DUBWASHA

Na.
Bin Zongo

atokapo ni gizani
meusi mavazi yake
usoni haonekani
kuua ndo kazi yake
ameagizwa na nani
siri kubwa jibu lake
wamfatao hatiani
mateso ndio hila yake

wengi sasa kitanzini
wachini hata wajuu
wengine wa kaburini
kwakuyataka makuu
hali tete duniani
roho zote juu juu
mwenyeji wake ni nani
hiyo ndio siri kuu

awahadaa vijana
nguvu kazi ya taifa
nusura yake hakuna
watu wengi washakufa
wazee pia vijana
kawamaliza kwa sifa
yaleo sio ya jana
hali sasa inatisha

sumu yake ladha tamu
ukiionja wanogewa
inachanganyika damu
hutaacha kurudia
kila mara una hamu
kuipata na kubwia
mgeni mwanaharamu
vijana wateketea

sababu zao dhaifu
eti hali ngumu chanzo
afya zao kama gofu
hawalioni tatizo
wanakaribia ufu
lakini sio kikwazo
matumizi maradufu
kuyaondoa mawazo

dubwasha jingi la hila
lateketeza kizazi
ukithubutu kulila
kuliacha tena huwezi
lina nyingi sana hila
vazi lake ubazazi
maombi kwako mola
muondoshe mpuuzi

afrika mpaka ulaya
kapenyeza mauaji
usoni hanayo haya
kuua ndo lake taji
si mzuri ni mbaya
yeye jumba la jinai
kijana pinga hizaya
izo dawa sio chai

muuzaji kwani nani
adui duniani hapa
nguvukazi hatiani
anauleta uhaba
mateja wengi mtaani
kazi yao nikukaba
pingu amfunge nani
kibosile muuza unga.

tupige goti tusali
tamati imeshafika
dunia sasa hatari
uozo kote wanuka
dubwasha kama jabali
limegoma kusagika
vijana mjihadhari
utu wenu waondoka.

wasanii nao kundini
wameuvaa mkenge
afya zao zitaabuni
akili zina mawenge
hawatupi burudani
mavazi yao mabwende
maji sasa yashingoni
mgeni fanya uende

Na.
Bin zongo

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »