SHEMEJI WA.COM


'Shairi lifuatalo ni utenzi wakubuni haujaakisi tukio wala kisa chakweli kutoka kwenye jamii, utenzi huu unaakisi hali ya maisha yalivyo kwa sasa na undugu usivyo na thamani katika mapenzi'

Na.
BIN ZONGO


alinifata chumbani
muda natoka kuoga
akanivaa mauongoni
ukanitawala woga
nguo kazitupa chini
shemeji wa dot.com

kaka yako hayupo
kasafiri kitambo
shemeji jilie vyako
usizilete Tambo
nina haja mwenzako
shemeji wa dot.com

ndani mimi nawewe
wengine hawatajua
shemeji haki nipewe
nateseka wajua
nataka nishughulikiwe
shemeji wa dot.com

butwaa lanipumbaza
naota ama nikweli
kichwani najiumiza
niache au nikubali
shetani kampumbaza
shemeji wa dot.com

umbo lake namba
mtupu maungo yake
kaidondosha khanga
aibana sauti yake
dhamira kaipanga
shemeji wa dot.com

hatunazo tena nguo
nikama tumezaliwa
ni lipi langu chaguo
shemeji asisitizia
nasita kusema sio
shetani kasimamia

shemeji wa dot.com
anivuta kitandani
naanza kujilaumu
kuna mtu mlangoni
yanisisimka damu
wanivaa uhayawani.

tamaa yanikimbia
hodi sasa naisikia
nikaka anigongea
niwapi ametokea
tamaa yaniponzea
shemeji wa dot.com

nafsi lawamani
kaka namwambia nini
mkewe chumbani
kwangu kafata nini
udugu hatiani
shemeji wa dot.com

ka..ka kaaa...karibu
sio kwa kusita huku
mwenzenu yamenisibu
hisia kama chiriku
ifuatayo ni aibu
shemeji wa dot.com

mlango haujafungwa
kaka chumbani aingia
fumanizi limetunga
usaha umepasuliwa
nawezaje kupinga
kaka anachojionea

shemeji wa dot.com
ajabu anikimbia
mikononi nina damu
ya usaliti yanukia
moyo wa mwanadamu
una siri kupindukia

mtoto wa mama
mdogo wangu faraja
siamini nachokiona
nastaajabu kioja
kaka yangu asema
aibu lanikaba

sina hukumu yako
rejea tu nyumbani
kwa hii tabia yako
huwezi kuishi nami
ikusute nafsi yako
shemeji wa dot.com

zote juu porojo
wala hazisisimui
utenzi huu mikogo
ukweli huujui
kaka kumbe muongo
kujifanya hajui

njama wamezipanga
yeye na mkewe ndani
majukumu kumshinda
kakosa afanye nini
usaliti kauunda
kuniweka hatiani

ukweli wote anao
mdada wao wakazi
kasikia njama zao
nafsini ikamuudhi
amesharudishwa kwao
kwakujifanya mjuzi.

shemeji wa dot.com
kaka wa dot.com
wamenirudisha dom
kupinga majukumu
mgeni kwao sumu
uko wapi ubinadamu??


SIMULIZI ZINAISHI!

JANA NILIKUOMBEA

'Yafutayo ni maneno yakubuni hayana uhalisia wa kweli, ni maneno kuhusu mapenzi na usaliti uliosheheni katika mahusiano ya kileo'

Na. Omar Zongo

Nimestaajabu sana kushtuka usiku saa tisa bila sababu ya mana eti mapenzi ndio kisa.

Hofu sauti za usiku na ndege wa ajabu ajabu, kelele za vyura na bundi zilishindana, kiza ndani ya chumba ilikuwa balaa sana.

isingekuwa kuniacha ungekuwa pembeni yangu nina uhakika ujasiri wa kiume ungeongezeka maradufu nisingeonesha kuogopa ningejikaza.

ningeigiza kukulinda nisingehitaji unidharau ningekuondoa woga ili unipandishe dau.

ni ule mgogoro wetu ndio umefanya niwe mpweke, niukumbatie mto wangu na huu ubaridi unipige.

sijui ni upendo wangu ndio ulifanya uniadhibu au ni ule upole wangu bado sijapata jibu.

mbona nilikupenda sana na heshima lukuki sikutaka uwe mpenzi bali mchumba wa heshima.
au ni ule upofu wangu ndio ulinifanya nisione, upofu wa mapenzi yangu ndio ukageuka pakashume, ukaugueza utu wangu kuwa kituko mbele za watu!

niwewe ndio chanzo nishtuke usiku huu.
usingizi kwangu kikwazo nakuwaza wewe tu.

ni hiki hiki kitanda ndio ulitumia kunisaliti na sio mara moja ni mara zaidi ya mbili, zote nilikusamehe sababu ya moyo wangu, licha ya kunitenda nilihitaji ubaki kwangu.

kisirani na kiburi vilizidi kisa pesa, uliniita masikini nastahili kuteseka, kisa wangu ufakiri upendo siwezi pata.
silaumu maamuzi yako kuniacha nastahili,
sikukidhi haja zako,
ni umasikini sio ubahili.
ulilinda hadhi yako nakshi urembo na uzuri.

ila ulipokwenda sipo jamaa ni laghai wa mapenzi
anacheza tu na warembo kukuoa kamwe hawezi.
hiyo ndio mbinu yake yakwanza anapowafata, mabinti wenye tamaa huingia miguu miwili.
hutumia kuwahadaa lengo lake ye ni mwili.
hujua kucheza nao yeye ni zaidi ya tapeli.

jana niliposhtuka dukuduku likanikaba.
huruma ikaniingia nimeota upo nae.
kukung'oa kwake siwezi ila dua ina uwezo!
umshtukie umkimbie kabla hujauvaa.
sio mzima huyo mgonjwa anasambaza bila huruma.
hakika jana mekuombea uendelee kuwa mzima.
ni mwanasiasa wamapenzi anajua kulaghai.
ni bingwa wa ahadi hewa hawezi kuzitimiza.
ana mke nyumbani kwake lkn hawalali wote.
ana watoto wakila rika wamama ni tofauti.
akikupata atakutupa kama wengine alowapata.
kama bado haujampa itunze hadhina yako.
ataiachia ufa uijutie nafsi yako
memuomba Mungu jalia akupe ukakamavu.
afanye upate jua tamaa ni kuti kavu.
ukiendelea kukalia utadondokea mbavu.

jana mekuombea nusura ikushukie.

me nilikupenda kweli japokuwa hukujua, nilishawahi kutapeli ili kukunywesha bia.

nikadanganya umesoma nje ili marafiki wakuheshimu! nikabadili mpaka dini sikutaka kuwa mkristo!
niliimba sana mapambio nikala pia kitimoto!
hata siyo nilisema ndio ulinifanya mdoli wako.
jana nilikuombea kweli isikuponze tamaa yako.
usiendelee kutumia mwili kuiandaa kesho yako.

katika maombi yangu yajana usiku sanane
nilieleza hisia zangu zakutaka turudiane
ila napenda afya yangu ukirudi tukapime.
isije hisia zangu zikafanya nami niumwe.
nikawaacha ndugu zangu mana kwetu ndio kidume.
namuomba sana mola wangu akulinde na vidume.
akutunze mpenzi wangu ukirudi tuoane.

Maombi niliyafanya kweli kabla sjashtuka ndotoni nanilipokuja shtuka nimelaani maombi hayo.
kamwe siwezi kukumbuka uovu ulonitenda eti niombe urudi kwangu hakika ndoto hii potevu.
natena bora nimeshtuka mana nimeota ujinga NASEMA NENDA MWANAKWENDA SAHAU VYOTE KUHUSU MIMI!

Mapenzi ni zaidi yaukifikiriacho!




TATIZO NAKAZA SANA

"Zongo nakubali sana uandishi wako ila tatizo unakaza sana" jamaa flani ananitext kwa inbox, naisoma text yake naitafakari najikuta nacheka mwenyewe sababu kutafakari kwangu kwenyewe nilikuwa nakaza sana kama vile nafikiria issue nguuumu! najikuta kicheko chakujicheka mwenyewe kinanikamata mwisho naishia kutabasamu badala yakucheka kabisa, najicheka huku najipiga kibao kidogo cha utani huku nikijiambia "zongo unakaza sana"

kama mbabu wa miaka mingi hahaa!

poah leo sikazi wala sitaki kabisa masuala ya kukaza mana hali yenyewe ya maisha kwa sasa imekaza automatically so namimi nikijifanya naandika kimkazo nitazidi kufanya mambo yawe magumu!

Nimesema leo sikazi naongea lugha yetu tunayoelewana vijana mtaani!

story yangu yaleo iko hivi,

jamaa angu, damu yangu, chafu yangu yani mwanangu kinomanoma zaidi nikisema jembe langu ndio utanielewa, jina sio lazima sana ila kitu cha msingi ni kajisehemu kadogo sana ka tabia yake ambako kanamfaya baadhi ya issue zimpite zikidhani kuwa siye kumbe ndiye.

jamaa sio mtu wakujikubali, mtu fulani ambaye anatamani sana angeumbwa kama fulani! mara zote akistorika nami hua namsikia akijishtukia "dah mwanangu jamaa ananifurahisha kinoma jinsi alivyo, siyo sisi wengine tumeumbwaje sijui!"
mie mwenye imani yangu hua namwambia unakufuru jamaa lakini ndio maumbile yake akishamaliza kusema leo nikimkemea kesho anarudia tena kwa mtindo mwengine "mshikaji anaongea vizuri kinoma, af body yake inakubali kila vazi" afanaleki!!!.... huyu jamaa kaumbwaje!? hua sometimes namaindi kimya kimya ila mwisho namaindi
mpk mwenyewe anajua, namchanaga, namwambia mwanagu unazogoa! kama vipi anza mapema kujikubali la sivyo nitakukataa,

mshikaji ni case study naamini wapo nyomi design ya jamaa! tunawasaidiaje sasa acha nikupe sasa kisanga kilichomkuta huyu mshikaji.

