"ISHI UKITAMBUA KUWA WAJA WALIKUJA WAKAWA NA KISHA WAKATOWEKA! NA HIVYO NDIVYO ITAKAVYOKUWA KWAKO NA KWANGU! TUTAACHA HISTORIA. HAKIKISHA INAKUWA HISTORIA YAKUIGWA"
Na.
Bin Zongo
Kama ikitokea nafasi iliyo ngumu kutokea kama yalivyo mapigo ya moyo kwa mfu,itumie!
usiikatae hata kidogo, hakikisha nafasi hiyo inakuwa ya kwako, imiliki na urudi tena maana ule upenyo uliouacha mithili ya pengo bado hauna namna yoyote yakuzibika.
sijui utofauti uliopo kati ya hapa ulipokuwa na huko ulipo sasa, lakini naamini wewe ni shahidi wa kitu kilichopo hapa kiitwacho 'bahati' kama ikitokea kitu hiki ama kinachofanana na hiki kinakudondokea kamwe usisite kukiokota.
naomba sana ukiokote kwa juhudi huku ukitambua kuwa tendo hilo ni msaada mkubwa kwangu yaani mithili ya ngumi nzito itakayomdondosha chini adui huyu aliyenizonga mwenye jina la Upweke.
nidhihirishie upendo wako! upendo ule ambao mpaka leo sijapata mfanowe, naomba unidhihirishie kwa kutumia nafasi hiyo itakayokupa abra yakurejea tena.
tendo lako lakurudi litazua taharuki, na litawasisimua wengi!! hapa sitaki kuficha hata mie nitastaajabu mno na pengine nitahisi nimezama katika tope la ndoto.
lakini naahidi kuwa sitadumu katika ulimwengu wa kustaajabu, nitarejewa na akili yangu nakutabasamu huku nikukufuata nakukumbatia kwa hisia.
sitakuwa na namna yoyote yakuzuia machozi yangu yasijenge mfereji katika mashamvu kabla yakutiririka kwa kasi kwenye mgongo wa ardhi, najua wengi watakutenga na pengine unaweza kujutia kabisa kuitumia nafasi hii ninayokuomba uitumie endapo ikijitokeza.
Naomba nitoe ahadi kwako, kamwe sitokutenga maana ni mimi ndiyo ninayekutana na adha ya ukiwa si mwengine! Nawezaje kukukimbia nakukuona wa ajabu wakati nimekuomba mwenyewe uitumie nafasi hiyo endapo ikijitokeza.
Ukipata nafasi hiyo rejea, mguu wako ukuelekeze kwangu! Hata kama ni usiku wa manane niite dirishani, nitakufungulia mlango, nitakukaribisha na nitakuelezea yote yaliyojiri katika maisha haya ya bila wewe.
Asubuhi ikifika nitawajulisha ndugu zangu ambao najua nao wanatamani sana ungekuwepo, nitamsikiliza kila mmoja amepokeaje taarifa hiyo yenye kuleta mashaka na kuondoa sifa ya ukawaida, kama atajitokeza mmoja akatamani tena kumbatio lako lenye kutia faraja nitamuelekeza ulipo. Laa kama wote wataniona mtu wa ajabu sana na hawatakubaliana na marejeo yako basi nitawatenga kama ambavyo watanitenga.
Ukipata nafasi rudi, naamini nitaacha vitu kama kuongea peke yangu nikiamini naongea nawewe, na kuhuzunika hasa nikikumbuka maneno yako ya mwisho kabla hujaniacha.
Ulisema unaondoka, tutakukumbuka na tutakulilia, ulisema unatupenda na tusijali hata huko uendako utatuombea! Mishale ya saa inakimbia sana ilijenga sekunde, dakika, saa, siku, wiki na sasa ni miaka kadhaa bila ya uwepo wako.
Kama ninavyotamani kula niwapo na njaa ndivyo niavyotamani urudi kipindi hiki ambacho nina dhiki ya faraja, muongozo na upendo.
Kama ninavyotamani kula niwapo na njaa ndivyo niavyotamani urudi kipindi hiki ambacho nina dhiki ya faraja, muongozo na upendo.
Kutamani ni tendo ambalo halifanani kamwe nakuomba! Siombi hayo yote niliyoyasema yawe kweli ni matamanio tuu ambayo naomba yaendelee kubaki matamanio YASIYOWEZEKANA.
Maombi ninayoyataka yaitikiwe ‘amin’ ni wewe upumzike kwa pumziko lenye amani huko uliko mpaka pale namimi nitakapokamilisha lile andiko lisilopingika nakuweka historia ya aliwahi kuwepo.
Naamini ipo siku tutakutana na kukamilisha ya vitabuni ya kuwa yapo maisha baada ya kuishi.
"ISHI UKITAMBUA KUWA WAJA WALIKUJA WAKAWA NA KISHA WAKATOWEKA! NA HIVYO NDIVYO ITAKAVYOKUWA KWAKO NA KWANGU! TUTAACHA HISTORIA. HAKIKISHA INAKUWA HISTORIA YAKUIGWA"