Na, Bin Zongo
ndani ya daladala
kanilipia nauli
kauepusha msala
konda ni baradhuli
suraye naikumbuka
ila jina simjui
ilikuwa ni patashika
ingekuwaje sijui
sikuwa nakupashika
abiria siwajui
suraye naikumbuka
ila jina simjui
alikaa pembeni yangu
hata sikumsalimia
nilijua mambo yangu
wala sikumzingatia
suraye naikumbuka
ila jina simjui
konda adai chake
nauli azikusanya
natazama ili nimpe
hapo naanza kuhanya
suraye naikumbuka
ila jina simjui
natazama mfukoni
nauli yangu siioni
aibu aibu gani
nauongeza umakini
suraye naikumbuka
lakini jina simjui
damu yangu nakonda
zilishakataana
tangu naanza kupanda
tulikuwa twarumbana
naanzaje kumpanga
yakwamba nauli sina
suraye naikumbuka
ila jina simjui
oyah nipe nauli
konda asisitizia
aibu kuikabili
ndio kitu nawazia
suraye naikumbuka
ila jina simjui
abiria jirani yangu
kituo chake kafika
ajabu alipa yangu
nauli kisha ashuka
suraye naikumbuka
ila jina simjui
tayari nimeshalipa
dirishani aniambia
gari laanza kuondoka
asante sijamwambia
suraye naikumbuka
ila jina simjui
fikira zaenda mbali
yule binti ninani
msaada wake johari
kunipa ameona nini
suraye naikumbuka
ila jina simjui
nawaza labda nimwizi
nauli yangu kaiba
zambi zinipiga mbizi
imani yangu ni haba
suraye naikumbuka
ila jina simjui
safari yatamatika
najiandaa kushuka
nauli nayo yaanguka
kitini nilipokaa
kumbe mapepe yangu
nauli ilikuwepo
najutia nafsi yangu
mawazo yalonijaa.