Na.
Bin Zongo
1:
moja ndio saa
dakika kadhaa
naamka nakaa
tumboni nnanjaa
hii siku itaisha
2:
mawazo yajaa
kichwani balaa
dunia hadaa
nna dhiki na njaa
hii siku itaisha
3:
miale yaangaza
siku mpya yaanza
ntaishije nawaza
dhiki zanimaliza
hii siku itaisha
4:
nakiacha kitanda
sinapo pakwenda
naanza kupanga
vipi ntashinda
hii siku itaisha
5:
mtaani nadaiwa
luku ni zamu yangu
kooni nimekaliwa
yaniponza hali yangu
hii siku itaisha
6:
kuoga bila sabuni
sijui naoga nini
mikosi mwilini
sinayo amani
hii siku itaisha
7:
chumba cha uani
karibu na chooni
asubuhi foleni
kumejaa pomoni
hii siku itaisha
8:
toka basi uani
asemavyo jirani
mekawia chooni
usoni nina soni
Hii siku itaisha
9:
narejea chumbani
chakuvaa sioni
hodi mlangoni
najiuliza ni nani
hii siku itaisha
10:
taulo kiunoni
nafika mlangoni
kufungua ni jeni
nadaiwa jamani
hii siku itaisha
11:
chai na maandazi
ulikula na maharage
kunilipa huwezi
mpaka tufatane
hii siku itaisha
12:
anena bila kificho
jeni mwanahizaya
hajui kama sinacho
usoni naona haya
hii siku itaisha
13:
nitakupitishia
kuvaa namalizia
najitutumua
uongo kumwambia
hii siku itaisha
14:
hayo maneno yako
nimeshayazoea
hesabu pesa zako
chakwangu kunigawia
hii siku itaisha
15:
pesa niitoe wapi
wazo naliwazua
sura niiweke wapi
jeni kang'ang'ania
hii siku itaisha
16:
jeni naomba nielewe
nitakupitishia
na chai niwekewe
nakuja kununua
hii siku itaisha
17:
ole wako usije
utaniona mbaya
acha nikungoje
Jeni aniambia
hii siku itaisha
18:
kabla sijaufunga
mlango babuu aja
baba mwenye nyumba
siku hii majanga
naamini itaisha
19:
kijana habari yako
naitaka pesa yako
luku ni zamu yako
wanalalama wenzako
hii siku itaisha
20:
aah eeeh mzee
kigugumizi lukuki
hii hali aisee
furaha siikumbuki
hii siku itaisha
21:
sitaki porojo zako
usumbufu tabia yako
ikiisha kodi yako
ruhusa uende zako
hii siku itaisha
22:
unadaiwa na maji
tumeshaletewa kodi
hii leo jitahidi
pesa izo kukabidhi
hii siku itaisha
23:
nawaza nisiku mbaya
hapana mawazo hasi
mola atajaalia
itaniisha mikosi
hii siku itaisha
24:
narudi ndani kinyonge
simu yangu yaita
apigaye kaka bonge
anayeishi geita
hii siku itaisha
25:
dogo metuma pesa
tumia ikiisha sema
mgodi haujaniangusha
juzi na jana umetema
hii siku inaisha
26:
mgao wako pokea
namama nimemtumia
msiache kuniombea
maisha huku hatia
hii siku inaisha
27:
chakujibu nimekosa
zaidi ya asante kaka
simu yake yakatika
shauku pesa kuiona
hii siku inaisha
28:
kiasi kingi balaa
mtaji wa biashara
elimu haikunifaa
ni ngumu sana ajira
hii siku inaisha
29:
mipango yapangika
kweli pesa ndio dira
jeni nitamlipa
ni nzuri sana subira
hii siku inaisha
30:
baada ya madeni
wafaa mradi gani
mawazo kichwani
mechoka umasikini
hii siku inaisha
31:
Fahari meziacha
mechagua kuzalisha
pesa naizungusha
naamini itanilipa
hii siku inaisha
32:
wazo nakamilisha
nautaka uwakala
mapesa kuyahamisha
sitakosa hata kula
hii siku inaisha
33:
hatua moja yaanza
utaratibu kuufata
mpaka kutanda giza
jawabu nimeshapata
hii siku inaisha
34:
ntalipa miezi sita
kizimba cha biashara
biashara zote naweka
sitaitaka hasara
hii siku inaisha.
35:
nalala na amani tele
mwishowe naiona nuru
muache Mungu aamue
kufuru isije kudhuru
Nasasa Siku Imeisha.
SIMULIZI ZINAISHI