MARIA & CONSOLATHA : KILELE CHA HUZUNI

Na.
Omar Zongo

Nimekaa juu ya kichuguu, katika kilele cha mlima wa huzuni, naangaza chini kutazama mandhari ya kijani kinachopamba msitu wa Mauti uliopakana na kijiji cha Majonzi kilichopo pembezoni kabisa mwa Taifa huru Tanzania.

Nimelazimika kuja huku juu ya kilima kukaa kwa siku saba za maombelezo ya wadogo zangu, dada zangu, watanzania wenzangu wazalendo Maria Na Consolatha.

Juu ya kichuguu cha mlima Huzuni, natafakari maisha ya mabinti hawa waliogusa mitima ya wengi afrika mashariki Na Duniani kwa ujumla.

Nani asiyeguswa Na khabari za wadada hawa!!??

Tangu maisha yao ya utoto mpaka ukubwa wao wakishangaza watu Na Utashi wao wakung'amua mambo katika masomo yao Na ndoto kubwa zakulitumikia Taifa lao.

Kuungana kwao ulikuwa ni umoja ulio Na nguvu ambao daima ulidhihirisha kuwa utengano ni udhaifu.

Kama mapambano ya kupigania uhai yangelikuwa Na mafanikio naamini Consolatha Na Maria wangelikuwa washindi Na mpaka Leo wangekuwa miongoni Mwa tulio hai.

Lakini sivyo!!

Maisha yao yanazidi kudhihirisha kuwa duniani kuna maneno mawili tu, KUWA na KUTOWEKA.

Kuwa, ndio maisha ya uhai, pumzi tusiyolipia, majigambo, huzuni, furaha, dhiki, faraja, uzima, maradhi Na vyoote vinavyokamilisha harakati za maisha.

Kutoweka, ndio tamati ya vyote hapo juu, hakuna wakupinga wakati ukifika kila mmoja atalazimishwa nguvu zake zote kuwa udhaifu na kutulizwa na jinamizi la mauti.

Juu ya kilele cha Mlima Huzuni, natafakari maajabu ya MUNGU, napatwa hofu hasa nikikumbuka ukweli usiopingika yakwamba HUJAFA, HUJAUMBIKA.

Katika kuonesha ujabari wake, utukufu Na Utashi wa kuumba, Mwenyezi huumba kila kitu kwa namna yake.

Wakati wewe unaona ni ajabu kwa Maria Na Conso kuungana, kwa MUNGU lilikuwa Jambo dogo mno Na alikuwa anajua nini anachofanya.

Kwa wenye imani mara zote hujikinga kwa MUNGU, madhara ya huzuni yasiwape udhoofu wa mwili.

Hakika yatupasa Kumkabidhi MUNGU huzuni yakuondokewa Na watanzania wenzetu hawa.

Tuwasindikize Na maombi wakapumzike kwa Amani, tuwaombee wakawe mabalozi mbinguni.

Wakalitangaze taifa letu huko, wakamuombe MUNGU atuzidishie imani watanzania.

Atuongezee uzalendo Na huruma baina yetu.

Azichome roho za wanafiki, wasaliti Na wenye kutakia madhara nchi yetu.

Hakika pengo la mabinti hawa halitaweza kuzibika kama mapengo kadhaa ya watu mashuhuri tuliowahi kuwapoteza katika nyakati tofauti.

MARIA NA CONSOLATHA  HAKIKA SIMULIZI ZENU ZITAENDELEA KUISHI KWENYE VICHWA VYETU.

Mungu awapumzishe kwa amani wapendwa, mmefariki Na tamaa yenu ya siku moja kuwa wake wa fulani(Kuolewa)

Mmefariki mkiwa mnatamaa yakuja kutumikia taaluma ya elimu.

Mmefariki wakati ambao Taifa linahitaji sana vijana wenye kiu ya kufanya kitu kwa ajili ya jamii yao.

Hakika kumbukizi za kifo chenu daima zitakuwa ni Maradhi yaunguzayo mioyo yetu watanzania.

Tutaendelea kuwaenzi.


Ningali juu ya Mlima wa Huzuni, sitashuka kwa simu saba za maombolezo, muda huu
Mvua ya radi inapiga, inanidondokea mwilini nakuyameza machozi yangu.

Naona namna ambavyo machozi yangu yanavyochanganyika Na maji kabla yakutiririka mabondeni kuungana na wanyama, ndege pamoja Na miti mikubwa inayounda msitu wa Mauti uliopakana Na Taifa huru Tanzania.

Sitaacha kuwaenzi kwa tenzi Maria Na Conso.

Huzuni hii moyoni,
Machozi haya jichoni,
Maisha haya kwanini,
Majonzi mpaka lini??

Maisha yenu huzuni,
Maradhi tele mwilini,
Pumzikeni kwa amani,
Afuataye sijui ninani??

Na
Omar Zongo

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »