NAKUSHIKA SIKIO

Aliposikia hatua za mtu akaongeza umakini nakusogea karibu, ghafla akashtuka paji la uso wake likitobolewa na vyuma vya moto, alikuja kugundua baadae kuwa ni risasi ndio zilipenya kichwani mwake, mwili wake ulianguka chini mithili ya mzigo...

ni hapa ndipo alipongundua SIKIO LAKE LIMEMPONZA kusikiliza hatua za watu hatari na wakatili kiasi kile....alijilaumu kwanini asingepuuza kusikia hatua zile lakini majuto yake hayakuweza kusaidia roho yake isitoke...sasa alikuwa chini akipigania roho yake ambapo dalili zote za kifo tayari aliziona...

SIKIO LILIPONZA ROHO YAKE! nina kila sababu ya kuzungumza na SIKIO LANGU!.
Nakushika sikio!

Na
Omar Zongo

Sikio langu ni dira nzuri ya kuupima muelekeo wa ngurumo za sauti zitokazo pande zote za dunia hii.

leo nasema nawe sikio maana namini wewe ndio kiungo pekee ambacho utanifanya ule umimi niliozaliwa nao, nisiupe nafasi kuwa kero kwa wengine.

usikasirishwe na mabezo ya watani wangu wanaodai nina sikio kubwa ka' upawa wa uji,naomba uyapuuze masikhara yao na utambue kuwa ni mie pekee ndiye unapaswa kusikiliza rai zangu na Thamani ninayokupa.

Sikio langu tafadhali sana nakusihi usije tamani hata siku moja kusikia uliyofumbwa kuyasikia.

leo nakushika sikio unielewe maana yangu na uitambue kuwa sio mbaya bali nikukuepusha wewe na maradhi ya umbea usiokuhusu.

unayopaswa kuyasikia naomba sana uyasikie kwa utashi na uyazingatie, yale yaso na maana kwako yafanye yatoke kwenye sikio la upande wa pili yaburuzwe na upepo kuelekea uendapo.

hivi unadhani ni kwanini duniani wapo watu wanaoitwa hawajiamini? kama ungekuwa una ubavu wakunijibu ningefurahia sana jibu lako lakini kwa vile kazi yako nikusikia na sio kuzungumza acha nikupe sababu za watu kuonekana hawajiamini.

sababu kubwa ni kutokuongea nawe sikio nakukutahadharisha kuhusu kusikia maisha ya wengine nakuruhusu maisha hayo yawavutie nawatamani kuishi kama wao.

kusikia kwako kunaweza kujenga lakini pia kunabomoa wakati mwengine, tafadhali sikio chunga sana na hayo uyasikiayo.

ndoa nyingi duniani zavunjika kutokana na kazi yako yakusikia maneno ya wafitini wasopenda mahusiano ya watu, unaonaje kuanzia leo ukaanza kuwa mpembuaji wa ukweli na umbea au kama huwezi kazi hiyo walau basi uwe na uvumilivu maana sio kila ulisikialo linapaswa kuchukuliwa hatua.

Sikio langu wahuba natambua kuwa niwewe ndio huufanya mdomo utabasamu usikiapo jambo zuri lakini niwewe pia ndio hulidondosha chozi jicho usikiapo jambo baya.

Ni juzi tu sikio langu ulinijengea uhasama na ndugu zangu baada ya wewe kuwasikia wakimsakama mke wangu nakuweka mbinu zakunigombanisha nae.

basi ungejifanya hujasikia nakuipa akili chakufanya lakini niwewe ndio uliuagiza ulimi uteme cheche zilizozaa moto ulioteketeza udugu wetu.

sikio langu wewe ni wewe ndiye ambaye fununu ikikujia hutanuka kuisikia, hupenda vyamotomoto vilivyopoa huvitiwi navyo.

nakushika hii leo uache kupenda ubuyu, madhila ya masuto fedhaha itakuwa yangu.
 tatizo lako ukisikia jambo kutulia nalo huwezi huushawishi ulimi utamke bila haya.

nakushika sikio langu asisikie ya umbea.
kwasasa maisha magumu wachawi nao ni wengi, huja kwako kunong'ona ili nikate tamaa nakusisitiza sana sikio usiwasikie.

maneno yakunidhoofu usiyapenyeze kwako tambua mie nidhaifu nitashindwa kustahimili, na hata yalo na sifa usiyapendelee sana mwisho hudhoofisha ufahari hauna maana.

sikio nakuhusia mie kwako ndio kiti juu yangu umenikalia usifanye tashtiti yawatu ukiyasikia jihimu kuyapuuza.

hivi sikio kwanini huna mashine yakuchuja, umbea na ukweli ungeweza kuuchekecha ningejifaghiri sana waongo kuwaumbua.

sikio sikia yao,
nakisha yapotezee
hauna faida nayo
muda wako usipotee,
kuyawazia ya kwao
ni kuuita uzee,

sio wote wakuombao
 umakini wako ni watu
wengine ni mafarao
wanajiona miungu watu
usiwafatize wao
ukauza wako utu,
nakuusia sikio
zingatia nisemayo.

tanua tundu zako
 kusikiliza adhana,
yadunia yana kutu
usiyafatize sana
yametawaliwa husda,
umbea na ufitina.

sikio tena sikia hili nimuhimu sana, uzima uliopewa usiuchezee rafu,
mwenzio najivunia kiungo wewe muhimu mana wapo walopewa uziwi na upofu.

sikiliza kwa kadiri,
mengi hukinaisha,
naukiombwa usubiri
uache kulazimisha
sikia usitafsiri
mengine utajichosha.
ikibidi  ghairi
wengine wanapotosha.

Jicho lilinisikia nilipotaka livumilie
nawewe nakuambia hadaa uiambae
moyo umeshatulia tangu nilipounanga
bado ulimi wangu kesho nitaupanga

Sikio natamalai naenda kuweka nukta
usiipuze rai ukanifanya kujuta.
utaileta  jinai usipokuwa makini.
kwa kila usikialo kulihifadhi moyoni.

Na
Bin Zongo

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »