umbo lake pambo, mvuto kwa jicho langu, rangi ladha tamu si mweupe si mweusi!
lafudhi yake wimbo lahaja iwe ya pwani, sikio lipumbazike aniitapo jina.
aniduwaze na mwendo mithili yake hapana kaumbwa kwa mapambo na Mungu wa sifa njema.
upole tabia yake si binti wa pekepeke imani vazi lake hofu kwa Mungu wake.
kajaaliwa midomo unene wa kitumbua jicho lake legevu MUNGU kalipaka kungu.
nijione Adamu naye ndiye Hawa Wangu tena anipe faraja tabasamu lake afya.
Ngozi yake mboga wala sio yakughushi mchicha na matembele si maji wala mchina.
kauli yake dira, upole ndo vazi lake wala hawezi kuzira subira tabia yake.
roho yake imani, uchamungu matendo yake, adui yake shetani tumaini lake MUNGU.
mwenye sifa hizi nani namgojea afike simtaki hayawani akija nifilisike.
sitaki jibu dhalili eti nimuumbe mwenyewe naahidi kumsubiri hata kama yu tumboni.
akijue kiswahili maneno yake matamu, kizungu sistahili mie sio lugha yangu.
usomi uwepo kwake tena umsaidie kunitunza mume wake sio anikimbie.
ugumu wa hali hii aje anipe msaada kazini iwe bidii ndio ngao sio mwili.
yeyote mwenye adili akili ilo kamili mtambuzi wa neno hili afike namsubiri.