TUMAINI LIPO

Kila siku mpya napata tumaini jipya hasa ninapouchunguza mwili wangu nakubaini hauna hitilafu yoyote ya maradhi, nashukuru nakuamka nikiwa na amani licha ya kwamba sina uhakika wakifungua kinywa, tumaini langu laniambia leo ndio siku ile ya mapinduzi ya maisha yangu.

siku ya kugeuza mawazo kuwa vitendo, siku ya ahadi kutekelezeka, siku ya nuru mpya katika kiza cha ufukara na maisha ya bahati nasibu.

naamka kwa miruzi, salamu zenye bashasha kwa majirani, utani wa hapa na pale pamoja na ucheshi unanifanya nionekane mwenye furaha nisiye na shida, mtu niliyeridhika na maisha, hakuna ajuae siri ya amani yangu!.

natembea kwenda kwenye mitego yangu, njiani nakutana na wengi waliokunja sura zao kana kwamba hawakufurahia kuamka kwao. natamani kuwaambia watabasamu hata kidogo lakini nashindwa nabaki kuwatazama mimi kwa tabasamu huku nikiwasalimia kwa furaha.

wananijibu kama mimi ndio chanzo cha matatizo yao lakini sijali, naendelea kutabasamu nikiamini kuwa ile ni siku mpya inayonihitaji tena nipambane kuleta mageuzi ya maisha yangu.

sijawahi kukata tamaa tangu nilipogundua kuwa kukata tamaa ni rafiki mnafiki anayekuelekeza kwenye njia yakushindwa pekee.

njaa inanikwangua tumboni lakini kwangu mimi naichukulia kama kengele inayonikumbusha wajibu wangu wakuhakikisha natafuta chakula cha kesho na keshokutwa na sio cha muda ule tu! kengele ile ya njaa inayolia tumboni kwangu inanikumbusha kuwa duniani wapo watakaonihitaji niwalishe wakiwa na njaa hivyo nihakikishe napambana kupinga watu hao wasije kuumizwa na njaa kama nilivyo mimi.

njaa yangu isiyopata shibe kutokana na ukata wangu ni ishara yakunionesha thamani ya kazi nakunijengea huruma siku moja nitakaposhiba nimuelewe mwenye njaa. naamini hii ndio tafsiri ya njaa yangu napata tumaini nazidi kukaza mwendo kuelekea mapambanoni.

nimimi pekee ndiye ninayejua kuwa sio kila anayecheka nakufurahi ameridhika kimaisha naamini kuwa wengi ni kama mimi wanaamini katika uzima wao na zawadi ya siku mpya waliyopewa.

hata wewe anza sasa kuiona thamani yako maana ni wewe ndio umeamka mzima wakati mamilioni ya viumbe hai duniani kote wamekufa usiku wa jana, kuna sababu gani yakutoiona thamani yako na sababu za wewe kuendelea kuishi!

ishi kikamilifu, igiza ukamilifu kuonesha udhaifu wako ni kupoteza tu muda wako hakuna atakayekusaidia katika hayo madhaifu zaidi watakucheka nakutumia fursa ya udhaifu wako kukudhoofisha zaidi.

Tumaini lipo katika kila siku mpya! hakikisha haukati tamaa, tafuta tumaini lako ukiwa na amani, usinune maana hakuna mtu sahihi wakumnunia sababu ya shida zako.

kila siki iitwayo leo amini tumaini lako lipo na upo mkono wa msada ambao hufanya kazi kwa siri kukusaidia ufikie malengo yako. Pambana usichoke!

IGIZA UKAMILIFU 2017

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »