Hekaheka
zachachama,kelele huko nyikani
Dawa
ya chachu kutema, isibakie kinywani
Usibaki
kutetema, ukavimbiwa tumboni
Nyikani kwa tanda giza, naisikia miluzi
Nyika
iliyo salama, hii miluzi ya nini
Kukiepuka
kihama, hiyo miluzi acheni
Mioyo
yote ya nyama, kutishana kwa fatani
Nyikani kwa tanda giza, naisikia miluzi
Ebu
simameni hima, acheni usubihani
Tulimuomba
Karima, atupatie aghani
Tukapewa
ilo vema, naomba tuitunzeni
Nyikani kwa tanda giza, naisikia miluzi
Ukivalia
pajama, huku machozi usoni
Utapata
tu lawama, nyika ikiwa motoni
Tuende
tukichechema, tutunze mali nyikani
Nyikani kwa tanda giza, naisikia miluzi
Miluzi
isiyo mema, yatanda masikioni
Hakuna
hata la wema, upoto sio kifani
Tumezaliwa
kusema, ila busara pimeni
Nyikani kwa tanda giza, naisikia miluzi
Mbele
tusirudi nyuma, tukachekwa na wageni
Tujengane
tu kwa wema, hekima za duniani
Tukithubutu
simama,tutaishia jangwani
Nyikani kwa tanda giza, naisikia miluzi
Bucha
lake ni nyama, sumu huuzwa dukani
Iweje
ukasakama, sumu kuuzwa buchani
Fateni
tulowatuma, kutuweka furahani
Nyikani kwa tanda giza, naisikia miluzi
Akili
za ukilema, zaweka nyika tabuni
Tujadili
kwa heshima, shaka zote za nyoyoni
Tupate
jibu la wima, kwa kudura ya Manani
Nyikani kwa tanda giza, naisikia miluzi
Hii miluzi kikoma, yatakwisha mdomoni
Nawaeleza mapema, yatazameni
ya ndani
Afya bora na uzima, ni jambo zingatieni
Nyikani kwa tanda giza, naisikia miluzi
Lifikapo la kusoma, someni bila miwani
Mmejaliwa karama, ulimbukeni wa nini
Kujiridhisha mtima, hiyo miluzi acheni
Nyikani kwa tanda giza, naisikia miluzi
By Fulgence Makayula