UJUMBE KWA WAKWE ZANGU

 ''Katika dunia yetu ya leo malezi ni suala ambalo halipatilizwi sana, wazazi wamekuwa wapuuzaji hivyo kufanya vijana wa kiume kutotambua maana ya uanaume wao na vijana wa kike
  kutoiona thamani yao, kama muandishi nimeona haja yakukumbushia suala la malezi kwa mtindo huu...ifuatayo ni barua kwa wakwe zangu''


Na
BIN ZONGO

Bado sijaoa lakini naamini ipo kaya moja duniani hapa anaishi mwanamke nitakayemuoa na pengine analelewa na wazazi wake Ujumbe huu nataka ufike kwao...
Ujumbe huu uwafikie wakwe zangu na najua mtastaajabu sababu bado binti yenu hamjamuozoesha wala pia barua ya posa hamjapokea.
me naamini ninyi ni wakwe zangu na sitasita kuwaita hivi sababu wahenga walisema NDOA HUFUNGWA MBINGUNI.
mimi na binti yenu tayari tumeshafunga ndoa mbinguni hata kabla nafsi zetu hazijaletwa hapa duniani.
nimewahi kuwaletea waraka huu wa barua ili kuwajulisha mengi ninayoyataka muyafanye kabla sijakutana na binti yenu.
naandika ujumbe huu nikiwa sina hata dalili yakuoa na wala sijui binti yenu yupoje lakini sababu naamini itafika wakati nitamuoa basi naombeni sana mumtunze vema.
mie bado ningali shuleni, nina uhakika hata yeye kwa sasa anasoma, hakikisheni mnamuhimiza basi asome kwa bidii maana dunia hii haimthamini mtu mjinga kabisa.
mwambieni apambane, aje kuwa mwanamke wa shoka mwenye kujiamini na aweze kujenga hoja zenye mashiko kwa lolote litakalomkabili mbele yake.
nataka akiwa mwanasiasa awe mwanasiasa ambaye hajawahi kuzaliwa duniani hapa au akisema awe mjasiriamali basi asimame imara kushinda wajasiriamali wanaotazamwa hii leo, laa kama jaala yake ni sanaa basi aje aifanye sanaa kwa mtindo utakaofanya hata ardhi itikisike kwa utashi wake.
muandaeni aje kuwa nuru kwenu na kwa familia yake atakayoijenga namimi.
nawaomba wakwe zangu muyatazame haya wayafanyayo mabinti wakileo kwa jicho la laana na msichoke kumlaani shetani asimsogelee binti yenu akapata kumshawishi ayaige.
zamani stara ilikuwa ngao yakumtambulisha binti mwema lkn siku hizi wadada wanapuyanga wakiwa nusu utupu, mkemeeni mke wangu kabla sijajuana nae,mwambieni mumewe sifurahii urembo wakujidhalilisha.
mwambieni ajue mie ni mfuasi wa haiba za kike zilizotiwa nakshi za nidhamu,utu wema na uchamungu mwambieni kamwe sitadumu nae kwenye ndoa kama akiwa mwingi wakuiga yaso na mana.
mwambieni mtoto wenu ajue mimi ndie yule wa ubavu wake niliyefunga nae ndoa mbinguni, hata mimi siamini hili wakati mwengine lkn ukweli ndio huo baada yakufunga ndoa yetu mbinguni tumeletwa duniani, kupoteana kwetu haimaanishi kuwa hatutaonana mwambieni ajue tutaonana na ndoa ile ya mbinguni tutairudia tena duniani.
mkumbusheni hili na mumsisitize awe mwingi wa subira maana ni wengi sana watakuja kwake na kwenu wakidai kuwa ndio wahalali.
