CHIZI MAFANIKIO SEHEMU YA 4

ILIPOISHIA
Bi getrude anasukumwa nakuanguka chini, huku mama yake salim akikimbilia ndani huku analia, tayari mawazo mabaya yalishamuingia kuhusu kifo cha mwanae_

SASA ENDELEA...

Alijisikia vibaya sana kusukumwa namna ile, alijiokota taratibu nakukaa kitako kabla hajaamka nakuanza kumfuata nyuma mama yake Salim.

tayari alishaona dalili mbaya ya chuki ambayo mara zote aliomba isijitokeze katikati yao hasa kuhusu kifo cha Salim.

alijisikia vibaya sana Bi Getrude, aliona namna ambavyo dunia inamgeuka ghafla.

hatua zake ziliishia kwenye mlango wa chumba alichoingia mama yake salim.

ulikuwa umefungwa kwa ndani, alijaribu kugonga mlango nakumsihi afungue lakini maneno aliyojibiwa ndio yalimuumiza zaidi. na alisita hata kuendelea kugonga mlango ule.

" Kamwambie mwanao aje animalize namimi, sioni thamani ya kuendelea kuishi kwakweli mwambie aje aniue kama alivyomuua Salim wangu, alikuwa na makosa gani masikini mwanangu"

kutoka ndani yalisikika maneno haya, ilikuwa ni ghafla mno mama yake salim kubadilika.

 hii ilimshangaza sana Bi Getrude, alinyong'onyea sana kwa maneno yale.

 alitamani hata ardhi ipasuke ajichomeke ndani yake.

licha ya miguu yake kuwa mizito kunyanyuka nakupiga hatua lakini alijitahidi baada yakujishauri kwa muda akaamua aondoke.

maumivu aliyokuwa nayo aliweza kuyahisi mwenyewe tu hakuna ambaye angeweza kuyasimulia, alijiona mwenye hatia, alijiona mkosefu, roho ilimuuma sana.

alianza kuacha viunga vya nyumba ya kina Salim kwa unyonge kabisa, mkononi mwake alikamata zile karatasi alizoandika salim lakini sina uhakika kama alijua amekamata karatasi zile.

ni mwili tu ndio ulikuwa unatembea barabarani lakini akili yake ilikuwa mbali sana kimawazo.

moyoni mwake alitamani Jef apone haraka ili alijue kosa lake, alitamani angegawana maumivu na mwanae huyo lakini aliumia zaidi alipobaini Jef hana uwezo huo wala hang'amui chochote.

akiwa katika wimbi la mawazo hayo ghafla alishtushwa na kelele za watu wakipiga mayowe,

ni hapa ndipo aliposhtuka kijana mmoja akimvuta kwa nguvu kumuondoa barabarani, mapigo ya moyo yalimuenda kwa kasi, mate yalimkauka mdomoni.

almanusura agongwe vibaya na pikipiki iliyokuwa ikijaribu kupenya kwa kulipita gari.

matusi mfululizo yasiyoweza kuandikika hapa yalitoka kinywani mwa dereva yule wa pikipiki.

ni sentesi moja tu ndio angalau naweza kuiweka hapa aliisema yule kijana aliyempakiza mtoto wa shule kwenye pikipiki yake "......kwani ulitumwa ujiuze kwa mkopo......." maneno mengine yaliyoendelea na yaliyoanza hayakuwa yenye heshima na utu hata kidogo kwa mama mtu mzima kama Bi Getrude, lakini ni nani angeweza kumnyamazisha dereva yule wa pikipiki, ambaye alitukana huku akivuta mafuta nakuendelea na safari.

Haikuwa siku njema kabisa kwa Bi Getrude alijiona ni mwenye mkosi mno.

wasiwasi na kihoro vikamfanya akae chini kwa muda kwenye kizimba cha baraza ya watu, kabla ya baadae kujishauri aendelee na safari.

wapo waliomsema kuwa aache mawazo barabarani, na pia wapo waliomfariji nakumtaka ashukuru Mungu kwa kunusurika na ajali ile.

muda alioamua kuondoka katika eneo lile ni muda ambao tayari watu walishaanza kusahau kilichokuwa kinataka kutokea.

kila mmoja sasa aliendelea na shughuli yake.

alibakisha mtaa mmoja tu ili aingie mtaa anaoishi yeye, hatua si chini ya ishirini ndipo sasa akapata pigo jengine ambalo lilimthibitishia kuwa kweli ile haikuwa siku nzuri kwake.

kwa macho yake bila kuhadithiwa na mtu alishuhudia namna ambavyo Jef anagongwa na gari wakati akivuka barabara.

kama kawaida Jef aliongozana na kundi la watoto wakimfuata na walipofika eneo lile la barabara watoto wale walisimama kutazama magari kabla hawajavuka lakini bila kutegemea Jef akawachomoka nakuingia barabarani.

Gari ndogo aina ya brevis iliyo kuwa mwendo kasi ilimvaa bila huruma.

kilichosikika ni milio ya kulalamika iliyotolewa na matairi ya gari kutokana na kusuguliwa kwa nguvu kwenye ardhi ya barabara.

Bi getrude alishindwa kukubali ukweli huu alihisi yupo ndotoni kwa kile alichokishuhudia! nguvu zilianza kumuisha miguuni na baadae machoni mbele yake akaona kiza kinene kikitanda.

karatasi alizokuwa amezishika mkononi zikamtoka bila kupenda na yeye alidondoka chini kama mlevi aliyezidiwa na kileo.

fahamu zikatoweka maungoni mwake....akabaki kimya pale chini! watu kutoka maeneo yote wakaanza kuzunguka eneo lile kushuhudia ajali ya kugongwa kwa Jef.

ni wachache sana ndio walimzunguka Bi Getrude.

Na Omar A. Zongo

INAENDELEA....

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »