NAKUSHIKA SIKIO

Aliposikia hatua za mtu akaongeza umakini nakusogea karibu, ghafla akashtuka paji la uso wake likitobolewa na vyuma vya moto, alikuja kugundua baadae kuwa ni risasi ndio zilipenya kichwani mwake, mwili wake ulianguka chini mithili ya mzigo...

ni hapa ndipo alipongundua SIKIO LAKE LIMEMPONZA kusikiliza hatua za watu hatari na wakatili kiasi kile....alijilaumu kwanini asingepuuza kusikia hatua zile lakini majuto yake hayakuweza kusaidia roho yake isitoke...sasa alikuwa chini akipigania roho yake ambapo dalili zote za kifo tayari aliziona...

SIKIO LILIPONZA ROHO YAKE! nina kila sababu ya kuzungumza na SIKIO LANGU!.
Nakushika sikio!

Na
Omar Zongo

Sikio langu ni dira nzuri ya kuupima muelekeo wa ngurumo za sauti zitokazo pande zote za dunia hii.

leo nasema nawe sikio maana namini wewe ndio kiungo pekee ambacho utanifanya ule umimi niliozaliwa nao, nisiupe nafasi kuwa kero kwa wengine.

usikasirishwe na mabezo ya watani wangu wanaodai nina sikio kubwa ka' upawa wa uji,naomba uyapuuze masikhara yao na utambue kuwa ni mie pekee ndiye unapaswa kusikiliza rai zangu na Thamani ninayokupa.

Sikio langu tafadhali sana nakusihi usije tamani hata siku moja kusikia uliyofumbwa kuyasikia.

leo nakushika sikio unielewe maana yangu na uitambue kuwa sio mbaya bali nikukuepusha wewe na maradhi ya umbea usiokuhusu.

unayopaswa kuyasikia naomba sana uyasikie kwa utashi na uyazingatie, yale yaso na maana kwako yafanye yatoke kwenye sikio la upande wa pili yaburuzwe na upepo kuelekea uendapo.

hivi unadhani ni kwanini duniani wapo watu wanaoitwa hawajiamini? kama ungekuwa una ubavu wakunijibu ningefurahia sana jibu lako lakini kwa vile kazi yako nikusikia na sio kuzungumza acha nikupe sababu za watu kuonekana hawajiamini.

sababu kubwa ni kutokuongea nawe sikio nakukutahadharisha kuhusu kusikia maisha ya wengine nakuruhusu maisha hayo yawavutie nawatamani kuishi kama wao.

kusikia kwako kunaweza kujenga lakini pia kunabomoa wakati mwengine, tafadhali sikio chunga sana na hayo uyasikiayo.

ndoa nyingi duniani zavunjika kutokana na kazi yako yakusikia maneno ya wafitini wasopenda mahusiano ya watu, unaonaje kuanzia leo ukaanza kuwa mpembuaji wa ukweli na umbea au kama huwezi kazi hiyo walau basi uwe na uvumilivu maana sio kila ulisikialo linapaswa kuchukuliwa hatua.

Sikio langu wahuba natambua kuwa niwewe ndio huufanya mdomo utabasamu usikiapo jambo zuri lakini niwewe pia ndio hulidondosha chozi jicho usikiapo jambo baya.

Ni juzi tu sikio langu ulinijengea uhasama na ndugu zangu baada ya wewe kuwasikia wakimsakama mke wangu nakuweka mbinu zakunigombanisha nae.

basi ungejifanya hujasikia nakuipa akili chakufanya lakini niwewe ndio uliuagiza ulimi uteme cheche zilizozaa moto ulioteketeza udugu wetu.

sikio langu wewe ni wewe ndiye ambaye fununu ikikujia hutanuka kuisikia, hupenda vyamotomoto vilivyopoa huvitiwi navyo.

nakushika hii leo uache kupenda ubuyu, madhila ya masuto fedhaha itakuwa yangu.
 tatizo lako ukisikia jambo kutulia nalo huwezi huushawishi ulimi utamke bila haya.

nakushika sikio langu asisikie ya umbea.
kwasasa maisha magumu wachawi nao ni wengi, huja kwako kunong'ona ili nikate tamaa nakusisitiza sana sikio usiwasikie.