toeni muda msikurupuke wazee wangu mkahadaika na posa na shilingi mbili tatu kisha mkamuuza mke wangu kwa waroho wa miili ya warembo.
tambueni mimi nipo na wakati wangu ukifika nitajitokeza mbele yenu na kila kitu kitaenda barabara sababu ndoa yetu tayari ilishapita mbinguni kwa MUNGU.
sio kila mtu anafaa kuwa rafiki wa binti yenu nawaomba sana msiruhusu mashosti wakamuharibu mana nitawalaumu ninyi kwa uhuru wenu mliompa.
samahani baba angu mkwe, naomba niongee nawe! kuchapa mtoto sio kumfunza naomba tumia busara kuongea nae kwa utaratibu hicho kipigo unachompa kinamtia usugu utanifanya nioe gendaeka lisiloogopa hata sauti yangu ikimfokea.
muelekeze kwa upole mwambie unavyopenda awe, usimvunje moyo katika ndoto zake na pia mkataze asipende vya bure, vijana wengi wanaweza kutumia nafasi hiyo kumgeuza chakula chao.
Mpeni sifa zangu, mwambieni mimi nipo naandaliwa vema na wazazi wangu ili nije kuwa mume bora kwake,
Mwambieni mama yangu kila siku ananisisitiza sana kuijua thamani ya mwanamke na baba akizungumza nami ananisisitiza kupambana ili nije kuimudu familia yangu, kumtunza mke wangu na kutokimbia majukumu yangu.
mwambieni binti yenu ajue mimi sihangaiki na wanawake sababu najua yeye yupo na itakuwa vema naye akifanya hivyo.
mwambieni athari zakuruka ruka kabla ya ndoa yetu atapata mimba asizozitarajia, na pengine atawaza dhambi yakutoa jambo ambalo litafanya aniharibie mtoto wangu wakwanza aliyepangwa azae na mimi.
haya mimba atatoa je maradhi yasiyo na tiba, mwambieni tu avumilie mengi matamu atakula na mie maana akifa kabla yamie kumuoa ni dhahiri atakuwa amemkosea MUNGU kwa kukiuka mipango yake na pia ataniachia kovu la maisha kwa mie kuoa asiye wa halali yangu.
naomba ajue hili ndoa nyingi hivi sasa zinavunjika kwa sababu hii, hakika nina mengi sana yakuwaomba wakwe zangu muhakikishe mnayafanya kwa binti yenu ili msije kupata dhambi kuniozesha mke wa mtaa mzima mnaoishi.
mchunguzeni mapema ili mjue kama angali bado ana usichana mwambieni wasahihi kuuona ni mie anisubirie maana tangu nijue ipo siku nitkuwa mume wa mtu sitaki hata binti aniite "baby" nazichunga sana nyendo zangu.
mama mkwe naomba uzingatie, muite binti yako umwambie ipo siku atakuwa mke wa mtu, mpe siri zote za kwanini wewe umedumu kwenye ndoa na mumeo kwa miaka mingi.
mwambie madini yako yanayomfanya mzee asing'oke kwako, mueleze namna ambavyo unalimudu jiko na mtambie kuwa wewe ni mwanamke imara lakini haukuwahi kutambulishwa hata siku moja na mawigi ya rangi rangi au nguo za kiuwenda wazimu mueleze ajue kuwa ulimi wako ndio ngao kwa mumeo.
kuulinda kwako ndio mana mmedumu mpka leo.
nawaachia jukumu wakwe zangu kunilindia mke wangu mpka nitakapokuja mwenyewe kuhalalisha ndoa yangu.
mwambieni nilipo namuombea ili aje kuwa faraja nanuru kwangu na kwa familia yangu.