ukiachana nayeye kuna manzi mkali kinoma, me mpaka nikisema manzi mkali ujue ana vigezo vyote!
acha nisanue sifa zake kuanzia za nje.
ameumbwa flani ivi kibantu haswaa, umbo lake lina mchoro wa nane kabisa na wala haujajificha yani ukimuona tu paap unauona ule mchoro pale kati!
ana rangi flani ivi haijakolea weupe wala weusi nao haupo yani sjui kaumbwaje lakini yuko soft usoni af ana unywele mmoja ivi balaa sana!

nywele zake sijawahi kumuona hata siku moja akishawishika kuzibust naminywele mingine isiyojulikana wamiliki wake ni kina nani aidha wapo hai au wameshavuta!

yani ni binti flani hivii wakiafrika kweli, midomo yake ilipendelewa nyama nyingi mnaziita lips af ongea yake utatafsiri kama huyu binti hapendi kuongea! tabasamu lake hua linaonekana kwa nadra sana usoni lkn mara zote akitabasamu maua, majani, mbingu na ardhi vinafarijika nakutukuza kazi yake muumba.

haiba yake ya kike sio chakaramu, haongei sana ingekuwa wewe ungesema ni wife material....hahaa af wewe bhana sjui unamaanisha nini kusemaga hivyo! utanipanga baadae acha me niendelee kukusanua sifa za ndani za huyu msichana.

Ah sorry nimesahau kwanza sifa moja ya nje, kifuani kwake kuna mzigo flani wa wastani sana nina uhakika watoto wake hawatakuja kulalamika njaa wakakosa kushiba kwa kifua kile.

sasa tuhamie sifa zake zandani kwa ufupi tu kifua kile chenye mzigo wa wastani ndani yake kilizawadiwa moyo wa ujasiri pamoja na upendo wa hali ya juu!

kichwa chake ambacho nje kilijaaliwa unywele uliojaa ndani yake kiliwekewa ubongo wa busara, tafakuri na mara zote alikuwa ni mja wakutenda baada ya kutafakari! hakuwahi kukurupuka katika maamuzi tangu kuzaliwa kwake.

ndani yake alikuwa mwanamke mwenye kujua thamani ya uanamke hakuwahi kutamani uanaharakati wakupinga mwanamme ndani yandoa asiwe kiongozi wake! alikuwa ni mwenye msimamo kamwe hakuwahi kuingia kwenye mahusiano yakipumbavu yeye aliishi leo akiandaa mazingira ya kesho!

mpenzi wake wakwanza hakuachana nae bali walitenganishwa nakifo! jamaa alivuta nakumuacha mrembo wa afrika akiumia kwa takribani miaka sita!

wapili alipoingia nae kwenye mahusiano alidumu nae miezi miwili tu akamuacha yeye, aliniambia sababu ni kuwa jamaa hakuwa mwanaume wa shoka, alikuwa hana msimamo, dhaifu na alikuwa tegemezi, wauongo maana aliishi maisha ya wengine!

jemeni namuongelea sababu ni rafiki yangu balaa kama nitapata nafasi baadae nitakwambia nilikutana nae wapi.

chamsingi nikuwa huyu binti namjua sababu ananiambia vitu vyake vya siri na vya dhahiri.

namjua pia mwanaume anayeweza kukaa nae wakadumu, na huwezi kuaimini ni yule jamaa wangu niliyeanza kukutajia mwanzo, yule asiyejikubali!

mara kadhaa nimeshawakutanisha lakini jamaa hajiongezi bado anaishi maisha ya watu wengine hivyo anafanya huyu binti hashtuki hata kidogo na jamaa.

unajua ipo ivii, jamaa ni rafiki yako na kwangu hua hajikwezi, namjua akiwa real anakuaje na mara zote nikiwa nae anakuwa real lkn anapoteza ureal wake anapokuwa mbele za watu wengine!

ngoja nikupange sifa za jamaa akiwa yeye bila kuishi maisha ya wengine!

jamaa ni ukweli kwamba hajengi mvuto wa aina yoyote ule anapojitokeza mbele ya mwanamke yoyote yule, hana zile sifa ambazo masister du wanazihusudu!

jamaa yeye ameumbwa na weusi tii unakaribiana na mkaa! alinyimwa rangi masikini halafu zaidi akanyimwa na kimo! alikuwa mfupi, sina chakumuongelea zaidi kwa sifa zake hizo za nje twende nikutajie tunu alizojaaliwa ndani yake!

alikuwa na misimamo, jasiri na mwenye akili balaa! alijaaliwa upendo na nidhamu na alikuwa mwanaume pekee mwenye kujua thamani ya mwanamke duniani hapa!

huyo ndio rafiki yangu! mwandani na jembe langu! kilichokuwa kinamuua yeye ni kitu kimoja tu hakuwahi kujikubali duniani hapa tangu kuzaliwa kwake, aliishi maisha yakuwaiga wengine na kuna kipindi alidiriki hata kuanza kunywa maji meeengi ili kutafuta rangi nyeupe teh teh!

akiwa nami hua anazungumza yeye sauti yake yakijasiri, yenye kuongea akili tupu na mipango thabiti naitamani na wakati mwengine hata namuiga lakini siwezi, nakuja kuchoka zaidi akiwa mbele za wengine anaiga ucheshi usio na mpango, anabadili sauti, anapindisha midomo akizungumza
na ananichosha zaidi muda ambao anang'ata midomo yake kutafuta vibes teh teh!

masikini ya mungu jembe langu hiki tu ndio kinamfanya asimpate rafiki yangu mrembo wa afrika!

tatizo hajikubali haishi kama yeye anatamani kuwa kama fulani!

Leo sikazi jamaa!! nakupa somo rahisi na ulizingatie, tambua kuwa kuna thamani kubwa yakuishi maisha yako nakuwafanya wengine wakukubali ulivyo!

kuna kipindi unaweza hisi una mkosi unarogwa au sijui MUNGu hakupendi kumbe ni maujinga yako mwenyewe ndio yanakufanya watoto wazuri wapite mbali nawe sababu wanatafutq mwenye sifa zako hawamuoni duniani kumbe upo lakini unakazana kuishi maisha ya wengine.

"sikia jamaa, hao unaotamani kuwa wao wapo wengi sana duniani TUMEWACHOKA tuletee thamani ya uumbwaji mpya ili nayo ituvutie" BIN ZONGO

Jikubali, ishi wewe, mfanye mwengine atamani kuwa wewe, ulivyo wewe hakuna mwengine tena duniani kama wewe!

simamia unachowaza, usikipuuze maana hich ndicho kitachokuoa thamani ya uumbwaji wako, TAMBUA HATA MWENDAWAZIMU ANA NAFASI YAKE KATIKA DUNIA.

"tatizo ZONGO unakaza sana," teh teh
Nimeacha kukaza!

SHAIRI: SIKU ITAISHA

'Shairi lifuatalo linalenga kutoa faraja kwa masikini anayeendea kukata tamaa ya maisha mwenye kudhani kuwa hakuna namna ya yeye kushinda vikwazo vya maisha magumu ya kila siku, MUNGU YU PAMOJA KATIKA HARAKATI ZETU ZA SIKU ZOTE'


Na.
 Bin Zongo

1:
moja ndio saa
dakika kadhaa
naamka nakaa
tumboni nnanjaa
hii siku itaisha

2:
mawazo yajaa
kichwani balaa
dunia hadaa
nna dhiki na njaa
hii siku itaisha

3:
miale yaangaza
siku mpya yaanza
ntaishije nawaza
dhiki zanimaliza
hii siku itaisha

4:
nakiacha kitanda
sinapo pakwenda
naanza kupanga
vipi ntashinda
hii siku itaisha

5:
mtaani nadaiwa
luku ni zamu yangu
kooni nimekaliwa
yaniponza hali yangu
hii siku itaisha

6:
kuoga bila sabuni
sijui naoga nini
mikosi mwilini
sinayo amani
hii siku itaisha

7:
chumba cha uani
karibu na chooni
asubuhi foleni
kumejaa pomoni
hii siku itaisha

8:
toka basi uani
asemavyo jirani
mekawia chooni
usoni nina soni
Hii siku itaisha

9:
narejea chumbani
chakuvaa sioni
hodi mlangoni
najiuliza ni nani
hii siku itaisha

10:
taulo kiunoni
nafika mlangoni
kufungua ni jeni
nadaiwa jamani
hii siku itaisha

11:
 chai na maandazi
ulikula na maharage
kunilipa huwezi
mpaka tufatane
hii siku itaisha

12:
 anena bila kificho
jeni mwanahizaya
hajui kama sinacho
usoni naona haya
hii siku itaisha

13:
nitakupitishia
kuvaa namalizia
najitutumua
uongo kumwambia
hii siku itaisha

14:
hayo maneno yako
nimeshayazoea
hesabu pesa zako
chakwangu kunigawia
hii siku itaisha

15:
pesa niitoe wapi
wazo naliwazua
sura niiweke wapi
jeni kang'ang'ania
hii siku itaisha

16:
jeni naomba nielewe
nitakupitishia
na chai niwekewe
nakuja kununua
hii siku itaisha

17:
ole wako usije
utaniona mbaya
acha nikungoje
Jeni aniambia
hii siku itaisha

18:
kabla sijaufunga
mlango babuu aja
baba mwenye nyumba
siku hii majanga
naamini itaisha

19:
kijana habari yako
naitaka pesa yako
luku ni zamu yako
wanalalama wenzako
hii siku itaisha

20:
aah eeeh mzee
kigugumizi lukuki
hii hali aisee
furaha siikumbuki
hii siku itaisha

21:
sitaki porojo zako
usumbufu tabia yako
ikiisha kodi yako
ruhusa uende zako
hii siku itaisha

22:
unadaiwa na maji
tumeshaletewa kodi
hii leo jitahidi
pesa izo kukabidhi
hii siku itaisha

23:
nawaza nisiku mbaya
hapana mawazo hasi
mola atajaalia
itaniisha mikosi
hii siku itaisha

24:
narudi ndani kinyonge
simu yangu yaita
apigaye kaka bonge
anayeishi geita
hii siku itaisha

25:
dogo metuma pesa
tumia ikiisha sema
mgodi haujaniangusha
juzi na jana umetema
hii siku inaisha

26:
mgao wako pokea
namama nimemtumia
msiache kuniombea
maisha huku hatia
hii siku inaisha

27:
chakujibu nimekosa
zaidi ya asante kaka
simu yake yakatika
shauku pesa kuiona
hii siku inaisha

28:
kiasi kingi balaa
mtaji wa biashara
elimu haikunifaa
ni ngumu sana ajira
hii siku inaisha

29:
mipango yapangika
kweli pesa ndio dira
jeni nitamlipa
ni nzuri sana subira
hii siku inaisha

30:
baada ya madeni
wafaa mradi gani
mawazo kichwani
mechoka umasikini
hii siku inaisha

31:
Fahari meziacha
mechagua kuzalisha
pesa naizungusha
naamini itanilipa
hii siku inaisha

32:
wazo nakamilisha
nautaka uwakala
mapesa kuyahamisha
sitakosa hata kula
hii siku inaisha

33:
hatua moja yaanza
utaratibu kuufata
mpaka kutanda giza
jawabu nimeshapata
hii siku inaisha

34:

ntalipa miezi sita
kizimba cha biashara
biashara zote naweka
sitaitaka hasara
hii siku inaisha.

35:
nalala na amani tele
mwishowe naiona nuru
muache Mungu aamue
kufuru isije kudhuru
Nasasa Siku Imeisha.

SIMULIZI ZINAISHI

SURAYE NAIKUMBUKA : SHAIRI

'Utenzi ufuatao ni moja ya ishara yakukumbusha watu kuthamini kila mtu maana wahenaga hawakukosea waliposema SICHAGUI SIBAGU ATAKAYENIZIKA SIMJUI, aidha pia somo la kutomdhania mtu mabaya linagusiwa katika utenzi huu Adhimu'

Na, Bin Zongo

ndani ya daladala
kanilipia nauli
kauepusha msala
konda ni baradhuli
suraye naikumbuka
ila jina simjui

ilikuwa ni patashika
ingekuwaje sijui
sikuwa nakupashika
abiria siwajui
suraye naikumbuka
ila jina simjui

alikaa pembeni yangu
hata sikumsalimia
nilijua mambo yangu
wala sikumzingatia
suraye naikumbuka
ila jina simjui

konda adai chake
nauli azikusanya
natazama ili nimpe
hapo naanza kuhanya
suraye naikumbuka
ila jina simjui

natazama mfukoni
nauli yangu siioni
aibu aibu gani
nauongeza umakini
suraye naikumbuka
lakini jina simjui

damu yangu nakonda
zilishakataana
tangu naanza kupanda
tulikuwa twarumbana
naanzaje kumpanga
yakwamba nauli sina
suraye naikumbuka
ila jina simjui

oyah nipe nauli
konda asisitizia
aibu kuikabili
ndio kitu nawazia
suraye naikumbuka
ila jina simjui

abiria jirani yangu
kituo chake kafika
ajabu alipa yangu
nauli kisha ashuka
suraye naikumbuka
ila jina simjui

tayari nimeshalipa
dirishani aniambia
gari laanza kuondoka
asante sijamwambia
suraye naikumbuka
ila jina simjui

fikira zaenda mbali
yule binti ninani
msaada wake johari
kunipa ameona nini
suraye naikumbuka
ila jina simjui

nawaza labda nimwizi
nauli yangu kaiba
zambi zinipiga mbizi
imani yangu ni haba
suraye naikumbuka
ila jina simjui

safari yatamatika
najiandaa kushuka
nauli nayo yaanguka
kitini nilipokaa

kumbe mapepe yangu
nauli ilikuwepo
najutia nafsi yangu
mawazo yalonijaa.

CHANDA CHA PETE


Nina jivika upofu, kwa navyo shindwa tazama
Kwa mawazo yangu nyofu, fikara sizo chutama
Hakuna cha upotofu,  jicho pevu kutazama
Azima ya moyo wangu, chanda cha pete fikiri

Chanda nilikuchagua, moyo wangu kutiisha
Tena nilikubagua, kwa misingi ya maisha
Kama jua limetua, joto umelikatisha
Azima ya moyo wangu, chanda cha pete fikiri

Wewe ndiye  wapekee, kwa ndugu zako watano
Ukipenda nikemee, ntajifunza kwa mifano
Sikupenda ulegee, tena niliuma meno
Azima ya moyo wangu, chanda cha pete fikiri

Chanda changu kitulivu, usie penda mapuro
Najua u msikivu, na usiyetaka kero
Yakatae machakavu, yamenipaka uchuro
Azima ya moyo wangu, chanda cha pete fikiri

Ni wapi nilikosea, hata nashindwa kung’amua
Kule niliko potea, ni vipi nitagundua
Mbona nilikupepea, kwa huba njema za dua
Azima ya moyo wangu, chanda cha pete fikiri

Mimi nilifunga nia, kwa penzi loshikamana
Nilifurahi kuingia, kwa pendo la kujichana
Siri sikujifichia, nilikuweka bayana
Azima ya moyo wangu, chanda cha pete fikiri

Ndugu niliwaambia, na bibi akaafiki
Ndugu wakanihusia, ni wachunge wanafiki
Tuiogope Dunia, isije kutupa chuki
Azima ya moyo wangu, chanda cha pete fikiri

Chanda usinichukie, husuda kuchukiana
Juto lisikuingie, moyoni likajazana
Msamaha nipe mie, tupate kuelewana
Azima ya moyo wangu, chanda cha pete fikiri

Nilikuvika dhahabu, nikakupa alimasi
Ni ipi kubwa sababu, inanipaka kamasi
Nalijitia  ububu, kukupatia wepesi
Azima ya moyo wangu, chanda cha pete fikiri

Ulizichukia gubu, nakumbuka ulisema
Ulijawa na  gadhabu, hata juu ukahema
Ila yote nilitubu, hali ikawa salama
Azima ya moyo wangu, chanda cha pete fikiri
 

MIMI NI BORA

Mimi ni mimi, wewe ni wewe, mimi ni jasiri, mbunifu, mtulivu, nina akili nzuri, mkweli, naheshimika hakika MIMI NI BORA!

Naishi maisha yangu, sina tatizo,nina furaha, najipenda, hakuna kama mimi, MIMI NI BORA ZAIDI.

Napenda ninavyoishi, sina mawazo, nina furaha naweza kukupokea ukinihitaji nakukupuuza ukinitenga, yaani ilivyo ni kwamba wewe ni nafsi yako nami ni nafsi yangu,
wewe hauna nafasi katika himaya ya amani na furaha ya MOYO WANGU!

kama wewe una thamani hiyo ni ya kwako wewe na wanaoamini una thamani, mimi hainihusu!, naiona thamani yangu pekee, thamani yenye ubora usiolingana na yoyote.

mimi nimebarikiwa, hakika mimi ndio mimi, kama mimi atoke wapi!?

mimi sio masikini, umasikini haufanani na mimi, mimi ni mtu mzuri, uzuri wangu duniani mfanowe hakuna.

mimi siijui shida maana shida hua naipuuza, naiweka kushoto natinga koti la ujasiri, napiga hatua za kujiamini naisogelea juisi ya bariidi iitwayo furaha nainywa kupoza koo langu.

mimi sura yangu inapambwa na tabasamu, maana tabasamu ndio adui wa uzee!,

mimi sijali kuhusu wewe, mimi najijali mimi, najipenda mimi sababu mimi nina mawazo mazuri, ni mbunifu, nina kipaji naamini katika utendaji wangu yaani mimi ni bonge la tajiri.

kama wasichana wabaya wapo mimi sio saizi yangu, mimi napenda mrembo, sura nzuri, mwenye mvuto, akili na anayejielewa.

siendani na mcharuko,kituko, roporopo,kilaza, malaya,mzandiki,mfitini,Mchonganishi,mchawi na mchafu, sijawahi na kama nimewahi kuwajua watu hao basi natema mate chini ptuu kamwe isije kujirudia.

mimi ni wa kazi nzuri, nyumba nzuri, gari kali, familia bora, vyakula bora, maisha mazuri No maradhi! No Mawazo yanayoumiza No Tabutabu yaani kwa ufupi mimi ni wa maisha flani hivi yasiyo na bugdha za ufukara.

mimi mchamungu, mimi mkarimu, mcheshi, mpambanaji,jasiri, mtetezi, nina roho nzuri mimi ni msaada mimi ni faraja mimi ndio chanzo cha furaha kwa wanaoijua thamani yangu.