maneno yakunidhoofu usiyapenyeze kwako tambua mie nidhaifu nitashindwa kustahimili, na hata yalo na sifa usiyapendelee sana mwisho hudhoofisha ufahari hauna maana.

sikio nakuhusia mie kwako ndio kiti juu yangu umenikalia usifanye tashtiti yawatu ukiyasikia jihimu kuyapuuza.

hivi sikio kwanini huna mashine yakuchuja, umbea na ukweli ungeweza kuuchekecha ningejifaghiri sana waongo kuwaumbua.

sikio sikia yao,
nakisha yapotezee
hauna faida nayo
muda wako usipotee,
kuyawazia ya kwao
ni kuuita uzee,

sio wote wakuombao
 umakini wako ni watu
wengine ni mafarao
wanajiona miungu watu
usiwafatize wao
ukauza wako utu,
nakuusia sikio
zingatia nisemayo.

tanua tundu zako
 kusikiliza adhana,
yadunia yana kutu
usiyafatize sana
yametawaliwa husda,
umbea na ufitina.

sikio tena sikia hili nimuhimu sana, uzima uliopewa usiuchezee rafu,
mwenzio najivunia kiungo wewe muhimu mana wapo walopewa uziwi na upofu.

sikiliza kwa kadiri,
mengi hukinaisha,
naukiombwa usubiri
uache kulazimisha
sikia usitafsiri
mengine utajichosha.
ikibidi  ghairi
wengine wanapotosha.

Jicho lilinisikia nilipotaka livumilie
nawewe nakuambia hadaa uiambae
moyo umeshatulia tangu nilipounanga
bado ulimi wangu kesho nitaupanga

Sikio natamalai naenda kuweka nukta
usiipuze rai ukanifanya kujuta.
utaileta  jinai usipokuwa makini.
kwa kila usikialo kulihifadhi moyoni.

Na
Bin Zongo

RUDI KAMA IKITOKEA, MAMA....!

"ISHI UKITAMBUA KUWA WAJA WALIKUJA WAKAWA NA KISHA WAKATOWEKA! NA HIVYO NDIVYO ITAKAVYOKUWA KWAKO NA KWANGU! TUTAACHA HISTORIA. HAKIKISHA INAKUWA HISTORIA YAKUIGWA" 
Na. 
Bin Zongo
Kama ikitokea nafasi iliyo ngumu kutokea kama yalivyo mapigo ya moyo kwa mfu,itumie!
usiikatae hata kidogo, hakikisha nafasi hiyo inakuwa ya kwako, imiliki na urudi tena maana ule upenyo uliouacha mithili ya pengo bado hauna namna yoyote yakuzibika.
sijui utofauti uliopo kati ya hapa ulipokuwa na huko ulipo sasa, lakini naamini wewe ni shahidi wa kitu kilichopo hapa kiitwacho 'bahati' kama ikitokea kitu hiki ama kinachofanana na hiki kinakudondokea kamwe usisite kukiokota.
naomba sana ukiokote kwa juhudi huku ukitambua kuwa tendo hilo ni msaada mkubwa kwangu yaani mithili ya ngumi nzito itakayomdondosha chini adui huyu aliyenizonga mwenye jina la Upweke.
nidhihirishie upendo wako! upendo ule ambao mpaka leo sijapata mfanowe, naomba unidhihirishie kwa kutumia nafasi hiyo itakayokupa abra yakurejea tena.
tendo lako lakurudi litazua taharuki, na litawasisimua wengi!! hapa sitaki kuficha hata mie nitastaajabu mno na pengine nitahisi nimezama katika tope la ndoto.
lakini naahidi kuwa sitadumu katika ulimwengu wa kustaajabu, nitarejewa na akili yangu nakutabasamu huku nikukufuata nakukumbatia kwa hisia.
sitakuwa na namna yoyote yakuzuia machozi yangu yasijenge mfereji katika mashamvu kabla yakutiririka kwa kasi kwenye mgongo wa ardhi, najua wengi watakutenga na pengine unaweza kujutia kabisa kuitumia nafasi hii ninayokuomba uitumie endapo ikijitokeza.
Naomba nitoe ahadi kwako, kamwe sitokutenga maana ni mimi ndiyo ninayekutana na adha ya ukiwa si mwengine! Nawezaje kukukimbia nakukuona wa ajabu wakati nimekuomba mwenyewe uitumie nafasi hiyo endapo ikijitokeza.
Ukipata nafasi hiyo rejea, mguu wako ukuelekeze kwangu! Hata kama ni usiku wa manane niite dirishani, nitakufungulia mlango, nitakukaribisha na nitakuelezea yote yaliyojiri katika maisha haya ya bila wewe.
Asubuhi ikifika nitawajulisha ndugu zangu ambao najua nao wanatamani sana ungekuwepo, nitamsikiliza kila mmoja amepokeaje taarifa hiyo yenye kuleta mashaka na kuondoa sifa ya ukawaida, kama atajitokeza mmoja akatamani tena kumbatio lako lenye kutia faraja nitamuelekeza ulipo. Laa kama wote wataniona mtu wa ajabu sana na hawatakubaliana na marejeo yako basi nitawatenga kama ambavyo watanitenga.
Ukipata nafasi rudi, naamini nitaacha vitu kama kuongea peke yangu nikiamini naongea nawewe, na kuhuzunika hasa nikikumbuka maneno yako ya mwisho kabla hujaniacha.
Ulisema unaondoka, tutakukumbuka na tutakulilia, ulisema unatupenda na tusijali hata huko uendako utatuombea! Mishale ya saa inakimbia sana ilijenga sekunde, dakika, saa, siku, wiki na sasa ni miaka kadhaa bila ya uwepo wako.
Kama ninavyotamani kula niwapo na njaa ndivyo niavyotamani urudi kipindi hiki ambacho nina dhiki ya faraja, muongozo na upendo.
Kutamani ni tendo ambalo halifanani kamwe nakuomba! Siombi hayo yote niliyoyasema yawe kweli ni matamanio tuu ambayo naomba yaendelee kubaki matamanio YASIYOWEZEKANA.
Maombi ninayoyataka yaitikiwe ‘amin’ ni wewe upumzike kwa pumziko lenye amani huko uliko mpaka pale namimi nitakapokamilisha lile andiko lisilopingika nakuweka historia ya aliwahi kuwepo.
Naamini ipo siku tutakutana na kukamilisha ya vitabuni ya kuwa yapo maisha baada ya kuishi.

"ISHI UKITAMBUA KUWA WAJA WALIKUJA WAKAWA NA KISHA WAKATOWEKA! NA HIVYO NDIVYO ITAKAVYOKUWA KWAKO NA KWANGU! TUTAACHA HISTORIA. HAKIKISHA INAKUWA HISTORIA YAKUIGWA"

IPO SIKU NITADONDOKA


"Safari ya kifo ni safari inayoumiza sana maana ina nguvu kubwa isiyoweza kupingwa na matakwa yako, ni mithili ya kuisha kwa mshumaa au kuzama kwa jua, ULAZIMA WA SAFARI HII NDIO UNASISIMUA NAKUSIMAMINZISHA MNO...lakini hakuna jinsi naomba niukubali ukweli IPO SIKU NITADONDOKA"

Na
Omar Zongo


Kamwe usije kusema utaniokota sababu safari hii ni ya kificho, hajulikani ni nani wa kuanza na nani wakumaliza.

sote tupo matayarishoni na huo ndio upekee wa safari hii, mimi nikidondoka ndio kipindi ambacho simulizi zangu zitasisimua zaidi kuliko hivi sasa na Pengine uthamani wake utaongezeka zaidi.
ipo siku ingawa siijui ni lini lakini naamini nitadondoka!

Wapo ambao watashtuka sana huku vichwa vyao vikirejea wasifu wangu na namna nilivyokutana nao nakufahamiana nao.

Nina uhakika siku hii itakua ni yakutaja mazuri yangu tu na hata walionichukia bila sababu za msingi watabaini kua sikuwahi kuwakosea mpaka wanichukie namna hiyo, hapa ndio watajua sikuwahi kuwa na makosa nao.

Siku nikidondoka wapo ambao watasadiki kua mpambanaji ameondoka.

Wapo wataokiri kwa vinywa vyao na wengine kwa mioyo yao tu.

Yaani sipati picha lakini nikidondoka kinywa changu hakitaweza kunyanyuka ishara kuwa hakuna la ziada nililo bakisha kulisema hapa duniani.

Kitu cha muhimu acha nikiseme kabisa kabla sijadondoka ewe mungu wangu nakuomba nisamehe dhambi zangu, nakiri kuwa mimi nimkosefu katika hili na lile nisamehe sana mana mimi ni kiumbe dhaifu kwako na ni wewe pekee ndio mwenye haki yakuabudiwa na kusujudiwa! Nisamehe leo nikiwa nimesimama na kesho nitakapodondoka! Msamaha pia upatikane kwa wote niliowahi kuwakwaza katika nyanja yoyote ile.

Najua nikidondoka macho yatafumba ishara yakutosheka na niliyoyaona duniani!
Hakika nitadondoka nafsi yangu ikiwa huru na yenye bashasha sababu hakuna ambaye atajigamba kuwa eti amenidondosha!

 nitadondoka kwa kudra zake allah, na nitadondoka huku dunia ikiamini kua mimi ni miongon mwa viumbe waliopangiwa kuongea maneno mengi ndio mana nikawa mwandishi.

Watu watakosea sana watakaposema pengo langu halitazibika katika sekta ya uandishi, watakosea sababu mimi nitakapodondoka amini usiamini pengo langu litaandaliwa wakuliziba kwa usiri na wala hakuna atakayejua hilo sababu inaweza kuchukua miaka mingi mpaka kujitokeza mtu huyo, wakuliziba pengo langu.

Hakika nitadondoka na mapigo ya moyo yatazima mithili ya mshumaa! Na mara kadhaa nitataka kujaribu kuwanyamazisha msinililie mimi bali mlilie nafsi zenu lakini ndio hivyo tena sitakuwa na nguvu hiyo tena.
Wengi duniani wataamini nimelala kimyaaa lakini ukweli utakuwa ni huu muda ule nitakuwa napiga soga na malaika wa kila namna wengine watakuwa wa adhabu ambao wengi wao watakuwa wamefura kwa hasira kutokana na makosa yangu niliyoyatenda duniani, watanihoji kwa dhihaka na kiburi. Maswali ya yako wapi yale majigambo yako uliyokuwa nayo duniani!?

Nitabaki kimya nikitahayari nakujutia zile sekunde zangu na dakika nilizotumia kutenda uovu duniani, nitalia nakusaga meno lakini ndio hivyo tena majuto ni mjukuu.

Baadae sana nitakuja kufarijiwa na malaika wapole wenye huruma ambao wao watakuja kwangu nakunipa mkono wakuume nakunipongeza kwa matendo yangu ya wema niliyowahi kuyafanya duniani.

Hakika ni hapa ndipo nitakaposadiki kuwa wema siku zote hauozi na nitajilaumu kweli kwanini duniani sikuwa mwenyekiti wa Chama cha watu wema.

Kitu nilicho na uzoefu nacho kupitia watu walio tangulia kudondoka ni kwamba taarifa zao zilisambaa haraka kwa ndugu na jamaa zao hakika hata taarifa zakudondoka kwangu zitasambaa nakuwafikia wengi wanao na wasio nijua na kila mmoja itamgusa kimtindo wake taarifa hiyo!

 Ingekua maamuz yangu ningesubiri hukumu ya dunia ifike nikiwa hai ili nishuhudie udhaifu wa wanaojiona ni miungu watu wanaotesa, kuua na kunyanyasa binadamu wenzao sababu ya uchu na tamaa ya matumbo yao!

nitadondoka siku na saa ambayo siijui ila nina uhakika nitakua nimetimiza alichonituma mungu wangu na kile nilichomuahidi mama angu siku ile aliyodondoka zakiem hospitali pale mbagala.

Nitajiandaa kwenda kukutana nae nakumpa taarifa ya yote aliyoyaacha duniani, baada ya kudondoka kwake. Hakika nitadondoka! Nalijua hili

na mengi yatabaki historia, sitakua na nijualo kuhusu niliyoyabakisha nyuma ila naamini wachunga mbuzi watanijuza kupitia soga zao! Pindi watakapokuja kuchunga mifugo yao maeneo ya porini ilipo nyumba yangu ya milele.

 nitadondoka nakusababisha bendera ya smulizi ipepee nusu mlingoti!

hakika kudondoka kwangu kutakua ni furaha kwa waliojali pesa kwa kutunga simulizi pendwa huku wakisahau jamii inapotoka kupitia simulizi zao kutokana na jumbe zao kuegemea upande wa starehe nakuacha kabisa elimu imuongozayo mtu.

Ukimya nitakaokuwa nao siku yakudondoka kwangu hautakuwa ukimya wa kiburi eti siwasikii ndugu, mke na watoto wakinililia ila ukimya huo utadhihirisha maridhio ya dhati kabisa yakuikubali safari hiyo chungu ambayo kwangu mimi itakuwa ni safari yakwenda kupumzika katika nyumba yangu ya milele.

Nina uhakika siku nikidondoka ujumbe huu ndio utakao somwa na kusikilizwa mara nyingi zaidi kwa wale watakaokuwa majasiri, nitawapongeza sababu ni ukweli kuwa hii ndio harusi ya tatu katika harusi tatu za mwanadamu, sijui tatizo nini mpaka harusi hii inaogopwa na watu wanalia badala yakucheza vigodoro kama wafanyavyo kwenye siku za kuzaliwa na siku ile ya ndoa.

Siku hii yakudondoka kwangu! Wapo watakaosema nilijitabiria jambo ambalo sio kweli hata kidogo kwa sababu niliiwaza hii siku tangu nikiwa bado kijana mdogo nilijua ipo siku ntadondoka na mpaka leo nimedondoka ni miaka mingi imepita tangu dhamira ya ujumbe huu kuumbwa.

Nitadondoka! Na wala sitataka kabisa kujua kinachoendelea duniani hapa sababu mengi nimeshajionea na mengi hayana faraja nafsini mwangu.

Huzuni nyingi zimenikumba kila niliposhuhudia dhulma, umimi pamoja naukatili uliokithiri nakusambaa  katika dunia hii.

Adha kadha wakadha lakini zaidi mateso makuu yanayowasibu watoto katika nchi nyingi afrika yakisababishwa na vita na mapigano katika nchi zao! Chanzo kikuu kikiwa ni uchu wa madaraka, udini na ukabila pamoja na tamaa ya maliasili zilizoumbwa kwa ajili yetu sote.

Hata ingetokea malaika wakunidondosha angenipa nafasi yakuniuliza kama nataka kuendelea kusimama ningemwambia laa...ni bora nidondoke walau nikaimbe tenzi na mzee wangu shaaban robert,  mwanagenzi mahiri aliyewahi kuishi tanzania hii na kisha akadondoka kama ilivyo ada.

Nitakutana na wengineo lakini kamwe sitakaa kupiga domo na wanasiasa maana watataka kuniulizia habari za wanasiasa wenzao duniani nami sitataka kuwaeleza sababu nilishaepuka kutoa maoni yangu kuhusu jambo hilo liitwalo siasa.

Maana sikuwahi kulielewa tangu nilipoanza kuufahamu utu wangu.

hakika nitadondoka nalijua hili na sijawahi kufanya juhudi zozote zakulipinga sababu ni sawa na kukataa kivuli changu!

nitadondoka na litaimbwa shairi hili!

chanzo nini
jibu fichoni
mwisho duniani
safari mbinguni
ipo siku nitadondoka

safari iso shaka
ipo siku itafika
wahuba nitamuacha
ndugu wote mashaka
ipo siku nitadondoka

mtume hakupinga
binZongo ninani
safari ishapangwa
twapita duniani
ipo siku nitadondoka

kuaga majaaliwa
nadra kutokea
safari ikiwadia
hakuna anayejua
ipo siku nitadondoka

Bendera ya Simulizi
pepea nusu mlingoti
duniani simanzi
safari haipingiki
ipo siku nitadondoka

siku hiyo kiburi
itafika kwakweli
utazimika mwili
duniani kwaheri
ipo siku nitadondoka

hakuna wa kujigamba
safari  kaipanga
mola mwenye kuumba
ndiye mwenye kupenda
ipo siku nitadondoka.

utenzi huu Tanzia
wengi wataupitia
watadai nilijua
kifo nikatabiria

ipo siku nitadondoka

Na.
Omar Zongo


MZEE BABA

Mzee baba

shikamoo mzee wangu, mzee baba!!

naheshimu sana uwepo wako ndani ya kaya hii ambayo ilipoteza kabisa heshima yake tangu kufariki kwa Baba angu mzazi.

kwa muda wote tangu pigo la kifo cha baba angu mama amekabiliwa na maadui wengi wakiongozwa na DHARAU, ambaye kila uchwao alikuwa akifanya kaya yetu ipuuzwe sababu ya UJANE wa mama.
 eti waliamini mwanamke pekee hana sababu yakuheshimiwa.

walikuja mababa wengi kila mmoja na namna yake aliyoitumia kumlaghai bimkubwa, wengi walikuwa hawasimamii uanaume wao ndani ya nyumba.

nimegundua mzee baba wewe unafanikiwa sana kwasababu ya ule mtindo wako wakujiuliza kila mara 'JE MIMI NI MWANAUME??'

wengi wanakusema vibaya eti mama anapata shida sababu wewe una chembechembe za mfumo dume lakini amini au usiamini mimi mtoto wa pekee wa kaya hii nakupa pongezi na wala sijaona kibaya unachofanya kwa mama angu mzazi ambaye mara zote mwenyewe anaongozwa na ile jaala yake ya upole na bashasha lake la amani usoni, amani iso kikomo.

Kaya yetu hii ilikuwa ni soko maarufu la wezi, walizoea kuiba bila hata hofu yakukemewa na kama ujuavyo mzee baba mama angu sio muongeaji kabisa na mie kijana wake ni dhalili, mnyonge sinalo hata jino moja lakuwang'ata wezi wa mali za mama angu.

najivunia wewe mzee wangu! mzee baba ambaye unanifanya nionekane mwenye hadhi sasa ingawa bado hujanihakikishia kusoma kwa kiwango kinachotakiwa
maana nikweli nasoma bureeee kabisa lakini elimu niipatayo shuleni ina changamoto na utofauti mkubwa na ile elimu wanayosoma watoto wa jirani yetu Baba Mariam.

halafu mzee baba hua mkinituma mahali wewe na mama hasa mishale ya jioni ROHO YANGU inakuwa REHANI.

kuna vijana wakihuni bila shaka watakuwa mateja wanatembea na nondo, viwembe na wakati mwengine hata mapanga, hutembea kwa makundi na wanajinasibu kwa majina ya ajabu ajabu na kazi yao kubwa nikupora watu. hua nawahofia sana na mara nyngine nashindwa hata namna yakufanya sababu ukiwaletea ubishi wanakutia upofu au kukudhulumu kabisa roho yako.

mzee baba naamini tamko lako moja tu kuhusu watu hawa waache kunijengea hofu mie mwanao na marafiki zangu litasaidia sana maana sauti yako iliyojaaliwa ukali na usisitizaji wa jambo inaonesha wazi UANAUME JASIRI ulinao.

nilitamani siku moja nione mfumo wa baba imara unakuaje, leo angalau nauona na najifunza sana vitu kutoka kwako.

mzee baba! naamini hata baba angu mzazi aliyetangulia mbele za haki anakuombea uendelee kumpigania mama angu mjane aliyebaki nasimanzi lakutendewa sivyo na wanaume waliompata baada ya kifo cha mzee na kabla yakumpata wewe.

"wewe reo kutwa nzima una kazi yakunisifia tu, mimi sitaki sifa nataka ufanye kazi! kafagie uwanja wa kaya yetu iri upendeze, sitaki maneno mengi mimi nataka kazi."

samahani kwa kukunukuu mzee baba naamini sijafanya makosa kurejea maneno yako ambayo unayasema mara kwa mara kwangu na kwandugu zangu wengine tunaoishi kwenye kaya hii.

MUNGU akubariki mzee baba naamini NIA yako kama niinavyo usoni mwako wakati ukiongea itasaidia sana kuzidi kumfanya MAMA awe mwanamke wa heshima DUNIANI hapa.

Mzee baba angu huwa hapendi maneno yeye anapenda kazi ACHENI NIKAFANYE KAZI.

SEHEMU YA 1&2

SEHEMU YA KWANZA


''Ni kawaida kwa hadithi nyingi pendwa kuwa na sehemu ya kwanza na sehemu ya pili na nyengine nyingi zenye mfululizo wa visa vya kusisimua, lakini ukweli wa mambo ni kuwa hali ni tofauti katika mapenzi, Hadith ya mapenzi inayonoga zaidi ni ile ya sehemu ya kwanza, ukiiharibu kwa kudhani kuwa utapata sehemu ya pili ni kosa kubwa sana ni sawa na ufa usioweza kurekebishika''

HII HADITH HAINA JINA INAITWA SEHEMU YA KWANZA NA SEHEMU YA PILI.....
NI KISA CHA MAPENZI .....

Na
 Bin Zongo
 
Mapenzi yamekolea hakuna aliyeona kero kwa mwenzie, kila mmoja anaishi kwa amani na hutabasamu kila wakati akikumbuka uwepo wa mwenzake.

marafiki zao walikuwa wanawaona machizi mana walipokuwa mbalimbali kila mmoja alikuwa busy na simu yake akichart na mwenzake nakucheka cheka kila saa kama chizi mpya aliyepelekwa kituoni kwa matibabu.

mapenzi yao yalikuwa yanavutia kama mapenzi ya kitabuni, yalifanya kila mmoja kati yao aone thamani yakuzaliwa kwake,

nafsi zao zilisonona kila zilipokumbuka kifo, hakuna aliyekuwa tayari kumuacha mwenzake maombi yao siku zote yalikuwa wafe wakiwa wote...ni nadra kutokea lakini walitamani sana kifo chao kitokee wakiwa wamekumbatiana!

mapenzi ya dhati yaliumbwa ndani ya mioyo yao! niseme nini mimi kudhihirisha namna walivyopendana!!!.

Raha ya mapenzi ya dhati ilidumu kwa muda mrefu kiasi hata ilipotokea mwanaume amebadilika tabia hakuna aliyeamini!.

lakini ukweli ulikuwa huo, jamaa alianza tabia ngeni kabisa.

alianza ubinafsi wakujiamulia mambo yake, alipanga ratiba zake bila kumuhusisha Bishosti.

tafakari wewe ni maumivu kiasi gani umpendae abadilike ghafla namna hii ilikuwa ni tanzia. hakuna aliyemudu kufuta chozi la bishosti.

kilio chake kilizidi kile cha msiba wa bibi yake mzaa mama ambaye walikuwa wakiitana shoga.

Bishosti alijuta kufahamu mapenzi ile taamu sasa iligeuka shubiri hakuna neno baya tena alilopata kulisikia duniani kama Mapenzi.

mtu aliyeyaita mapenzi ni Upuuzi aliona kama bado anayasifia yeye aliyafananisha na Jinamizi litembelo usiku kutafuta roho za wapendanao.

Bwanamkubwa alibadilika simu yake ilikuwa ni kawaida sasa kutumika hata usiku wa manane huku swali anaongea na nani akiwa halitaki kutoka kwa Bishosti.

kama ni maji yalimfika shingoni Bishosti taratibu akaamua kujifunza kuwa mbali na Bwana mkubwa.

ilikuwa ngumu lakini angefanya nini na bwamkubwa keshaamua?

utengano wao ulikuwa ni wa bila kuambiana TUACHANE sasa kila mmoja akawa na maisha yake. no simu no salamu. walipotezeana kwa herufi kubwa kabisa huku maumivu makuu yakiwa yametanda zaidi mauongoni mwa Bishosti.

siku, wiki na hatimaye Miezi ikapita.

Nani alikwambia penzi la historia kufutika mioyoni mwa wapendanao ni rahisi?

Bwana mkubwa nafsi ikaanza kumsuta! lawama ndani yake zikaanza kurindima, alijituhumu kuwa mkosefu mkubwa.

hamu ya mpenzi wake ikarejea kwa mabavu ikimkaba koo sambamba na shutuma kibao za kwanini amtenge mwanamke aliyekuwa akimpenda kwa dhati.

kuna siku moja Usiku  bwanamkubwa alishindwa  kabisa kuumaliza yaani hakubahatika kutembelewa kabisa na usingizi, alijikuta anatamani sana uwepo wa Bishosti.

mwanzo alidhani masikhara ila mwisho uzalendo ukamshinda usiku uleule
akaitafuta simu yake nakuisaka namba ya Bishosti akaipiga kwa unyonge akiomba msamaha akihitaji penzi lirudi tena..

mishale ya saa ilikuwa ni saa nane za usiku bila shaka shetani aliyeharibu penzi lao alikuwa kajisahau na amelala fofofo, hivyo bwana mkubwa pamoja na bishosti wakatumia fursa hiyo kurudiana.

LAKINI KUMBE NI HERI UFA WA UKUTA WA NYUMBA HUREKEBISHIKA LAKINI UFA WA UKUTA IMARA WA PENZI KAMWE HAUREKEBISHIKI....IlE LADHA YA PENZI LAO LA MWANZO WALIJITAHIDI KUIRUDISHA LAKINI WAPI!


KUMBE BI SHOSTI ALIRUDI KWA BIMKUBWA SABABU YA MAZOEA TU ZILE SIKU WALIZOKUWA WAMETENGANA TAYARI ALISHAMPATA MWENGINE.....HEBU FUATANA NAMI SEHEMU YA PILI KUJIFUNZA ZAIDI UJUE MAPENZI NI NINI....

  SEHEMU YA PILI


Ucheshi wa bishosti, ukarimu, utani na kucheza pamoja ndiyo vitu vikubwa vilivyomfanya Bwanamkubwa atake kurejeana na Bishosti.

mwanzo alijidanganya kuwa anaweza kuachana na bishosti kirahisi na kusiwe na tatizo lolote lakini nafsi ilimsuta hakuona mwanamke wakutengeneza nae historia zaidi ya bishosti wake.

aliomba msamaha akitaka penzi lao lirudi tena, bishosti alikubali lakini tayari alishatafuta faraja kwa jamaa mwengine lakini angefanya nini wakati ni ukweli kwamba muda mwingi akiwa na jamaa alikumbuka uwepo wa bwanamkubwa?

bishosti aliyajua maumivu ya mapenzi na alijua jinsi yanavyotesa mioyo ya watu, kila alipokumbuka alivyoteseka hakuwa tayari kabisa kumuumiza kijana wa watu hivyo hakutaka kumuacha mpenzi wake mpya aliamua kutumikia mabwana wawili.

pengine hilo ndilo lililoleta kasoro kwenye penzi lake na bwanamkubwa,

historia yao ile ya sehemu ya kwanza ilibaki kuwa historia kweli, sehemu ya pili ya penzi lao ilikuwa ni tofauti kabisa.

bishosti alikuwa mkali na simu yake, alificha maovu yake, bwanamkubwa alibaki na tahamaki huku akijilaumu kuwa yeye ndiye chanzo cha yale yote.

bishosti alikuwa mpole sana kwa bwanamkubwa lakini safari hii alimuchukulia kawaida tu bwanamkubwa na alikuwa tayari kabisa hata baadhi ya vitu kumkatalia.

"hakika bahati kurudi mara mbili katika mapenzi nayo ni bahati"

mara zote bwanamkubwa alikuwa akijiwazia maneno hayo kichwani mwake alipokuwa akiyaona mabadiliko ya mpenzi wake.

alirudi nyuma kimawazo nakukumbuka kuwa alitumia muda mrefu sana kulijenga lile penzi la sehemu ya kwanza na aliumia zaidi kuona hawezi tena kumfanya bishosti kuwa yule wa mwanzo.

Kwa mara ya kwanza kabisa bwanamkubwa aliyaona makosa yake akajifunza kutumia vema nafasi aipatayo kwa maana nafasi kurudi tena ikipotea ni ngumu.

alijiona pia kuwa ni mume bora baadae kwa mkewe atakayempata sababu hatamdharau nakumuumiza kama alivyofanya kwa bishosti, aliona hapaswi kuendelea kuwa mtumwa kwa biahosti ambaye alisamehe kwa mdomo lakini hakuwa tayari kuenzi mapenzi kwa moyo wake wote wa mwanzo.

kwa mara ya pili wakaachana tena safari hii wakiambiana TUACHANE baada ya bishosti kudanganya anaenda kulala kwao kumbe alienda kwa jamaa ake mwengine.

bwanamkubwa aligundua hili akahisi awezi kuendelea na bishosti SASA RASMI WAKAACHANA.

lakini nikwambie kitu kuhusu mapenzi ni kwamba kama ingeendelea sehemu ya tatu bila shaka BISHOSTI yeye ndio angekuwa ndiye mwenye majuto sababu katika mahusiano kinachoumiza zaidi ukiachana na mtu ni pale unapogundua wewe ndio ulikuwa mkosaji...

BILA SHAKA KUNA FUNDISHO KATIKA SEHEMU YA KWANZA NA SEHEMU HII YA PILI YA SIMULIZI HII...

"MAPENZI NI ZAIDI YA UKIFIKIRIACHO"
Bin Zongo....

MWISHO....