IPO SIKU NITADONDOKA


"Safari ya kifo ni safari inayoumiza sana maana ina nguvu kubwa isiyoweza kupingwa na matakwa yako, ni mithili ya kuisha kwa mshumaa au kuzama kwa jua, ULAZIMA WA SAFARI HII NDIO UNASISIMUA NAKUSIMAMINZISHA MNO...lakini hakuna jinsi naomba niukubali ukweli IPO SIKU NITADONDOKA"

Na
Omar Zongo


Kamwe usije kusema utaniokota sababu safari hii ni ya kificho, hajulikani ni nani wa kuanza na nani wakumaliza.

sote tupo matayarishoni na huo ndio upekee wa safari hii, mimi nikidondoka ndio kipindi ambacho simulizi zangu zitasisimua zaidi kuliko hivi sasa na Pengine uthamani wake utaongezeka zaidi.
ipo siku ingawa siijui ni lini lakini naamini nitadondoka!

Wapo ambao watashtuka sana huku vichwa vyao vikirejea wasifu wangu na namna nilivyokutana nao nakufahamiana nao.

Nina uhakika siku hii itakua ni yakutaja mazuri yangu tu na hata walionichukia bila sababu za msingi watabaini kua sikuwahi kuwakosea mpaka wanichukie namna hiyo, hapa ndio watajua sikuwahi kuwa na makosa nao.

Siku nikidondoka wapo ambao watasadiki kua mpambanaji ameondoka.

Wapo wataokiri kwa vinywa vyao na wengine kwa mioyo yao tu.

Yaani sipati picha lakini nikidondoka kinywa changu hakitaweza kunyanyuka ishara kuwa hakuna la ziada nililo bakisha kulisema hapa duniani.

Kitu cha muhimu acha nikiseme kabisa kabla sijadondoka ewe mungu wangu nakuomba nisamehe dhambi zangu, nakiri kuwa mimi nimkosefu katika hili na lile nisamehe sana mana mimi ni kiumbe dhaifu kwako na ni wewe pekee ndio mwenye haki yakuabudiwa na kusujudiwa! Nisamehe leo nikiwa nimesimama na kesho nitakapodondoka! Msamaha pia upatikane kwa wote niliowahi kuwakwaza katika nyanja yoyote ile.

Najua nikidondoka macho yatafumba ishara yakutosheka na niliyoyaona duniani!
Hakika nitadondoka nafsi yangu ikiwa huru na yenye bashasha sababu hakuna ambaye atajigamba kuwa eti amenidondosha!

 nitadondoka kwa kudra zake allah, na nitadondoka huku dunia ikiamini kua mimi ni miongon mwa viumbe waliopangiwa kuongea maneno mengi ndio mana nikawa mwandishi.

Watu watakosea sana watakaposema pengo langu halitazibika katika sekta ya uandishi, watakosea sababu mimi nitakapodondoka amini usiamini pengo langu litaandaliwa wakuliziba kwa usiri na wala hakuna atakayejua hilo sababu inaweza kuchukua miaka mingi mpaka kujitokeza mtu huyo, wakuliziba pengo langu.

Hakika nitadondoka na mapigo ya moyo yatazima mithili ya mshumaa! Na mara kadhaa nitataka kujaribu kuwanyamazisha msinililie mimi bali mlilie nafsi zenu lakini ndio hivyo tena sitakuwa na nguvu hiyo tena.
Wengi duniani wataamini nimelala kimyaaa lakini ukweli utakuwa ni huu muda ule nitakuwa napiga soga na malaika wa kila namna wengine watakuwa wa adhabu ambao wengi wao watakuwa wamefura kwa hasira kutokana na makosa yangu niliyoyatenda duniani, watanihoji kwa dhihaka na kiburi. Maswali ya yako wapi yale majigambo yako uliyokuwa nayo duniani!?

Nitabaki kimya nikitahayari nakujutia zile sekunde zangu na dakika nilizotumia kutenda uovu duniani, nitalia nakusaga meno lakini ndio hivyo tena majuto ni mjukuu.

Baadae sana nitakuja kufarijiwa na malaika wapole wenye huruma ambao wao watakuja kwangu nakunipa mkono wakuume nakunipongeza kwa matendo yangu ya wema niliyowahi kuyafanya duniani.

Hakika ni hapa ndipo nitakaposadiki kuwa wema siku zote hauozi na nitajilaumu kweli kwanini duniani sikuwa mwenyekiti wa Chama cha watu wema.

Kitu nilicho na uzoefu nacho kupitia watu walio tangulia kudondoka ni kwamba taarifa zao zilisambaa haraka kwa ndugu na jamaa zao hakika hata taarifa zakudondoka kwangu zitasambaa nakuwafikia wengi wanao na wasio nijua na kila mmoja itamgusa kimtindo wake taarifa hiyo!

 Ingekua maamuz yangu ningesubiri hukumu ya dunia ifike nikiwa hai ili nishuhudie udhaifu wa wanaojiona ni miungu watu wanaotesa, kuua na kunyanyasa binadamu wenzao sababu ya uchu na tamaa ya matumbo yao!

nitadondoka siku na saa ambayo siijui ila nina uhakika nitakua nimetimiza alichonituma mungu wangu na kile nilichomuahidi mama angu siku ile aliyodondoka zakiem hospitali pale mbagala.

Nitajiandaa kwenda kukutana nae nakumpa taarifa ya yote aliyoyaacha duniani, baada ya kudondoka kwake. Hakika nitadondoka! Nalijua hili

na mengi yatabaki historia, sitakua na nijualo kuhusu niliyoyabakisha nyuma ila naamini wachunga mbuzi watanijuza kupitia soga zao! Pindi watakapokuja kuchunga mifugo yao maeneo ya porini ilipo nyumba yangu ya milele.

 nitadondoka nakusababisha bendera ya smulizi ipepee nusu mlingoti!

hakika kudondoka kwangu kutakua ni furaha kwa waliojali pesa kwa kutunga simulizi pendwa huku wakisahau jamii inapotoka kupitia simulizi zao kutokana na jumbe zao kuegemea upande wa starehe nakuacha kabisa elimu imuongozayo mtu.

Ukimya nitakaokuwa nao siku yakudondoka kwangu hautakuwa ukimya wa kiburi eti siwasikii ndugu, mke na watoto wakinililia ila ukimya huo utadhihirisha maridhio ya dhati kabisa yakuikubali safari hiyo chungu ambayo kwangu mimi itakuwa ni safari yakwenda kupumzika katika nyumba yangu ya milele.

Nina uhakika siku nikidondoka ujumbe huu ndio utakao somwa na kusikilizwa mara nyingi zaidi kwa wale watakaokuwa majasiri, nitawapongeza sababu ni ukweli kuwa hii ndio harusi ya tatu katika harusi tatu za mwanadamu, sijui tatizo nini mpaka harusi hii inaogopwa na watu wanalia badala yakucheza vigodoro kama wafanyavyo kwenye siku za kuzaliwa na siku ile ya ndoa.

Siku hii yakudondoka kwangu! Wapo watakaosema nilijitabiria jambo ambalo sio kweli hata kidogo kwa sababu niliiwaza hii siku tangu nikiwa bado kijana mdogo nilijua ipo siku ntadondoka na mpaka leo nimedondoka ni miaka mingi imepita tangu dhamira ya ujumbe huu kuumbwa.

Nitadondoka! Na wala sitataka kabisa kujua kinachoendelea duniani hapa sababu mengi nimeshajionea na mengi hayana faraja nafsini mwangu.

Huzuni nyingi zimenikumba kila niliposhuhudia dhulma, umimi pamoja naukatili uliokithiri nakusambaa  katika dunia hii.

Adha kadha wakadha lakini zaidi mateso makuu yanayowasibu watoto katika nchi nyingi afrika yakisababishwa na vita na mapigano katika nchi zao! Chanzo kikuu kikiwa ni uchu wa madaraka, udini na ukabila pamoja na tamaa ya maliasili zilizoumbwa kwa ajili yetu sote.

Hata ingetokea malaika wakunidondosha angenipa nafasi yakuniuliza kama nataka kuendelea kusimama ningemwambia laa...ni bora nidondoke walau nikaimbe tenzi na mzee wangu shaaban robert,  mwanagenzi mahiri aliyewahi kuishi tanzania hii na kisha akadondoka kama ilivyo ada.

Nitakutana na wengineo lakini kamwe sitakaa kupiga domo na wanasiasa maana watataka kuniulizia habari za wanasiasa wenzao duniani nami sitataka kuwaeleza sababu nilishaepuka kutoa maoni yangu kuhusu jambo hilo liitwalo siasa.

Maana sikuwahi kulielewa tangu nilipoanza kuufahamu utu wangu.

hakika nitadondoka nalijua hili na sijawahi kufanya juhudi zozote zakulipinga sababu ni sawa na kukataa kivuli changu!

nitadondoka na litaimbwa shairi hili!

chanzo nini
jibu fichoni
mwisho duniani
safari mbinguni
ipo siku nitadondoka

safari iso shaka
ipo siku itafika
wahuba nitamuacha
ndugu wote mashaka
ipo siku nitadondoka

mtume hakupinga
binZongo ninani
safari ishapangwa
twapita duniani
ipo siku nitadondoka

kuaga majaaliwa
nadra kutokea
safari ikiwadia
hakuna anayejua
ipo siku nitadondoka

Bendera ya Simulizi
pepea nusu mlingoti
duniani simanzi
safari haipingiki
ipo siku nitadondoka

siku hiyo kiburi
itafika kwakweli
utazimika mwili
duniani kwaheri
ipo siku nitadondoka

hakuna wa kujigamba
safari  kaipanga
mola mwenye kuumba
ndiye mwenye kupenda
ipo siku nitadondoka.

utenzi huu Tanzia
wengi wataupitia
watadai nilijua
kifo nikatabiria

ipo siku nitadondoka

Na.
Omar Zongo


Share this

Related Posts

Previous
Next Post »