MFALME WA THAMBO

''Imepitia mengi kabla yakuwa nchi yenye kuheshimika duniani, busara zilitumika na hatadamu za watu wengi waasisi wa taifa hilo zilimwagika, historia inaonesha ni miongoni mwa mataifa ambayo yamepiia changamoto nyingi sana na mfalme wa sasa anatimiza idadi ya wafalme 19 waliowahi kuitawala nchi hiyo iitwayo THAMBO''

Na
Bin Zongo

"Mwanangu huyu ni mpendwa nampenda toka moyoni, nashangaa mnavyomponda hata haya hamuoni, acheni mambo ya kijinga hapa kazi hebu fanyeni
siendeshwi na propaganda mie ni baba najiamini..."
Hayo ni maneno ambayo aliyatoa mfalme kwa mwanae wa mwisho ambaye alimpa ucrown prince bila kujali kuna mtoto wa kwanza ambaye kisheria alistahili yeye ndiye awe crownPrince(mrithi wa mfalme).
kwa sababu ambazo mfalme mwenyewe hakuziweka wazi alikuwa akimkingia kifua sana mwanae huyo wa mwisho.
majigambo na mavuno vikamtawala, kiburi kikamgumbika hakujali tena kujenga uhasama na watu mbalimbali tena wazito katika utawala wa baba yake.
watu wengi wakabaki wakitumia uhuru wao wakuongea kumlaumu mfalme kwa kitendo chake chakumkumbatia mwanae bila yakujibu kashfa zinazomuandama.
mwanzoni kabisa iliibuka kashfa ya kuwa yule hakuwa mtoto wake halali hivyo hakustahili kumpa ucrown prince.
kelele hizi zikazagaa kwa kasi mithili ya moto kwenye nyasi kavu! mfalme ambaye ni bingwa wakufukuza watu wazembe kwenye uongozi wake kamwe hakutia neno, aliwaacha watu wabwatuke nakusema bila mipaka.
wengi walimuona mfalme amepotoka, anapendelea na hafuati haki!

* * *
kila siku ya alhamisi mfalme alikuwa anaitumia kukaa ndani tu, siku hii hakupenda kabisa kukutana na mtu, alipendelea kukaa ndani akiiacha nafsi yake iongee!
ilikuwa ni ajabu sana lkn ukweli ulibaki kuwa hua chumba alichokuwa anatumia kukaa mwenyewe kilikuwa na kiza tupu, hakuruhusu hata mwanga uingie, kelele ya aina yoyote hakuipa nafasi kumsumbua mfalme!
hii ilikuwa ni desturi yake, watu wake wakaribu wengi wakawa wanaelezea hali ile kuwa ni ushirikina nanguvu za kijini ndizo zilikuwa zinamuagiza kufanya vile, jambo ambalo lilikuwa ni kinyume kabisa na ukweli wenyewe.
mara zote mfalme aliamini katika kuacha nafsi izungumze, aliona ni ujinga kuruhusu akili yake iishi katika mawazo ya wengine au sauti anazozisikia kila siku, alipenda mawazo yake nayo ayaruhusu yamuongoze, hivyo kwa imani hii alichagua siku ya alhamisi iwe siku yakujitathmini nakuruhusu mawazo yake yavinjari akilini mwake.
Huyu ndiyo mfalme, ambaye pengine siku ya alhamisi ndiyo iliyomfanya awe tofauti kabisa na wafalme wengine waliowahi kuongoza nchi yao.
siku hii ya alhamisi aliamka na msemo uliojirudia sana kichwani mwake, ule msemo usemao "mti mwema ndio unaopigwa mawe".
hata alipokuwa amejifungia ndani peke yake msemo huo bado ulijirudia akilini mwake, aliutafakari kwa kina nabahati iliyo mbaya akauhusisha na mwanae wa mwisho ambaye alikuwa akipigwa vita sana na watu wengi.
mawazo ya mfalme aliyarudisha nyuma akakumbuka siku anamtangaza kuwa crown prince, wiki sita zote za mwanzo hali ilikuwa shwari! maneno maneno kuhusu mwanae huyo yalikuwa sio mengi, hata zile fununu za kwamba yule si mwanae hazikuibuka.
lakini zilikuja kuibuka ghafla kipindi ambacho mwanae alitangaza vita kali dhidi ya wafanyabiashara haramu waliokuwa wakiingiza silaha kinyume na utaratibu.
ile ilikuwa ni biashara inayofanywa kwa usiri mkubwa na watu wazito wenye vyeo vikubwa ndio waliokuwa wakijihusisha na biashara hiyo.
ni biashara ambayo ilisababisha uhalifu na ujambazi katika nchi ya Thambo.
crownPrince aliibua majina yawanaojihusisha nakuhitaji sheria ichukue mkondo wake, hakusita kabisa kusema kuwa amedhamiria kuwataja woote wanaojihusisha na biashara ile iliyowafanya vijana wengi wawe majambazi na wahalifu wakupora na kunyang'anya mali za watu.
mfalme wakati bado akiwa anawaza akabaini kuwa vita dhidi ya crownprince iliongezeka baada ya kuanza zoezi lakudhibiti silaha haramu.
mfalme alimuona mwanae ni mfano wa mti ambao una matunda na ndio mana unapigwa mawe.
Tangu hapo mfalme hakutaka kabisa kusikia maneno yanayoibuka kumuhusu crownPrince, yoote aliyapuuza akiamini ni uzushi ambao unasimama kama mawe yakumponda mwanae mpendwa ambaye ni mchapakazi.
miongoni mwa watu waliotajwa kuhusika na biashara ya kuingiza silaha kinyume nasheria ndio wale wale waliohusika kuibua hoja nzito yakuwa CrownPrince sio mtoto halali wa Mfalme hivyo hafai kuwa katika cheo kile.
Mfalme alibaki kimya bila kujibu hoja ile, aliwapuuza walioanzisha akiamini ni warushaji mawe kwenye mti wenye matunda.
crownPrince kiburi kikamzidi akathubutu kutumia jeshi la Thambo kuvamia kaya za watu nakuwataka waoneshe akiba za pesa zao pamoja na thamani zote walizonazo.
haikujulikana sababu ya crownprince kufanya haya ingawa wananchi wenyewe walithibitisha kuvamiwa na crownprince na ushahidi wa picha ulionesha..
wengi walilaani kitendo kile wakiamini ni ubakaji wa madaraka na ukiukwahi mkubwa wa haki na sheria.
wakukemea tukio lile alikuwa ni mfalme ikibidi kumvua ucrown prince lkn ajabu hakuthubutu hata kuongelea hilo zaidi alimtaka CrownPrince achape kazi, asijali maneno ya watu.
wengi walibaki wakilaumu wakiwemo viongozi wakubwa kwenye uongozi wa Mfalme, bila kujua kuwa mfalme anaongozwa ba mawazo ya alhamisi.
mfalme anaamini crownprince yupo kwenye vita na wafanyabiashara haramu wa silaha, anaamini wapo mstari wambele kumuangusha crownprince ili wafurahi nanafsi zao, mfalme anaamini kuwa crownPrince yote yanayomtokea yanatokana na uhasama wa vita aliyoainzisha dhidi ya silaha haramu zinazoingizwa nchini Thambo.
mfalme anaongozwa na mawazo ya alhamisi, hataki kusikia upande wa pili nahata kama yana ukweli hayajafika katika kipindi ambacho mfalme anaweza kumuamini mtu,
wananchi wote wa thambo wanaamini mfalme huteuliwa na MUNGU wapo baadhi yao wanaamini katika kile ambacho anakiamini mfalme wao na wapo ambao hawataki kuamini wakiamini mfalme anamkingia kifua crownprince.....
UONGOZI WA MFALME BADO UNAENDELEA NA MATENDO YA CROWNPRINCE BADO YANAENDELEA NANI YUPO SAHIHI???? HIYO NDIO SIRI KUU!
Maana hata tafiti duniani zinaonyesha THAMBO ni nchi inayoongoza kwa UONGO unaogeuzwa kuwa UKWELI.
Na
Bin Zongo
MR. EXPERIENCE

UTENZI WA MAHABA

''Zawadi ni chachu ya mahusiano ya aina yoyote ile, mzawadie ulicho nacho yule ambaye unahisi ni sahihi kuzawadiwa nae, naamini tabasamu lake usoni ni ishara tosha yakufarijiwa na zawadi uliyompa, kuna aina nyingi za zawadi, lakini katika mapenzi Maneno matamu ni zaidi ya zawadi zote unazozijua wewe, waswahili huamini NENO HUUMBA......''

UTENZI WA MAHABA
Na
Bin Zongo
leo nachana kifua
nautoa moyo nje
nataka kuyaachia
yalo ndani uyaone

si joto wala baridi
ni wastani kipupwe
leo nataka kuahidi
ukweli wangu nikupe

kupenda kama umbea
masuto nastahili
naapa sitokimbia
majivu ntayakubali

laa kupenda ni homa
matibabu weka mbali
nataka kuumwa homa
joto mwili liwe kali

mapenzi kama ugali
mpunga mie wanini
sitaitaka zohari
mahindi weka chumbani

kupenda jambo geni
sijawahi kabla yako
naapa kwa rahmani
nafsi yangu mali yako

mwenzako kwetu pwani
kudekeza nimefunzwa
kuoga nawe bafuni
Tanga nimesisitizwa

kupiga ni ukatili
uuaji na ujangili
ili niwe kamili
nimeaswa kukujali

mie kwako zawadi
nitunze nitakufaa
nitatimiza ahadi
hutaikata rufaa

sharti langu moja
tulia na ujiheshimu
usije leta vioja
eti hakuna ushemu

urembo wako shani
kumbuka ni mali yangu
tulia nao nyumbani
siuze kilicho changu

mahaba niache hai
ukiniua utanionea
kuwa nawe najidai
upendo wangu pokea

uongo ni msongo
uambae utanitesa
usije shiriki hongo
mwili wako si kipusa

heshima maji baridi
nipe nipoze koo
kiburi kisikuzidi
nisije kusema poo

pesa sio mapenzi
kama ndio ntakuhonga
ubahili sitaridhi
wakati nimeshapenda

matani machombezo
kufinyana ni mchezo
weka mbali mawazo
mahaba yangu tulizo

niite kwa jina langu
lafudhi weka ya pwani
zijue hisia zangu
faraja nipe chumbani

mwengine atoke wapi
kwako nimesharidhika
mitala wala sitaki
mapenzi sio shirika

mapenzi kama ni tenzi
nunua kabisa zeze
usiifanye ajizi
pokea huu utunze.
Na.
BIN ZONGO

MAJIBU YA BARUA YAKO MAKAYULA

''Nimeipata nafasi yakujibu salamu zako ulizoniandikia Makayula. sina shaka utaniambia mbeya wangu ninani"

Na
Bin Zongo

Mpaka kuandika waraka, najua umesalimika
Afya yako sina shaka, nilipo nina uhakika.
taharuki imenifika ,yanigubika mashaka.
ninani mbeya wangu, Makayula nieleze.

Urafiki nishakataa, wanafiki waja waleo
Mabingwa wakuhadaa, sikitaki icho cheo
Waraka nimeshangaa, usemayo yote siyo
ninani mbeya wangu, Makayula nieleze.

Nyumba yangu ipo sawa, amani iko pomoni
Fikira hasi ondowa, zibakishe tu moyoni
Sisikie yakuambiwa, mengine ni ya kubuni
Ninani mbeya wangu, makayula nieleze.

Mie ni yuleyule, watangu tungali shule
Haiba yangu upole, sijayaiga ya wale
Ndoto zangu zilezile, kesho nifikie kule,
Ninani mbeya wangu, Makayula nieleze.

Umechotwa na mtego,umevalishwa hasara
Wamekugeuza zigo, kukupa habari uchwara
Hebu liambae pigo, kwa kusimama imara
Ninani mbeya wangu, Makayula nieleze.

Shemejio ana raha, mie tunda la peponi
Kwake hakuna karaha, furaha yake moyoni,
Usemayo yakuzua, pinga usiyaamini,
Ninani mbeya wangu, makayula nieleze

Majivuno kwangu sumu, alinihusia mama
Tena kitu haramu, kwangu hayajatuwama,
Nimefundishwa nidhamu, vazi langu heshima.
Ninani Mbeya wangu, makayula nieleze.

Kama haya umezua, rafiki chunga ulimi,
Nafsi yangu yaugua, tabia hizi simimi,
Ninani alokwambia, ni ruhusa kujihami,
Namtaka mnafiki wangu, makayula nieleze.

Uchawi ndio kitu gani, dhahania sizijui
Mie kwetu muumini, shiriki sizitambui,
Kwanza mgeni Handeni, Muheza najidai
Ninani Mbeya wangu, makayula nieleze.

Haya maji marefu, kuoga yataka mbavu.
Tena uwe mrefu, kichwani usiwe mkavu,
Kuepuka mapungufu, ujihami nazo nyavu.
Ninani mbeya wangu makayula nieleze.

Mwenzako mie mgema, leo umeiba muda,
Umenitaka kusema, pombe yote mdabwada
Hasara imesimama, ila sawa hamna shida,
Nimtakaye mbeya wangu, makayula nieleze
Na.
BIN ZONGO

SALAAM BIN ZONGO

''Katika kuenzi tenzi na ushairi, moja ya vijana wa leo ambao nawaheshimu sana katika utenzi ndugu yangu Fulgency Makayula, ameamua kuogelea katika bahari ya ushairi kwa kuonesha uwezo wake wa tenzi kwa kuandika ushairi huu ndani yake wenye dhima ya barua inifike....sina shaka haina uhalisia wowote na kweli bali ni katika kuonesha ushababi wake katika tenzi....HAKIKA NAKIRI AMENIPA CHANGAMOTO KATIKA KUJIBU UTENZI HUU''



Kwa kheri zake karima, natumai u buheri
Na mimi wa afya njema, tena nina mpya ari
Nimesharudi salama, kwa ile ndefu safari
Salaamu bin Zongo, nisalimie Handeni

Ni miaka mingi sasa, na sikukuandikia
Kama vile tuna visa, kumbe tu kufikiria
Urafiki namba tasa, mimi nawe hesabia
Salaamu bin Zongo, nisalimie Handeni

Isome barua hii, bin zongo usipuuze
Nitapata kufurahi, akisoma na Rupaze
Nitakuja nikiwahi, nikuletee na zeze
Salaamu bin Zongo, nisalimie Handeni

Rafiki yangu wa damu, umeponzeka na nini
Nimeyasikia magumu,yanipa upunguwani
Umekosa ubinadamu, tabia hiyo ya lini!
Salaamu bin Zongo, nisalimie Handeni

Nimesikia nyumba yako, haina amani tena
Kwa hizo kauli zako, watoto walia sana
Uko wapi utu wako, na inaniuma sana
Salaamu bin Zongo, nisalimie Handeni

Nakumbuka enzi zile, tulipokuwa shuleni
Ukarimu na upole, uliuvaa mwilini
Ziko wapi ndoto zile, kuwa bora maishani
Salaamu bin Zongo, nisalimie Handeni

Na hukusita kusema, utajenga nyumba bora
Familia salama, hekima nyingi fikara
Ulimuomba karima, akunyime ufukara
Salaamu bin Zongo, nisalimie Handeni

Naye kakupa nyumba, uzao kakujalia
Na sasa unajitamba, wana wanakulilia
Yanini kujigamba, huku walikusalia
Salaamu bin Zongo, nisalimie Handeni

Ongoka rafiki yangu, unaenda kupotea
Wanipatia machungu, nyumbayo yateketea
Na humuogopi Mungu, nani atakutetea
Salaamu bin Zongo, nisalimie Handeni

Umekuwa mnafiki,tena usiye na soni
Mbele ya halaiki,unalopoka mdomoni
Eti mwanao Maliki, mchawi wa handeni
Salaamu bin Zongo, nisalimie Handeni

Kiti ulichokalia,wanne walishaketi
Kitanda unacholalia,ni chuma sio makuti
Na huyo mkeo pia, kaliwazika kwa noti
Salaamu bin Zongo, nisalimie Handeni

Mimi ni rafiki yako, ukweli nina kwambia
Kwa hizo ziara zako, utakuja kujutia
Ulizaga na wenzako, yajue walopitia
Salaamu bin Zongo, nisalimie Handeni

Ni kweli nyumba ni yako, hakuna kuingilia
Familia pia yako, yanini kututambia
Hilo ni limbuko lako, kupata sichopangia
Salaamu bin Zongo, nisalimie Handeni

Yapunguze majivuno, kwa kauli za kibabe
Embu iga na mifano, hekima nzuri zibebe
Ipunguze minong’ono, na uhuru usizibe
Salaamu bin Zongo, nisalimie Handeni

Bin zongo kwaheri, leo hapa naishia
Ni vema kutafakari, usije kupuuzia
Naenda kwa maakuri, msalimu Faudhia
Salaamu bin Zongo, nisalimie Handeni
Na
 Fulgence Makayula

DUBWASHA

Na.
Bin Zongo

atokapo ni gizani
meusi mavazi yake
usoni haonekani
kuua ndo kazi yake
ameagizwa na nani
siri kubwa jibu lake
wamfatao hatiani
mateso ndio hila yake

wengi sasa kitanzini
wachini hata wajuu
wengine wa kaburini
kwakuyataka makuu
hali tete duniani
roho zote juu juu
mwenyeji wake ni nani
hiyo ndio siri kuu

awahadaa vijana
nguvu kazi ya taifa
nusura yake hakuna
watu wengi washakufa
wazee pia vijana
kawamaliza kwa sifa
yaleo sio ya jana
hali sasa inatisha

sumu yake ladha tamu
ukiionja wanogewa
inachanganyika damu
hutaacha kurudia
kila mara una hamu
kuipata na kubwia
mgeni mwanaharamu
vijana wateketea

sababu zao dhaifu
eti hali ngumu chanzo
afya zao kama gofu
hawalioni tatizo
wanakaribia ufu
lakini sio kikwazo
matumizi maradufu
kuyaondoa mawazo

dubwasha jingi la hila
lateketeza kizazi
ukithubutu kulila
kuliacha tena huwezi
lina nyingi sana hila
vazi lake ubazazi
maombi kwako mola
muondoshe mpuuzi

afrika mpaka ulaya
kapenyeza mauaji
usoni hanayo haya
kuua ndo lake taji
si mzuri ni mbaya
yeye jumba la jinai
kijana pinga hizaya
izo dawa sio chai

muuzaji kwani nani
adui duniani hapa
nguvukazi hatiani
anauleta uhaba
mateja wengi mtaani
kazi yao nikukaba
pingu amfunge nani
kibosile muuza unga.

tupige goti tusali
tamati imeshafika
dunia sasa hatari
uozo kote wanuka
dubwasha kama jabali
limegoma kusagika
vijana mjihadhari
utu wenu waondoka.

wasanii nao kundini
wameuvaa mkenge
afya zao zitaabuni
akili zina mawenge
hawatupi burudani
mavazi yao mabwende
maji sasa yashingoni
mgeni fanya uende

Na.
Bin zongo

Twasubiri BIN ZONGO

Lile eneo la Dhania, eneo la kufikirika, eneo tata lenye mashaka na nyingi Hadithi, eneo lakusadikika ndilo nalizungumzia hapa.

Eneo ambalo mababu na watu wote wakale mpaka wa leo wanalitambua kwa jina moja tu 'MBINGUNI'
eneo hili ndilo limesheheni katika simulizi hii muktasi yenye kusisimua na kukujulisha thamani ya simulizi zangu adhimu ambazo daima dumu ZINAISHI na nafarijika kila uchwao lugha adhimu yakiswahili ikiendelea kunithibitishia uhai wa MILELE WA SIMULIZI HIZI hakika naamini uhai wa simulizi hizi ni DAWAMU hazitakufa abadani.

Na. Omar Zongo

katika anga la mbingu lenye mapambo ya rangi nzuuri yenye kuvutia inayotambulika kama buluu kulionekana vivuli vya mawingu meupe yasiyo na umbile maalumu! mawingu yale yalivinjari kwa mbwembwe yakionekaba kujongea kutoka sehemu moja kwenda nyengine.

Binaadamu yeyote makini ambaye ameruhusu macho yake yakatuwama angani kwa muda huu sina shaka ataona purukushani za mawingu kujongea kwa maringo, sina uhakika kama kinachoonekana ni zao lakuzunguka kwa dunia ama ni kuzunguka kwa mawingu, bila shaka wataalamu wa anga wenyewe wanayajua haya kwa undani.

kwa nje ya anga hilo haya ndio pengine unaweza kuambulia kuyaona lakini kwa ndani ya anga ni Majonzi makuu!!.

Malaika wa mbinguni wanaonekana wamekaa kimafungu, taswira ya kila malaika mmoja ni simanzi kuu iliyowagubika nakuwafanya wengine hata sura zao zinyimwe kabisa nuru ya amani.

Malaika wote mbinguni walitia huruma hakuna hata aliye thubutu kuzungumza kitu chochote sababu ya huzuni iliyowavaa nakuwagubika kote maungoni mwao.

ule utenzi wao waupendao uitwao NIPENI JINA hata hawauimbi tena kwa furaha, utenzi ule adhimu ulioandikwa na Mtunzi wa simulizi na Mashairi maarufu kwao kama BIN ZONGO waliupenda sana na mara zote waliuimba asubuhi na jioni.
walikuwa wakiuimba kwa furaha nakupokezana beti lakini sasa hali ilikuwa ni tofauti.
walipigwa na radi la upweke nakuwadhoofisha vibaya kutokana na miili yao kunywea kwa homa kali la simanzi.

katika utenzi wa NIPENI JINA kuna beti muktasi walizokuwa wakizipenda sana nakuvutiwa nazo.

ubeti wakwanza:

langu jina Omari
kwa uandishi hodari
kama cheo jemederi
waungwana nipeni jina


ubeti wa tisa ulisema hivii.

vyandani siri yangu
hizi ni falagha zangu
watakani mlimwengu
*jamani nipeni jina*

basi walikuwa wakivutiwa sana na shairi hili ambalo walilitumia pia katika shughuli zao za kila siku waliimba huku wakichapa kazi.

ni wao ndio walipigwa na huzuni kwa wiki mbili mfululizo baada yakuona kimya kingi bila ya Bin Zongo kutuma simulizi mpya wala shairi.

ni wao ndio ambao walikuwa washabiki namba moja wa JUKWAA LA SIMULIZI ZINAISHI.

walivutiwa na makala fupi zilizo na mvuto na ni wao pia walikuwa wakipendelea ushairi aziz uliokuwa ukiwekwa kule.
walibaki na huzuni kuu iliyotokana nakukosa simulizi mpya kwa kitambo.

walijitahidi kujifariji na utenzi wao waliouandika wao wenyewe kama njia yakujifariji, waliuita SUBIRA ushairi wao.

waliuimba hivii....

subira jambo bora
tena inafaa sana
aso nayo hasara
Twasubiri Bin Zongo

subira imeelezwa
kwa undani vitabuni
tena ikasisitizwa
twasubiri Bin Zongo

Subira uvumilivu
zao lake ni mbivu
subira bila uvivu
twasubiri bin zongo

huzuni latuandama
kutokana na ukimya
simulizi hujatuma
twasubiri bin zongo.

hizo ni baadhi tu ya beti za shairi lao.

malaika walipokezana kuimba beti za utenzi huo huku wakisisitiza kusubiri bila kuchoka.

Tanzia iliyotokana na kukosekana kwa simulizi mpya mbinguni inanifanya niione thamani yangu nakulikosoa shairi langu la DUNIA YAPENDELEA.

Ubeti wa tano wanena.

Vizuri havifanani
nami mwanafukara
dunia haivioni
vile vya kwangu bora
haina ulinganifu
Dunia yapendelea.

funzo ni moja tu katika mengi yanayopatikana ndani ya simulizi hii.

usikate tamaa na chochote unachoamini kipo ndani yako maana ukikitoa mbele ya kadamnasi kisha wakakipuuza sababu ya hila zao za kibinaadamu amini au usiamini MIITI, MILIMA NA MABONDE WAKIWEMO MALAIKA WATAKUTUKUZA NAKUKUENZI DAIMA.

WATAKUSIFU NAKULIWEKA JINA LAKO KWENYE KITABU CHA HESHIMA MAANA THAMANI YA ULICHO NACHO INAWAFANYA WAFARIJIKE NAKUONGEZA SIKU ZAO ZAKUISHI.

Mungu akutie nguvu usipigwe na Gharika la KUKATA TAMAA.

SIMULIZI ZINAISHI.