Marafiki wazuri, wenye sifa kama zangu! waelewa,wenye busara, matajiri, wachapakazi, wabunifu, wenye roho safi, hawana wivu hawa ndio marafiki zangu watanashati, wanavutia, mawazo yao ni chanya hawajawahi kuota dhiki na wanauchukia umasikini! hawa ndio wenzangu mimi.

hee! wewe mbona unataja maneno mageni??? kukata tamaa ndio nini! hiyo ni laana ambayo siitaki iniingie mawazoni mwangu, kwangu hakuna msamiati CHANGAMOTO yoote mitihani ya maisha inayokuja mbele yangu naiita UZOEFU!

mimi niko tofauti nawewe mwenzio muda wote ni wafuraha, alikufa rafiki yangu kipenzi nikahisi kwa ajili ya upendo wake ametangulia peponi kuniandalia mazingira mazuri huku mimi nikisimamia ndoto zake alizoziacha duniani, sihuzuniki tena kwa kifo chake naamini ipo siku ntakutana nae tutaendeleza urafiki wetu.

niliwahi umwa nikachungulia kaburi! nilianza kuhesabu dakika kabla hatua za malaika mtoa roho kunifikia lakini wauguzi wangu hasa mpenzi wangu alikuwa akistaajabu nikitabasamu badala yakuogopa kifo, hakuwa anajua kuwa muda ule tayari nilikuwa nimeshajiandaa kwenda kukutana na rafiki yangu peponi, mama angu na baba, hakuwa anajua kabisa kuwa muda ule tayari nilishaawandalia watu hao simulizi lukuki za maisha y
alivyokuwa baada ya wao kuondoka.

hakuna chakunisimanzisha duniani hapa sababu nafsi yangu ni nafsi huru,inajipenda nakujithamini, hua kuna wakati nalia lakini huwezi kuamini sijawahi kulia kwa uchungu mara zote machozi yangu ni yafuraha tu.

mimi ni bora kuliko kitu chochote nasijawahi kutamani kuwa yoyote naishi kwa msaada wa akili yangu na jinsi inavyoniagiza niheshimu nisiogope hakika mimi ni bora.

Kuna faida yakuiona thamani yako, kuipinga sauti inayokudhoofisha kuwa umeumbwa vibaya, wewe ni masikini au sijui una mapungufu gani! anza sasa kuiongolea nafsi yako kuwa ni bora kama ulivyoiongelea hapo juu.

mawazo yako yanaakisi matendo yako hakikisha mawazo yako ni chanya muda wote, utajikuta una furaha pia muda wote
MIMI NI BORA
WEWE NI BORA
YULE NI BORA
Hakika kila mmoja anayo thamani yake katika dunia hii.

TUMAINI LIPO

Kila siku mpya napata tumaini jipya hasa ninapouchunguza mwili wangu nakubaini hauna hitilafu yoyote ya maradhi, nashukuru nakuamka nikiwa na amani licha ya kwamba sina uhakika wakifungua kinywa, tumaini langu laniambia leo ndio siku ile ya mapinduzi ya maisha yangu.

siku ya kugeuza mawazo kuwa vitendo, siku ya ahadi kutekelezeka, siku ya nuru mpya katika kiza cha ufukara na maisha ya bahati nasibu.

naamka kwa miruzi, salamu zenye bashasha kwa majirani, utani wa hapa na pale pamoja na ucheshi unanifanya nionekane mwenye furaha nisiye na shida, mtu niliyeridhika na maisha, hakuna ajuae siri ya amani yangu!.

natembea kwenda kwenye mitego yangu, njiani nakutana na wengi waliokunja sura zao kana kwamba hawakufurahia kuamka kwao. natamani kuwaambia watabasamu hata kidogo lakini nashindwa nabaki kuwatazama mimi kwa tabasamu huku nikiwasalimia kwa furaha.

wananijibu kama mimi ndio chanzo cha matatizo yao lakini sijali, naendelea kutabasamu nikiamini kuwa ile ni siku mpya inayonihitaji tena nipambane kuleta mageuzi ya maisha yangu.

sijawahi kukata tamaa tangu nilipogundua kuwa kukata tamaa ni rafiki mnafiki anayekuelekeza kwenye njia yakushindwa pekee.

njaa inanikwangua tumboni lakini kwangu mimi naichukulia kama kengele inayonikumbusha wajibu wangu wakuhakikisha natafuta chakula cha kesho na keshokutwa na sio cha muda ule tu! kengele ile ya njaa inayolia tumboni kwangu inanikumbusha kuwa duniani wapo watakaonihitaji niwalishe wakiwa na njaa hivyo nihakikishe napambana kupinga watu hao wasije kuumizwa na njaa kama nilivyo mimi.

njaa yangu isiyopata shibe kutokana na ukata wangu ni ishara yakunionesha thamani ya kazi nakunijengea huruma siku moja nitakaposhiba nimuelewe mwenye njaa. naamini hii ndio tafsiri ya njaa yangu napata tumaini nazidi kukaza mwendo kuelekea mapambanoni.

nimimi pekee ndiye ninayejua kuwa sio kila anayecheka nakufurahi ameridhika kimaisha naamini kuwa wengi ni kama mimi wanaamini katika uzima wao na zawadi ya siku mpya waliyopewa.

hata wewe anza sasa kuiona thamani yako maana ni wewe ndio umeamka mzima wakati mamilioni ya viumbe hai duniani kote wamekufa usiku wa jana, kuna sababu gani yakutoiona thamani yako na sababu za wewe kuendelea kuishi!

ishi kikamilifu, igiza ukamilifu kuonesha udhaifu wako ni kupoteza tu muda wako hakuna atakayekusaidia katika hayo madhaifu zaidi watakucheka nakutumia fursa ya udhaifu wako kukudhoofisha zaidi.

Tumaini lipo katika kila siku mpya! hakikisha haukati tamaa, tafuta tumaini lako ukiwa na amani, usinune maana hakuna mtu sahihi wakumnunia sababu ya shida zako.

kila siki iitwayo leo amini tumaini lako lipo na upo mkono wa msada ambao hufanya kazi kwa siri kukusaidia ufikie malengo yako. Pambana usichoke!

IGIZA UKAMILIFU 2017

IGIZAUKAMILIFU 2017

kwanini uigize ukamilifu mwaka 2017?

sababu ni hizi........

Na.
Mr Experience

Udhaifu wako ni moja ya sifa zinazo kutambulisha kuwa wewe ni binaadamu lakini haimaanishi kuwa ndio uutangulize mbele nakuwa muumini wa makosa.

anza sasa kufikiri kuigiza ukamilifu katika kila jambo.
pengine hali ni ngumu umezongwa na majukumu! kipato hakiridhishi na umeandamwa na kila dhiki duniani hapa, acha nikwambie kuwa udhaifu nikusononeka nakuacha mawazo yakutafune taratiibu ndani yako.

unaonaje sasa ukianza maisha mapya kwa kuvaa vazi la ukamilifu, kujiveka tabasamu la kuridhika hata kama unateseka.

lengo nikuficha wengine wasijue dhiki zako, wasiyajue maisha yako, wasione kuwa dhiki inakuchapa nawe unachapika.

Igiza ukamilifu, weka tumaini mbele hakika nakuambia utakujia ukamilifu kwa kuuishi ndani yake.

ndio fukara lakini unatabasamu, huchoki kutafuta, unaamini katika pumzi na uzima wako na unaishi maisha yanayompendeza yoyote kwa kumjali kwa hali maana mali huna, hakuna kitakachozuia usiwe mkamilifu.

ni rahisi kumdhoofisha nakumkatisha tamaa adui yako endapo utamficha asiujue udhaifu wako.

muda ndio huu igiza ukamilifu mpaka mwaka huu mpya ukiisha utayaona matunda yake.

furaha ya watoto wako na tumaini lao lipo katika nguvu yako, tabasamu na ujasiri, kujidunisha na huzuni ya kukosa itasambaratisha kabisa vipawa vyao, matumaini yao nakujiona dhaifu wasio na thamani mbele ya dunia hii.

kwanini upoteze ndoto za watoto wako au watu wanaokutegemea kwakuonesha udhaifu mbele yao mfano kusononeka, kulia au kuhuzunika sababu ya changamoto za maisha?

ni muda wakubadilika, igiza umekamilika, wape moyo waambie kila kitu kipo sawa! huo ndio ujasiri na taadhima apewayo shujaa.

Igiza ukamilifu ndugu yangu mwajiriwa, kazini unaonewa haki zako huzioni, suluhisho halichukuliwi kwa kununa, kutukana au kuharibu kazi za watu!

tabasamu liwe utambulisho wako kila siku uingiapo kazini, ishi kwa uaminifu wape maswali wabaya wako wajiulize Huyu ni mtu wa aina gani??

amini kuwa malipo kwa mwenye imani hayachelewi hufika hapahapa duniani, amini daraja lako litakuwa kutokana na uaminifu wako, unyenyekevu nakuyaficha mapungufu yako kama binadamu, mapungufu yakugombana,kurumbana na kutukanana. Igiza ukamilifu, ona kama hakuna baya linalokughasi.

acha sasa kugombana na mwenza wako kwa kukataa asishike simu yako, ukamilifu wako utakufanya uone haja ya yeye kuwa nafuraha utasahihisha mapungufu yako na utakuwa huru bila woga wakufumaniwa wala kugundulika maovu yako.

hii ndio mbinu anza sasa mapema kuifanyia kazi
IGIZA UKAMILIFU 2017
#Actperfect2017