuomba ulinzi wake! napiga dua za kujihami na shari za ubaya wa aina yoyote unaotaka kunidhuru asubuhi ile.

Naam! MUNGU ni mwema ghafla tumaini lanivaa, woga waniepuka sina tena wasiwasi,
imani yangu kwa MUNGU bila shaka imeniweka mbali na mabaya yote yaliyokuwa yananisisimua mwili wangu, kiukweli muda ule sikuona lolote baya lakini waswahili husema kuwa ukihisi mwili wako unakusisimka ujue kuna shari karibu yako, hivyo mie nikaona busara kujikinga kwa MUNGU wangu mlezi.

kama una imani nawe nakushauri kufanya hivyo! kila unaposisimkwa na mwili katika mazingira hatarishi

Hatua zangu Imara hatimaye zikakomea msikitini, Kabla yakuingia ndani ya nyumba hii tukufu namshukuru Mungu kwa kunifikisha salama, maana kutopishana hata na vibaka,wezi au majambazi ni baraka tosha kwakweli.

Jicho langu sasa laangaza msikitini, uzuri ni kwamba tayari nilishachukua udhu nyumbani hivyo nikaingia tuu nakuketi msikitini kusubiria adhana ili niswali sunna!

wakati nimekaa kitako mule msikitini navuta uladu taratabu kumtaja MUNGU wangu kwa wingi ndipo wazo likanijia, wazo muktasi ambalo nikaona si sahihi kuliacha linipite, wazo lakuwatazama watu wachache waliowahi asubuhi ile msikitini kama mimi!

Nikaruhusu jicho langu liangaze kwa kila mmoja, hakika walikuwa sio wengi hata kama ningetaka kuwahesabu ningeibuka na idadi ya watu saba au nane lakini sio zaidi ya kumi, nakiri katika mtazamo wangu kwa waumini wenzangu wale kuna kitu nilikibaini kuwa ni mimi pekee ndiye nilikuwa kijana kati yao!

wengi walikuwa watu wazima, wazee kabisa wenye umri sawa na baba yangu na wengine babu zangu kabisa! wazo langu likakwamia hapa nikajikuta najiuliza kwanini wazee tuu ndio wana muamko wakufanya ibada kwa wingi???

swali langu hili likaibuka na majibu yangu mepesi ambayo naamini kama tukiyatafakari kwa kina labda huenda tukayafanya yawe mazito.

jibu langu kubwa kati ya mengi niliyoyajibu ni kwamba tunapoelekea wazee hawatakuwepo!!
Ni tafakuri yangu ambayo sina shaka itapigwa vita nakuonekana laana kwa vijana lakini kamwe sitaifuta kirahisi na itaendelea kusalia wazoni mwangu labda ikitokea niyaonayo yakibadilika!
huko twendako, siku baada ya hizi nina uhakika wazee watakuwa viumbe adimu kuonekana katika sura ya dunia hii! sababu ni nyingi lakini chache kati ya hizo ndizo nitakazoziwekea mkazo katika andiko langu la leo!

Kwa mahesabu ya haraka haraka yasiyo hitaji akili kubwa kufikiria utabaini kuwa kwa kipindi kirefu sasa misiba mingi tunayoisikia ni ya vijana wadogo ambao bado damu zao zingali mbichi na zenye nguvu yakuzunguka mwilini kwa kasi iliyo kuu.

hali hii ni tofauti na hapo kale, sitashangaa vijana wa leo wakileta mzaha katika neno langu hili wakiniita Mhenga! lakini ukweli nitausimamia daima sitauacha uniponyoke nafsini mwangu.

nahisi sababu ya vijana kufa kwa wingi katika karne hii ni kutokana na dhambi zetu nakuhatarisha maisha yetu kwa kufanya kwa wingi yale ambayo MUNGU ametukataza kuyafanya.

Uzinzi, Uasherati, Ulevi, Utovu wa Nidhamu na Starehe zilizo kinyume kabisa na maandiko kutoka kwake Jabbar.

Uzinzi huo niliyoutaja matokeo yeke mengi ni sambamba na Maradhi yanayosababisha kifo.

Uasherati pia nimeujumuisha ingawa hauna tofauti na uzinzi lakini nahisi huu umepita mipaka ndipo tunapoona hata matendo yaliyoangamiza kizazi cha Nuhu, hakika hili nalo matokeo yake ni kifo.

Ulevi nao huchangia kwa asilimia kubwa Ajali na mengine mengi yanayokatisha maisha ya vijana, kama vile matumizi ya dawa za kulevya yanayonyonya nguvu na ushababi wa mamia kwa maelfu ya vijana duniani kote.

Utovu wa nidhamu na starehe zilizo kinyume na maandiko haya yote kwa ujumla na mengine yanayofanana na haya huzalisha wivu, visasi, tamaa na mabalaa yanayosababisha wenyewe kwa wenyewe kuuana.

Vijana kwasasa tunaisha kwa kasi inayoogopesha ni nadra sasa mtu kufika umri walau wa miaka 40, yaani thelathini na tano yenyewe mtu amekwepa mengi yaliyotaka kummaliza au kama sio hivyo ndio yuko mbioni kufa aidha kwa virusi vilivyo mwilini mwake au kwa visasi alivyowekewa na wenzake kutokana na kuiba mwanamke wa watu au kuzulumu mali ya mtu.

Nionavyo Mimi miaka ijayo Dunia haitakuwa na wazee au kama watakuwepo basi wachache sana! hawa tulio naso sasa masikini ya Mungu wanadondoka taratiibu sana ukilinganisha na vijana lakini utaratibu huo nina uhakika utawamaliza wote na hakutakuwa na wazee tena maana tunaotakiwa tukawe wazee ndio hivyo tena tumezongwa na vikwazo vyakukanyaga anga hilo la uzee.

Masikini ya Mungu bila shaka wazee wana ile hofu ya kuwa umri wao umeenda mbele, nguvu zao zinawaisha mauongoni mwao kwa hivyo wameamua kujikurubisha kwa MUNGU wao walau watubu dhulma walizozifanya kipindi chote cha ujana wao.

dhana hii inawasaidia wazee wengi kufanya ibada na natamani vijana nao tungekuwa tunajijengea hofu hii kwamba sasa izrael anatuwinda sisi kwa hiyo tuanze kumrudia MUNGU, maana hatuijua saa wala dakika.

lakini Masikini vijana sisi tupo tofauti kabisa na dhana ya wazee, daima tunajiona wenye nguvu na tunaweza kufanya lolote kwa kipidi hiki, mbaya zaidi wakati mwengine tukidiriki kusema kuwa "Muda wakutumia ndio huu, kutubu tutaanza uzee ukitufikia"

Hakika kizazi hiki kinapotea kwa kukosa maarifa! uvivu wakufikiri na kuzifuata hadaa za mpumbavu, mjaa lana, maaluni ibilisi, shetani kiumbe ninayemchukia kuliko wote duniani! MUNGU anilinde na kuniepusha na shari zake mjinga huyu.

Tafakari sasa na unipe jibu jee unadhani TUENDAKO WAZEE WATAKUWEPO??? baada ya hawa waliopo kuisha!

MUNGU atujaalie mwisho mzuri! atuondoe gizani na atufanye tuwe wenye kumtukuza kwa kufuata amri zake!

amen!!!

Muda wa swala umefika, acha nisimame na waumini wachache waliofika msikitini leo, vijana nao tupo ila wengi wazee.

nakuahidi nitakutaja katika swala yangu hasa muda wakusujudi ili uwe mwenye kukumbuka kuwa duniani Tunapita!

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »