SALAAM BIN ZONGO

''Katika kuenzi tenzi na ushairi, moja ya vijana wa leo ambao nawaheshimu sana katika utenzi ndugu yangu Fulgency Makayula, ameamua kuogelea katika bahari ya ushairi kwa kuonesha uwezo wake wa tenzi kwa kuandika ushairi huu ndani yake wenye dhima ya barua inifike....sina shaka haina uhalisia wowote na kweli bali ni katika kuonesha ushababi wake katika tenzi....HAKIKA NAKIRI AMENIPA CHANGAMOTO KATIKA KUJIBU UTENZI HUU''



Kwa kheri zake karima, natumai u buheri
Na mimi wa afya njema, tena nina mpya ari
Nimesharudi salama, kwa ile ndefu safari
Salaamu bin Zongo, nisalimie Handeni

Ni miaka mingi sasa, na sikukuandikia
Kama vile tuna visa, kumbe tu kufikiria
Urafiki namba tasa, mimi nawe hesabia
Salaamu bin Zongo, nisalimie Handeni

Isome barua hii, bin zongo usipuuze
Nitapata kufurahi, akisoma na Rupaze
Nitakuja nikiwahi, nikuletee na zeze
Salaamu bin Zongo, nisalimie Handeni

Rafiki yangu wa damu, umeponzeka na nini
Nimeyasikia magumu,yanipa upunguwani
Umekosa ubinadamu, tabia hiyo ya lini!
Salaamu bin Zongo, nisalimie Handeni

Nimesikia nyumba yako, haina amani tena
Kwa hizo kauli zako, watoto walia sana
Uko wapi utu wako, na inaniuma sana
Salaamu bin Zongo, nisalimie Handeni

Nakumbuka enzi zile, tulipokuwa shuleni
Ukarimu na upole, uliuvaa mwilini
Ziko wapi ndoto zile, kuwa bora maishani
Salaamu bin Zongo, nisalimie Handeni

Na hukusita kusema, utajenga nyumba bora
Familia salama, hekima nyingi fikara
Ulimuomba karima, akunyime ufukara
Salaamu bin Zongo, nisalimie Handeni

Naye kakupa nyumba, uzao kakujalia
Na sasa unajitamba, wana wanakulilia
Yanini kujigamba, huku walikusalia
Salaamu bin Zongo, nisalimie Handeni

Ongoka rafiki yangu, unaenda kupotea
Wanipatia machungu, nyumbayo yateketea
Na humuogopi Mungu, nani atakutetea
Salaamu bin Zongo, nisalimie Handeni

Umekuwa mnafiki,tena usiye na soni
Mbele ya halaiki,unalopoka mdomoni
Eti mwanao Maliki, mchawi wa handeni
Salaamu bin Zongo, nisalimie Handeni

Kiti ulichokalia,wanne walishaketi
Kitanda unacholalia,ni chuma sio makuti
Na huyo mkeo pia, kaliwazika kwa noti
Salaamu bin Zongo, nisalimie Handeni

Mimi ni rafiki yako, ukweli nina kwambia
Kwa hizo ziara zako, utakuja kujutia
Ulizaga na wenzako, yajue walopitia
Salaamu bin Zongo, nisalimie Handeni

Ni kweli nyumba ni yako, hakuna kuingilia
Familia pia yako, yanini kututambia
Hilo ni limbuko lako, kupata sichopangia
Salaamu bin Zongo, nisalimie Handeni

Yapunguze majivuno, kwa kauli za kibabe
Embu iga na mifano, hekima nzuri zibebe
Ipunguze minong’ono, na uhuru usizibe
Salaamu bin Zongo, nisalimie Handeni

Bin zongo kwaheri, leo hapa naishia
Ni vema kutafakari, usije kupuuzia
Naenda kwa maakuri, msalimu Faudhia
Salaamu bin Zongo, nisalimie Handeni
Na
 Fulgence Makayula

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »