Nina jivika upofu, kwa navyo shindwa tazama
Kwa mawazo yangu
nyofu, fikara sizo chutama
Hakuna cha upotofu,
jicho pevu kutazama
Azima
ya moyo wangu, chanda cha pete fikiri
Chanda
nilikuchagua, moyo wangu kutiisha
Tena nilikubagua,
kwa misingi ya maisha
Kama jua limetua,
joto umelikatisha
Azima
ya moyo wangu, chanda cha pete fikiri
Wewe ndiye wapekee, kwa ndugu zako watano
Ukipenda nikemee,
ntajifunza kwa mifano
Sikupenda ulegee,
tena niliuma meno
Azima
ya moyo wangu, chanda cha pete fikiri
Chanda changu
kitulivu, usie penda mapuro
Najua u msikivu, na
usiyetaka kero
Yakatae machakavu,
yamenipaka uchuro
Azima
ya moyo wangu, chanda cha pete fikiri
Ni wapi nilikosea,
hata nashindwa kung’amua
Kule niliko potea,
ni vipi nitagundua
Mbona nilikupepea,
kwa huba njema za dua
Azima
ya moyo wangu, chanda cha pete fikiri
Mimi nilifunga nia,
kwa penzi loshikamana
Nilifurahi kuingia,
kwa pendo la kujichana
Siri sikujifichia,
nilikuweka bayana
Azima
ya moyo wangu, chanda cha pete fikiri
Ndugu niliwaambia,
na bibi akaafiki
Ndugu wakanihusia,
ni wachunge wanafiki
Tuiogope Dunia,
isije kutupa chuki
Azima
ya moyo wangu, chanda cha pete fikiri
Chanda usinichukie,
husuda kuchukiana
Juto lisikuingie,
moyoni likajazana
Msamaha nipe mie,
tupate kuelewana
Azima
ya moyo wangu, chanda cha pete fikiri
Nilikuvika dhahabu,
nikakupa alimasi
Ni ipi kubwa
sababu, inanipaka kamasi
Nalijitia ububu, kukupatia wepesi
Azima
ya moyo wangu, chanda cha pete fikiri
Ulizichukia gubu,
nakumbuka ulisema
Ulijawa na gadhabu, hata juu ukahema
Ila yote nilitubu,
hali ikawa salama
Azima
ya moyo wangu, chanda cha pete fikiri